Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na uhai na kuweza kusimama ndani ya Bunge hili tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake kwa utendaji mzuri katika Wizara hii. Lakini kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa programu nzuri ambayo aliizindua tarehe 22 Aprili, kule Marekani programu hii ya Royal Tour nina uhakika na ninaamini kwamba itakuja kuleta matunda makubwa zaidi. Nina kila sababu ya kusema hivyo kwa sababu ukitizama nchi mbalimbali ambazo zime-practice hii programu ya Royal Tour tukienda East Africa tu hapa Rwanda na mwigizaji alikuwa yuleyule Bwana Peter Greenberg walifanya vizuri baada ya programu hiyo na matunda yanaonekana watalii wengi Rwanda wameweza kwenda. Lakini si Rwanda tu zipo nchi mbalimbali ikiwepo Mexico, Poland, Ecuador, Israel wote hao wame-practice hii programu ya Royal Tour na matunda, matokeo chanya yameonekana kwa nchi zote hizi. (Makofi)
Kwa hiyo, sina shaka, sina hofu, nampongeza Rais wangu Mama Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi huu kwa sababu naamini Tanzania itakwenda kukuza utalii kupitia programu hii ya Royal Tour. Hongera sana Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile hata kwenye interview ambayo Mama Samia Suluhu Hassan aliyofanyiwa pale New York City aliweza kujitanabaisha na kuainisha vivutio mbalimbali vya utalii ndani ya nchi ya Tanzania na watu wengi wakaweza kuvifahamu. Lakini tukienda mbali zaidi hata Gazeti la New York Times lilimuandika vizuri sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kumpongeza na tukumbuke jamani gazeti hili siyo la udaku ni kati ya magazeti ambayo yanaheshimika Marekani. Kwa hiyo, naamini kabisa kwa kupitia programu hii matunda makubwa yanakuja kwa kupata watalii wengi sana ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi kubwa hii iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni wajibu sasa Wizara ikaangalia namna bora ya kuendelea kumuunga mkono mama na kuendelea kuchakata suala hili la utalii kuelekea Nyanda za Juu Kusini. Nyanda za Juu Kusini kama tutaweza kuchakata vizuri suala hili la utalii tutakwenda kufanya vizuri zaidi. Nyanda za Juu Kusini ukianza tu pale Mkoa wa Njombe kuna Hifadhi ya Kitulo, hifadhi ile ni bustani ya Eden, hifadhi ile hakuna inayofanana na ile ulimwenguni ni hifadhi ya kipekee ina ndege wazuri, ina maua mazuri, kama tutaweza kuipigia chapuo tutakwenda kuongeza watalii Nyanda za Juu Kusini. Lakini ukienda pale Rukwa, kuna maporomoko yale ya Kalambo, maporomoko ya Kalambo Afrika ni maporomoko ya pili yakitanguliwa na Victoria Falls kule Zimbabwe, bado tuna kitu kikubwa cha kuweza kukiuza na watalii wakaja nchini kwetu kwa kupitia kule Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile tuna mbuga nzuri ya Ruaha, ni ya kipekee ina makundi makubwa ya simba ambayo East Africa hakuna makundi yale makubwa ya simba, tunaweza tukaweka kwenye package ya Nyanda za Juu Kusini na utalii ukaweza kukua na kuweza kuongeza mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile tuna utalii wa picha kwenye mashamba mazuri ya chai, mashamba mazuri miti, Mufindi kule, Njombe, Mbeya pamoja na huko Rukwa pia. Lakini vilevile tuna Kimondo kiko Songwe, hivi vitu vyote vikiwekwa kwenye package moja ya Nyanda za Juu Kusini tutaweza kuendelea kukuza utalii wetu na kuendelea kuongeza mapato katika sekta hii ya utalii. Tuna beach nzuri, kuna mzungumzaji hapa wa kutoka Zanzibar alizungumza masuala ya fukwe, tuna beach nzuri kule ya Matema beach Nyanda za Juu Kusini. Lakini vilevile unazikuta beach hizi na kule Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wakati sasa Wizara iangalie namna bora ya kuendeleza na kukuza utalii Nyanda za Juu Kusini ili kuweza kuendeleza watalii zaidi, lakini vilevile kuongeza kipato katika sekta hii ya utalii. Tusing’ang’anie tu Kaskazini, Kaskazini inajulikana sana, tuangalie tuna fursa nyingine za Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine. Bado hayajafanyiwa kazi inavyotakiwa, yakifanyiwa kazi inavyotakiwa tuna vivutio vya kipekee sana ambavyo vinaweza vikaongeza mapato ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukienda kule Ruvuma Jimbo la Mheshimiwa Jenista kuna mapitio yale ya Wakatoliki na Makanisa makubwa ambayo yamejengwa zamani, tukiweka vizuri wale wakoloni, Wajerumani ambao walijenga yale makanisa watavutiwa kuja kuona. Nafikiri kuna umuhimu sana wa Wizara kuangalia…
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nataka kumuongezea taarifa Mheshimiwa Neema kwamba kule Nyanda za Juu Kusini, lakini kwenye Jimbo la Momba tunayo pia maporomoko ambayo yako kwenye Kijiji cha Mfuto na Yala, kwa hiyo pia na yenyewe tunaomba Wizara ya Maliasili yaweze kuyatambua ili yaendelee kuongeza watalii.
