Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia sisi wote kuwa na afya njema kuwepo hapa. Mimi ni balozi wa utalii, lakini mimi ni Mwenyekiti wa Caucus ya Bunge ya kusimamia ulinzi wa wanyamapori akiwemo tembo na wanyama wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile mimi ni mama mjusi, nalizungumzia suala la mjusi kwa miaka, lakini leo nitazungumzia sana suala la Selous. Nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana aliyoifanya ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni kote kwa kupitia Royal Tour na nilizungumza miaka nyuma Tanzania inahitaji kutangazwa na utangazaji wake wa namna hii, tunahitaji kutangaza katika mitandao mbalimbali ikiwemo hii aliyoifanya kwenda Marekani kuitangaza Royal Tour na kwa kweli dunia kwa ujumla wake umemtambua kama Tanzania ina vivutio vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania ina vivutio vingi na hasa ukiangalia katika kanda, kuna kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kule tunakwenda Katavi kuna Rukwa Lukwati hili ni eneo la wanyamapori ambao wanatokea Zambia kila mwaka wakija Tanzania wakifika mpaka katika mbuga za Katavi na kuendelea sehemu mbalimbali iwe Gombe na baadhi ya game reserve. Ni hasa Selous corridor hii corridor ni maalum Mwenyezi Mungu aliiumba ile corridor na corridor ile ni kwa ajili ya tembo, nyati, simba, mbwamwitu wale wanatoka katika hifadhi ya Nyasa wanavuka Mto Ruvuma kwa makundi kama ile ile kwa Serengeti Masai Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania tukubali tunahitaji uchumi, tunahitaji maendeleo, lakini tunahitaji wananchi wetu. Hawa wananchi wengine wasijiingize katika migogoro ya wanyamapori, mimi mwaka 2014 nilipewa nafasi ya kuzunguka na Wabunge na ndio maana nasema elimu kwa Wabunge inabidi iletwe hapa ndani watambue haki za wanyamapori na haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kuondoa migogoro ambayo inaitwa wildlife and human being conflict, tukifanya hivyo wanadamu wataacha kuziharibu njia za wanyamapori, ukitoka Nyasa unataka kuingia Namtumbo, binadamu wame- intervein njia za tembo, tembo anashindwa pakupita anaingia katika mashamba ya watu, hivyo anashindwa kuingia Selous mle ndani ya Selous binadamu amejiigiza mle ndani anafanya uwindaji haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe nilipewa fund na GIZ kuzunguka na waandishi wa habari, tumevumbua mambo mengi sana ya binadamu. Nilikuwa na mama Mary Masanja tukaenda Tendaguru wamevamia wafugaji wako ndani ya Tendaguru wanyama wote wanakimbia na wanapokimbia hawana mahali pa kwenda wanakwenda kwa binadamu. Nafikiri Mama Masanja ni shahidi, sasa akatoa tamko kuwa atakapokwenda tena wale watu watakuwa wameoondoka wote na alitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya wavamizi wote waliovamia katika eneo la Tendaguru waondolee nataka nipate majibu akitoka hapa je maagizo yale yametekelezeka?

Mheshimiwa Spika, leo unamkuta tembo anataka kutulia Tendaguru tena msitu mkubwa sana, lakini binadamu mle amekaa analima katika hifadhi ambayo imeshatunzwa iko chini ya TFS sasa unasema migogoro mingine ni binadamu anasababisha migogoro hiyo kwa ajili ya kupitia njia ya wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaizungumzia Selous ambayo ni mbuga ya kwanza katika Afrika, lakini ni mbunga ya pili duniani kwa ukubwa, na Selous inazunguka katika mikoa sita Mkoa wa kwanza naanza Morogoro, Iringa, Ruvuma, Pwani Lindi na Mtwara katika hiyo mbunga ndio inazunguka humo ndani kuna wanyama wa kutisha, lakini sasa nenda ndani ya Selous utaona ni vurugu tupu binadamu anavamia anachimba humo ndani, lakini maendeleo yote hayapelekwi Selous, maendeleo yanapelekwa Kaskazini tu.

Mheshimiwa Spika, sasa tujiulize kama huko hamkuangalii mtategemea migogoro haitakwisha? Nimesikiliza katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri humu ndani kote wamepanga fund lakini siioni fund ambayo itakweda Selous haipo, lakini jiulize kama mbuga kubwa kama hii inaachwa tunategemea kuna maendeleo makubwa ya kimkakati? Mikoa hii kwa mfano Mkoa wa Lindi, Ruvuma na Mtwara tuna mradi mkubwa wa LNG unakwenda katika miaka mitano kama mkipanga watalii na watu mbalimbali watakaotembelea Selous tulitegemea.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, tulitegemea itakuwa na miundombinu, lakini kama hamjatengeza miundombinu msitegemee mafanikio katika Selous.

