Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi nianzie hapa ambapo ameishia Mheshimiwa Dkt. Samizi kuhusiana na TANESCO. CAG amesema ni miongoni mwa mashirika yanayoendeshwa kwa madeni, ina madeni zaidi ya mtaji kama ambavyo mwezangu aliyetangulia amesema na katika mashirika 16, shirika la TANESCO ni Namba Mbili, deni Trilioni 13, mtaji Trilioni Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jana Mheshimiwa Waziri umesema kwamba haya madeni ya TANESCO ni ya makaratasi, sasa ni muhimu kwa sababu hili ni shirika letu muhimu na tunapenda lifanyiwe reform, utuchambulie kinagaubaga kiwango kipi ni madeni ya makaratasi, kiwango kipi ni uzembe wa baadhi ya watu na kukosa kuwajibika. Ninasema hivi kwa sababu ukisikia deni linalozungumzwa na TANESCO sana ni lile Bilioni 500 la TPDC, lakini madai ya TANESCO kwa watu wengine nadhani ni kama zaidi ya Bilioni 400. Sasa hapa katikati kuna nini, na anayejua huo mzizi siyo mwingine ni wewe, lakini pili tumeambiwa hivi karibuni na nilikuwa napitiapitia hapa kwenye Mafungu yako nikifikiria kwamba nitaona sijaona, kwamba tunatakiwa kuilipa Symbion Shilingi Bilioni 355, kwa sababu gani, kuna jamaa mmoja tu pale TANESCO baada ya mkataba wa Symbion wakati 2011 na 2013 ulipoisha, yeye mwaka 2015 alisaini mkataba lakini 2016, Tarehe 24, Mei Serikali ikasitisha mkataba. 2017 wenzetu wakaenda Mahakama za Kimataifa, 2019 wakaendelea kwenda Mahakama za Kimataifa 2021 hatimaye Serikali mkakubaliana na TANESCO mkaingia mkataba na symbion kuilipa Bilioni 325. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tu kuna watu wamefanya maamuzi, ya kuingia mkataba whether ilikuwa ni kwa dili ama siyo kwa dili lakini Serikali hiyohiyo na baada ya miezi kadhaa ikasitisha mkataba, halafu Serikali hiyohiyo inakuja inaingia makubaliano na symbion kulipa kodi za wananchi Bilioni 355. Sasa unajua kuna wakati unakaa unafikiri hivi hizi hela za Watanzania, hizi pesa za walipa kodi hizi hivi tuna uchungu nazo kweli kama tunavyosema?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nnamshukuru Mwanasheria Mkuu yuko hapa, majuzi rafiki yangu Mheshimiwa Reuben wa Muheza alisema hivi kwa nini Mawakili wetu Wanasheria wetu hawapelekwi kwenye mafunzo ya kuwa wabobezi kwenye mikataba? Yaani kwenye mambo muhimu pesa hatutengi leo tunaambiwa nchi yetu eti tukamlipe symbion Bilioni 355 kwa kuvunja mkataba wa kizembe! Wanasheria wa nchi wako wapi Mwanasheria Mkuu tunaomba majibu haya! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wanalia umeme hapa hivi tujiulize tu….

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ndiyo Mheshimiwa wa Mbunge wa Tabora, taarifa.

T A A R I F A

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Halima Mdee anapouliza wanasheria wa nchi wako wapi sijui, yeye mwenyewe ni Mwanasheria ameuvua lini uanasheria? (Kicheko/Makofi).

