Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya Wizara ya Nishati kuhusu bajeti yao kwa mwaka 2022/2023. Kwanza nijiunge na Wabunge wote wanaotoa pongezi kwa Wizara hii. Nimefurahi sana Mheshimiwa Rais kumteua mwanangu Makamba kwa sababu baba January tunajuana sana mimi na yeye, ni marafiki. Wamefanya kazi nzuri sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele hivi walivyoviweka hapa vikitekelezwa nchi hii haitaingia tena gizani, tuwapongeze sana. Unajua ukisema juu juu bila kuzama chini huwezi kufanikiwa, ukitaka kuijua Wizara hii, uende ukaone mitambo yao, ukaone station zao, ukaone wanakozalisha umeme na kazi ngumu. Wizara hii peke yake ndiyo umeme ukikatika unarudi baada ya muda mfupi. Zamani tulikuwa na simu unaripoti simu mbovu, wiki nne, wiki tano haijatengenezwa. Umeme unaripoti na mjue Waheshimiwa Wabunge kila mtu anayewasha umeme haukuja kwa rimoti kama microwave, umeungwa na waya mpaka Kidatu mpaka unaposindikwa umeme huu, ni jambo gumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema katika Jimbo langu tulipoingia madarakani Awamu hii ya Sita na Awamu ya Tano kulikuwa hamna hata kijiji kimoja chenye umeme leo nina Vijiji 41 vina umeme na unawake. Hata juzi wamewasha umeme katika vijiji vyangu vinne Kinyamwe, Ibelamirundi, Ikongolo, Utemini na Ndono na kule ni msituni, sisi Tabora tuna misitu, lakini wanapitisha umeme katikati ya msitu na unakwenda katika vijiji. Hili si jambo la kubeza, ni jambo la kuwapongeza sana, hongereni sana Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mama Samia Suluhu Hassan kurithi mradi ule mkubwa wa umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere, ni fedha nyingi sana linajengwa lile bwawa, amejikita na Mawaziri wake Waziri Makamba na mwenzie Naibu Waziri kumalizia mradi huu, siyo jambo rahisi tumpongeze Mama Samia Suluhu Hassan sana. Ni moja ya miradi waliyosema itatelekezwa mbona inaenda sana! lakini panapokwenda meli Zanzibar na mawimbi yapo tutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa mpango wa kuwa na miradi mingi ya kuzalisha umeme nchini, inalenga kutatua matatizo ya umeme kabisa. Zamani tulikuwa na mradi mmoja na mashine za kukodisha, lakini leo kuna mkakati wa kujenga mitambo yetu wenyewe ya kufua umeme. Mimi nina hofu ndogo sana, nina hofu ambayo sijui naogopa nini? Kituo cha Umeme cha Msamvu (Vital Installation) kimeungua mara mbili, unajua kwa nini naogopa? Kituo hiki kinaunganisha umeme unaotumika kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere na kila kinapoungua mradi kule unasimama, ni moja ya sababu ya kuchelewesha mradi ndiyo maana naogopa hii Vital Installation itaunguaje mara mbili pale pale? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kujiuliza ni hujuma au ni uzembe, ni nini sasa? Mheshimiwa Makamba tafadhali sana, naomba sana muweke kitengo cha uchunguzi, hii Vital Installation kuungua mara mbili kwa muda mfupi isiungue tena mara ya tatu inatuchelewesha. Nashauri sana hebu fungueni macho muangalie kuna nini huko? Zamani TANESCO walikuwa na kitengo kile cha Business Intelligence na kulikuwa na watu kutoka TISS wanafanya kazi huko, Mheshimiwa marehemu Kasanzu na Mheshimiwa Kiza walitoka TISS kwenda kusimamia ulinzi na usalama wa vituo Vital Installation ya TANESCO. Sijui kama imerithiwa au inaendelea sina hakika, naomba sana Mheshimiwa Makamba usimamie ulinzi wa vituo vyako vya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utafutaji wa mafuta, mimi sijui kwa nini Tanzania hatujapata mafuta, sina sababu inayoniweza nikawaza nikajua kwa nini hatuna mafuta Tanzania? Kwa sababu wenzetu walivyopata mafuta ni ushoroba ule ule wa Bonde la Ufa na sisi linaanzia kwetu hapa kwanini sisi hatuna mafuta? Najiuliza ni teknolojia tu tunayotumia kutafuta mafuta au utaalam ni mdogo au uwekezaji mdogo au hakuna utashi ni hujuma ni ukosefu wa uzalendo na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Makamba hili mimi nitakukamata wewe, kwa sababu wewe ni kijana unayejua sana mambo haya, hivi kweli kwa nini hatupati mafuta? Huko Uwembele Tabora huko kuna mahali wanasema hapo panafaa mafuta yapo, uchunguzi ni mdogo sana unaokwenda kufanya kazi kule, wataalam wanaokwenda kule hatuwaoni wakabeba vitu vikubwa vya kutafutia mafuta, hamtaki kupata mafuta hapa? Kipaumbele cha kutafuta mafuta na gesi mmekiweka Namba 11 kwa nini kisiwekwe cha kwanza? Maana yake mafuta tunahangaika hovyo hata hatujui tufanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia gesi kule wenzetu Ruvuma kule wale watu wa Mozambique kwenye Jimbo lao wanaloungana na Ruvuma ndiyo wamepata gesi, trillion na trillions za cubic, sisi bahati mbaya hata hatujaanza kutafuta kule. Tafuteni gesi kule la sivyo gesi inatembea kama mkondo kule chini wakitoboa kule gesi itahamia kule yote, naombeni sana jaribuni kutafuta mafuta Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja ahsanteni sana. (Makofi)