Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nikushukuru sana wewe, lakini pia tumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kibali cha pekee cha kutufanya leo tuendelee kukutana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha kwanza niendelee kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi ya pekee hasa tukio la jana ambalo mimi naona limevunja rekodi kwa mara ya kwanza kuweza kukutana na Makatibu Mahsusi, ni mwanamke ambaye anajua uhitaji wa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niendelee kumshukuru sana Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana pamoja na dada yangu Naibu Waziri Mary Masanja na Katibu Mkuu Dkt. Francis Michael kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika nchi hii wanamsaidia ipasavyo Mheshimiwa Rais, wanaisaidia na wanaitendea haki Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijikite kwenye mada hasa kwenye maslahi ya hawa ndugu zetu wa maliasili, hawa Jeshi la wenzetu Jeshi la Maliasili, Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori, hawa watu ningemuomba Mheshimiwa Waziri waangaliwe sana ni askari ambao iwe mvua ya kwao, liwe jua la kwao, wanyama wakali porini ni wa kwao, majangili ni wa kwao. Kwa hiyo, ningeomba Serikali iwaangalie kwa mapana sana hasa suala la marupurupu na namna gani ya kuweza kukaa nao karibu, wanafanyakazi ngumu sana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naangalia kwenye taarifa kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri eneo la uhifadhi lipo zaidi ya kilometa 307,800 ni zaidi ya asilimia 32 ya eneo la nchi lakini wanaolinda na kuzungukia hili eneo ni maaskari wa uhifadhi. (Makofi)

Kwa hiyo, ningemuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na mambo mengine mazuri wanayoyafanya hawa watu lazima waangaliwe sana kwenye suala la marupurupu. Ninajua sana hata watakapoangaliwa suala la marupurupu hawa ni askari ambao wanalinda rasilimali za nchi. Kwa hiyo, mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri hili liangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri nilikuwa na suala la watu wa TFS sijajua hawa watu wanaochoma mkaa wanakosea wapi. Ukiona mwananchi amepakia gunia lake la mkaa anasafirisha kwenda kuuza, ukifuatilia wakati mwingine, aidha, ana mgonjwa au mke wake anaumwa au kafanyiwa operation hospitalini. Anataka akatafute fedha ya dharura aidha ya kwenda kulipia matitabu au kwenda kumkomboa mke wake hospitalini aweze kurudi nyumbani. (Makofi)

Kwa hiyo, ningeomba anakutana na wenzetu hawa maaskari ambao ni watanzania wenzetu anakamatwa ananyang’anywa hata baiskeli ananyang’anywa hata gunia lake la mkaa na ametembea labda kilometa 20, anarudi kwa mguu. Ningeomba wizara iangalie utaratibu rafiki wa kuweza kuwaelimisha hawa watu, wawaelimishe hawa watu namna nzuri ya kuvuna mkaa wao. Wakati mwingine hata hajakata mti, amechimba mizizi kule kwenye shamba lake, akaikausha vizuri ili angalau aweze kuhudumia. Aidha, ameondoka kabisa nyumbani, ameacha hakuna hata unga hamna hata chakula angalau akauze gunia lake la mkaa au debe lake la mkaa aweze kurudi na unga, aweze kurudi angalau na mahindi kwa ajili ya kuhudumia watoto wake lakini madhara yake anakumbana na hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningeomba tuwabadilishe wenzetu askari hasa TFS wawe angalau na muda wa kuwapa elimu hawa watu tusiendelee ku-copy toka zamani, mimi nikiangalia hata asilimia kubwa ya Wabunge humu tunatumia mkaa huwezi kula tu na hata huyu aliyeenda kumkamata nyumbani kaacha gunia la mkaa, ugali aliokula umepikwa kutumia mkaa, sasa inakuwaje tena anageuka kuwa mwiba kwa wenzetu hawa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Ni kweli.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ningeomba sasa huyu mwenye gunia moja hawezi kwenda Wilayani akatafute kibali. Mfano, nikiongelea Jimbo la Ushetu kutoka kule ukapate kibali zaidi ya kilometa 40 aende akatafute kibali cha gunia moja halafu arudi kwa ajili ya kusafirisha, huku ana tatizo nyumbani, huku hana chakula, mimi ningeomba wenzetu wa TFS wajikite kwenye kutoa elimu, lakini wajikite kwenye kuwafundisha hawa vijana waweze kuwa na mashamba yao ya miti kwa ajili ya kwamba sasa pandeni miti yetu hapa na utaratibu unakuwa ni bora zaidi kuliko wanavyofanya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niongelee eneo la Ushetu, tuna mgogoro ambao naona umedumu kwa muda mrefu, mgogoro wa pori letu la halmashauri, Usungwa Forest Reserve pamoja na Kigozi – Muyoyozi ambao toka tarehe 31 Disemba, 2019 kuna timu ilikuja kwa ajili ya kutatua huu mgogoro, lakini haikutoka na matokeo wala haikutoa jibu na mbaya zaidi haikukutana na Madiwani wala Mwenyekiti wa Halmashauri hata Mkurugenzi wa Halmashauri haikukutana naye.

