Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Wizara hii ya Maliasili. Nina vipengele vitatu, pongezi, malalamiko na hatimaye ushauri kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa heshima kubwa kabla sijaanza kuchangia naomba niamini kwamba mimi ni Mkristo, ni-quote kifungu cha Biblia, Kitabu cha Mwanzo, mstari wa 24 hadi wa 30 kinasema hivi na naomba Maliasili mnisikilize; “Mungu akasema, nchi na ijae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitaambacho na wanyama wa mwituni kwa jinsi zake, ikawa hivyo. Mungu akamfanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake na kila kitu kitaambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, Mungu akaona kuwa ni vyema. Mungu akasema, na tumfanye mtu kwa mfano wake, kwa sura yake, wakatawale samaki...,” naomba mnielewe, huyo mtu aliyeumbwa huyo, akatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na wanyama wote wa nchi yote pia na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi, huyo mwanadamu akavitawale. (Makofi)

“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke. Mungu akawabariki wote, akawaambia zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha, mkawatawale samaki wa baharini, mkawatawale ndege wa angani na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi mkakitawale.” (Makofi)

“Mungu akasema tazama nimewapa kila mche utoao mbegu anampa binadamu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia na kila mti ambao matunda yake yana mbegu vitakuwa ndivyo chakula chenu. Mungu akasema na chakula cha kila mnyama wa nchi na kila ndege wa angani na cha kila kitu kitambaacho juu yake chenye uhai, majani ya miche yote ndiyo chakula chenu ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu ni chema alichokifanya, ikawa asubuhi, ikawa usiku, siku ya sita.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeyasema haya nikiwa na maana kwamba yawezekana miaka hii ambayo nimekaa Bungeni huu mwaka wa kumi na mbili sijawahi kuona kabisa Wizara ya Maliasili na Utalii ikileta sheria za kubadilisha kwa haya mambo tunayoyasema, kwa sababu kila siku ni manung’uniko ya Wabunge. Wenyeviti wa Vijiji wanalalamika, watu wanauliwa na mamba na tembo na simba, lakini no reaction na fidia yenyewe ni ndogo sana, hakuna hata sheria yakuja kubadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye fidia hapa, nilikuwa naandika hapa, mtu aliyejeruhiwa na tembo analipwa shilingi 200,000 majeruhi wa kawaida, lakini aliyejeruhiwa jeraha la kudumu yaani maana yake amekatwa mkono, amekatwa mguu yaani hajafa analipwa shilingi 500,000 maskini ya Mungu; toka mwaka 1980 sheria haijabadilika. Mtu aliyekufa anapewa shilingi milioni moja basi na inawezekana wengine hata wazazi walishafariki hata hii milioni moja hatujawahi kuiona.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Maghembe amesema hajawahi kunipa, Mheshimiwa Kigangwalla amesema hajawahi kunipa, huyu Bwana Ndumbaro hajawahi kunipa, Mheshimiwa Pindi Chana naye miezi mingapi sijui kama atanipa. Lakini ninachotaka kusema ni nini? Wizara ya Maliasili tufumue sheria zote. Wizara ya Maliasili tutawaonea bure hata wale maafisa kwa sababu ni sheria zimekuwa za hovyo hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka ya 1980 wakati sheria zinaundwa hizi za maliasili, vijiji sasa hivi vimepanuka. Ukienda pale Mkwajuni makao makuu ya Wilaya ya Songwe kilikuwa ni kijiji na vitongoji viwili, leo ndiyo makao makuu ya Wilaya na ndiyo mji mkubwa wa Mkwajuni. Ukitembea mita 500 wanakwambia hii ni TFS, ukitembea upande mwingine mita 200 huwezi kukusanya kuni, huwezi kuvuna mkaa yaani ni shida tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mkwajuni, mdogo wangu Shaibati anafanya kazi nzuri pale, haki ya Mungu tena bila yeye sijui mimi ingekuwaje, kwa sababu anaunganisha watu, wanakwenda wanaomba hata TFS angalau wakatiwe kaeneo kadogo wanatafuta kuni, lakini imeshindikana. Nao TFS wanakuja na sheria.