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mdee unapokea taarifa?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijatumika tu rafiki yangu, tatizo mkiona tunafunguka mnafikiria sisi ni enemies hapana sisi ni Watanzania tunapigania Tanzania hii, kwa hiyo, Wanasheria ninaowazungumzia hapa na waliopewa dhamana na nchi hii kwa kusomeshwa kwa kodi za nchi hii, kusimamia mikataba ya nchi hii, kwamba leo tunaenda kuilipa Symbion Bilioni 355. Sasa naamini Mheshimiwa January utakuja kunijibu vizuri kwanza huo mpunga huko wapi maana hapa siuoni kwenye bajeti yako siuoni na kwenye bajeti iliyopita hatukuona.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee kwa hiyo taarifa umeipokea au umeikataa?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeikataa taarifa kwa mantiki niliyoieleza hilo la kwanza. Pili, ningependa kujua vilevile hawa watu wote walioshiriki katika mnyororo hadi Taifa limefika hapa, wanawajibika kiasi gani, wameshachukuliwa hatua, kama hawajachukuliwa hatua, mna mpango gani wa kuchukuwa hatua? Haiwezekani watu ‘wanavijikesi’ vya hovyo hovyo huko wako ndani, wakati kuna watu wenye kesi makubwa ya uhujumu uchumi tumekaa nao tu haiwezekani! Huwezi kutofautisha hili jambo uhujumu uchumi, kwa hiyo naomba nipata majibu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika muhtadha huohuo Bwawa la Julius Nyerere, katika mradi ambao Serikali imewekeza asilimia 100 kwa pesa za ndani ni mradi huu kutokana na maandiko yenu, 6.5 trilion. Mradi huu ulitakiwa ukamilike tarehe 14 Juni, kwa mujibu wa mkataba wa awali. Leo tunaambiwa umefikia asilimia 57, tunajua kwenye mkataba kuna sura mbili, Mwanasheria Mkuu yuko hapa, kwamba upande mmoja ukiwa na uzembe upande mwingine lazima ufidiwe, ninaomba Waziri ukija kutujibu hapa utuambie hasara ambayo Tanzania imeipata kwa Mkandarasi huyu kutokumaliza Tarehe 14 Juni, tunalipwa kiwango gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya nimesoma taarifa ya Kamati, taarifa ya Kamati ya sasa na taarifa ya Kamati ya Mwezi wa Pili vinatofautiana. Mwezi wa Pili Kamati ya Nishati na Madini imeeleza sababu Tisa za msingi, hizo sababu Tisa ni uzembe wa Mkandarasi. Eti leo wanatuambia UVIKO wakati Mheshimiwa Naibu Waziri unakumbuka ulikuja Kamati ya Bajeti ukatuambia Mkandarasi anasema UVIKO, ninyi kama Serikali mmegundua tatizo siyo UVIKO ila Mkandarasi alikosea, alitakiwa ajenge matuta mawili, kajenga tuta moja wakati wa mafuriko mchezo mzima ukavurugika ninyi mlisema! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka leo haiwezekani kila siku sisi tunapigwa haiwezekani! Sasa leo tunampa mtu kazi tena tunamlipa vizuri, yaani kama kuna mtu analipwa kiroho safi ni huyu jamaa, yaani hana hata stress! Sasa nataka hivi, huyu mtu anayekula pesa zetu bila stress,s hajamalliza ujenzi kama mkataba unavyotaka, sababu zake alizozitoa ni za uwongo, sababu za Kamati ya Bunge zilikuja hapa zikabaini, Waziri ulikuja ukatuambia kabisa tena hamkutaka kuzikubali tena, tukakuambia subiri mwezi wa Sita si bado? Hasa mwezi wa Sita ndiyo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Taifa lipate majibu kiroho safi, mimi sina bifu na ninyi, wote tunajenga nyumba moja kiroho safi. 6.5 Trillion ambazo tunampa huyu kwa heshima kubwa, nchi inapata nini kutokana na uzembe ili tujue kumbe bado tunashida mikataba, ili tujue Wanasheria wetu bado hatujajifunza kutokana na makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sina mengi sana leo hayo mawili tu, naomba nipate majibu kwa nia njema na nisipojibiwa tutakamata Shilingi tu ili tuweze kujiachia zaidi. (Makofi)