Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kwa kukushukuru kwa nafasi ya kuchangia kwa njia wa maandishi.
Pili, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya katika kukuza sekta ya utalii, tumeona kazi yake nzuri ya filamu ya Royal Tour.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie hoja nilizotumwa na wananchi wa Jimbo la Kwela kwenye Wizara hii muhimu. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, wewe na Naibu wako. Ni imani yangu na wananchi wa Jimbo la Kwela kuwa mtamsaidia vema Rais wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kupitia Bunge lako tukufu, niwasilishe kwako mgogoro wa muda mrefu sana kati ya wavuvi wa forodha ya Ilanga, Nankanga na Legeza dhidi ya mapori ya akiba ya Lwafi na Uwanda. Lakini pia Hifadhi ya Uwanda na Vijiji 16 vilivyopo kata ya Nankanga, Kapenta, Kipeta na Kilangawana.

Mheshimiwa Spika, utangulizi; Hifadhi ya Uwanda Game Reserve iliyoanzisha mwaka 1959 na wakoloni. Mwaka 1974 ilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali na ikawa chini ya Halmashauri hadi mwaka 2013 walikabidhiwa TAWA. Mwaka 2014 TAWA walianza kazi rasmi kwenye Pori la Akiba la Uwanda Game Reserve. Pori la Uwanda Game Reserve linazungukwa na vijiji 16 na wakazi zaidi ya 50,000 wa vijiji hivyo ni wakulima, wafugaji na wavuvi.

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Uwanda Game Reserve wakati inaanzishwa eneo hilo lilikuwa ardhi kavu na baadae kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, maji ya Ziwa Rukwa yaliingia na kuungana na nchi kavu na kuwa ziwa kwa asilimia 80 ambapo eneo hilo ni ziwa kwa sasa. Hivyo eneo la nchi kavu la pori limebaki asilimia 20 tu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mabadiliko hayo, Hifadhi ya Uwanda Game Reserve imebaki inatumia mipaka ile iliyowekwa na wakoloni haijabadilishwa hadi sasa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hali halisi kwa sasa; baada ya TAWA kukabidhiwa Hifadhi ya Uwanda Game Reserve wakulima, wafugaji na wavuvi wanaishi kwa manyanyaso makubwa kwa maslahi ya askari mmoja mmoja wa TAWA.

Mheshimiwa Spika, wavuvi wanaishi kwa shida na kupoteza mali zao na maisha yao. Kuanzia mwaka 2016 hadi 2021 wavuvi waliokufa wamefikia 40 na chanzo cha wavuvi hao kufa ni askari wa TAWA. Wapo waliojitosa majini kwa kuogopa kipigo kutoka kwa askari. Mvuvi anaona bora ajitose majini kuliko kukamatwa na askari. Pia wapo wavuvi waliokamatwa na waliopigwa sana na wengine kupata ulemavu wa kudumu. Wapo wavuvi waliopigwa risasi na kufa kwa sababu ya kunyang'anywa samaki wao walipojaribu kuzuia samaki wao wasinyang’anywe wakiwa hawana hata silaha yoyote.

Mheshimiwa Spika, kutokana na matukio ya kikatili kwa wavuvi kuna wengine walijeruhiwa na kuwa walemavu wa kudumu. Mfano mwaka 2020 Ndugu Jeko wa Kata ya Kilangawana alijeruhiwa na risasi mpaka leo ni mlemavu wa mkono na shingo. Wakati huo Ndugu Mwakilima alipigwa risasi mpaka kupoteza maisha na askari wa TAWA anayeitwa Manyama akiwa na askari mwenzake. Pamoja na tukio hilo kuripotiwa Kituo cha Polisi Laela bado hamna hatua zozote zilizochukuliwa na askari huyo yupo bado kazini. Kitendo hiki cha kinyama, kimeleta chuki kubwa sana kati ya wahifadhi na wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, kuanzishwa kwa vibali vya uvuvi; baada ya wavuvi wengi kufa na kuwapo kwa msuguano mkali kati ya wananchi na wahifadhi, TAWA walikuja na mpango wa vibali maalumu kwa kila mvuvi anayetaka kuingia kuvua ndani ya Ziwa Rukwa. Kuanzishwa kwa mfumo wa vibali vilivyotengenezwa na TAWA, badala kuwa suluhu ya tatizo, imekuwa sasa kama nyezo ya kumkomoa mvuvi. Kwa sababu mtindo wa kibali umeleta adha nyingi sana tena za kinyonyaji kama ifuatavyo: -

Kwanza, mvuvi anatakiwa awe na kibali toka TAWA kinachomruhusu kuingia ndani ya ziwa na kuvua kwa miezi sita wanalipa shilingi 15,000. Mvuvi anatakiwa awe analipa kibali cha ngalawa toka TAWA kinachomruhusu kuingia ndani ya ziwa na ngalawa na kuvua kwa miezi sita wanalipa shilingi 15,000.

