Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye bajeti ya Wizara yetu ya Nishati. Kwa kuanza kabisa bila ya unafiki napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa maana ameonekana kuwa mwepesi sana kujibu hoja na kufanya maamuzi mazito na magumu kuhusu masuala ya nishati. Tumemuona Mheshimiwa Rais tangu Oktoba - Novemba aliruhusu baadhi ya tozo ziweze kutolewa kwenye mafuta ili kuleta unafuu katika bei ya mafuta ambayo imekuwa ikipanda kila mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona namna gani baada ya Bunge kuomba unafuu wa bei kwa ajili ya kuweka maisha mazuri kwa wananchi wetu ameweza kutoa kwa kujibana matumizi yake Serikalini Bilioni 100 kama ruzuku na tumeona matokeo yake mwezi huu bei zimeshuka lakini pia tumeona akitoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha na ninaamini Waziri wa Fedha yuko hapa na punde si punde atakuja kutuletea Bajeti Kuu pamoja na marekebisho ya Sheria za Forodha kwa kuleta upungufu kwenye baadhi ya tozo ambazo zitaweza kutolewa kwa ajili ya nishati hii ya mafuta. Kwa hiyo, ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa mwepesi kutoa maamuzi ambayo yanaleta unafuu kwenye bei za mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona namna gani anaguswa na sekta hii na anataka mapinduzi makubwa katika sekta hii ndiyo maana Mheshimiwa Rais ametulia sana kwenye teuzi zake za wataalam na Mawaziri kwenye Wizara hii. Mimi nilipata ukakasi mkubwa sana kwa baadhi ya watu walipobeza uteuzi wa Mheshimiwa Rais kumteua January Yusuf Makamba kuongoza Wizara hii. January namfahamu vizuri tangu naanza ufahamu wa akili ni Kiongozi Kijana ambaye ni kielelezo kwa vijana wengi ambao tuko nyuma katika siasa. Kama hamumjui January Yusuf Makamba ndiye kijana aliyehusika kuandika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020 ambayo Ilani hiyo ndiyo imetuletea ushindi mkubwa wa kihistoria kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Mheshimiwa Spika, nitasema alama yake kubwa mbili tu alizoziacha kwenye baadhi ya Wizara alizoziongoza, alipata nafasi ya kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, waswahili wanasema mzigo mzito apewe Mnyamwezi lakini mzigo mzito alipewa Msambaa na akauvusha, alipewa kwenda kufuta mifuko ya plastic ili kunusuru mazingira yetu January aliweza na alama ameiweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili alipewa mzigo mzito wa kufuta viroba kwenye nchi yetu, viroba havipo na tunaona afya za vijana wetu zikiimarika baada ya viroba hivi kuondoka. Kwa hiyo sina mashaka na weledi…
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Taarifa.
MWENYEKITI: taarifa.
T A A R I F A
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumpa taarifa mchangiaji anayeendelea kutoa mchango wake ni mzuri sana hasa Bilioni 100 zilizotolewa kwa ajili ya kupunguza makali kwa wananchi wale wadogo lakini cha kushangaa bado nauli hazijashuka bei kwa hiyo tuendelee kuishauri Serikali ili kusudi wananchi waweze kufikia ile hatima ya Mheshimiwa Rais aliyokusudia. Ahsante sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam Ditopile, unapokea taarifa?
