Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii kwenye Wizara hii muhimu sana na hotuba ya Waziri wa Nishati. Mwanzo kabisa kwanza niĀ¬-appreciate mchango wa Mheshimiwa Festo Sanga ambao aliutoa jana, wakati anachangia alikuwa anaeleza vizuri sana kuhusiana na uwezo wa wawekezaji wa ndani kwenye kuzalisha umeme. Alitoa mfano wa Kiwanda cha Kagera Sugar ambao wanatumia malighafi zinazobakia za sukari, yale mabaki ili kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya ziara hapo karibuni na kwenye ziara ile walituonesha mitambo anayosimika sasa hivi yenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 za umeme wakati mahitaji ya Mkoa wa Kagera tuseme kama megawati 10 hivi ukitoa yeye mahitaji yake, lakini mpaka kufikia miaka mitatu, minne ijayo, atakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 60. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri azingatie ule mchango wake na aone namna ya kuondoa hii sheria kandamizi inayowazuia watu wenye uwezo wa kuzalisha umeme kwenye baadhi ya maeneo kuingiza kwenye gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, pamoja na pongezi zangu kwao Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyofanya kazi zake na weledi wake kwa kulisaidia Taifa hili na naamini Mheshimiwa Rais, Mama, anamwamini sana kwenye kazi hii. Nafahamu Waziri sasa hivi ndio kiongozi wa majadiliano yanayoendelea kuhusu kukamilika kwa Mradi wa Gesi ya Lindi kwa maana ya LNG wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 30. Nimwombe sana, mradi huu ni mkubwa na wenye manufaa makubwa sana kwa watu wa Mikoa ya Kusini kwa maana ya Mtwara na Lindi, lakini kwa Taifa lote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutegemei mradi huu ni wa muda mfupi, uwekezaji unaofanyika ni wa muda mrefu, utasaidia vizazi na vizazi. Sasa nimwombe Waziri, katika kukamilisha majadiliano ya mkataba huu ahakikishe wanaweka kule ndani clause inayowataka wawekezaji wawe na ulazima wa kutumia Bandari ya Mtwara kwa maana ya kuleta vifaa vitakavyosaidia kwenye uboreshaji wa mradi, lakini pia kutumia Uwanja wa Ndege wa Mtwara pia ambao sasa hivi ni mkubwa sana, umeboreshwa kwa maana ya run way, ina urefu zaidi kidogo ukilinganisha na Uwanja wa Ndege wa Dar-es-Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sasa hivi pale kuna uwezo wa kutua Antonov yenye uwezo wa kubeba tani nyingi tu ya vifaa. Kwa hiyo, hebu tuwalazimishe hawa watu watumie Uwanja wa Ndege wa Mtwara, watumie pia na Bandari ya Mtwara ili iweze kuchakachua, kuchenjua uchumi wa maeneo haya kwa ajili ya wananchi wa Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nishukuru sana kwa namna wanavyofanya kazi zao na nilimfuata nikamweleza na tulikwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri mara nyingi tu, Miradi ya REA inatekelezwa kwenye maeneo yetu, lakini kwa bahati mbaya sana scope inakuwa ni ndogo, kwa hiyo, niliomba hapo nyuma katika miaka miwili, mitatu iliyopita, nilikuwa naongea sana kuhusu kata mbili kwa maana ya Kata ya Mpanyani pamoja na Kata ya Msikisi; wakandarasi, mkandarasi wetu Namis Corporate yuko pale na anashirikiana vizuri sana na Meneja wa Wilaya na yeye tumpongeze kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini sasa niombe kwa makusudi kabisa kuongeza scope. Watakapokuwa wanatoka kwenye hizi kata wahakikishe vitongoji vyote vya kata hizi vimepata umeme ndipo twende maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu kuna tatizo, sasa hivi ukienda Kata ya Ndanda tunaambiwa kuna umeme, lakini umeme huo haujafika zahanati ya Ndanda na sisi tunasema kwamba, umeme lazima ufike kwenye vituo vya kutolea huduma za kijamii. Umeme pia, haujafika zahanati ya Nasindi, zahanati ya Chihoro, zahanti ya Ngalole, Kituo cha Afya cha Mpanyani, Kituo cha Afya cha Lukuledi, Kituo cha Afya cha Namatutwe, Kanisa Katoliki la Nanganga, pamoja na Kanisa la Chikunja, maeneo haya yote hayajapatiwa umeme, lakini ukisikiliza wanakwambia kata hizi zina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ndefu kidogo. Kuna kitongoji kimoja kinaitwa Ndolo, kiko kwenye Kata ya Ndanda. