Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara iliyoletwa mbele yetu na baada ya kuunga mkono naomba nichangie baadhi ya maeneo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la uunganishaji wa Mkoa wa Rukwa na gridi ya Taifa; ili kuwa na umeme wa ukakika kwa Mkoa wa Rukwa ni sisi kuunganishwa na gridi ya Taifa. Sisi wananchi wa Mkoa wa Rukwa tumekuwa na umeme usio na uhakika ukitokea nchi ya jirani ya Zambia ambao umekuwa ukikatika mara kwa mara. Zipo taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa na TANESCO kwamba kukatika huko kumekuwa kukitokana na umbali mrefu ambao umeme huu umekuwa ukisafirishwa, wakati mwingine tunapoambiwa hitilafu inatokea nchi jirani, lakini kiuhalisia unakuta nchi jirani umeme unakuwa unawaka bila matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijaribu kufanya utafiti tunaambiwa mkataba ulioingiwa wa kuuziwa umeme kutoka Zambia bei ni ndogo ukilinganisha na bei wanayouza kwa wananchi wao, hivyo wanaona hakuna tija ya kuuza umeme upande wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na umeme wa uhakika ni pale tu Mkoa wa Rukwa utakapounganishwa na gridi ya Taifa mpango ambao ulikuwa ukitajwa na Serikali kwa muda mrefu. Jambo la kushangaza katika kipindi hiki cha bajeti ya Wizara katika kazi ambazo zimepewa kipaumbele kutekelezwa ni pamoja na kuiunganisha mikoa ya Katavi na Kigoma kwenye gridi ya Taifa bila kuutaja mkoa wa Rukwa ambao ndiyo mkoa uliouzaa mkoa wa Katavi. Siamini kama Wizara imekusudia kuuruka mkoa wa Rukwa. Hivyo niiombe Wizara ihakikishe mkoa wa Rukwa unawekwa kwenye vipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo hoja ya wakandarasi waliopewa kazi za kusambaza umeme vijijini kwa kupitia REA kwa kuachia miradi njiani bila kuikamilisha na bila kutoa maelezo kuonesha tatizo ni nini na ukubwa wa tatizo na kwamba tatizo hilo linatatuliwaje ili wananchi wapate huduma yao ya msingi, tatizo hili ni kubwa sana kwa wananchi wa Kalambo ambapo katika vijiji 111 kuna vijiji zaidi ya 40 havina umeme. Naiomba Wizara itupie macho yake kwa upekee katika Wilaya yetu ya Kalambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba kuwasilisha.