Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii naomba nichangie na mimi kwenye hotuba hii ya Waziri wa Nishati ambayo ameileta kwetu ili tuweze kufanya uchambuzi, lakini kabla sijaendelea naomba nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba nimpongeze mdogo wangu Mheshimiwa January kwa kazi nzuri anayofanya kwenye Wizara hii na mimi lazima niwaambie na nimwambie kwamba Mheshimiwa January ninamfahamu na kwa kweli Mheshimiwa January yupo makini katika uongozi wake lakini ninaimani kabisa kwamba Wizara hii ipo kwenye mikono salama pamoja na Naibu wake Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiit, sisi Wabunge wa Kigoma naamini tulikuwa tuwe wakali sana kama Mheshimiwa January hakuja na mpango wa kuhakikisha kwamba tunapata umeme wa Gridi ya Taifa katika Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa Gridi ya Taifa imekuwa ni kizungumkuti kwa maana ya kwamba Wabunge wengi waliopita walikuwa wakizungumza na kulalamika sana kuhusu Gridi ya Taifa kutokuingia katika Mkoa wa Kigoma na imepelekea Kigoma kuendelea kubakia nyuma sana kimaendeleo kwa sababu tuliendelea kukosa umeme wa uhakika, haiwezekani kukawekezwa viwanda katika Mkoa wa Kigoma ambao unaendelea kutumia mashine zinazotumia dizeli, isingewezekana kupata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa January kwa kuja na mkakati wa kuhakikisha kwamba kabla ya mwaka huu haujaisha tumepata umeme wa Gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kigoma mimi ninakuhakikishia sisi Wabunge wa Kigoma sasa tunakwenda kukuunga mkono katika kupitisha bajeti yako hii ili kusudi tupate huo umeme wa Gridi ya Taifa ili na sisi tuweze kupata viwanda sasa kwa sababu tunaenda kuhakikisha kwamba tunakwenda kuwekeza kwenye kilimo cha michikichi, sasa je, michikichi itakapolimwa, je, bila umeme kiwanda kitakwenda kupatikana namna gani, kwa hiyo hili jambo ni jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba nizungumzie kwenye eneo la umeme wa maji wa Mto Malagarasi. Mheshimiwa Waziri eneo hili huu mradi umekuwa ukitajwa katika miaka mbalimbali iliyopita, lakini nafurahi kuona kwamba Mheshimiwa January anakwenda kuandika historia katika mradi huu kwenda kuanzishwa mwaka huu wa fedha, naomba nikupongeze sana Mheshimiwa January na jambo hili ukilifanya kwa kweli utakuwa umeandika historia kwa wananchi wa Kigoma kwa sababu huu mradi utakwenda kutusaidia sisi Kigoma lakini pia na Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye eneo hili naomba uhakikishe wananchi wanafidiwa maana yake huu mradi unakwenda kuutekeleza kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini, wananchi walisimamishwa katika maeneo yao wasiendeleze kilimo, sasa naomba uhakikishe kwamba unapokwenda kutekeleza mradi huu wananchi hawa wawe wamefidiwa. Ninayo taarifa kwamba Gridi ya Taifa inapopita kote tayari wananchi wamekwisha tambuliwa wa maeneo yale wanaokwenda kupoteza baadhi ya mazao na maeneo kwamba tayari, lakini sina taarifa ya kwamba tayari wamelipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo hilo waweze kulipwa fidia wananchi, wasibaki wanalalamika, mradi wanautaka lakini tafadhali sana Mheshimiwa Waziri fidia itolewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la umeme wa REA mimi nina vijiji 61 lakini nashukuru kuona kwamba kusema kwamba tunavyo vijiji 29 tayari vimeshapata umeme, lakini bado vijiji 32 havijapata umeme, lakini ninavyo vitongoji 350. Sasa unaposema umeme unakwenda kupatikana mwishoni mwa mwaka huu, mimi siamini kwamba vitongoji hivi vitakuwa vimekwenda kupata umeme kwa sababu kuna Mbunge mwenzangu alizungumza juzi kwamba yeye alipata t-shirt ambayo inaonesha kwamba sasa tunakwenda kwenye vitongoji wakati kumbe hata vijiji vyenyewe bado hatujakamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina vijiji 32 ni vingi sana, lakini ukienda kwenye vitongoji 350 yaani vitongoji vyenyewe vina ukubwa sawa na vijiji, sasa kama umeme umechelewa kwa muda huu kwa vijiji 61 tu, je, vitongoji 350 itachukua muda gani, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri wananchi tuwaambie ukweli kwamba ni lini umeme utapatikana katika vijiji vyetu, lakini ni lini umeme utapatikana kwenye vitongoji. Lakini tukizungumza kwamba ni mwaka huu mwezi wa 12, mimi siamini kwamba hilo jambo litawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika Jimbo langu pia wapo wawekezaji wa umeme mmoja anaitwa Jumeme na mwingine anaitwa Power Corner; hawa watu wamechukua baadhi ya kata kwa maana ya vijiji wamepeleka umeme lakini wananchi wanalalamika sana, wanalalamika mambo mawili, kwanza moja umeme haupo yaani umeme haupo wakati wa mvua umeme haupo, hata wakati wa kiangazi umeme haupo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaweza ukajiuliza hivi hawa wananchi kupewa huu mradi kwa hawa watu wa Jumeme na Power Corner maana yake ilikuwa ni nini, wanahisi kwamba Serikali iliwadanganya, lakini kero nyingine ya pili ina maana wao wanapewa unit mbili kwa wiki, sasa unit mbili ni ndogo sana na ukilinganisha kwamba umeme wenyewe haupo, kwa hiyo wananchi wanalalamika, wakati mwingine wanaweka vitu vyao kwenye deep freezers zao, lakini mwisho wa siku vinaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini makampuni haya ofisi zao hazijulikani, wananchi hawajui waende kulalamika wapi, lakini pia lipo jambo ambalo limelalamikiwa na Wabunge wengi hili ambalo baadhi ya vijiji vimeongezewa kutambuliwa kwamba ni miji waweze kulipa shilingi 320,000 kuingiza umeme; kwa kweli ni jambo la kushangaza sana.

Mheshimiwa Waziri unafahamu Nguruka na unafahamu Uvinza hivi ni vijiji, imekuwaje na hawa Nguruka na Uvinza waweze kuwekwa kwenye tariff ambayo inalipwa na mijini? Naomba hili jambo uende kuliangalia, nimefurahi kwenye taarifa yako ulipokuwa unatusomea bajeti kwa kweli imeonesha kwamba lalamiko hilo limefika kwako Wizarani, lakini umetuma Tume ya kwenda kuchunguza uhalisia huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jitahidi sana Mheshimiwa Waziri Nguruka watu waende waone na Uvinza wafike, hawa wakifika Uvinza au wakifika Nguruka hakuna sifa ya kuongezewa ikawa shilingi 320,000 hawana hiyo sifa hata Uvinza hawana hiyo sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nimpongeze Mheshimiwa Waziri, lakini nakuomba sana umeme wa Gridi ya Taifa ufike Kigoma, lakini na huu mradi wa umeme wa Malagarasi tuanze kuona kazi ikiendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo mimi naomba niunge mkono hoja nasema kazi iendelee, ahsante kwa nafasi. (Makofi)