Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, mchango wangu ni kuhusu biashara ya viumbe pori hai, specifically inayohusisha wadudu wadogo yaani vipepeo, mijusi, jongoo, ndege na vinavyofanana na hivyo ifunguliwe.

Mheshimiwa Spika, biashara hii ilikuwa inafanyika kwa miaka kadhaa kabla ya kupigwa marufuku na kusitishwa tarehe 17 Machi, 2016 kwa agizo la Serikali. Watanzania waliokuwa wanashiriki biashara hii wameingia hasara kubwa na kurudishwa nyuma sana kiuchumi, na mfano halisi ni wananchi na wafanyabiashara waliokuwa wanashiriki biashara ya vipepeo jimboni kwetu Muheza, Mkoani Tanga.

Mheshimiwa Spika, ninazo hoja kadhaa za kwa nini Serikali inatakiwa kuirudisha biashara hii. Kwanza, miradi ya kufuga na kusafirisha vipepeo kibiashara haina madhara yoyote ya kimazingira, haipunguzi idadi ya vipepeo na kinyume chake inawaongeza. Kwa kawaida muda wa kuishi wa vipepeo ni majuma mawili na vipepeo hutaga mpaka mayai 400 na kwa njia zao za kawaida hutotoa mawili ama matatu tu, ila wakitotoleshwa kwa njia za kibinadamu zilizokuwa zikifanyika mayai yote hutoa vipepeo.

Pili, inasaidia sana kwenye uchumi wa wananchi mmoja mmoja. Wananchi wa vijiji vyetu walikuwa wana uwezo wa kupata mpaka shilingi milioni moja kwa mwezi ambazo ni fedha nyingi mno kwa mazingira yetu. Kwa kusitisha biashara ile, wananchi wetu wamerudi kwenye ufukara wa kabla haijaanza kufanyika na kwa vile wanaishi pembeni ya hifadhi tunahatarisha mno kwao kuvutiwa na kufanya shughuli za kihalifu kwa misitu yetu. Kwa hiyo, biashara ile ilikuwa inasaidia ulinzi pia kwa misitu yetu.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika biashara ile ilisaidia miradi ya kijamii yenye faida kubwa. Tuliweza kujenga madarasa kadhaa, miradi ya maji ya bomba na fedha taslimu zilizolipwa kwa Serikali za Vijiji. Yote hayo yamepotea kwa kusitishwa kwa biashara ile. Kwa kifupi ni kuwa zuio lile lilikosa macho kama lilivyokosa mashiko. Halina faida yoyote iwe ya kimazingira ama kiuchumi na ni wakati sasa wa Serikali kuliondoa. Serikali kama ilivyo kwa wananchi wa maeneno husika Wilayani Muheza, inapoteza fedha nyingi kwa kuendelea kuizuia. Serikali kuruhusu tena usafirishwaji wa vipepeo nje ya nchi kuna mantiki kubwa kwa ustawi wa wananchi wale na pato la Taifa pia kiujumla.

Kwa kuongezea, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jerry Silaa ambayo ilitembelea maeneo ya Tarafa ya Amani, Wilayani Muheza kunakofanyika ufugaji wa vipepeo iliishauri Serikali kuondoa zuio na kuifungulia biashara ile. Faida ni nyingi na hakuna hasara yoyote kwa kufanya hivyo.

Niiombe tena Serikali kupitia Bunge lako tukufu, iondoe zuio lile ili kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwanza kwenye nia yake ya kuwarahisishia maisha wananchi wa Tanzania, lakini pia kuendelea kuitangaza Tanzania kama alivyofanya kwenye filamu ya Royal Tour kwani vipepeo hawa wanakwenda kutumika kwenye maonesho ya vipepeo nje ya nchi na sifa za uzuri wao zinaipamba nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.