Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bumbuli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini labda makofi haya ni kwa sababu ya kuwezesha mapumziko ya nusu saa asubuhi. Lakini naomba nianze na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuomba radhi na ni uungwana kwa Mheshimiwa Spika, kwa Bunge na Wabunge wote kwamba asubuhi kutokana na wingi na uzito wa hoja zilizotoka jana, asubuhi tuliamkia kwenye kuandaa majibu tukiamini kuna uwezekano tukamaliza mchana na kosa tulilofanya tulichojifunza ni kutabiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutabiri kwamba maswali huwa yanaisha saa nne na dakika 10 au 15 na utabiri huo umetokana na uzoefu wetu tu wa hapa kwamba dakika tano mpaka pale nimeshaingia. (Makofi)
Kwa hiyo, kumbe leo yameisha kabla ya saa nne, kwa hiyo, tunaingia tunapishana na msafara hapa wote na Naibu Waziri, tukatamani kuingia chini ya viti, lakini tunashukuru kwa uelewa wa Bunge na Waheshimiwa Wabunge tumejifunza. Kila jambo lina elimu, kuanzia leo hatutatabiri tena maswali yanachukua muda gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa shukrani, shukrani nyingi sana kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kweli tumepata michango mingi na mizuri na yenye tija sana, sana, sana na imetusaidia sana na wataalam wetu kwa kweli wa Wizara nzima mmefanya wachemshe mbongo zao sana katika kutafuta majibu. Kwa hiyo, quality, ubora wa michango ya Waheshimiwa Wabunge kwenye Wizara yetu ulikuwa kiwango cha juu sana, sana, sana. Kwa hiyo, sisi tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia kwa pongezi nyingi ambazo mmezitoa na kwa kweli hatukuzitegemea kwa sababu kuna mambo mengi yalikuwa yanapitapita kuhusu bajeti ya Wizara yetu, lakini sisi tulikaa kimya, tukawa tunafanya kazi, kila akija Mbunge tunampa msaada, tunajaribu ku-engage, tunajaribu kutoa taarifa na naamini kwamba kutokana na hayo kazi mmeiona na pongezi tunazipokea na pongezi ni deni. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba yale ambayo tumeyaahidi, tutayafanya na sisi tunaahidi ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa mchango wake ambao umesaidia kueleza baadhi ya mambo. Sasa michango ni mingi, ni zaidi ya 50 na ningependa kuwataja Waheshimiwa Wabunge wote na nataka kuahidi kwamba kwa yale ambayo sitayafikia tutawajibu kwa maandishi kabla ya Bunge hili la Bajeti kuahirishwa ili kila mmoja apate majibu ya yale ambayo tumeyaeleza. Nitajaribu kujibu kwa ujumla na nitarajibu kupitia michango ambayo imetolewa kwa Mbunge mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa masuala ya jumla ambayo nadhani ni muhimu nikayazungumza la kwanza ni hili la TPDC kushiriki kwenye biashara ya mafuta. Kwa sababu nadhani hili ni kubwa na la kisera na lazima tulitolee kauli na msimamo.
Kwanza ili uamue kwamba taasisi gani inafanya shughuli gani, lazima urudi nyuma uangalie imeundwa kwa mamlaka gani, kwa instrument gani na imepewa kazi gani ilipokuwa inaundwa yenyewe kwa sheria yake na sheria mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukienda kwenye sheria kubwa kabisa tuliitunga hapa ya Petroleum Act ya mwaka 2015. Sheria ile ina i-define TPDC kwamba ni National Oil Company, ni Kampuni ya Mafuta ya Taifa na imepewa kazi gani mle? Imepewa kazi nyingi, lakini moja ya kazi mle ni kwamba itashiriki katika mnyororo mzima wa biashara ya mafuta na gesi. Tunaposema mnyororo mzima, maana yake kuanzia utafiti, utafutaji, uendelezaji na uuzaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu tukayajua pia matakwa ya sheria kuhusu hili jambo, acha tu mambo mengine ya kibiashara lakini matakwa ya sheria kuhusu hii taasisi yetu. Lakini sisi imani yetu ni kwamba kushiriki kwenye mkondo wa juu kwa maana kutafuta na kuchimba siyo mutually exclusive na kuuza huku chini, unaweza kufanya vyote na vyote vikawa sahihi. Sisi tunayo mifano ya National Oil Companies za nchi nyingi na baadhi ya hizi tuna ushirikiano nazo. Mimi nilipata bahati ya kusafiri na Mkurugenzi wa TPDC kwenda