Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nami nitumie fursa hii kukushukuru sana kwa kupata nafasi hii niweze kutoa mchango wangu kwenye sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nami niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na kazi nzuri sana ambayo ameifanya ya kuutangaza utalii wetu duniani kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo kwamba napingana na wenzangu, sisi watu wa Arusha ndiyo wanufaika wakuu wa utalii na ndiyo maana utaona leo watu wakizungumza kuhusiana na mateso ya tembo, sisi tunazungumza kuhusiana na ajira ambazo zinameongezeka kwenye mahoteli yetu, tunazungumza mapato ambayo yanapatikana kwenye nchi yetu, tunazungumza faida nyingi, tunazungumza mama ambaye analima mbogamboga anaweza akauza bidhaa zake kwenye hoteli, tunazungumza mfugaji kutoka Ngorongoro ambaye anafuga anaweza akauza maziwa kwenye mahoteli. Kwa hiyo, sisi watu wa Arusha tukiwaambia kwamba ni wanufaika wakubwa wa masuala ya utalii ni vizuri wakatuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kwenye upande wa usalama; tunauza bidhaa nyingi sana, tunauza wanyamapori, tunauza big five na vivutio vingine, lakini lazima tukubali kwamba component ya usalama ni component kubwa sana ndiyo maana sisi katika Jiji la Arusha kwa kushirikiana na Serikali katika ngazi ya Mkoa, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa usimamizi mzuri wa IGP Simon Sirro pamoja na RPC wa Arusha vimewezwa kujengwa vituo vya kisasa maalum kwa ajili ya kuwahudumia watalii. Tuna kituo kikubwa pale Central, tuna kituo pale Kikatiti kama unatoka airport, tuna kituo kule Engikaret kama unatoka Namanga kwa maana ya Kenya, tuna kituo Makuyuni na tuna kituo Karatu maalum kuhakikisha kwamba watalii hawasumbuliwi barabarani. Wanakuwa na kituo kimoja wanasimama, wanakaguliwa na maisha yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwenye hoja hii, tunawaomba wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii watusaidie kuwaunga mkono Jeshi la Polisi kwenye masuala ya usalama kwa sababu usalama ndiyo bidhaa namba moja kwenye utalii, kama hakuna usalama hakuna utalii. Wana shida ya magari kwa ajili ya patrol, tunataka wazungu/wageni wakija kwenye nchi yetu wanapokelewa kwa escort kuanzia airport wanapewa red carpet, wanakwenda kwenye mahoteli ili wakirudi wakaongee hadithi nzuri ya namna watu wa Tanzania tulivyo wakarimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini tunaomba pia Wizara ya Maliasili itusaidie, wenzetu wa TATO hawa wa masuala ya utalii, private sector, wao wamejenga kile kituo kilichopo pale Arumeru, wenzetu wa TATO wamejenga kituo kilichopo pale Central, wametoa gari brand new Land Cruiser na Wizara ya Maliasili kwa sababu wao ndiyo wanufaika wakuu watusaidie kwa kuwaunga mkono kwa kutusaidia hayo magari kwa ajili ya polisi, lakini pia na kuboresha na kituo kilichobaki cha Makuyuni na kile kituo cha Engikaret. Pia niwashukuru wenzetu wa CRDB kwa sababu wameahidi kutuchangia pikipiki kumi kwa ajili ya kuimarisha usalama na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwenye programu nzima ya Royal Tour. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo langu la tatu; kuna leseni ya biashara kwa ajili ya mountain guide. Kipindi kilichopita tulizungumza kuhusiana na tour guide, hawa tour operators ambao walikuwa hawana kampuni wana gari moja moja walikuwa wanalazimika kujichomeka kwenye makampuni mengine ili wafanye biashara. Serikali ikashauriwa ipunguze tozo ili iweze kuwashawishi watu wengi zaidi kuweza kujisajili na kufanya biashara, wakaweza kupunguza ile TAA license gharama yake kutoka kwenye dola 2,000 hadi kufika dola 500 mpaka ninavyoongea sasa hivi wale wafanyabiashara wadogo wadogo zaidi ya 270 wameweza kujiandikisha na Serikali inaweza kuwatambua, inaweza ikapata mapato na masuala yanaendelea. (Makofi)
