Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa fursa hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunipa fursa hii pia ya kuongea na nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nahutubia Taifa hapa. Kwa makofi haya naona kwamba Wabunge tuko tayari kusikiliza Hotuba ya Taifa ambayo itatufanya tuitekeleze kikamilifu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo jambo la kulizungumzia ambalo kama sitalisema naona nitakuwa sitaitendea haki nchi hii. Sisi Watanzania, lakini sisi Wabunge ambao tumepewa dhamana hii kubwa ya kutengeneza maono na kutengeneza mwenendo wa nchi hii kwa maana ya uchumi wake, lakini na mahusiano yetu na nchi zingine na ustawi wa nchi hii, kwa kweli tunalo jukumu la kusimamia sana haya tunayoongea na siyo kusema tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia jukumu tulilokuwa nalo, kumekuwa na manung’uniko mengi sana yakijitokeza kwamba hatuna usimamizi mzuri katika bajeti zetu na hiyo inapelekea utekelezaji wa maeneo mengi sana, siyo bajeti hii lakini takribani bajeti zote unasuasua. Sasa ndugu zangu nataka nikwambieni kwamba pesa tunazozitenga hapa, ni nyingi sana, ukichukulia mfano kwenye bajeti hii peke yake kuna takribani bilioni 2.7, hii ni pesa kubwa sana. Ukiangalia kwenye bajeti nzima ni zaidi ya asilimia tano ya bajeti, ni pesa nyingi sana. Kwa hiyo tunayo kila sababu ya kuisimamia pesa hii kuhakikisha kwamba inafanya kazi inayostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya tunayo Wabunge, Wabunge ndiyo tumepewa dhamana ya kusimamia pesa hii, wale ndugu zetu wengine kwa maana ya wananchi wa kawaida, hawana nafasi hata kama watataka kufanya hivyo, lakini wanaona kwamba sisi ndiyo watu thabiti ambao tunatakiwa tuifanye hii kazi kikamilifu. Kwa hiyo nawaomba ndugu zangu Wabunge kwa pamoja kabisa na ndugu zangu Mawaziri ambao ndiyo watekelezaji wa haya majukumu ya Wizara zao, tusimamie kikamilifu kabisa hizi bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano kwenye bajeti iliyotengwa mwaka jana, mwaka jana kwa ujumla tulitengewa takribani trioni 2.3 za bajeti hii ya Nishati. Katika kiasi hicho cha pesa kumekuwa na changamoto katika maeneo fulani ya utekelezaji, kwa mfano, Mradi wa Kinyerezi wa kufua umeme ulitengewa takribani bilioni 88.5, lakini katika kiasi hiki cha pesa kiasi kilichopokelewa ni sifuri. Mnaweza mkaona hapo, sasa hatujui ni kwa nini kiasi hiki hakikupokelewa, wakati kuna umuhimu sana wa kupata huu umeme ambao ungetakiwa kufuliwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa REA pia tulitengea bilioni 363, lakini katika kiasi hicho kilichotengwa mwaka jana ni asilimia 59 pekee ndicho kilichopokelewa, lakini utekelezaji wake sasa katika hizo pesa zilizopokelewa ni mdogo sana. Ukiangalia kwa mfano, Kamati inayohusika na masuala ya Nishati ilivyokwenda kutembelea baadhi ya miradi, ilikwenda ikakuta eneo la Pwani ambako kulikuwa kumetekelezwa mradi mmojawapo wa REA ulitekelezwa kwa asilimia 20 tu. Sasa kama utekelezaji ni asilimia 20 kwenye REA, hivi mnafikiria kwamba tunaweza tukaendelea kwa kiasi gani. Hapa tunaweza tukasema kwamba utekelezaji umekuwa ni finyu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukulie katika Mkoa wangu wa Mtwara, Mkoa huu umekuwa na changamoto kubwa sana ya umeme, ni katika Mikoa ambayo tunaweza tukasema ina shida kubwa ya umeme ukiondoa Mkoa wa Tabora. Utekelezaji wake ni mdogo kabisa, kumekuwa na shida ya kubwa sana ya kukatikatika kwa umeme kwa mfano Masasi ukatikaji wa umeme umekuwa takribani mara nne kwa siku. Jambo hili hatuwezi kulivumilia kama kweli tunataka maendeleo ya kweli katika masuala ya kiuchumi. Bajeti iliyopangwa katika Jimbo la Lindi kulikuwa na takribani vijiji 30 ambavyo vilitakiwa kufikiwa na Mradi huu wa REA, kitu cha kushangaza mpaka hivi ninavyosema hata kijiji kimoja hakijafanyiwa utekelezaji wa Mradi wa REA. Sasa ndugu zangu tunaweza kufika kwa mtindo huu kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuna baadhi yetu tumekuja hapa tumepongeza sana katika hii Wizara. Siyo vibaya kupongeza, lakini je, tukienda katika uhalisia hizi pongezi hii Wizara inastahili kweli, kwa sababu nikiangalia ni katika Wizara ambazo performance yake iko chini kabisa chini ya kiwango. Tukiangalia kama kweli tunahitaji kuendelea na hii Wizara ina-perform chini kiasi hiki katika bajeti zake, nashindwa kuelewa kwa kiasi gani hii bajeti iliyoko sasa hivi itaweza kutekelezwa. Ndipo pale niliposema ndugu zangu Wabunge kwa pamoja, kwa umoja wetu, naomba sana tuisimamie hii Wizara kikamilifu kwa sababu hii Wizara imepewa pesa nyingi sana hatuwezi kuziacha hizi pesa zikapotea kwa mtindo kama huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mradi wa Julius Nyerere kwa mfano, kuna pesa nyingi pale zimewekwa kwa ajili ya utekelezaji, lakini mpaka sasa hivi kitu cha kushangaza ni kwamba mradi huu haujakamilika wakati ulitakiwa at least kwa asilimia 98 uwe umekamilika. Sasa hivi uko kwa takribani kwa asilimia kwa kama 56 hivi, yaani takribani asilimia kama 40 hivi na kitu uko nyuma. Kwa hiyo tunaweza kuona ni kwa jinsi gani najaribu kuzungumza kwamba performance ya Wizara hii siyo nzuri japo kama sisi baadhi yetu tunasifia. Sina nia kuvutana na mtu yoyote, nisije nikaeleweka vibaya. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa Mchungahela.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naam.

MWENYEKITI: Nilikuongeza dakika moja, nikifikiri ndiyo unahitimisha lakini naona bado unataka kuendelea kuhutubia Taifa. (Makofi/Kicheko)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekushukuru sana. Naomba sasa baada ya shukrani hiyo, niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)