kumtambulisha na kutambulishana kwenye National Oil Companies za nchi rafiki na nyingine tumeingia nazo makubaliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulienda Abu Dhabi National Oil Company kubwa sana, hii kampuni ina visima vya kuchimba, lakini wana-training wanauza rejareja na sisi kampuni tunayoshirikiana nayo ukisikia TPDC imeshinda tender, imenunua mafuta haya yaliyochakatwa kutoka Abu Dhabi National Oil Company ambayo ina mafuta, ina visima lakini pia inauza. Kuna kampuni inaitwa Sonatrach National Oil Company ya Algeria kubwa, ina visima, ina ma-refinery lakini inauza mafuta pia rejareja. Kuna nyingine inaitwa Sonangol ya Angola. Vilevile naweza nikataja kuna Aramco ya Saudi Arabia kama alivyosema ndugu yangu Mheshimiwa King.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa lazima tuliweke sawa, sisi kama Serikali tutaendelea kuiunga mkono TPDC na kuiwezesha ifanye kazi zake katika mnyororo mzima wa biashara ya mafuta na gesi. Lakini pia tukumbuke hili jambo ni kubwa la kimkakati, huwezi kuliacha. Sisi tulienda vitani, mzee wangu Kepteni George Mkuchika anafahamu, tulienda sisi na majeshi ya Idd Amin. Nchi zote na wauzaji wote wa mafuta walikataa ku-supply mafuta, nani alipeleka mafuta mstari wa mbele? Ni TPDC. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale kwenye ofisi zetu kuna nishani imesainiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nishani wamepewa TPDC kutunukiwa na Mwalimu kwa kuhudumia nchi katika kipindi cha vita. (Makofi)
Kwa hiyo, kuna baadhi ya mambo hauwezi ukayaacha, ukaweka mkono wa Serikali na moja wapo ni mafuta. Hata hizo nchi tunazoziita za mabepari na nini kwenye haya mambo yaziondoi mkono zipo kwa sababu ni suala la usalama wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hapa katikati kidogo tulilegea legea lakini tumerudi kwa nguvu kabisa kuiwezesha TPDC liwe shirika kubwa la mafuta ya Taifa na la kimkakati na liweze kufanya hii shughuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na pale kwenye TPDC kuna idara mbalimbali, kuna idara ya exploration wao wataendelea nao. Lakini kuna directorate/ Kurugenzi ya Oil and Gas Business ndiyo wanafanya hii shughuli. Kwa hiyo, idara hii wanaendelea, idara ile wanaendelea na shughuli nyingine wala haina mgogoro. Kwa hiyo, nisingependa hili likawa ni jambo ambalo likaaminika hapa na sisi tukalichukua. Kwa hiyo, hilo nilitaka niliseme kama jambo kubwa la kisera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili suala la kukatikakatika kwa umeme, amelizungumza Naibu Waziri na nataka niseme kwamba ipo miradi kuna package, labda niseme wote mnafahamu, sisi tulivyopewa nafasi hii na hapa Bungeni ikajitokeza hoja ikiwemo tuunde tume ya kusema kwa nini Waziri Makamba ameingia na umeme unakatikakatika sana. Ikawa ni kama jambo msukumiwa la mtu. Lakini sisi tukafanya utafiti na timu pale TANESCO, maana yake kulikuwa na maneno hujuma, hujuma, Hapana, siyo hujuma, mimi nilikuwa siamini kabisa kama watumishi wa Serikali na wa TANESCO wanaweza wakaihujumu nchi yao, kabisa hilo halipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na tukagundua kwamba kuna baadhi ya maeneo na Wabunge ni mashahidi mmesema kuna baadhi ya line ni ndefu sana na zimewekwa kipindi kirefu kabla matumizi hayajapanuka na ni dhahiri kabisa hayatoshelezi. Kwa hiyo, tukafanya utafiti kila eneo ni karibu nchi nzima kuna vituo vidogo, kuna nyaya ndogo, nyembamba, kuna nyaya zingine zina-serve watu wengi, kuna transfoma nyingine zinahudumia wateja wengi zaidi kuliko uwezo na tukatengeneza package ya miradi inaitwa National Grid Stabilization Project ambayo ukiiweka thamani yake ni shilingi trilioni nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa safari hii tumebarikiwa, tumepewa shilingi bilioni 500. Nafahamu nimesikia suala la Mheshimiwa Kimei kwamba itaisha lini kwa sababu bilioni 500 ukilinganisha na trilioni nne na hapa ni under investment tuna-cover vitu ambavyo havikuwekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hatutategemea