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea taarifa nia yake ni njema. Kwa hiyo, nilikuwa namalizia kusema kwamba Mheshimiwa January Yusuf Makamba nimefuatilia mjadala tangu jana ulipowasilisha bajeti yako, kila Mbunge anayeinuka anakusifia na tayari wamekuelewa na wameahidi kwamba wanaenda kupitisha bajeti hii kama kipimo, basi mimi nakwambia Mheshimiwa Waziri tunakukopesha imani sisi kama Wabunge wenzako, kailinde hii imani na ukawatendee haki wananchi wa Tanzania katika sekta ya nishati na sina mashaka kwa sababu unae msaidizi mzuri, kijana mwenzako, Wakili Msomi na umemkuta hapa kwenye Wizara hiyo, kwa hiyo naona kwa umoja wenu mtashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye teuzi hizi za Mheshimiwa Rais amemleta Katibu Mkuu ambaye anaijua hii Wizara, nani asiyemjua Mramba katika sekta ya nishati? Pia amemsindikiza Mramba na Msaidizi wake kaleta kijana mdogo Maimbali yuko vizuri amekulia kwenye mfumo kwa hiyo ninaimani kwamba katika Wizara kwa kweli huko chini mjipange mna uongozi wa juu ambao wana dhamira njema na wanaielewa hii sekta vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hakuishia hapo tumeona teuzi zake za wenyeviti wa Bodi kuanzia TANESCO, REA analeta watu ambao wanaelewa nini wanaenda kukifanya. Hakuishia hapo pamoja na Wakurugenzi, leo hii Ndugu Maharage tumeona namna gani ameiwakilisha nchi kwenda kufanya makubwa nje ya Tanzania kwenye mashirika makubwa ambayo yapo significant ndani ya dunia hii, kwa hiyo amekuja nyumbani kuja kuvusha Shirika letu la TANESCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitachangia kwenye maeneo machache sana, Mheshimiwa Waziri umetuletea bajeti yako ambayo mimi naichukulia kama ni action road map katika kufikia maono ya Wizara. Kiukweli umetupa mpaka vipaumbele vyako lakini umekuja na ideas mpya kusema kwamba namna gani utaihusisha private sector ili kujipunguzia mzigo lakini namna gani utapata fedha nje ya fedha kutoka Serikali Kuu ili uweze kuendesha mashirika na kuweza kuleta maendeleo katika Wizara yako. Kwa hiyo, mimi nakutakia kila la kheri na tumeona kabisa namna gani unaenda kutekeleza mambo yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TANESCO ninakupongeza sana Mheshimiwa Mkurugenzi Mkuu tangu uingie umeanza kuonyesha kile ulichokuwa unakifanya namna gani unataka kuki-impact ndani ya TANESCO kwa mambo mawili tu ya mabadiliko ya haraka, ni-connect umeianza kwa muda mfupi lakini tayari wananchi wameishaipokea very positively. Kuna hizi mita janja kwa sababu ilikuwa ni kitu cha ajabu unachukua simu unaigiza mita unanunua umeme tena uende ukatafute pa kuweka zile mita lakini yote ina-portray ni namna gani una maono makubwa ya kuja kubadilisha Shirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Shirika ni kubwa lina na sehemu tatu kuu ambazo ni kubwa sana lakini nina uhakika kwa timu uliyonayo mtaweza kutekeleza yale ambayo mmeyakusudia na mwisho wa siku kweli mkasadifu ile kauli ya kuliangaza Taifa. Tumeona shida kubwa ambayo inatutatiza ndani ya TANESCO ni kukatika kwa umeme. Mimi naomba nitoe ushauri wangu msichukulie kukatika kwa umeme kwamba ni kadhia tu kwa wananchi na watumiaji wa umeme. Pamoja na huduma mnazotoa TANESCO mnafanyabiashara ya umeme. Mtu anatumia umeme regardless ni wa TANESCO ama ni wa generator sasa kile kipindi ambacho umeme umekatika yule mtu anaenda kutafuta source nyingine ya kutumia umeme, ina maana nyie mnapoteza mapato. Hata hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha upo CAG anapoenda kufanya ukaguzi kwenye mahesabu ya Shirika hili, aende akaangalie ule muda ambao TANESCO umeme umekatika mapato wanayopoteza. Kwa