Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika hotuba hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kufanya katika nchi yetu na hasa ile subsidy ambayo imetolewa kwenye bei ya mafuta na hata tumepunguziwa kidogo namshukuru sana. Pia niwapongeze Wizara ya Nishati, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa ambayo pia inaendelea kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri bado kuna changamoto katika Wizara hii na napenda kuzungumzia baadhi ya changamoto ambazo nimeziona. Changamoto ya kwanza ni huu Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini ambao unasimamiwa na REA. Umeme umesambaa katika vijiji vingi katika nchi hii, lakini ukienda katika hivyo vijiji utakuwa umeme umewekwa katika center ya kijiji, kijiji kimoja kinakuwa na nguzo 20 au chini ya 20, kwa hiyo unakuta sehemu kubwa ya kijiji hakuna umeme. Hii imesababisha malalamiko mengi sana kwa wananchi. Ningeshauri sana jambo hili walizingatie, haitakuwa na maana tukisema tumeweka umeme katika vijiji vyote katika nchi hii, wakati wanaonufaika katika vijiji ni asilimia ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni Mradi wa Kusambaza Gesi Majumbani. Mradi huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, lakini usambazaji wake unasuasua sana. Hadi sasa gesi hii imesambazwa katika Mikoa mitatu Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na katika viwanda ni viwanda 53 tu ambavyo vimesambaziwa gesi, lakini pia nyumba ambazo zimesambaziwa gesi ni 1,379, nadhani tunaweza kuona ambavyo speed yake ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya gesi kwenda majumbani ni kubwa sana, itatusaidia kutunza mazingira yetu. Watu wengi wakisambaziwa gesi majumbani wataepuka matumizi ya mkaa na kuni, hivyo tutalinda mazingira yetu. Kwa hiyo ningeomba sana Wizara hii iendelee kwa speed ile ambayo watu tulikuwa tunaitarajia, ikiwezekana miji yote au mikoa yote ya Tanzania ipate huduma hii ya gesi majumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye Jimbo langu la Mpwapwa, bado usambazaji wa umeme sio wa kuridhisha sana. Mpaka sasa hivi kuna zaidi ya vitongoji 50 ambavyo havina umeme, lakini vijiji ni zaidi ya 15 bado havina umeme. Nimesikia wengine wanasema kimebaki kijiji kimoja, lakini mimi ni zaidi ya vijiji 15. Kwa hiyo ningeomba sana speed ya usambazaji pia iongezeke, vitongoji zaidi ya 50 ni vingi mno, hata tunashindwa kuelewa kama kweli katika Jimbo la Mpwapwa tuna katika umeme vijiji vyote. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri na wenzake wazingatie sana jambo hili. Umeme ndio suluhisho la uchumi katika nchi yoyote duniani, kama nchi haina umeme maana yake hata uchumi wake utaendelea kudumaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni muhimu katika viwanda na tumesema viwanda vikubwa au vidogo ndio vinavyotoa ajira kwa wananchi wengi, sasa kama hatuna umeme wa uhakika maana yake viwanda havitakuwepo na hata tukiwa navyo havitafanya kazi kama inavyotakiwa. Kwa hiyo ni muhimu sana tukazingatia kwamba, tukiwa na umeme wa uhakika tutakuwa tumejitahidi kutoa ajira kwa vijana wetu na viwanda vitakuwepo, lakini vijana wa vijijini ambako pia hakuna viwanda watafungua viwanda vidogo vidogo. Watafungua viwanda vya kuchomelea vyuma, wengine watafungua saloon, kuna kazi nyingi sana ambazo zinategemea umeme. Kwa hiyo, Wizara hii ni muhimu inatakiwa iangalie sana na izingatie jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la bei ya kuunganisha umeme, jambo hili bado halijaeleweka vizuri, utasema kijijini ni Sh.27,000, lakini bado wananchi hatujaelewa vizuri au hawajaelewa vizuri wapi ni mjini na wapi ni kijijini. Kwa hiyo unakuta kamji kapo nje ya mkoa lakini kwa sababu kuna ka-centre kidogo, basi gharama ya kuunganisha umeme inakuwa ni kubwa. Nadhani jambo hili kama Wizara ingeweza kuli-address vizuri ili wananchi waelewe ni maeneo gani ambayo gharama ya kuunganisha umeme inatakiwa iwe Sh.27,000 na maeneo gani yanayotakiwa kuunganisha umeme kwa bei ya Sh.300,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila hivyo kumekuwa na migongano mingi sana, wananchi wa vijijni wakiambiwa hiyo bei ya Sh.300,000 hawawezi ku-afford, matokeo yake hawa watu wanaamua kuacha, kwa hiyo hakuna umeme vijijini. Kwa hiyo naomba hilo nalo liwekwe vizuri ili tuelewe ni maeneo gani yanaunganishwa kwa Sh.27,000 na maeneo gani yataunganshwa kwa bei ya Sh.300,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine au changamoto ambayo ipo kwenye Wizara hii ni kukatika katika kwa umeme hovyo na hii nadhani inasababishwa na uchakavu wa miundombinu. Wizara ingejikita sana kuboresha miundombinu kwasababu kukatika katika kwa umeme katika maeneo yetu kumesababisha hasara kubwa sana kwa wananchi, vifaa vyao vinavyotumia umeme vimeungua na taratibu za kupata compensation ni ngumu, kwa hiyo watu wamekutana na tatizo hili, umeme unakatikakatika kila wakati. Kwa hiyo tunaamini kwamba jambo hili wanalijua na watajitahidi sana kuimarisha miundombinu. Miundombinu iliyopo sasa katika maeneo mengi ya nchi yetu imechakaa sana na ndio maana umeme hauwezi ku-flow vizuri. Hivyo, tunawaomba sana kama Wizara wazingatie hili na ikiwezekana ule mradi wa kusambaza nguzo za zege uendelee katika maeneo yote ili umeme uwe stable, nchi iwe na umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)