SPIKA: Mheshimiwa Riziki Lulida kutoka kwa Mheshimiwa Zuberi Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi, nataka nimpe taarifa mama yangu anayechangia, kuna fedha zilitoka kwa ajili...

SPIKA: Ngoja, ngoja anaitwa Mheshimiwa Riziki Lulida.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, sawa Mama Lulida.

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nilitaka nimuongozee taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka, anaitwa Mheshimiwa Riziki Lulida.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Riziki Lulida. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nilitaka nimpe taarifa mchangiaji kwamba anavyosema ni sahihi kabisa kwamba kuna fedha zilitoka kwa ajili ya utalii Kusini zile fedha ziliishia Mikumi. Kwa hiyo kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Maliasili wao Kusini maana yao ni Mikumi na Iringa sio Lindi na Mtwara. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hizi taarifa hizi tunazozisema humu ndani hizi tuwe makini kidogo. Mheshimiwa Riziki Lulida.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, taarifa naipokea hizo fedha zilitolewa na World Bank kwa ajili ya maendeleo ya kutengeneza barabara katika maeneo mbalimbali katika mbuga zetu, lakini nililizungumza mwaka juzi kuwa Lindi na Mtwara hela zile hazikupelekwa hasa kwa Selous na hii naizungumzia kwa vile Jimbo la Liwale ndio tunategemea kupata barabara na kuna viwanja vya ndege, lakini hazikupangiwa bajeti hata kidogo katika maeneo hayo. Hivyo matokeo yake mtalii anavyotaka kwenda kuwinda Liwale inamuia vigumu sana kwa vile hakuna njia ya kupita kumfikisha Liwale na wala barabara ya kutoka Dar es Salaam au kutoka Nangulukuru kwenda Liwale inapitika kwa msimu, hivyo taarifa yake naipokea.

Mheshimiwa Spika, tunataka kuisaidia Serikali katika kuendeleza utalii ni lazima tuunganishe na private sector na hii itatusaidia katika maendeleo. Nataka nitoe mfano wa private sector ilivyosaidia sekta ya utalii, Bakhresa Group of Companies ameleta meli ambazo zinakwenda Zanzibar, amefungua mahoteli makubwa Zanzibar, matokeo yake ameliletea urahisi Zanzibar kwa ajili ya watalii kwa vile watapata mahali pa kukaa, usafiri wa uhakikia kwa kutumia boti mbalimbali za Zanzibar, tulitamani sisi mkishirikisha private sector katika masulala ya maendeleo ya utalii nina imani Visiwa vya Mafia nao wataibuka katika utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona mapato ya utalii yameingia kwa asilimia tano tu, lakini kama mtafungua maeneo mbalimbali kwa mfano Kanda ya Ziwa, mkaifungulia mawasiliano makubwa kati ya Burundi, Rwanda na maeneo ya Burigi tutapata utalii mkubwa mpaka Kigoma. Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Zambia - Tanzania mkifanya mashirikiano katika masuala ya utalii tutavuta katika masuala ya utalii. Lakini Mozambique - Tanzania tukiisimamia katika hilo suala tutafika mbali katika suala la maendeleo, lakini je, tuna mahoteli? Mahoteli maana yake leo tukitangaza tunategemea tupate na mahoteli ya kuwapokea wageni wetu, tunahitaji mawasiliano ya barabara na miundombinu, leo tunahitaji fund kubwa ili hii sekta iweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru watu wa TANAPA wanafanya kazi kubwa sana, siyo kazi ndogo kushindana na binadamu, binadamu anataka kumuwinda tembo ili amuue na tembo na yeye vilevile ni mnyama mwenye akili kuliko binadamu anakuwa hakubali vilevile kuuana. Hivyo hapa ni lazima tuungane nao watu wa TANAPA, watu wa Ngorongoro na watu wa TAWA hii kazi ni kubwa binadamu anategemea kufanya ujangili apate maslahi yake. Nina mfano hai sasa hivi ujangili umerudi tena, sasa tuseme vizuri kuwa hapa ni binadamu na wanyama wako katika mgongano. Serikali simamieni tunahitaji mapato makubwa na wananchi wapate faraja kwa kupitia sekta ya utalii. Tanzania tunategemea utalii kwa ajili ya wanyama watano; simba, tembo, nyati, chui na faru. Ivory Coast walikuwa na wanyama kama Tanzania kwa fujo za binadamu sasa hivi ni historia.

Naiomba Serikali yangu na wananchi kwa pamoja tushirikiane katika ulinzi huu, siyo ulinzi wa kuiachia peke yake Maliasili, ni jambo letu na maendeleo yetu, Mama anatangaza utalii na sisi tuwe wadau wa kusimamia utalii huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nasema ahsanteni sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)