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, atuongezee nguvu kwenye eneo hili, watu hapa wanapata shida sana kwa sababu, miaka mitano, sita iliyopita walikuwa na umeme; walikuwa wanapata umeme kutoka kwa wamisionari wa Ndanda kama msaada, lakini baada ya kuzidiwa mitambo inayozalisha umeme kwenye hiki kitongoji, kwa hiyo, watu wa Ndanda wameamua kuchukua umeme wao, sasa wale watu wamefanya wiring kwenye nyumba zao. Ni kipande kama cha mita 200 tu. Ni suala sasa la kufanya uamuzi ili kuweza kupeleka umeme kwenye kitongoji hicho kwa sababu, watu wale sasa wako gizani wakati miaka mitano iliyopita walikuwa na umeme wa kutosha. Kwa hiyo, niombe sana Waziri tusisitize tufanye kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tulifanya ziara kama nilivyosema kwenye Mkoa wa Kagera, tuliweza kufika kwenye Kiwanda cha Minza wanaozalisha kahawa, lakini kule kwetu Mtwara pia, kuna viwanda vinavyozalisha korosho, kuna viwanda vinavyozalisha pamba. Kuna sheria moja kandamizi inayolazimisha viwanda hivi wakati hawafanyi uzalishaji wachajiwe kitu kinaitwa capacity charge. Capacity charge inachajiwa asilimia 75 ya matumizi ya mwezi uliopita, kwa maana ya previous. Kwa mfano, kama huu ni mwezi Juni nimesimamisha kiwanda kuzalisha, nalazimika kulipa asilimia 75 ya invoice yangu ya umeme ya mwezi uliopita, nisipoendelea kuzalisha bado nitakuwa naendelea kulipa hivyohivyo kwa kuonesha kama ni capacity charge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ni kandamizi. Sheria ya capacity charge ilitungwa wakati huo ili kuweza kupunguza matumizi ya umeme kwenye viwanda. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya review ahakikishe sheria hii anaileta tubadilishe ili tuweze kuwasaidia wawekezaji, tuweze kuwavutia wawekezaji. Hata sisi kwenye Kamati yetu ya Viwanda na Biashara na ukiangalia iko mpaka kwenye blue print, haijafikiwa kwenye utekelezaji wake, lakini tunaomba sana capacity charge iondolewe ili wawekezaji wawe na uhuru, asipotumia umeme asiulipie, haina maana ya kumchaji invoice ya umeme na hivi ndio vitu ambavyo tunasema vinaongeza inflation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kwenye masuala ya gesi haya ambayo niliyasema pale mwanzoni. Tunaomba sana sisi watu wa kusini mijadala hii inayohusiana na masuala ya gesi kwa sababu, sasa hivi wanasema wanaelekea kwenye hatua ya kuwekeana saini, basi baada ya kuwekeana saini mara moja mijadala yote inayohusu masuala ya gesi, matumizi yake na mengine tuyaone yanaletwa kwenye Mikoa ya Mtwara, Lindi na mikoa mingine ya kusini ili iweze kuwachangamsha watu na kuwafanya waone kuna kitu pale kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia kuchangamsha biashara, lakini pia, itawafanya watu wawe aware kwa sababu, wao ndio walinzi wa miundombinu hii. Tusipofanya hivyo kwa sababu kwa miaka karibu takribani kumi, kumi na tano nyuma, shughuli za gesi Mkoa wa Mtwara zilisimama ndio zilizosababisha uchumi wa mkoa wetu sisi kuyumba. Bandari haifanyi kazi vizuri wakati ile bandari ilikuwa inakusudiwa kupeleka vifaa vya gesi pia baada ya Serikali kuongeza kwenye ile berth moja walikuwa wanakusudia pale kutulia vifaa kwa ajili ya kupeleka Mozambique kwenye miradi ya gesi. Sasa miradi ya gesi ya Mozambique haiendi vizuri kutokana na hali ya kiusalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa bahati hii imerudi kwetu, kutoka Bandari ya Mtwara mpaka Lindi ni karibu kilometa 125. Kwa hiyo, tuombe kabisa mizigo itakayokuwa inatakiwa ifike kwa ajili ya uboreshaji wa huu Mradi wa LNG ishuke moja kwa moja Bandari ya Mtwara iweze kupelekwa pale. Ndugu zetu wa Mtwara watachangamka, uchumi wa mkoa wetu utachangamka na utaanza kuona manufaa ya gesi mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri asisahau kabisa kuangalia hilo jambo na nimshukuru sana kwa kazi kubwa anazozifanya, sasa hivi Kijiji cha Mumburu kilichopo Jimbo la Ndanda wakandarasi wa REA wako pale. Kijiji cha Nanganga, tunaomba sasa akaongeze nguvu kwa maana ya kupeleka umeme katika Kijiji cha Nanganga A, Kijiji cha Mkwera, Kijiji cha Mumburu kama nilivyosema A na B, isipokuwa baadhi ya vitongoji vinakosa. Tuangalie pia, uwezekano wa kupeleka umeme Kijiji cha Tungani, kuna baadhi ya maeneo yanakosa, lakini pia Kijiji cha Mwongozo pamoja na Mkangu kwenye maeneo yote ya Jimbo la Ndanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri., kama ambavyo nilisema awali kwamba, kazi hizi zinakwenda na tulikutana wakati ule na Mheshimiwa hapa Mkurugenzi wetu wa REA. Yale tuliyoyaongea basi Waziri ataendelea kuyafanyia kazi, lakini kimsingi kazi za umeme Jimbo la Ndanda zinakwenda na naamini hivi karibuni tu watakwenda kuwasha. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na naunga mkono bajeti yake, nimtakie kila la heri katika kutekeleza yale yote aliyoyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)