Sasa jamani ndio maana nimesoma hata neno la Mungu hapo; Mungu amemuumba binadamu akaitawale dunia, akaitawale na nchi na vitu vyote vilivyoumbwa tuvitawale sisi. Leo hii eneo la mapori tengefu Tanzania nzima yako maeneo 26. (Makofi)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mulugo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nani huyo tena?

T A A R I F A

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, kataarifa kadogo tu kwa ajili ya kizuri unachozungumza Mheshimiwa Mbunge. Hata Nusu Maili iliyokuwa imewekwa kwenye hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na mkoloni toka mwaka 1923 hawa wameiua. (Makofi)

SPIKA: Haya; Mheshimiwa Mulugo, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, lakini Wabunge hebu mniache niongee vitu vya maana, leo nalihutubia Taifa hapa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe hii elimu, nimesema eneo la mapori tengefu Tanzania idadi ni maeneo 26 yanatawaliwa na TAWA; Mapori ya Akiba Tanzania yako 27 yako chini ya TAWA; Mapori ya Hifadhi ya TANAPA ni maeneo 22; Mapori ya Hifadhi ya Misitu (TFS) yako 419. Nchi yetu ni eneo kubwa sana square kilometer 946,000. Lakini square meter 307,800 zote ni maeneo ya hifadhi, asilimia 32.5 ni maeneo ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Mungu amesema nendeni mkazae, mkaongezeke, tunaongezeka kila siku. Mwaka 1970 anaosema Mheshimiwa pale mwaka 1980, mwaka 1990, 2000, 2010, 2020 vizazi na vizazi vimeongezeka. Ninaposema Mkwajuni ilikuwa ni kijiji leo ni Wilaya, sasa wananchi waende wapi? yaani kule kwetu sisi maeneo yote ya Kapalala, maeneo ya Udinde, maeneo ya Gua, maeneo ya Kanga, maeneo ya Ngwala ni shida tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana ukienda kwa wachimbaji wadogo kila wakitaka kuziona dhahabu, wameziona nina dhahabu zile pale, TFS anakuja, anasema ondokeni, wanawafukuza, wanawapiga, ni shida tupu. Hii nchi jamani ni ya kwetu sisi, Mungu alituumba tuitawale. Hata neno la Mungu linasema, zaeni mkaongezeke, tutawale. Mama wa watu anakwenda kukusanya kuni, anafukuzwa, anakwenda kukusanya mkaa anafukuzwa. Sasa wakinamama ambao hawana umeme maskini ya Mungu, hata gesi hamna kwenye vitongoji. Mheshimiwa Waziri wa Umeme juzi ananiambia kwamba vitongoji tutaanza kupeleka umeme, lakini unaweza kushangaa ikachukua hata miaka 10, ni maneno tu tunayopewa kama sera. Lakini leo wananchi wanaishije jamani? Hali ni ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie Wabunge, toka tumeanza kuchangia hii Wizara, mimi ni mwanakamati pale, nani ameipongeza Wizara ya Maliasili hapa? Tunapongeza Royal Tour tu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kutuletea Royal Tour. Hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba labda hongereni, TAWA mmefanya hivi, TANAPA mmefanya hivi, TFS mmefanya hivi. Bila Royal Tour hapa hii Wizara haiwezi hata kupongezwa, ni hatari, ni malalamiko tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kila siku Wabunge wanalalamika, sasa kwa nini Serikali isichukue hatua? Ni kweli wale wanatumia sheria, sasa sheria ni sisi Wabunge tuzibadilishe, hali ni mbaya sana huko, maeneo ni yetu sisi wenyewe. Ukienda kuvuna mbao hupati kibali. Juzi Mkuu wa Mkoa kule kwetu ameenda kule Kapalala, ameenda kule Buha, maana yake sasa hivi wananchi wa Kapalala hawawezi kulima. Mheshimiwa Bashe ametupa mpaka na zile mbegu za korosho, hawawezi kulima kwa sababu hakuna maeneo ya kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Mkwajuni Mji umetapakaa, umeenea, huku wanaweka sekondari za kata, huku sijui wanajenga majengo ya Serikali, wanaingia kwenye hifadhi, jamani hii hali tuibadilishe. Ukienda kwenye tembo huko ndiyo nisiseme, Kata ya Buha, Kata ya Kapalala, tembo wanaua watu, tembo wanakanyaga watu, mazao ya wananchi, hapa nina list ya majina karibuni 84 ningeweza kuyasoma, nitakuandikia, nitakuletea. Watu 84 mazao hakuna na mwaka huu kuna njaa sana. Tembo ni nani? Tembo ni nani mpaka atuzidi sisi wakati Mungu ametupa kibali cha kuwatawala hawa wanyama? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mungu ametupa kibali cha kutawala wanyama. Tutawale na wanyama na kwenye maji kule. Ndugu zangu…

