Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi siku za karibuni dunia na Taifa letu kumekuwa na shock kubwa sana ambayo imepelekea upandaji mkubwa sana wa bei ya bidhaa muhimu kiasi ambacho Watanzania lakini na wananchi wengi duniani wamepata ugumu wa kukabiliana. Kama Taifa lakini kama Serikali ukilinganisha na Serikali zingine zote duniani moja katika majukumu yao muhimu katika eneo hili ni kuhakikisha kwamba inafanya intervention ambayo itasaidia kupunguza gharama za maisha itasaidia kupunguza upandaji wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu unaonyesha moja katika bidhaa ambazo zina madhara makubwa sana kwenye upandaji wa bei ya bidhaa na huduma katika nchi yoyote ni mafuta ya petrol, diesel na kadhalika. Changamoto hii bado tunayo na kwa sehemu imepata utatuzi kulikuwa na sera za kifedha na za kikodi ambazo Serikali ilizifanyia kazi na tukapata ruzuku na sasa tumeona faida yake kwamba mafuta kwa sehemu kubwa yamepungua bei ukilinganisha na vile ambavyo ingekuwa kama Serikali isingechukua hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili naomba niipongeze sana Serikali imechukua hatua muhimu lakini niombe sana hatua hizi zisiishie kwenye ruzuku peke yake, mikakati mingine yote ambayo Serikali imeiweka ikiwemo pamoja na Strategic Reserve iendelee ili Watanzania waweze kupata nafuu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni ule ule kwamba gharama ya maisha imepanda duniani kote, bei ya nishati imepanda duniani kote kinachotofautisha kati ya Taifa moja na lingine ni hatua ambazo Serikali inazichukua ili kupunguza gharama hizo. Tanzania tumeongoza njia Mheshimiwa Rais ameongoza njia kwa kutoa hizo Bilioni 100 ambazo zimekuja kama ruzuku kwenye sekta ya mafuta ili Watanzania wapate unafuu. Unafuu huu utapatikana zaidi iwapo jitihada zingine ambazo Mheshimiwa Waziri umezisema utaendelea nazo na utaenda kuzikamilisha na mimi nitaunga mkono hoja ya bajeti hii kwa sababu naamini watakwenda kuitekeleza hii mikakati ambayo imewekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni kuhusu Jimboni kwangu. Naishukuru Serikali, kwa sehemu Madaba tumepiga hatua kwenye upatikanaji wa umeme vijijini, asilimia karibu 95 ya Vijiji vya Madaba na maanisha Madaba kama Halmashauri, vijiji vyote vimepata umeme isipokuwa Kijiji kimoja cha Ifinga. Kwenye hili naipongeza sana Serikali. Kijiji kilichobaki ambacho ni Ifinga kipo kilometa 48, Mheshimiwa Waziri alituletea wataalam wa masuala ya umeme hapa na wakandarasi, tumezungumza nao na wametuhakikishia kwamba mwezi Desemba, Kijiji cha Ifinga kitakuwa kimepata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanaifinga wanasubiri Desemba waende kusherehekea Krismasi wakiwa na umeme kwenye nyumba zao. Pia pamoja na jitihada nzuri za Serikali, yapo baadhi ya maeneo ndani ya Madaba hayajafikiwa na umeme, nayo ni maeneo muhimu sana. Kwanza tunazo sekondari mbili, hizi naomba Mheshimiwa Waziri aziandike tafadhali, tunayo Sekondari Kongwe ya Lipupuma, ipo ndani ya Kata ya Mkongotema, Kijiji cha Mkongotema, sekondari hii ni ya muda mrefu wakati wana-design umeme sekondari ilikuwepo, wakati wanaleta nguzo sekondari ilikuwepo, wakati wanafunga nyaya sekondari ilikuwepo, lakini hadi leo haijapata umeme na mtaa mzima wa Lipupuma haujapata umeme. Watanzania wanaoishi maeneo yale wana imani na Mheshimiwa Waziri, tunaomba tupate umeme haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madaba pia kuna sekondari mpya inajengwa pale na sekondari hii amepewa heshima Mbunge wa Jimbo la Madaba, Joseph Kizito Mhagama na inaitwa kwa jina hili. Tunaomba tupewe umeme haraka sana kwa sababu mwezi Januari tunaanza masomo pale. Kwa hiyo tunaomba sana eneo hili lipate umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo eneo la sekondari mpya vile vile inayojengwa Maweso, ni pembezoni kidogo cha kijiji, hatuna umeme. Watanzania wanaoishi eneo lile wanasubiri wapate umeme. Maeneo ambayo yamesambazwa umeme kwenye vijiji vyetu hayajasambazwa kwa ukamilifu. Tunaamini kwenye programu ya kujaziliza umeme na kupanua umeme, Madaba itapewa kipaumbele. Kijiji cha Mtepa mitaa yake mitatu Mtumbika, Makaraveti na Miembeni kote umeme haujafika. Wananchi hawa wanategemea Waziri awape kipaumbele

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Vitongoji vya Ngadinda, Lilondo na baadhi ya vitongoji vya Mahanje havijapata umeme. Hata Madaba Mjini pale pale katikati ya mji kuna vitongoji havijapata umeme, Kijiji cha Gumbilo, kijiji Kongwe kabisa nacho baadhi ya vitongoji havijapata umeme. Mimi binafsi sina mashaka juu ya commitment ya Serikali kwenye kupeleka umeme vijijini, naelewa jambo hili lina bajeti implication, lakini kwa sababu tulishawaahidi Watanzania na kwa sababu mama amedhamiria kufanya kazi hii kwa weledi mkubwa, naomba Wizara imsaidie mama kufikisha umeme vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukuza uchumi kama hatutafikisha umeme vijijini ili vijana wa Kitanzania waweze kujiajiri kwenye shughuli ndogo ndogo za ufundi umeme, ufundi simu, ufundi redio, lakini wafanye masuala ya welding. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maslahi ya muda, nakushukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Madaba na naunga mkono hoja. (Makofi)