Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nianze kwanza kwa namna ya pekee kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kupeleka fedha takribani Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya kunusuru suala hili la upandaji wa bei ya bidhaa hii ya mafuta. Nimpongeze Waziri na Wizara yake na Watendaji wote wa Wizara na Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nianze kuishauri Serikali kupitia Wizara hii muhimu. Tunachangamoto kubwa hasa kwenye suala la gharama za kuunganishwa na huduma ya umeme kwa mwananchi mmoja mmoja lakini pia na taasisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri leo hii kwa nini Serikali isije na mpango huu kwamba mwananchi anapotaka kuunganishwa na huduma ya umeme, asilipe chochote aunganishiwe gharama halafu aje kutozwa hiyo gharama kwenye bili yake ya kulipia umeme kama huduma zingine. Kwamba unaunganishiwa umeme bure, ukishaunganishiwa umeme unapotaka kuingiza umeme kwa maana ya LUKU, basi unalipa gharama yenu mnakata humo kidogo kidogo, hii niwaambie mkiweza kutekeleza hili litasaidia, kwanza mtaongeza wigo ya wateja wengi wataunganishiwa umeme watu wote wenye mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia upande wa pili mwananchi ataona unafuu kwamba anaunganishiwa umeme bila gharama yoyote. Sasa hivi tunaombwa sijui Shilingi 27,000, sijui Shilingi ngapi inatupa shida tu. Lakini Mheshimiwa Waziri wewe ni Kaka yangu najua wewe ni fresh minded na unafikra nzuri, nikuombe katika hili jambo hili ukilifanya kwa kweli kama Wizara yako inakwenda kupata credit, kubwa zaidi na Serikali inakwenda kuongeza wigo wa mapato kwamba kundi kubwa la wananchi, wataunganishiwa umeme, pia ulipaji utakuwa kwenye gharama zake kwa maana ya bili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili ninashauri kwamba tumeona wengi tunatumia television kuna ving’amuzi mbalimbali, Azam sasa hivi nikiunganisha tu huduma ya Azam moja kwa moja napata huduma na napata huduma ile ya television, leo hii LUKU kwa kutumia hizi LUKU zetu za TANESCO kwanza unanunua umeme halafu unakwenda unaanza kubofya tena kuunganisha umeme, hii teknolojia imepitwa na wakati kwa kweli, jambo hili mimi nadhani halileti afya. Kama kwenye ving’amuzi tunaweza kwa mfano mimi leo hii niko Jimboni, mlinzi ameniambia umeme umekatika na nimefunga nyumba yangu LUKU iko ndani, maana yake nini, ninaweza kuunganisha umeme nikiwa Jimboni Morogoro hapa Dodoma nyumba yangu ikawaka, jambo hili linafanyika na ni jambo la kawaida tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe kushauri Serikali ni vyema ikaja na mpango huu hii ndiyo teknolojia ya kisasa na naamini Wizara ikienda kufanya jambo hili itasaidia na sisi wananchi kupata unafuu wa huduma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niguse eneo lingine la mradi wa REA mimi Jimboni kwangu ninaishukuru Serikali mradi huu unatekelezwa kwenye vijiji 11, lakini changamoto kubwa ambayo tunaipata wananchi wa Mlimba ni Mkandarasi. Kwa mfano, kuna Kijiji cha Lugala na Kaka yangu Mheshimiwa Waziri mpaka leo huyu Mkandarasi hata kuchimba mashimo hajachimba hata nguzo wananchi wa Lugala hawazioni pale Uchindile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa muda bado na mnasema Disemba mradi unakamilika, lakini kama hajaanza kazi hofu yangu anaweza akaomba tena extension. Kwa hiyo, jambo hili mimi niombe kwamba kwa Wizara ni muhimu sasa likachukua hatua kwenye eneo hilo, hali kadhalika Kijiji cha Tanganyika pale Masagati kuna hiyo changamoto. Kama haitoshi nimesikia sikia kama ni kweli au la na kama ni kweli Mheshimiwa Waziri nikuombe unapokwenda kufanya majumuisho, nimesikiasikia mnataka kutuongezea ile Low Voltage (LV) kwenye vijiji vyote ambavyo viko kwenye hii miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna huo mpango Serikalini kwenye Wizara yako kwamba, mnatuongezea kilomita nyingine katika hili nianze kukupongeza kabla hujasema. Kwa kuwa, imekuwa ni changamoto kubwa sana kule kwenye vijiji vyetu, LV umeme mdogo unakuwa na kilomita moja haufiki maeneo muhimu, lakini kama mnakwenda kutuongezea ushauri wangu mwingine ni muhimu sasa umeme huu uguse kwenye maeneo muhimu ya huduma za jamii. Kwa mfano, vituo vya afya, zahanati na shule zetu, hii itatusaidia wananchi hawa kupata huduma, kwa hiyo kama kuna jambo la namna hiyo Mheshimiwa Waziri kwetu sisi wana Mlimba tunasema ukiweza kutuongezea hiyo kilomita moja, unapokwenda kuhitimisha hapa sisi tutashangilia na kwa kweli utakuwa umeupiga mwingi sana Kaka yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ni eneo la suala la utafiti wa mafuta na gesi nchini. Nchi yetu ni tajiri sana isingefaa tuendelee na changamoto za mafuta, isingefaa tuendelee na changamoto za umeme. Mimi nishauri jambo hili inawezekana na niliwahi kusema hapa huko nyuma nchi yetu ina kila kitu, hatuna changamoto ya rasilimali fedha wala rasilimali watu changamoto tulizonazo ni tatu tu kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza ni uzalendo, Mtanzania yeyote mwenye mapenzi mema na nchi yake anaweza kufanya jambo kubwa sana. Pili, ni mindset kwamba it can be done, inawezekana! Watanzania wengi hatuna jambo hili. Jambo la Tatu, ni commitment. Mtu yeyote kwenye Taasisi yoyote akiwa na mambo haya matatu anafanya miujiza. Tumekuwa tukizungumza fedha fedha fedha jambo moja, lakini uzalendo, tukiweka mbele mindset kwa maana ya positive attitude na mwisho commitment inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu na nishauri Wizara hii na ninaamini naendelea kusema my brother naamini uwezo wako naujua, nafahamu pia na uwezo wa Naibu Waziri wako, katika hili nadhani mnayo nafasi bado. Mnayo nafasi Watanzania tunayo imani na ninyi kwa kutumia hayo mambo matatu naamini, mnakwenda kufanya miujiza kwenye Wizara hii na sisi wote Watanzania tukafurahia huduma ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana ahsante sana. (Makofi)