peke yake pesa hizi za bajeti kila mwaka katika kutafuta rasilimali za kurekebisha hali ya umeme. Zipo njia nyingi ambazo tunazifanya za kutafuta fedha ikiwemo hii ambayo tuliisema kwamba tukirekebisha vitabu vya TANESCO na Serikali ikafuta au ikachukua nusu ya deni; TANESCO itakuwa na uwezo wa kifedha wa kwenda kutafuta resources na kufanya hii miradi ambayo iko kwenye grid stabilization bila haja ya kuja hapa Bungeni mara kwa mara, kwa hiyo, hilo tunaendelea nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la kisera ambalo napenda kulizungumza hapa ni suala ambalo limezungumzwa kidogo kwa kirefu, ni hili suala la strategic reserve ya mafuta na amelizungumza Mheshimiwa Mwijage, Kamati imelizungumza, Mheshimiwa Kimei pia amelizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa labda niweke vizuri, hifadhi ya mafuta ya kimkakati ni nyenzo ya usalama wa Taifa vilevile. Sisi hapa sheria zetu zinahitaji kwamba kwa wakati wowote hapa nchini mtu mwenye maghala ya mafuta au kituo cha mafuta awe na mafuta ya siku 15 za mbele kwa sababu ya dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tayari katika hiyo sheria, hiyo kanuni kuna element za kutaka kujikinga, kuwa na hifadhi nchini incase kuna dharura. Sasa sisi tumeweka siku 15 kwa sababu tu ya uwezo, uwezo wa hifadhi, uwezo wa mafuta na kadhalika. Kuna nchi nyingine zinahitaji siku 90, kuna nchi nyingine mpaka miezi sita kwamba at any given time nchi iwe na mafuta ndani ya nchi ya kutosheleza miezi sita, sisi tumeweka siku 15 zinatosha. Sasa ikitokea dharura ya siku ya zaidi ya siku 15 maana yake ni kwamba hamna mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tumeamua safari hii tufanye mambo ambayo yatatupeleka zaidi ya siku 15. Sasa mambo yenyewe ni yapi? Hifadhi ya kimkakati ya mafuta ya Taifa siyo lazima iwe ni physical kwamba mmechimba mashimo au matenki kuna mafuta pale yanasubiri tu dharura. Ukifanya hiyo, hiyo ni dead capital na mafuta pia yenyewe yanapungua ubora kadri yanavyokaa. Kwa hiyo, tunaposema hifadhi ya kimkakati ya mafuta hatuna maana tununue mafuta tuyaweke kwenye matenki, tusubiri dharura, hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna instruments nyingi za kuwa na petroleum strategic reserve na mojawapo ni aliyosema Mzee Kimei. Kikubwa ni kwamba at any given time ndani ya nchi either kupitia instrument mojawapo ni kuifanya nchi yetu iwe kituo kikubwa cha biashara ya mafuta, yaani nchi zote za ukanda huu ziwe zinanunua mafuta hapa, zinapitishia hapa, pana matenki hapa pia iwe trading hub, kwamba kama upo nchi nyingine unapiga simu kwamba nataka kununua mafuta chapchap basi unaambiwa Tanzania kuna tani 200,000 unaweza kuzipata haraka haraka na zile zinarudishwa haraka haraka. Hiyo ndiyo strategic reserve kwamba unayo at any given time, siyo ipo imelala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa tunachosema ni kwamba tutatumia na tutaleta hapa Bungeni, tutatumia baadhi ya hizi instruments za kisasa na za kibiashara za kuwa na mafuta mengi ya kutosha hapa nchini ikiwemo kuibadilisha Tanzania iwe kituo kikubwa cha mafuta katika ukanda huu. Kwa hiyo, hili ni jambo la kisera nataka niliweke, kwa sababu ukisema pesa, ukiwa na cash kwamba mimi nimeweka pembeni cash nikipata dharura niwe na uwezo wa kuagiza mafuta, saa nyingine unaweza kuwa na pesa za kutosha tu lakini physical huwezi kuyaleta mafuta hapa nchini. Kwa hiyo, lazima uwe na namna ambayo mafuta yanakuwa traded hapa hapa nchini. Kwa hiyo, hiyo tutaendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine la kisera ni suala la umeme kwa ujumla. Malengo yetu ya kufikia megawati 5,000, tunafikaje, mahitaji ya nchi tunayajuaje, tunayapangaje, umeme wa aina gani, tunaufikishaje kwa watumiaji. Sasa moja ya vielelezo vya maendeleo ya nchi ni moja ni alilosema Profesa Muhongo per capital consumption ya energy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ni aina ya nishati watu wanayotumia, nyingine ni idadi ya watu wanaofikiwa na nishati hiyo na mwisho ni nishati hiyo