Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwisho.
Kwanza kabisa na mimi nichukue fursa hii ya kuwapongeza Waziri na wenzake kwa hotuba nzuri sana. Kiukweli katika hotuba za safari hii zilizokuja vizuri kama ikitekelezwa inaweza kutusogeza sana. Hotuba hii inajibu maswali mengi, changamoto nyingi za kisera na mimi naamini watu waliopo kwenye Wizara hii wanatosha kutekeleza mambo waliyoandika wenyewe, kwa sababu hizo, mimi naomba nieleze zaidi mambo ya Chemba. Naomba nieleze changamoto tulizonazo hasa za umeme kwenye Jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza, wenzangu wameongea juu ya Wakandarasi, sisi kwenye awamu hii REA round ya tatu awamu ya pili ina-cover vijiji 50, sasa hivi Mkandarasi yuko site mwaka mzima lakini kwenye vijiji hivi 50 amewasha kijiji kimoja tu ndani ya mwaka mmoja, tafsiri yake kumaliza atatumia miaka 50 vijiji vingine vilivyopo. Wenzangu wameiongelea changamoto hii sasa mimi sipati majawabu kwa nini changamoto hii ipo hivyo. Nafahamu kabla ya kuomba kazi walifanya survey walitafuta majawabu namna gani watapita kuweka kazi hii, lakini hiyo changamoto imeonekana kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri katika hili, zipo Wilaya au Majimbo jiografia yake ni ngumu sana kumpa mwaka mmoja, mwaka mmoja na nusu au miaka miwili kumaliza vijiji vyote 50, mimi hapa maeneo yangu kutoka kijiji kimoja hadi kijiji kingine ni kilomita 50 mpaka 70, unaweza ukaona kabisa jinsi gani kazi hii ilivyokuwa ngumu. Mimi ninawashauri kama wanataka kazi hii itekelezwe kwa wakati, zipo Wilaya ambazo ni lazima waweke Wakandarasi wawili otherwise tutaendelea kugombana leo kwenye mkutano, unaeleza ndugu zangu Serikali hii tiifu imeleta fedha kwa ajili ya vijiji vyote na ndani ya miaka miwili vijiji vyote vitakuwa na umeme lakini inachukua miaka minne. Mimi nimuombe Waziri muangalie uwezekano kwenye Wilaya ambayo jiografia zimekaa vibaya, tuangalie kama tunaweza kuongeza Wakandarasi ili kazi hii ifanyike kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zipo changamoto nafikiri changamoto zingine ni za kiutawala huko huko. Kwa mfano, mimi ninavyo vijiji ambavyo miundombinu yote imemalizika tangu miezi sita iliyopita lakini hawajawasha umeme. Kila ukienda ukiuliza vipi unaambiwa tunakuja kesho kuwasha, sasa changamoto hii nafikiri ni ya kiutawala zaidi, mimi niwaombe watu wanaohusika hebu tusaidieni yale maeneo ambayo tayari miundombinu ya umeme iko tayari wawashe. Wamesema wenzangu umeme huu una fursa nyingi kwamba tukiwasha umeme, zipo faida za kiuchumi zinapatikana kule sasa kwa nini tunawachelewesha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilipata simu ya mteja mmoja ana kiwanda kidogo cha kukamua alizeti, yeye anakimbizana na alizeti inayotoka shambani sasa hivi, amekamilisha lakini amefika pale wanamuambia kesho, kesho kutwa, kesho kutwa sasa hii ni changamoto kubwa sana. Mimi niwaombeni sana umeme huu unafaida kwetu sisi kule Chemba kwa sababu vijana wengi sasa watapata ajira huko. Niombe sasa hawa watu wanaohusika hebu mjitahidi, pale ambapo maeneo yale miundombinu imekamilika waende kuwasha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vipo vijiji kama Magandi, Machiga tangu mwaka jana miundombinu iko tayari, mpaka imefika mahali wanagombana na Meneja wa TANESCO kwa sababu wanamuambia kesho, kesho kutwa mtu anafika mahali anachoka. Mimi niwaombeni sana kwamba tunawajibu wa msingi sasa wa kuhakikisha hili zoezi la kuwasha umeme, miundombinu ikikamilika mfanye kwa haraka ili watu hawa wanufaike na huo umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni muhimu sana na wenzangu wameliongelea, Wilaya yangu tunaposema Chemba ni Wilaya mpya hakuna mjini kote ni vijijini, sasa tunashindwa kutafsiri ni nani anapaswa kulipa shilingi 300,000 ni nani anapaswa kulipa shilingi 27,000? Ninaiomba Wizara hebu waje na mfumo sahihi ambao sasa utatofautisha kwa sababu nyie wenyewe mnapita Chemba ni barabarani hapo, Chemba ni kijijini bado na nina uhakika watu wenye uwezo wa kulipa hiyo shilingi 300,000 ni wachache sana, hebu tuangalie namna bora ambayo tunaweza kuwasaidia hao watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, kuna jambo ambalo halijafanyika, tunafahamu umeme utasaidia sana kupunguza shida za maji huko vijijini. Sasa hizi projects za umeme hazikuweka bajeti ya kuweka umeme maeneo yenye taasisi, kama shule za msingi ukiona shule ya msingi ina umeme labda imejengwa kijijini pale pale, lakini ni ukweli usiopingika visima vingi vya maji viko pembezoni kidogo ya kijiji, sasa nafikiri tuangalie upya namna gani ambavyo tunaweza tukasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo yangu mimi, yapo maeneo ambayo maji yanauzwa shilingi 400, shilingi 300 kwa dumu, kwa sababu tu wanatumia dizeli ku-pump zile mashine ili maji yapatikane. Mimi niwaombe sana ndugu zangu nami nakuamini sana Waziri, namuamini sana Naibu Waziri na Viongozi wote mlioko huko jambo hili liko ndani ya uwezo. Nawaombeni mtusaidie, naombeni muangalie namna bora umeme ambao unaweza ukafika kwenye visima hivyo vya maji shule za msingi na zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema siku moja hapa kwamba nina Kituo cha Afya cha Makorongo, ninakumbuka siku Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alivyokuja kukifungua aliwaambia leteni umeme nikasema mpaka leo umeme haujafika. Sasa unaanza kujiuliza alikuja Waziri, alikuja Mkuu wa Mkoa akasema maneno hayo, alikuja Waziri Kalemani akasema maneno kesho kutwa umeme uwe umefika hapa, sasa wewe ndugu yangu haujafika pale, najua wewe ukifika mambo yatakuwa sawa, ndugu zangu nawaombeni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)