Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kipekee namshukuru Mungu sana kutuweka hapa kwenye nchi hii yenye amani tukizungumzia maendeleo ya nchi yetu. Nimpongeze sana Waziri Dkt. Pindi Chana - Balozi na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Mary Masanja, Katibu Mkuu Francis na Naibu Katibu Mkuu wake pamoja na timu yote ya Maliasili na Utalii wakiwepo TANAPA, TAWA, NCAA, TFS na NMT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumzia Wizara ambayo ni muhimu sana, lakini pia inaungana na Wizara nyingi sana katika kutekeleza mambo yake, lakini imempendeza Mungu leo tunazungumza bila barakoa. Natala niseme wazi ule ugonjwa wa Covid-19 uliathiri sana Wizara hii kuliko kwingine kote na ndio maana waliishia sana wote wanaohusika na Wizara hii ya Maliasili walikwenda katika hali ngumu sana. Haijatangazwa rasmi kwamba umeisha, lakini angalau wameanza kuja watalii, lakini wamekuja watalii hao katika kipindi ambacho sasa tumeshapokea ile shilingi trilioni 1.3 ya kurekebisha mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nikwambie Maliasili na Utalii walipokea asilimia 6.9 ya hela hizo ambayo ilikuwa ni shilingi bilioni 90.2 na wamezifanyia kazi vizuri, japo bado hawajamaliza, nilikuwa nawaomba sasa zitumike kwa kasi zaidi kwa sababu muda umeisha. Miezi sita ambayo aliizungumzia Mheshimiwa Rais ndio inaishia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zimetumika vizuri na sina muda wa kutaja maeneo yote yaliyoguswa, lakini nitake tu kusema mimi kama nilivyosimama hapa nilitaraji elimu ifanyike zaidi kwa maeneo yote nchi nzima ambayo inagusa Wizara hii ya Maliasili na Utalii ili wote na sisi tuweze kuizungumzia kama Kiti kilivyoelekeza leo. Nataka niseme wazi haikugusa wanawake wa Kilimanjaro ili waweze kusemea vizuri na kwa nini Kilimanjaro? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuung’oa ule Mlima Kilimanjaro ukaupeleka kwingine, huo ni mlima ambao unaitangaza na ni kilele kirefu kuliko vyote Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba na ninamuomba sana Mheshimiwa Balozi Pindi Chana atakaposimama aeleze kwenye elimu wanawake wa maeneo yote yenye maeneo ya utalii nchi hii kuanzia Kaskazini mpaka Kusini, Mashariki na Magharibi wamenifaikaje na ile hela ya UVIKO katika kuelimika kuendeleza utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumzia Wizara ya Maliasili na Utalii huwezi kuiacha Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambako ndio huko kuna hizo barabara za TARURA. Huwezi kuacha afya ambako ndio huko wakija watalii wanataka maeneo mazuri ya kutibiwa. Huwezi kuacha Wizara ya miundombinu ambako ndio viwanja vya ndege viko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani inagusa Wizara nyingi mno, sasa nilikuwa naomba Wizara zote hizo tajwa na nyingine ambazo sikuzitaja wakae pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii waone kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza utalii duniani kwa kuwa guide sisi tunaipokeaje? Ametangaza na ninajua, kama inavyosema kwenye Ilani ya mwaka 2025 tutakuwa tumeshapokea watalii milioni tano, mimi nahisi watazidi, lakini tumejiandaa vipi sasa katika kupokea hao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani, Uhamiaji, wamekaa vipi na wamesaidika vipi kutoka Maliasili kuona kwamba wakifika sasa wanaingia moja kwa moja? Vibali vya kazi ambavyo labda watakuja na ma-expatriate wao wachache wanapewa bila vikwazo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais sio ya kupuuzwa kabisa, sisi wenyewe wanawke wa Kilimanjaro tunamuomba mama aje Disemba kwetu. Disemba atakapokuwa na likizo yake ikimpendeza tunamsubiri kwa hamu tumpandishe pale juu ya Mlima Kilimanjaro, alikuja kama guide wakafika pale chini akafanya aliyofanya katika utaalamu wake, lakini sisi tunataka tukamwambie jambo letu la kumpongeza na mengineyo mengi. Tuna hamu kubwa ya kuja kumpongeza, lakini wanawake wote Tanzania kila aliyesimama hapa, wake kwa waume wamempongeza mama sana na mimi naungana nao. Na siwezi kurudia mambo yote aliyoyafanya ikiwa ni pamoja na hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili la Wizara hii nimeona nizungumzie tu utalii, nikianza kurukaruka mambo ya fukwe, ningetamani kuona fukwe zetu zinafanana na Malindi, wanakuja kwa wingi, lakini mpaka leo hata pale Dar es Salaam, bado. Ni maeneo mengi mno ambayo tunatakiwa tuyaendeleze.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuzungumzia utalii na kutangaza utalii yamefanyika kwenye balozi zetu. Ukitamka mambo ya nje, balozi zetu zote zilizo nje ya nchi zinatangaza utalii, lakini wakija tunafanya nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata watu wenyewe wanaokuja wanataka vitu organic na sio lazima tufanye tena vile vitu vya kuweka dawa nyingi, nini, wanataka kuondoka wakiwa wametangaza vyakula, wametangaza kahawa nzuri, wametangaza mavazi yetu. Kila mtalii anayeondoka awe anaondoka na rubega shingoni, amemuona Mmasai kava ana yeye anataka kuondokanayo. Nilikuwa naomba Wizara hii ya Maliasili na utalii itoe zaidi kipaumbele kuhakikisha wananchi wote sasa wanaweza kuwasikiliza na kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mwanachama wa Kilimanjaro Animal Crew, nilikuwa naomba kuanzia wanafunzi wa shule wapende wanyama. Ni kweli, wanyama ni hatari, lakini kuna wanyama wadogo, hata paka ni mnyama, hata nyani ni mnyama, hawana madhara, hata nyoka ni mnyama. Sasa usiniulize utampendaje nyoka, wewe ukimuona nyoka kama hajakung’ata wewe unamuua wa nini? Muache nyoka apite. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndio hiyo kupenda wanyama. Inatakiwa uwaache na wenyewe waishi kwa sababu Mungu aliumba na alipoumba aliwaumba hao. Wewe usimtafute uadui, hata sisimizi usimuuwe kama hajakung’ata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba shuleni waanzishe clubs hizo za kuendeleza utalii wetu ili wakuenalo. Ukienda Denmark na kama hujafika Denmark unaanza kusikia pale kwenye embassy yao aah, have you heard the story of Hans Christian Andersen? Wanakueleza, mimi siku hizo nilikuwa nasafiri kwenda nikasema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Shally, mchango mzuri.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono, ahsante sana. (Makofi)