Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ya kisayansi, vilevile na timu yake yote kwa ujumla katika Wizara hii. Mimi nimemsikiliza kwa makini sana, kutokana na hii hotuba yake labda nichangie tu kwenye maeneo mawili. Eneo la kwanza ni eneo la huu umeme wa vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba huu umeme vijijini kwa maana ya REA ni umeme ambao umesaidia sana watu wetu wengi na umekuza uchumi wa nchi hii kwa speed kubwa. Ndiyo maana hata Serikali ikafika mahali ikasema umeme huu uende hata kwenye yale maeneo ya pembezoni mwa Miji ambapo kati ya Miji ni pamoja na Musoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niseme kwamba Mji wangu wa Musoma ulibahatika kuwa miongoni mwa Miji ambayo ilianza kupata umeme huu katika zile mitaa za pembezoni, kwa hiyo nashukuru kwa hilo, katikati hapa ukawa umesimama lakini jana Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwamba umesema kwamba unatoa ndani ya miezi Sita kwa ajili ya kufanya tathmini. Sasa mimi ombi langu ni moja tu kwamba pale kwangu Musoma Mjini kama ni tathmini ilishakamilika na baada ya kuwa imekamilika tulianza kupata umeme wa REA katika ile mitaa ya pembezoni. Mfano, kwa pale Musoma Mjini kuna mtaa kama Morembe, mtaa kama Songambele, mtaa wa Bweri, Nyabisare, Mwisenge Mtakuja, Zanzibar pamoja na kule Makoko - Bukanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule tumepata umeme wa shilingi 27,000 lakini sasa bahati mbaya moja tu ni kwamba, ule umeme wamekuwa wakipewa watu mita 60 yaani pale ambapo nguzo inapita. Katika hiyo mitaa zaidi ya mitaa 15 unakuta mtaa mmoja ni nyumba tano ndiyo zimepata umeme wengine hawana. Kwa hiyo, mimi ombi langu kwako kwa heshima zote hebu basi hapa Musoma Mjini kwa sababu, tayari hili zoezi lilishafanyika na watu wameshapata umeme, kumbe ni kwamba hatuna sababu ya kufanya tathmini tena. Maana leo tukisema kwamba twende kufanya tathmini maana yake ni kwamba, kwa mwaka huu watu wetu hawawezi kupata umeme wa Shilingi 27,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu suala la umeme linasaidia sana watu wetu kupata ajira na kusema kweli katika nchi hii kati ya eneo ambalo nadhani Serikali inahitaji kuweka nguvu sana ni kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata ajira, maana vijana wetu wengi wanamaliza vyuo, wanamaliza shule lakini wakifika mahali hawana kazi ni imani yangu kwamba, ule umeme ukisambaa, umeme wa shilingi 27,000 anayetaka kufanya kazi ya welding atafanya, anayetaka kutengeneza kiosk cha chake soda baridi zinapatikana ataendelea, biashara ya saloon itaendelea, na ukiangalia leo mahali popote ambapo umeme umepita tayari vijana wengi wanapata ajira kwa sababu wanaweza kujiajiri. Kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba pamoja na ahadi uliyoisema ya kufanya tathmini lakini kumbe yako maeneo ambayo huhitaji kufanya tathmini isipokuwa tu unahitaji kuelekeza ni suala tu la nguzo kuongezeka pamoja na nyaya basi na kwa kufanya hivyo watu wengi wataendelea kujipatia umeme na maisha yao yatakuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo mimi nishauri kwamba leo katika bahati tuliyonayo tayari mpaka sasa kwa mujibu wa hotuba yako, tunazalisha karibu megawatt 1,694 lakini matumizi yetu ni chini ya megawatt 1,400. Kwa hiyo, kwa maneno mengine tunazo megawatt zisizopungua 400 lakini inaonekana ndani ya miaka miwili, tutakuwa na megawatt zingine siyo chini ya 2,000 ambazo hazitakuwa na matumizi. Sasa mimi niseme tu kwamba Watanzania wengi wangependa kuweka umeme lakini ni kwamba ule uwezo wa Shilingi 300,000 kwenda juu, maana leo tunazungumza Shilingi 320,000 lakini unapokuja kwenye hali halisi kwamba hata yule mtu wa mjini mwingine ni zaidi ya nguzo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kumbe mahitaji yake ni zaidi ya shilingi 300,000, tunakwenda shilingi 500,000 mpaka shilingi 1,000,000. Sasa mimi ombi langu ambalo linawezekana kabisa hasa kutokana na projection ya umeme ambao tunatarajia kuupata, hivi kwa nini tusiendelee na zoezi la shilingi 27,000 lakini kwa utaratibu wa kuwakopesha. Yaani leo mimi ni vigumu nikapata shilingi 500,000 ya kuweka umeme au shilingi 1,000,000 ya kuweka umeme lakini ni rahisi sana ukaniwekea umeme kwa gharama nafuu, lakini kwenye charge ile ya kila mwezi labda badala ya kulipa shilingi 20,000 kwa mwezi basi nikawa nalipa shilingi 30,000 au shilingi 50,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba tukifanya hivyo watu wengi zaidi wataweza kuweka umeme na wakiweka umeme kwa sababu, tunatarajia kuwa na umeme mwingi basi kumbe ni kwamba na mauzo yetu nayo yatakuwepo. Hata kama ungetafuta Financial Institution kama benki wakatoa mkopo tukawawekea watu wengi umeme, maana yake ni kwamba Shirika lingeweza likapata fedha zaidi. Kwa hiyo, mimi nikuombe kwamba Mheshimiwa Waziri ikikupendeza basi ni vizuri Mji kama wa Musoma ungekuwa pilot study ya kuona kwamba namna gani tunaweza tukawa-finance watu wetu wakapata umeme kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu pale Musoma Mjini tulikuwa na tatizo la maji kwa sababu watu wetu hawakuwa na uwezo wa kuweza kulipa maji kwa pamoja. Tulipoweka utaratibu wa kuwakopesha mabomba na vifaa vya maji, leo karibu Mji wa Musoma kote sasa tunadhani ndani ya kuja kufikia bajeti hii watu wote wa Musoma watakuwa wamepata maji zaidi ya asilimia 95. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba kumbe tukienda hivyo kwenye umeme na katika maeneo mengine basi watu wetu watapata huduma bora ambayo itawasaidia sana, katika kuondoa hasa tatizo la ajira ambalo ndilo tatizo kubwa linalowasumbua watu wetu wa Musoma lakini na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilidhani tu kwamba niweze kutoa huo mchango kule kwingine kwenye mafuta kwa leo kwa sababu na mimi naye nina-interest huko, nadhani sitachangia sana kwa sababu ya muda, zaidi ya hapo naendelea kusema nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)