Mheshimiwa Spika, mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha aje anisaidie ni lini tutaenda kushughulikia mgogoro wa wananchi hawa wa Ushetu ambao wanaoteseka hasa wananchi waliopo katika Kata ya Nyankende, Kata ya Ulewe, Kata ya Idahina, Kata ya Ulowa, Kata ya Ubagwe na Kata ya Sabasabini ni maeneo ambayo wananchi wake wanateseka na mgogoro huu ambao umedumu kwa muda mrefu. Niombe sana ndugu zangu waziri kwa sababu uwezo wako wa kazi ni mkubwa, tuje tukashughulikie huu mgogoro ili tuuondoe kati ya Usungwa Forest Reserve ambayo ilikuwa ni bonde la Halmashauri ya Ushetu lenye GN number 442 ya mwaka 1959 lakini kwenye mgao wa mwaka 2020 wakati Kigozi inapanda kuwa TANAPA ukaingizwa huko sasa ni mgogoro ambao unawatesa sana wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningekuomba Mheshimiwa Waziri kwasababu uwezo wako wa kazi ni mzuri na Naibu Waziri na Katibu Mkuu mje sasa mtuambie ni lini tutaambatana pamoja kwenda kukaa na wananchi na wazee wa eneo hili maeneo yote haya ambao ni wazaliwa wa eneo hili ili tuone namna gani tunatatua. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Sawa.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, lingine nilikuwa nashauri ndugu zangu wa maliasili, tunajua tunachangamoto nyingi, lakini kubwa sana ninawaomba Mheshimiwa Waziri fanya ziara kwenye maeneo haya ukifanya ziara kwenye maeneo haya kutana na wazee, kutana na Madiwani kwenye haya maeneo yote ya migogoro watakusaidia sana nakumbuka hata hawa mawaziri wanane ambao waliteuliwa kwa ajili ya kuzungukia kutatua hii migogoro hawajawahi kukanyaga Ushetu, hatujawahi kuona Ushetu wanakuja kututatulia hii migogoro. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba ndugu zangu mnapokuja kushughulikia hii migogoro mje na Ushetu mkutane na Madiwani na maeneo mengine mkikutana mkakaa na Madiwani, Madiwani wa maeneo husika na Wenyeviti wa Vitongoji wana mambo mengi ambayo wanaweza wakawaelezea na namna nzuri ya kuweza kusimamia sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja unisaidie sana ili wananchi wangu wasiendelee kuteseka na suala la mkaa tuje na utaratibu mzuri ambao tutawasaidia wananchi wetu namna nzuri ya kuboresha na namna nzuri ambayo itafanya sasa wawe wapandaji wazuri wa miti na kujenga uoto mzuri wa asili wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye nchi hii. Ninajua kila Mbunge kwenye eneo lake barabara zinajengwa, hospitali zinajengwa, kila kitu kinafanyika. Mheshimiwa Rais anafanya kazi, hata kwenye gharama ya mafuta katoa shilingi bilioni 100. shilingi bilioni 100 ukiziweka humu tunaweza tukakosa hata mahali pa kukanyaga. Mama anaupiga mwingi, kwa kweli tumshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)