inatumika wapi. Hiyo ndiyo energy profile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi yetu aina ya nishati inayoongoza kwa matumizi siyo mafuta, siyo umeme, siyo gesi ni nishati inaitwa biomass. Kuni, mkaa, pumba, mavi ya ng’ombe na kadhalika. Asilimia zaidi ya watu 80 ya Watanzania ukichukua unit ya energy, magari yote yanayosafiri, mitambo yote inayozalisha umeme bado kiwango cha nishati kinachotumika ni kidogo kuliko kuni, mkaa, pumba. Sasa hiyo peke yake proportion ya biomass consumption inaelekeza kiwango cha maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maendeleo yanapatikana mnapoondoka kwenye biomass na kuingia kwenye commercial traded modern cleaner energy, kwa sababu biomass moja ya sifa yake kwa mwaka hapa watu 22,000 wanakufa kwa kuvuta moshi wa kuni na mkaa watu 22,000, hizo ni statistic za Wizara ya Afya. Kwa hiyo, kwa kadri unavyoenda kwenye nishati safi ndivyo ambavyo unaokoa watu wako na unaingia kwenye uchumi wa kisasa. Sasa hiyo ya kwanza aina ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili je, nishati ya hapa Tanzania inatumika zaidi wapi kwenye usafirishaji, kwenye viwanda, majumbani? Ukitizama profile ya nishati hapa nchini haitumiki viwandani, inatumika majumbani na majumbani inatumika wapi. Je, kupoza vichwaji? Je, kupoza hewa? inatumika kupika. Kwa hiyo, utaona kwamba kwa nchi yetu kama wewe ni Waziri wa Nishati haujajielekeza kwenye nishati ya kupikia haujafanya kazi yako, kwa sababu ndipo ambapo consumption kumbwa ya energy ilipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka kwenda kwenye maendeleo ya viwanda, tunahitaji umeme zaidi, nami nakubaliana kabisa kwamba per capital energy consumption yaani kiwango cha nishati kinachosomeka kwa mtu lazima kipande, lakini hiyo ni function ya unazalisha kiasi gani; Pili je, una uwezo wa kuusafirisha huo umeme kwa hao watumiaji; Tatu je, wana-appliances za kutosha za kutumia umeme mwingi; na mwisho je, una viwanda vya kutosha kutumia umeme wa kutosha? Lakini ni yai na kuku kipi kimeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutazalisha umeme mwingi tumeongea na wenzetu wa TANESCO, tunataka sisi kama tutapata dhambi, dhambi yetu iwe kuwa na umeme mwingi kuliko unaohitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuweze kuusambaza na kuupeleka kila mahala katika nchi hii, ndiyo maana utaona bajeti yetu hii ya safari hii ambayo sio mwisho ni mwanzo wa safari inatupeleka kwenye kuzalisha umeme mwingi lakini mtaona miradi mingi ya usafirishaji na mradi wa usambazaji ni hii ya vijijini. Kwa hiyo jambo la kisera sisi la kwetu ni siku zote kuendelea kuzalisha umeme mwingi wa kuwafikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri tuliyonayo sisi katika ukanda huu tuna natural resource base ya kuzalisha umeme kuliko nchi nyingi katika uwanda huu ukiondoa Congo. Tunayo makaa ya mawe, gesi, jua, upepo na tunayo maporomoko ya maji. Kwa hiyo, ukilinganisha sisi leo tulikuwa tunapiga hesabu uki-exhaust resource base yote tuliyokuwa nayo sasa hivi tuna uwezo hata wa kufika hata megawatt 60,000 hatuzihitaji sasa lakini ndiyo safari hiyo tunayoelekea. Sasa nilitaka kusema kisera huo ndiyo mwendo na mwendo wa haraka na hatutasita kukimbia kwenye kupata umeme mwingi kiasi kikubwa, sasa hili nilitaka nisema jingine la kisera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Symbion ambalo alilizungumza Halima Mdee na suala la Mwalimu Nyerere na suala la TANESCO kwa ujumla. Sasa nianze na suala la Symbion sasa hili ni muhimu niliseme hapa Bungeni ili kuliweka vizuri kwa sababu limekuwa linasemwasemwa...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri una dakika Kumi.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nahitaji zaidi lakini nashukuru. Suala la Symbion limekuwa linasemwa sana, nataka kulisema kama ifuatavyo na hili litaendana na Mwalimu Nyerere ambalo nitalieleza. Suala la Symbion tunaweza tukarudi sana lakini nianzie 2011 ambapo TANESCO iliingia kwenye mkataba wa muda na kampuni hii Symbion ambayo ilikuwa na mitambo pale, ilikuwa mitambo ipo pale imekaa huko nyuma kulikuwa na mambo mengine kulikuwa na shida ya umeme wakaingia mkataba wa muda wa miaka miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba ukaisha 2013 wakaingia mwingine wa muda mpaka Septemba 2014, EWURA wakaandikia barua TANESCO kwamba hii mikataba ya muda mfupi mfupi ina gharama, TANESCO wakachukua ushauri wa EWURA wakaingia mkataba wa muda mrefu kati ya TANESCO, Symbion na muda mredu kati ya TANESCO na symbion Julai 2015. Septemba mwaka huohuo EWURA ikapitisha huo mkataba na mwezi Disemba Mwanasheria Mkuu naye akaupitisha, Tarehe 10 Disemba, 2015 Mkataba ukasainiwa lakini siku hiyohiyo ukaitishwa na baada ya hapo Tarehe 24 mwezi Mei mwaka 2016 mkataba ule ukavunjwa rasmi Machi 27, Symbion akaenda kwenye Mahakama ya Kimataifa ICC kudai fidia ya dola za Kimarekani Milioni 566 kwa kuvunjwa mkataba isivyo kufuata utaratibu na hasara ambayo itapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye shareholders wa Symbion wakaenda kudai Dola Bilioni Moja kutokana na kuvunjwa kwa industrial protection treat, tukawa tunadaiwa Dola Bilioni Moja na Nusu kutokana kwenye huo mkataba, mashauriano yakafanyika baadaye ikakubalika kwamba tuzungumze nje ya court na mazungumzo hayo yalikubalika Julai 28 na Februari 2021 makubaliano yakafikiwa, yalikuwa na sehemu tatu, Serikali TANESCO kulipa zile bilioni 300 na aliyosema Mheshimiwa Mdee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ilikuwa baada ya Serikali kulipa TANESCO kuchukua ule mtambo wa megawatt 112 kwa sababu ile ndiyo kisehemu kinaachwa, kukawa na ratiba ya kulipa hayo malipo la sivyo inarudi kwenye Mahakama. Sasa mwezi Agosti malipo yakafanyika kulingana Deed of Settlement ambayo Serikali ilisaini ili kuokoa adhabu kubwa ambayo tulikuwa tunaelekea kushindwa na mwezi Oktoba TANESCO ikauchukua mtambo, sasa kuanzia mwezi Novemba mtambo ukaanza kuzalisha umeme na tangu umeanza kuzalisha umeme mwezi Novemba mpaka sasa umezalisha unit hapa ziko nyingi ninazoweza kuzitaja, TANESCO imezalisha umeme na kuuza kwa faida, kwa hiyo ukipiga hesabu thamani ya mtambo wa megawatt 112 na mauzo ya umeme yanayopatikana katika mtambo ule basi unaweza kujua kama hayo makubaliano yalikuwa na tija, lakini sisi tunaamini kwamba Serikali kupitia Wanasheria na waliamini kabisa kwamba ni jambo ambalo lilipaswa kuiepushia Serikali hasara kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huo ndiyo ukweli kama unaweza kuutafsiri unavyotaka lakini mwisho wake maamuzi yalichukuliwa na Wanasheria wa nchi yetu walioangalia maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mradi wa Bwawa la Julius Nyerere, sisi tuna mkataba mradi ule unaendeshwa kwa mkataba, mkataba unatoa haki na wajibu kwa kila upande, mkataba umeweka utaratibu wa kushughulikia kutofautiana, mkataba unatoa adhabu na sanctions mbalimbali, muda wa mkataba haujaisha, nasi tusingependa ku-litigate contractual matters kati ya two parties kwenye contract ambayo its operational hapa ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mkataba huo unaendelea zitakapofika ratiba ambazo zimepangwa basi zitafika. Je, mradi utachelewa ndiyo mradi utachelewa kwa miaka miwili. Je, implication ya kuchelewa ipoje ipo ndani ya mkataba. Sisi kwetu mkataba uishe ukiwa bora na usalama mradi na sisi hatuoni kuchelewa kwa mradi wa Julius Nyerere kama ni disasters, mradi hapa wa Kidatu umejengwa miaka mitano, Kihansi miaka minne, Mtera miaka minne, Pangani miaka mitano, duniani kote miradi hii inapita ratiba, sisi focus yetu uishe kwa ubora na viwango na malengo yake yatimie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hasa naomba nitumie muda mchache uliobaki harakaharaka kumaliza na ndugu zangu wa Kigoma. Grid naomba Mzee Bidyanguze, Mama yangu Samizi, Kaka yangu hapa Kirumbe na wananchi wa Kigoma na Wazee wangu wa kule Buhigwe wote mnafahamu mimi ni wa Kigoma lakini siyo sababu ya kuweka grid. Kwa hiyo nafahamu ipo miradi minne ya kupeleka grid Kigoma. Katika miradi hiyo