Tunaomba pia kwenye jambo kama hilo tulifanye wale mountain guides ambao wanatakiwa walipe dola 2,000 kila mmoja. Hebu niambie mtu leo ametoka pale Mweka kusoma au ametoka chuo chochote cha utalii anataka kuanza kazi ya kupeleka wageni mlimani, anaambiwa bila kuwa na dola 2,000 ya leseni huwezi kuanza kazi, matokeo yake sasa wanatafuta wale wenye biashara za utalii wanawapa dola 10, 10 kwa kila mgeni ili wapate vocha na waweze kupeleka watu kwenye utalii. Ni vizuri Serikali ikaliangalie suala hilo, mkawapa nafasi, mkapunguza angalau kutoka mtu anayepandisha Mtalii mmoja mpaka 100 mkampa dola 500, wanaopandisha watalii 100 na kuendelea mkawapa dola 2,000 na kuendelea na mkifanya hivyo watakuwa wamewatambua wale watu wa wadogo, wameingiza kwenye mfumo rasmi, watafanya shughuli zao, lakini baadae pia itakuwa rahisi kuweza kulipa kodi pamoja na masuala mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna changamoto kwenye upande land base rent. Unajua kule Serengeti kuna tozo nyingi sana, kuna mtu analipa park fee, kuna ambao wanalipa concession fee, mtu akilala tu kwenye hoteli yoyote kwenye park kama siku kama ni high season dola 60, kama ni low season dola 50 bila VAT. Lakini bado hawa Maliasili wamekuja kuleta kitu kinaitwa land base rent. Sisi ushauri wetu kwa sababu ukileta hii tozo inaonekana kwa makadirio watapata dola milioni 3.2, ni bora wangeongeza fee kidogo angalau dola tano au dola 10 ili waweze kupata ile kodi na ni kodi ambayo italipwa na mgeni kutoka nje, haitalipwa na yule mwekezaji itaweza kupunguza changamoto na maisha pale yataweza kuendelea.
Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusiana na tozo mchanganyiko; ukienda kwenye ma-gate yetu, leo mtalii mfano kutoka Arusha akitaka kwenda Lake Natron anakutana na vijiji kama vitatu kila kijiji analipa dola 10, kingine dola 10, kingine dola 10, baadae anakwenda TAWA analipa dola 25. Sasa unashindwa kuelewa Serikali ni moja kwa nini kila mtu akusanye tozo kana kwamba Serikali hii haina usimamizi? Ni vizuri Serikali iratibu tozo zote, kama zinalipwa TAWA zilipwe TAWA, kama ni Halmashauri walipe Halmashauri, halafu wao ndani ya Serikali watagawana kidogo kidogo ili kuondoa usumbufu na siku hizi fedha zote zinaenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali sasa kuna haja gani ya kila mtu kulipa moja moja.
Mimi nilikuwa naomba Serikali yetu izungumze Lugha moja kwa maana ya TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Wizara ya Fedha wakae chini waje na utaratibu mmoja ili kuondoa usumbufu kwa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pale Arusha tuna eneo linaitwa Clock Tower; Clock Tower ndiyo center ya Afrika kati ya Cairo kule Misri na Cape Town kule Afrika ya Kusini. Pale Clock Tower tunaambiwa kwa sababu ni center sisi tunataka tuitumie kama kivuko…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Sekunde 30 malizia sentesi.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, tunataka tuitumie kama ni kivutio cha utalii. Tumeongea na Balozi wa India yuko tayari kushirikiana na Wizara ya Maliasili pamoja na Serikali ngazi ya Mkoa ili tutengeneze tower pale ambayo mwisho wa siku watalii wakija watafika pale, watapanda kwenye ile tower watalipa tozo, tutaitangaza Arusha yetu, wataangalia Mlima Meru ulioko jirani pale, mapato yatapatikana. (Makofi)