Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kupewa tuzo ya kipekee kabisa kwa uendelezaji wa miundombinu, ambapo ninaamini kabisa kwamba miundombinu hii ni pamoja na ile ya sekta ya nishati, kwa hiyo nampongeza sana. Vilevile ninaipongeza Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo inaifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masuala makubwa mawili katika eneo hili la nishati. Nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kutenga shilingi bilioni 1.48 kwa ajili ya kusambaza gesi asilia majumbani katika viwanda na katika taasisi mbalimbali. Kwa kweli ni jambo moja la muhimu sana, na niseme kwamba usambazaji huu wa gesi asilia hasa kwa ajili ya kupikia utasaidia sana kupunguza matatizo ya uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile itasaidia kupunguza matatizo ya kiafya kama yale ya maradhi ya mapafu na maradhi ya macho wenzetu katika nchi za wenzetu wameshafanya utafiti na kuonyesha kwamba matumizi hasa ya muda mrefu ya kuni na mkaa yana athari kubwa sana kiafya kwa akina mama na watoto na hasa kwa upande wa mapafu na upande wa macho, nasi wenyewe tumekuwa ni mashahidi, wakati mwingine Bibi zetu wanauawa kutokana kuonekana na macho mekundu wanakuwa na imani za kishirikina, wanawaua kwa sababu hizo lakini kumbe tatizo kubwa ni matumizi ya kuni na mkaa kwa muda mrefu, kwa hiyo ninaipongeza Serikali lakini niiombe iongeze fedha kwenye eneo hili kwa sababu kazi inayofanyika kwa kweli inakwenda taratibu sana tunaomba kasi iongezeke ili kusudi kuweza kuwanusuru hawa akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze tena faida nyingine kubwa ambayo inatokana na matumizi ya gesi asili kwa kupikia ni ile ya kusaidia kupunguza matatizo ya lishe kwa katika kaya hasa kwa upande wa Watoto. Wenzetu wa FAO mwaka 2018 waliweka mkakati kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala kama vile gesi na umeme kutasaidia sana kuimarisha lishe majumbani. Hii inatokana na kwamba akina mama wale watapata muda mwingi wa kuwahudumia watoto vilevile wanaweza wakapika vyakula vya aina mbalimbali. Kwa mfano unga wa dona kupika ugali unahitaji nishati ya uhakika lakini hata uji ambao tunashauri watoto watumie uji wa dona unahitaji muda mrefu, kwa hiyo niombe sana wizara iliangalie hili iongeze fedha ili kusudi wenzetu kule vijijini waweze kupata nishati ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili ni kuhusiana na zile uzalishaji wa megawatt 300 kule Mtwara, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba uwezo wa kituo cha kuzalisha umeme kule Mtwara ni megawatt 30 tu, lakini kwa sasa kuna mashine tatu ambazo ziko nje, kwa hiyo wanazalisha umeme megawatt 24, lakini matumizi ya umeme Mtwara la Lindi ni megawatt 22 kwa hiyo utaona kitu kinachobaki ni kidogo sana ni takribani megawatt Mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana hizi megawatt 300 ambazo wizara imesema kwamba itatoa kipaumbele kwenye huu mradi ifanya hivyo kweli. Kwa nini ninasema hivyo, nimeangalia kwenye randama nimeona hakuna bajeti katika miradi mingine ambayo Wizara imewekea kipaumbele kwenye mradi huu wa megawatt 300 wa Mtwara hakuna bajeti hata Shilingi Moja! Kwa hiyo niombe sana wakati wa majumuisho Mheshimiwa Waziri atuambie Wizara ina mpango gani kuhusiana na suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ningependa Bunge lako Tukufu litambue ni kwamba, wakati wastani wa Kitaifa wa usambazaji wa umeme vijijini imezidi asilimia 80 kule Mtwara bado asilimia 51 ya vijiji havijafikiwa na umeme. Hata hivyo, bado tunayo mahitaji makubwa ya umeme ukiangalia sasa hivi tunahimiza sana viwanda vya uchakataji korosho, vipo viwanda 20 ambavyo havifanyi kazi hatujui tatizo ni nini, hata hivyo tunaendelea kuhimiza uanzishwaji wa viwanda vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo eneo la EPZ kule Mtwara maeneo ya bandari lile eneo wakienda wawekezaji pale tutahitaji umeme mwingi sana wa kutumia, kuna miradi mingine ya maji mikubwa kama vile miradi ya Makonde, mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma, miradi hii itahitaji umeme mkubwa, sasa Wizara iniambie hizi megawatt Mbili sasa hivi tukikamilisha hiyo miradi itatosha kweli kuzalisha kutumika katika pampu kubwa za kuzalisha maji? Kwa kweli niseme Mtwara hatujatendewa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kiwanda cha Dangote pekee chenyewe kinahitaji zaidi ya megawatt 30 lakini wenyewe wanazalisha umeme wao, kwa maneno mengine tunataka kusema kwamba kwa umeme huu tulionao, kama tuta-neglect hizi megawatt 300 ina maana hakuna fursa za uwekezaji zaidi katika Mikoa ya Mtwara na Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali ituangalie watu wa Mtwara na Lindi ituanzishie huu mradi wa uzalishaji umeme ili kusudi nasi tuweze kuwa na fursa za uwekezaji, nakushukuru sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.