minne, miradi miwili Wakandarasi wapo site, mmoja anaitwa TATA anapeleka wa Kv 400 kutoka Nyakanazi mpaka Kigoma tumemlipa yupo site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi wa pili yupo site anaitwa Sinotech anautoa Nyakanazi - Kakonko mpaka Kibondo tunayo line, kwa hiyo Kibondo – Kasulu - Buhigwe - Kigoma hii inaisha Oktoba, hii siyo story wako site. Kwa hiyo tunaposema grid inakuja Kigoma kabla ya Oktoba tunamaanisha hivyo. Waheshimiwa Wabunge nimalize kwa kusema Mzee wangu Salum nimekusikia mchango wako tumeuchukua, Mheshimiwa Mwakasaka vijiji vyako tumevichukuwa, Mheshimiwa Zedi, Mheshimiwa Jesca Kishoa tutakujibu kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shanif Mansoor, Mzee Usi Salum Pondeza, Mheshimiwa Lucy kutoka Simiyu tumetenga Milioni 725 kwenye mradi ule wa kupeleka umeme Bariadi, kwa sababu ndiyo kazi za kuanzia ikiwemo kulipa fidia, tukishalipa fidia na kumaliza ile EIA pesa Bilioni 65 zipo za kupeleka umeme wa grid Bariadi. Mheshimiwa Vuma nimeshajibu kuhusu grid na kukatika kwa umeme tumejibu, Mheshimiwa Makoa ndugu yangu vijiji vyako Kondoa Mjini na hapa siyo mbali, Mheshimiwa Monni nitakuja Chemba siyo mbali na Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava suala la mafuta tutakujibu kwa maandishi na umeme kukatikakatika tumejibu. Mheshimiwa Gulamali Bwawa la Mwalimu Nyerere hongera tumezipokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la hii Tume tuliyoiunda ya kwenda kuchunguza, labda niseme tu kwamba samahani tulipata shida moja, kwamba kama TANESCO na kama Wizara, tunaposema kwamba bei ya kuunganisha itokane na nguvu ya kiuchumi ya wahusika ambayo assumption ilikuwa ni aina ya settlement wanazokaa, kwamba watu wa mjini wana nguvu za kiuchumi wanaweza kulipa zaidi, watu wa vijiji tuwasaidie walipe chini. Sasa problem tuliyoipata ni hiyo katika miji kuna watu pembezoni mwa miji ambao pamoja na kwamba jiografia imewaweka ndani ya mji lakini hali yao inafanana na vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na option mbili, either kutengeneza a general rule ambayo itakuwa applicable kwa maeneo ya aina hiyo, jambo ambalo ni gumu, pili ni sisi kwenda physically wenyewe kuuchukua mtaa kwa mtaa inayofanana kama kijiji. Nadhani kwa hoja kama itachukuwa muda nadhani ni njia salama zaidi itakayo-target wahusika moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tunaomba mkubali hii na kama tulivyosema kwenye hotuba yetu tutawashirikisha katika hii, watu wetu mtawaona watakuja huko na tutafanya kazi.
Meshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Vita suala la kupeleka umeme kwenye hizi sehemu za huduma tumelipokea, kwenye bajeti tunao mradi wa kupeleka umeme katika mashule vituo vya maji na zahanati. Mheshimiwa Festo nimekuelewa sana vizuri sana kuhusu mchango wako ambao umetokana na experience yako ya kutembelea kiwanda cha kule ulipoenda, kuhusu Lumakali na Luhuji naomba niseme kwamba tumepata watu ambao wana-interest ya kuwekeza. Zile hela ulizoziona Bilioni Nane ni za kazi za awali kuhuisha ile feasibility study lakini tunakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la GGM ambalo limezungumza na Mheshimiwa Musukuma nadhani na wewe na mwingine, pale kuna confusion, tumeingia nao mktaba nao mwezi Novemba tuwapelekee umeme, sasa ile substation inayoonekana pale Geita Mjini siyo yenyewe ya kupokelea umeme wa GGM. Tulikubaliana sisi tutaupeleka mpaka getini wao watajenga substation ndani, kwa hiyo kuna substation inayojengwa ndani ya mgodi ambayo inaisha mwezi Oktaba kwa mujibu wa makubaliano yetu, kwa hiyo bado tutapeleka umeme GGM na ile sheria uliyosema ya hovyo ya kwamba ukizalisha umeme huu, lazima tutaipitia kwa hakika kabisa ili kuwezesha wawekezaji wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Deo Mwanyika, suala la Mapembasi tutalimaliza na la Masista pia tutalimaliza. Mheshimiwa Getere mambo mengine uliyosema umepitisha kidogo lakini tunapokea pongezi. Hiyo Tume itakuja nashukuru kwamba umeona mambo yanaenda vizuri. Mzee