NAIBU SPIKA: Haya, Mheshimiwa Neema, taarifa.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naipokea taarifa kwa mikono yote kwa sababu nayo itaingia kwenye package ya utalii wa Nyanda za Juu Kusini na kuweza kuinua utalii Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuzungumzia suala la migogoro katika hifadhi, game reserve na forest reserve ambazo zinazunguka ndani ya Mkoa wetu wa Njombe. Mpanga Kipengele upande wa Makete na upande wa Wanging’ombe kuna changamoto ya migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda upande wa Makete kuna Kijiji cha Ikovi, Kimani, Ibaga hivi vyote vina mgogoro katika game reserve hii ya Mpanga-Kipengere. Nilikuwa naiomba Wizara itafute namna ya kutatua mgogoro huu, umekuwa mgogoro wa miaka mingi sana, ifike namna sasa ijulikane game reserve mipaka yake iko wapi na vijiji viko wapi. Lakini vilevile, upande wa Wanging’ombe kule kuna vijiji kama vya Ruduga, Igando, Ihanja, Hanjawanu, Mpanga, Malangali, Wangamiko, Iyai na Mayele bado nako kuna shida ya migogoro ya mipaka kati ya vijiji na hiyo game reserve. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vil vile ukienda Mpanga-Kipengere Forest Reserve kuna vijiji vya Masage, Wangama, Ikanga na Kipengere yenyewe bado napo kuna changamoto ya migogoro hii ya mipaka ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Wizara hii Mheshimiwa Waziri unatoka Njombe ninamatumaini makubwa mgogoro huu utakwenda kuumaliza hivi punde. Vilevile Waziri wa Ardhi kipindi hicho akiwa Naibu Waziri nilishawahi kuzungumza hapa ndani ya Bunge, akaja kule Wanging’ombe, tatizo lililokuja alikuja mwenyewe, issue kama hizi Mheshimiwa Waziri wa Maliasili mnatakiwa mshirikiane na Waziri wa Ardhi, wote mkifika site kwa pamoja mkakubaliana mtaweza kumaliza matatizo haya, lakini mmoja akienda mwingine akienda siku nyingine hamuwezi kufikia muafaka. Kwa sababu, kila mtu atakuwa anaangalia upande wake ni vizuri mkafanya kazi kwa kushirikiana, ili kuweza kumaliza matatizo haya ya hifadhi na vijiji vinavyozunguka hifadhi na mapori ya akiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Hifadhi ya Kitulo pia bado kuna changamoto hiyo kuna changamoto kubwa sana maana yake Hifadhi ile ya Kitulo ilianzishwa mwaka 2005 lakini migogoro ikaanza mwaka 2019 mpaka mwaka 2020; sababu ya migogoro hiyo ni kwa sababu waliweka beacon mpya kwa mara ya pili. Kwa hiyo, kuna vijiji kama cha Misilo, Lugoda, Igenge… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Neema kwa mchango mzuri.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)