Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii muhimu ya kuchangia Wizara hii ambayo ni engine ya maendeleo ya nchi yetu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu wake vijana hawa, ukisikiliza hata hotuba yao imesheheni na imeshiba mambo ambayo wananchi yakifanyika hakika tutafika mbali katika sekta hii ambayo ni engine ya maendeleo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nianze mchango wangu kwanza na Jimbo langu la Iramba Mashariki Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. Katika suala zima la bei za kuvuta umeme kwa mara ya kwanza. Wilaya zetu hizi ni mpya kwa mfano, Wilaya yangu ya Mkalama ni Wilaya mpya. Wilaya kama Wilaya inapotamkwa kwamba ni Wilaya mpya ni kwa sababu tu ya utawala lakini maisha ya wananchi ni maisha ambayo bado ni ya kijijini na uwezo wao ni mdogo, sasa hili suala la kwamba kwa sababu ni Makao Makuu ya Wilaya lakini vilevile kuna Miji Midogo tu iliyochangamka tu kwa mfano, Mji wa Iguguno. Iguguno ni Mji mdogo sana ambao haujawa Mji rasmi lakini kwa sababu tu pamechangamka tayari TANESCO wanasema kwamba eneo kama hili watavuta umeme kwa 320,000 sasa lengo la Serikali la kufikisha umeme kwa wananchi katika maeneo kama haya kwa bei hizi linakuwa si rahisi kulifikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri Wizara iangalie namna nyingine yakufanya assessment nani avute umeme kwa 320,000 na nani avute umeme kwa Shilingi 27,000 tusitumie maeneo tu kwamba kwa sababu ni Wilaya kwa sababu ni Mji lakini wananchi wanaoishi katika mazingira haya katika maeneo haya, maisha yao ni ya chini sana, ni maisha ya kijijini. Kwa hivyo suala la kusema kwa sababu pamechangamka tu kwa mfano pale Iguguno watu wavute umeme kwa 320,000 wananchi wengi wataendelea kuishi bila umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye Wilaya hizi mpya kama Wilaya ya Mkalama ukifika pale Nduguti Makao Makuu ya Wilaya, kwa sababu tu kuna jengo la halmashauri nanini lakini maisha ya wananchi wa kawaida ni maisha ya kijijini kabisa. Kwa hivyo, mimi ningeomba kabisa suala hili la kuvuta umeme kwa 320,000 na hii 27,000 Wizara iangalie namna nyingine ya kufanya assessment nani avute umeme kwa njia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika suala zima la hizi tariff za umeme kuna hii tariff ya D1 ambayo ni kwa ajili ya wananchi wa chini unalipa Shilingi 10,150 unapata unit 75, TANESCO wamekuwa hawatoi elimu vizuri kuhusu hii tariff inakuwa kama vile inawategea tegea wananchi, kwamba ukinunua huu umeme wote unapata unit 75 unatumia kwa mwezi mzima, hasa haitoi elimu matokeo yake wale wananchi wananunua umeme kidogo kidogo mwisho unaisha kabla ya mwezi inabidi anunue tena, sasa anakuja anatolewa na system kwenye hii tariff na akitolea anakwenda kwenye gharama kubwa zaidi. Kwa hiyo, mimi ningeiomba TANESCO watoe elimu kwa wananchi kuhusu hii D1 ya malipo ya umeme ili wananchi waweze kujua masharti yake waweze kufaidika nayo, kwa sababu lengo la kuiweka hii nikuwasaidia wananchi wa chini waweze kutumia umeme vizuri na waweze kupata umeme na waweze kulipa bill zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nataka pia niupeleke kwenye bomba la gesi. Bomba hili limetumia fedha nyingi sana mpaka kufika pale Dar es Salaam, mpaka sasa asilimia karibu 50 ya matumizi ya bomba hili ni matumizi ya kuzalisha umeme na tunakuja na miradi mikubwa kama Nyerere Hydro Power na mingine mingi Waziri ameisema kwenye hotuba yake, kwamba tutakuwa na umeme mwingi sana wa maji ambao ni umeme cheap. Kwa hiyo, nina hakika baada ya muda fulani TANESCO haita-opt kutumia gesi kuzalisha umeme kwa sababu watakwenda kwenye umeme wa maji ambayo ni rahisi. Sasa naamini kabisa baadaye hili bomba litakuja kuwa white elephant kwa sababu litakuwa limekaa pale na matumizi makubwa ni kuzalisha umeme na sasa tunakwenda kwenye umeme wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu Waziri amesema miradi mingi sana mikubwa ya mabilioni ya fedha lakini sijaona akigusia suala la kusambaza bomba hili kutoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza ili lipite kwenye miji hii na bomba hili likipita maana yake likitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, maana yake litapita Pwani, litapita Morogoro, litapita Dodoma, litapita Singida, litapita Shinyanga mpaka kufika Mwanza na litakapopita huku, sasa litasambazwa kwenye nyumba kuweza kutumia gesi kwenye nyumba zetu na hapo sasa tutakuwa tumetumia vizuri fedha nyingi ambazo zimetumika katika kutengeneza bomba hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakoelekea bomba hili halitatumika kwa sababu umeme tutakwenda kwenye maji na huo umeme wa maji ni mwepesi. Kwa hiyo, ningeshauri wizara katika miradi yake mikubwa ya mabilioni iliyoiweka suala la kutoa bomba hili Dar es Salaam na kulipeleka Mwanza liwekwe kama kipaumbele ili gesi hii iweze kutumika. Nimesikia kwenye hotuba yake amesema kutakuwa kuna vituo vile vya kupeleka gesi huku kwa kutumia vile vituo ambavyo gesi tutajaza kwenye magari na nini, najua imeenda kwenye private sector lakini itakuwa na gharama ikianza hivyo si mbaya, lakini Serikali iangalie jinsi ya kulitoa hili bomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile walaji wakubwa wa mkaa ni watu wa mijini kwa hiyo, bomba hili likipita hata mazingira yetu yatakuwa salama kwa sababau wananchi watatumia gesi hii kwenye nyumba zao na hivyo mazingira yatakuwa salama na tutaokoa gharama kubwa sana ambayo inatumika kulinda mazingira ya nchi yetu. Kwa hiyo, ningeomba Wizara ya Serikali kwa ujumla iangalie suala la kulitoa hili bomba Dar es Salaam na kulipeleka Mwanza kwa maana lipite kwenye mikoa mingi ili tuweze kutumia vizuri hii gesi ambayo Mungu ametujalia na Serikali imetumia fedha nyingi kuitoa huko iliko mpaka kufikisha Dar es Salaam, sasa iende kwenye matumizi ya wanatanzia ili iweze kuokoa maisha ya Watanzania iweze kuokoa mazingira yetu na hakika kama tukifanya hivi maisha yetu yatakuwa bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilipenda niseme katika mambo haya lakini nikupongeze sana Waziri, hotuba yako ni nzuri tuombe tu kwamba fedha zifike ili haya ambayo yameanza kutekelezwa yatekelezwe na ili nchi yetu iweze kufika mahala pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)