Magessa naomba tisheti uivai ya vitongoji kwa sababu siyo tu tumeanza lakini dhamira ya kupeleka umeme kwenye vitongoji ipo kwenye bajeti yetu tunazo Shilingi Bilioni 140 za maandalizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, migodini mtaleta lini? Mkitazama kwenye bajeti yetu ya sasa tumetenga Shilingi Bilioni 20 kupeleka umeme migodini, viwandani na kwenye maeneo ya uzalishaji wa kilimo, haijawahi kutokea na tutaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee wangu rafiki yangu Kamonga Ludewa tumekupata tumekusika, Mheshimiwa Mohamed Saidi Issa ile sheria geothermal tutaifanyia mabadiliko, Mheshimiwa Ighondo Abeid tutakuja pamoja kama ulivyosema katika vijiji Tisa kuwasha pale Singida, Mheshimiwa Shabiby suala la bili la KVA naomba sana kwa ridhaa yako tuchukue haya makaratasi yako tuende pamoja TANESCO tukalitazame kama ni suala la mahsusu kama suala la jumla tutalifanyia kazi lakini suala la mafuta hizo taarifa ulizonazo za kuhusu bei zinavyopigwa tuko tayari kuzipokea, tuko tayari kuzifanyia kazi, wewe tuletee kwa pamoja ukitaka unaweza kuja na mtu mwingine ambae atakuwa shahidi wako namna tunavyolishughulikia hilo jambo kama huna imani na uwezo wetu wa kushughulikia hilo jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nusrat kuhusu Singida kuna miradi mitatu, katika hiyo uko mradi wa Manyoni, mradi wa Singida pale DC na Ikungi yote hiyo ipo katika uelekeo wa kutekelezwa. Manyoni tayari wako Masdar kampuni ya UAE kubwa kabisa ya renewable huu mwingine ipo kampuni ya upepo ambayo imepata zabuni na iko kwenye majadiliano na kampuni, lakini sasa muhimu kujua ni umeme unapozalishwa pale Singida siyo kwamba ni wa Singida ni kwa sababu tu Singida ipo kwenye grid utaenda pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la hospitali hazijaunganishwa ukitazama kwenye bajeti yetu utaona kwamba katika mwaka huu tuna hospitali zaidi na vituo vya afya zahanati zaidi ya 114 ambazo tumezipelekea umeme mahsusi na hapa ndipo tunapoanza, tunaongea na wenzetu katika TAMISEMI na kwingineko kwamba tunapopanga hii miradi tupange pia na component ya umeme, kwa sababu saa nyingine tunasahau unaweka kule halafu kumbe umeme hakuna kwa hiyo REA leteni, kwa hiyo kwenye cost ya miradi tuta-coordinate na wenzetu ili cost ya mradi wote iwe pia na gharama ya kupeleka umeme pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mhagama nimekupata, Mzee George Malima, REA ipo center ni kweli, Mpwawa na bei ya kuunganisha nimezungumza, Mheshimiwa George Mwenisongole suala la wakandarasi amelizungumza Naibu Waziri, suala la Mkuu wa Mkoa nadhani mimi na wewe tutalizungumza pamoja na Waziri wa TAMISEMI kuliweka vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dada yangu Mariam Mtanda megawati 300 za Mtwara ambayo pia amezizungumza Mheshimiwa Mwambe megawati 300 za Mtwara pesa imepatikana na siyo tu ya megawati 300 lakini pia na waya wa kuleta mpaka Somangafungu, Wajapan watatuchangia.
Mheshimiwa Francis Isack, Mkalama nimechukua, tutakujibu kwa maandishi; ndugu yangu Mheshimiwa Hassan Kungu kutoka Tunduru naelewa kabisa ile KV 33 kutoka Songea ni ndefu bila shaka na katika ule Mradi wa Grid Stabilization ipo ya ku-upgrade ule waya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mjomba wangu Mheshimiwa Rweikiza kazi bado sana; ni kweli na umeme unazimika sana tumelizungumza, Mheshimiwa Florence Samizi, gridi nimezungumza, Malagarasi pia tunaanza; Mheshimiwa Bidyanguze pesa ipo tumamazila evaluation, ndani ya mwezi tuna-award Mkandarasi aanze ujenzi pale.
Kuhusu madeni makubwa TANESCO labda niweke tu vizuri status ya TANESCO, TANESCO assets value yake ni trilioni 17, madeni yake ni trilioni tatu, katika hayo madeni trilioni mbili ni madeni ya Serikali ya on landing na trilioni moja ni watoaji huduma ikiwemo TPDC, PAET na kadhalika. Kwa hiyo, ni vizuri hizi takwimu za financial position ya TANESCO zikajulikana kwa sababu saa nyingine tunachanganya, ukisema TANESCO ina deni la trilioni 13 si kweli ni ina asset ya trilioni 13.
