Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya makadirio na mapato ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Pili, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa kutayarisha na hatimaye kuiwasilisha hotuba hii katika Bunge lako tukufu kwa ufasaha na umakini mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo; nikianza na usambazaji wa umeme vijijini. Napenda kuipongeza Serikali yetu kwa kuendelea na utararibu wa kusambaza umeme vijijini. Katika nchi yetu ya Tanzania sasa hivi kuna engezeko kubwa la mahitaji ya umeme. Hivyo ni jambo jema sana kuwapelekea nishati hii wananchi wetu. Umeme una matumizi mengi lakini mpaka sasa wananchi wa vijijini wanaelewa kuwa umeme unatumika kwa matumizi ya taa za majumbani mwao tu, hii sio sahihi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika jambo hili kwa Wizara ni kuweka utararibu maalum wa kwenda vijijini kwa lengo la kuwaelimisha matumizi sahihi ya umeme, kama vile kupikia ili kunusuru ukataji wa miti ambao hivi sasa unaendelea kwa kasi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mradi wa gesi asilia; Tanzania tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutujaalia kuwa na gesi asilia katika nchi yetu. Gesi ni nishati muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Nchi yetu ilipogundua nishati hii wananchi tulijawa na matumaini makubwa. Tulidhani kuwa usambazaji wa nishati hii tulitegemea kuwa itasambazwa kwa speed ile kama inavyosambazwa nishati ya umeme inavyosambaa, lakini mpaka leo usambazaji wa nishati hii hauridhishi hata kidogo. Bado wananchi wanaotumia nishati hii ni wachache mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika jambo hili kwa Wizara ni kuweka utaratibu maalum wa kuisambaza huduma hii kwa wananchi wa mijini na vijijini ili kukidhi matumaini ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu deni la TANESCO kwa TPDC; TANESCO kwa muda mrefu sasa wamekuwa wa kudaiwa fedha nyingi na TPDC. Deni hili ambalo ni zaidi ya bilioni mia tano ni deni ambalo linaudhi sana kuona kila mwaka linajitokeza kwenye vitabu vya bajeti na wakati mwingine kwenye vitabu vya wakaguzi. Masharika haya mawili yote yako chini ya Wizara moja hivyo ni jambo la aibu kidogo kuona kuwa mpaka sasa halijapatikana ufumbuzi wake.

Ushauri wangu katika jambo hili kwa Wizara ni kuwaelekeza Maafisa Mausuuli wa Mashirika haya mawili kukaa pamoja kutafuta namna ya kulisawazisha deni hili. Matumaini yangu ni kwamba suala hili litapatiwa ufumbuzi muafaka na halitajitokeza tena kwenye vitabu vya ripoti za wakaguzi na ripoti nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa ushirikiano kati ya TANESCO na ZECO; ZECO na TANESCO ni mashirika mawili katika nchi yetu ya Tanzania yanayoshughulika na usambazaji wa umeme. Mashirika haya ni vyema yakaimarisha ushirikiano wao katika nyanja zote. Hivi sasa inaonekana ushirika wao upo kwenye mambo ya kiufundi tu na sio kwenye ngazi za maamuzi. Hapo zamani ushirikano wao ulikuwa mpaka kwenye mambo ya maamuzi. Kwa mfano ulikuwepo ushirikishwaji wa member wa bodi ya mashirika hayo kuhudhuria kwenye vikao vya maamuzi ya mashirika hayo. Kulikuwa na utaratibu wa mjumbe mmoja wa kila upande kuhudhuria kwenye vikao vya maamuzi ya mashirika haya. Ushauri wangu kwa Wizara kuchukua juhudi za makusudi kuurejesha utaratibu huu kwa maslahi ya pande zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwakilisha.