Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Nami nianze kwa kumpongeza Rais wetu, Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kujali maisha ya Watanzania na kipekee kwa jinsi ambavyo ametoa pesa kwa ajili ya kupunguza makali ya bei ya mafuta. Niwaombe watendaji bei hii iwanufaishe watu wote na siyo wa mijini tu. Kwa sababu tayari kumeshakuwa na malalamiko kwamba huko kwetu vijijini imepungua Sh.150. Naomba taasisi husika tulifuatilie kwa sisi tunaotoka vijijini ili keki hii basi wote tuweze kufaidika sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Waziri wa Nishati na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. Kipekee pia nimpongeze Mkurugenzi wa REA kwa kazi nzuri anayofanya, lakini na Mkurugenzi wa TANESCO, ndugu yetu Maharage Chande ameanza vizuri, amekuja na mikakati mizuri tunaiona, Nikonekt, Mita Janja tunaamini zitaenda kuondoa changamoto kubwa tulizokuwa nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisimama katika Bunge hili mwaka jana kama sasa ambapo Jimbo langu la Muhambwe lilikuwa lina vijiji sita tu vilivyowekewa umeme, lakini leo nisimame kuishukuru Serikali na kuipongeza kwamba kwa sasa nina vijiji 25 ambavyo vimefikiwa na umeme. Hii ni kazi nzuri inayofanywa na Shirika letu la REA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ninavyo vijiji 15 ambavyo hivi vinatakiwa kuwekewa umeme kwa sababu vimeshapelekwa nguzo lakini vimekumbwa na hii changamoto ya nyaya, MV na LV imekuwa ni changamoto. Tunaambiwa low voltage na medium voltage imepanda bei. Niombe Wizara, niombe Serikali iingilie kati hili suala la wakandarasi kukosa hizi nyaya. Vijiji vyangu hivi 15 ukivipa hizi nyaya vinaenda kuwashwa umeme, nitakuwa na vijiji 40, hii ni quick win.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jitihada za makusudi zichukuliwe kabisa kuhakikisha tunapata hizi nyaya kwa wananchi wangu ambao katika Jimbo la Muhambwe ambao wamesubiri umeme kwa muda mrefu sana. Maana vijiji hivi ni utekelezaji wa REA awamu ya III, mzunguko wa kwanza, maana tulipitia changamoto kubwa, naomba jitihada hizi zifanyike kwa haraka ili wananchi waliosubiri umeme kwa muda mrefu wa Muhambwe, Kukinana, Kumsenga, Kwakijina, Lukaya, Magarama, Kumkubwa wanasubiri umeme kwa muda mrefu. Naomba Serikali ichukulie kwa uzito wake ili tuweze kupata umeme katika jimbo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niungane na wenzangu kuhusiana na bei ya kuunganisha umeme. Sisi wananchi wa Muhambwe mradi wetu mzunguko wa kwanza ulichelewa sana, kwa hiyo, hatukufaidika na hiyo shilingi 27,000. Nimpongeze Waziri ameliona hili na amesema ndani ya miezi sita atakuja na jibu zuri. Niombe Jimbo la Muhambwe lipewe upendeleo wa kipekee kwa sababu hatujafaidika na hiyo bei ya shilingi 27,000 ili wananchi wangu waendelee kulipa shilingi 27,000 ili waweze kuunganisha huu umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuiomba Serikali, pamoja na jitihada hizi nzuri bado umeme haujawafikia wananchi. Kipekee niwasemee wananchi ambao wanatumia hizi taasisi mbalimbali ikiwemo taasisi za afya;- mahospitali na zahanati, lakini taasisi za elimu; mashuleni, taasisi za dini; makanisani na misikitini bado ni changamoto kubwa. Naomba REA wachukue jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba taasisi hizi zinapata umeme, kwa sababu tunapozipatia taasisi hizi tutakuwa tumewagusa watu wengi kwa wakati mmoja na vilevile tutakusanya mapato zaidi kwa hizi taasisi kwa sababu zina uhakika wa kulipa zaidi. Naomba zipewe kipaumbele cha makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kilio chetu Mkoa wa Kigoma kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa. Niipongeze Serikali na kumshukuru Waziri, nimeona kwenye vipaumbele ni kipaumbele cha kwanza kuunganisha Mkoa wa Kigoma kwenye gridi ya Taifa. Namwomba Mheshimiwa Waziri kama walivyotuahidi kwamba mwezi Oktoba, Mkoa wa Kigoma tunakwenda kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa, basi bajeti i-reflect kile walichotuahidi kwamba kwa bajeti ambayo wametuwekea basi iweze kuunganishwa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tutengewe bajeti ya kutosha ili tuweze kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa kama walivyotuahidi mwezi Oktoba ili na sisi wananchi wa Mkoa wa Kigoma basi tuanze hizo biashara wenzetu wanazofanya kama za vinyozi, vijana wanasubiri kwa hamu, basi na sisi tuuze soda baridi, tuuze maji baridi, maana yake tumesubiri kwa muda mrefu, naomba lizingatiwe, kama tulivyopewa kipaumbele cha kwanza, basi na pesa pia tupewe mgao wa kutosha kama kipaumbele cha kwanza kinavyoonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali vile vile, mwaka jana tulikuwa na mradi wa kupata umeme kutoka maporomoko ya Mto Malagarasi, megawati 49.5. Nimeona safari hii tumetengewa Bilioni 13. Nichukue nafasi hii kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa sababu kupata umeme katika maporomoko ya Mto Malagarasi itakuwa ni suluhisho la kudumu. Naomba tulichukue kwa umuhimu wake ili wananchi wa Muhambwe waweze kupata umeme kutoka katika Mto Malagarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zote hizi niendelee pia kuipongeza TANESCO. Mkurugenzi amekuja na mikakati mizuri, lakini nimepitia taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali. Ili tuweze kulisaidia hili shirika na tuweze kulikwamua hapo lilipo, lazima tulisaidie hili shirika. Shirika hili la TANESCO ni kati ya mashirika ya Serikali ambayo yana deni kubwa kuliko mtaji. Hii imeoneshwa kwenye ukurasa wa 36 wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shirika hili linadaiwa Tritioni 13.4 na huku likiwa na mtaji wa Trilioni 3.0. Hii ni uwiano wa takribani asilimia 356. Hii ina maana gani? Shirika hili haliko himilivu, shirika hili halijasimama kibiashara. Kwa hiyo, naiomba Serikali iisaidie shirika hili. Tunafahamu katika deni hili liko principle na kuko na interest. Pia yapo na madeni mengine kama hapa Wabunge wengi wamesema jinsi ambavyo wanadaiwa kwenye gesi, basi Serikali ichukue jitihada za makusudi kulisaidia hili shirika ili tuweze kulipima kwa sababu madeni yao wameyarithi, ni madeni ya miaka mingi, mengine ni ya makaratasi lakini mengine ni kama hayo nimesema ni interest.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lisaidiwe hili shirika kuweza kulipa hili deni, aidha Serikali ilichukue hili deni au iligeuzwe hili deni liwe mtaji au iipe ruzuku TANESCO hasa kwenye hii gesi ambayo matumizi ya gesi ni makubwa takribani Bilioni 40 mpaka Bilioni 50 tumeona TPDC wanawadai Bilioni 400 shirika hili haliwezi kwa nini nasema haliwezi, nimepitia mahesabu ya mapato ghafi ya shirika hili, hawa wanakusanya takribani Bilioni 120 hadi Bilioni 150 kwa mwezi ina maana kwa mapato yao hata tukiwaambia wasitumie hizi pesa kwa jambo lolote hili deni watalilipa ndani ya miaka Nane mpaka Tisa, hawawezi kulilipa, Serikali ichukuwe jitihada za maksudi kuisaidia TANESCO ili ilipe hili deni au ilichukue hili deni ili TANESCO iwe na mtaji mkubwa kwa ajili ya uhimilivu wa shirika hili kuweza kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu umeme ni uchumi, umeme ni siasa na wananchi wanahitaji umeme, wanahitaji kuona siyo kuwaambia na Ilani yetu imewaambia tunakwenda kumaliza kupeleka umeme, sasa tukiwa bado shirika haliko imara hivi basi itakuwa ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao viongozi wazuri wamewekwa pale katika Wizara Waziri, Naibu Waziri na Wakurugenzi wote, kwa hiyo Serikali itawasaidia waweze kufanya kazi zao vizuri na hii itakuwa kipimo kwamba tutaona matokeo chanya haraka kwa ajili ya ufanisi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naomba kuunga mkono hoja asilimia 100 nikitegemea yale yote niyoyashauri yataenda kutekelezwa kwa ajili ya maslahi mapana ya Jimbo la Muhambwe, ahsante sana.