Mheshimiwa Anastazia Wambura la megawati 300 nimelizungumzia, Mzee Mulugo, lile suala la helium tumelizungumza ofisini, ni la ndani ya Serikali tutaliweka vizuri; Mzee Felix wa Buhigwe nimejibu na mengine tutajibu; Mheshimiwa Issa Mchungahela, umelihutubia Taifa, hotuba yako imepokelewa basi tutayafanyia kazi ambayo umeyasema. (Makofi)
Mzee Almas nimeelewa sana kuhusu Msamvu na ni critical na kuungua mara mbili ndani ya miezi sita ni jambo ambalo inabidi lituinue, na mambo mengine hatuyasemi hapa, lakini kuna hatua tumechukua za kiusalama za kuuchunguza lakini pia na kuimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafutaji wa mafuta tumeongea kwenye bajeti tutaenda nao; Mheshimiwa Godwin Kunambi na Mheshiwa Vedasto tulizungumza kuhusu watu wanataka kuunganisha umeme, je, kwa nini tusiwakopeshe halafu wakalipa kidogo kidogo kwenye bili zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tumelitafakari na tunaendelea kulitafakari, tumepokea proposal mbalimbali na wachambuzi wa fedha wanafanya, challenge iliyopo ni kwamba vifaa vya kuunganisha vile vinaweza vikafika labda shilingi 200,000 au shilingi 300,000 lakini kasi ya kununua umeme ikawa ni shilingi 2,000 kwa mwezi au mtu ananunua LUKU anakaa nayo miezi sita, mnalazimika kutafutana, kutaka kung’oa, kukatiana umeme, mtu akiongeza tu umeme wake umeukata, kwa hiyo inaweza ikaleta ugomvi.
Kwa hiyo the debt collection component ya hii programu ni lazima tuiweke vizuri ili tusigombane na watu wetu kwa sababu kama mtu yuko nyuma ya deni akiweka LUKU tu maana yake imeliwa, sasa tutakuwa tunagombana na wateja. Lakini ni jambo ambalo tunalitafakari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa mafuta Mheshimiwa Mohamed Monni nimeshazungumza; Mheshimiwa Mama Stella Manyanya ile evacuation ya umeme kutoka Julius Nyerere nielezee kidogo tu, Julius Nyerere siyo mradi mmoja, siyo bwawa; kuna bwawa, kuna usafirishaji yote inaenda kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwambe kuhusu LNG, tutafanya na tunafanya na tumeanza bila shaka yoyote Bandari ya Mtwara na miundombinu ya Mtwara itatumika katika utekelezaji wa mradi huu.
Mheshimiwa Mariam kuhusu teknolojia ya live wire na usalama kwenye LNG tumepokea; Mheshimiwa Kingu ahsante sana kwa shukrani, kuhusu tender iliyofutwa, tender hii safari hii ilisimamiwa na GPSA, GPSA iko chini ya mamlaka mengine na sisi tutakachofanya ni kufuatilia nini kilitokea, ila jambo ambalo ni la kweli kabisa ni kwamba fuel marking bado ni shida, haifanyiki kwa mtu yoyote wa mafuta atakwambia fuel marking haifanyiki kwa viwango vinavyohitajika na bado ni mtihani capacity ya TBS bado iko chini, tunaongea na wenzetu kuweza kuiinua. Kwa hiyo la tender tutalifuatilia halafu tutatoa taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee Bidyanguze, nimezungumzia la Malagarasi nashukuru na umeme utapatikana lini kwenye vitongoji tutaeleza kwenye siku zijazo; Mzee Kimei tumezungumza kuhusu densification inaendelea na kutafuta sources zingine kwa sababu umeme vijijini ndiyo densification yenyewe; ndugu yangu wa Mbinga kweli basi kwa kuchelewa basi tutafika na mimi ahadi yangu iko palepale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwisho kabisa najua huwezi kuzungumza hapo ulipo ila Mfindi Kusini hatujaisahau kupeleka umeme katika sahanati, shule na sehemu za huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi na niseme tu kwamba nishukuru tena kwa michango kwa kweli mmetutia moyo sana, mmetupa nguvu na haya ambayo tumeyaweka kwenye kitabu chetu ni safari ni mwanzo wa safari siyo yote yataisha mwaka ujao wa fedha, tumeyaweka pale mengine ni endelevu kama mnavyojua yanaonekana ni masuala ya kuendelea. Lakini naomba niwashukuru sana kwa ushirikiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.