hiyo, nimeona dhamira nzuri ambayo mmeionyesha kutaka kwa mara ya kwanza mnataka kwenda kubadilisha kwenda kufanya marekebisho kwenye mfumo wa grid na tayari tumeona inahitajika zaidi ya Trilioni Nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Rais ndiyo maana nimesema anaenda kufanya maamuzi magumu ya kimapinduzi tayari kwenye bajeti hii mmetenga 500 billion, that’s not small money! Niliwahi kuongea hapa lazima TANESCO muende na teknolojia kwa sababu mnapoenda kubadilisha sijui transformer kupitia hizi 500 billion, mtapoenda kubadilisha nguzo na nyaya itabidi mkate umeme ili mfanye hayo marekebisho lakini duniani ipo teknolojia ya kufanya haya na umeme uendelee kuwepo, ipo live line technology tunaomba muitumie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Dar es Salaam mnabadilisha nguzo kutoka za miti kwenda za zege inabidi mzime umeme mnapoteza mapato, wakati mnaweza mkaichukua live line mukaiweka kwenye hilo zoezi lenu mkaendelea kupata hela za umeme na mkabadilisha mifumo yenu. Kwa hiyo, naomba kwa kweli Wizara ichukulie kwa umakini sana suala la kutumia live line.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaenda kuweka transformers kupitia kwenye miradi ya REA, TANESCO kama hivi, maana yake hapa mna bajeti kuweka transformer zaidi ya 6,000, tunajua kuna baadhi ya maeneo kama kwa Babu zangu huko Usukumani, Rukwa kuna radi nyingi sana, kuna sehemu unaweza ukapoteza kwa mwaka transformer tatu, yaani transformer hiyo moja inaharibika mara tatu kuna vifa vinaitwa combi units, vile vifaa vinaenda kuzuia ile transformer isiungue kutokana na radi hii itasaidia pia kuokoa kwa sababu tayari Shirika letu lina madeni mengi. Kwa hiyo, kupunguza gharama ambazo zinaweza zikaepukika naomba pia mkaangalie hiyo teknolojia ya combi unit.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu REA ninawapongeza sana Wizara kwa sababu wote tulikuwa tushaweka kwenye mindset kwamba Rural Energy Electrification Agency kwamba ni wakala wa kupeleka umeme vijijini. Lakini mmebadilisha kwa sababu siku umeme ukishafika nchi nzima REA ife, mmeenda kusema kwamba sasa hivi ni wakala wa kupeleka nishati vijijini, that’s the way to go! Hayo ndiyo mambo ambayo tunataka kuyaona, mkimaliza kuweka umeme nchi nzima mnaenda sasa kupeleka nishati mbadala na nishati zingine kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimependa kuunga mkono mpango wenu wa vitongoji, kwa sababu kuna Mheshimiwa Mbunge aliwahi kusema hapa, kadri unavyozidi kutanua unazidi kutamani. Sasa umeme umefika vijijini haujafika vitongojini, kwa hiyo mpango huu wa kupeleka umeme vitongojini ni mzuri sana lakini kabla ya kuendelea nao kuna baadhi ya Waheshimiwa walishauri tuangalie yale maeneo ambayo umeme umefika lakini baadhi ya nyumba hazijapata umeme ili tunapoenda kwenye hili la vitongoji hili la vijiji liwe limekaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri sasa nakuja kwenye jambo kubwa ambalo nina imani kwa utulivu wako, kwa akili zako, kwa uweledi wako, ukitulia kwenye mradi wa LNG unaenda kuacha historia ya kudumu katika Taifa hili, kwa kweli vizazi na vizazi vitakukumbuka, mfupa huu umeshindikana zaidi ya miaka 10 leo hii umetutolea kauli baada ya Tarehe 09 Juni tunaenda kusaini HGA kwa hiyo nikupongeze kwa hilo. Naomba uangalie sana vitu viwili, tunaye jirani yetu Msumbiji ameanza hili tumeona anavyosumbuka kwenye suala la usalama nasema kwa sauti ndogo kwa sababu tunajua, naomba tujipange vizuri neema lazima inaambatana na hofu ya usalama.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mariam Ditopile kwa mchango wako mzuri.
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.