SPIKA: Sasa Mheshimiwa Mulugo umesema unalihutubia Taifa, lakini tuongozane vizuri hapa. Umetaja hapo watu 84, umeanza kwa kusema watu wanauawa, watu wanakanyagwa na tembo, mazao. Sijajua hao 84 wako kundi gani? Maana unasema na wewe una majina hapo.

Waheshimiwa Wabunge, lazima ukisema jambo humu ndani tuwe na uhakika nalo. Kwa hiyo, tutarejea kule kwa Mheshimiwa Waitara. Hebu tuweke vizuri kwenye hao watu 84 hapo.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ukiona mtu kama Mulugo anasema haya Bungeni nina ushahidi. Hii taarifa nimetoa kwenye Halmashauri ya Wilaya yangu ya Songwe kwamba kuna watu hapa wamekufa kwa mamba ni wengi. Nimekusanya taarifa za miaka mitano iliyopita. Nimekusanya taarifa za miaka mitano za watu walioharibiwa na tembo mazao yao. Kwa hiyo, kama ni hivyo nitakupa, wako watu 84 wameathirika na mamba pamoja na tembo. Kwa hiyo, ni kitu ambacho nina uhakika. (Makofi)

SPIKA: Sawa. Ngoja, ngoja twende vizuri, twende vizuri.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

SPIKA: Kwa sababu unao huo ushahidi na unasema Halmashauri yako ndiyo iliyoleta hizo taarifa.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, yes. Ndio, ndio.

SPIKA: Na wewe hizo taarifa Jumanne nitaomba nizipate.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nitakuletea, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ni masuala ya mipaka, hizi GN za hawa watu wa hifadhi, Maliasili. Kijiji cha Ngwala na Kijiji cha Buha hali ni mbaya, wakati Mheshimiwa Waziri anachangia hapa, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi namheshimu sana, alisimama akasema Tume ilikuja. Nasema kwa ushahidi nilionao, Tume ya Mawaziri haijawahi kufika Songwe kwenye vijiji vyangu vya migogoro. Mimi ndiyo Mbunge kule na kila nikifika wanasema hawajawahi kuona, hawajawahi kufika Ngwala, hawajawahi kufika Kapalala, hawajawahi kufika Udinde, hawajawahi kufika Mkwajuni, hawajawahi kufika Patamela, hawajawahi kufika Saza, hawajawahi kufika Ngwala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapana tusidangaye hapa, kama walienda maeneo mengine lakini siyo maeneo yetu wengine, ni migogoro mitupu. Jamani alisema Mheshimiwa Silaa siku ile pale, tunakwenda kwenye uchaguzi 2025, tupeni raha na sisi huko tukaseme vizuri kwa wananchi. Naomba taarifa ambazo Wabunge tunatoa ndani ya Bunge humu tunakuwa tumezikusanya kwenye vijiji, kwenye kata, kutoka kwa Madiwani, zinakuwa ni taarifa rasmi. Naomba Serikali itusikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda maeneo kama ya Guha pale, sasa watu walime nini sasa?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, muda wako umeisha. Sekunde 30 malizia.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo inasema tulime, lakini Wizara ya Maliasili tuvune mbao, tuvune na mkaa, maeneo hakuna.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba, ombi langu la mwisho tufumue Wizara ya Maliasili yote, tubadilishe sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)