Pili, mvuvi anatakiwa kulipa kila siku anapoingia ziwani kuvua shilingi 5,000; tatu, mvuvi anatakiwa kulipia ngalawa ya kuvulia kwa kila siku anapoingia ziwani shilingi 2,000; na nne, mvuvi anayetumia boti anatakiwa kulipia engine ya boti kila siku anapoingia ziwani kuvua shilingi 20,000 na boti yenyewe analipia shilingi 2,000.

Mheshimiwa Spika, tano, mnunuzi wa samaki hata kama ananunua samaki mmoja anatakiwa kulipa kila siku anpoingia ziwani kwenda kununua samaki analipa shilingi 4,000; na mwisho akina mama wachakataji kwa maana kuparua samaki nao wanalazimika kulipa kila siku anpoingia ziwani kufanya kibarua hicho analipa shilingi 4,000. Pamoja na ukweli kwamba kipato chao ni cha chini sana kwa kazi hiyo ambapo akipata kiasi kikubwa kwa siku ni shilingi 6,000 na mara nyingine wanaweza wasipate chochote kutokana na upatikanaji wa samaki siku hiyo.
Kwa hiyo, TAWA kwa kipindi cha miezi sita inatoza wastani wa shilingi 4,890,000 ambayo ni sawa na shilingi 815,000 kwa mwezi mmoja ambayo ni fedha nyingi sana kwa mvuvi wa hali ya chini. Wakati huo huo mvuvi ana tozo nyingine kwenye taasisi nyingine za Serikali ambazo anawajibika kulipa kama ifuatavyo; leseni ya mvuvi ya Halmashauri analipa kwa mwaka shilingi 20,000; leseni ya ngalawa ya Halmashauri analipa kwa mwaka shilingi 20,000; na leseni ya TASAC mvuvi analipia ngalawa kwa mwaka shilingi 50,000.

Mheshimiwa Spika, kutokana na tozo kuwa nyingi tena kandamizi kwa wavuvi wamelalamika sana kwenye uongozi wa Uwanda Game Reserve, lakini majibu yao kwamba wao hawana mamlaka yoyote isipokuwa Waziri mwenye dhamana na Wizara hii ya Maliasili na Utalii japo nao wanakiri kuwa tozo hizo ni nyingi mno na kandamizi sana kwa wavuvi ila zipo juu ya uwezo wao.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo yangu kwanza Uwanda Game Reserve ambayo kwa sasa ni ziwa kwa asilimia 80, tunaomba eneo la hifadhi kwenye ziwa liwe mita 500 kama ilivyo kwenye hifadhi zingine zinazopakana na ziwa.

Pili, kipindi tunasubiri kurekebisha kwa mipaka ya hifadhi kama Serikali itaridhia; tozo zile za kila siku kwa mvuvi kuingia ziwani kuvua zipunguzwe walau ziwe hata shilingi 500 na tozo ya ngalawa nayo iwe shilingi 500 kwa kila siku ambapo kwa mwezi mvuvi atalipa jumla ya shilingi 30,000. Hapo tutakuwa tumemsaidia mvuvi kujikwamua kutoka kwenye umaskini. Kwani ilivyo sasa ni kama kumkomoa mvuvi.
Tatu, kipindi tunasubiri kurekebishwa kwa mipaka ya hifadhi kama Serikali itaridhia; tozo zile za kila siku kwa wanunuzi na akina mama wachakataji wa samaki kuingia ziwani kufanya shughuli zao zipunguzwe walau ziwe hata shilingi 500 kwa siku.

Nne, tozo za miezi sita kwa mvuvi kuingia ziwani kuvua zenyewe zibaki; tano, kipindi tunasubiri kurekebisha kwa mipaka ya hifadhi kama Serikali itaridhia hasa kwa wavuvi; tunaomba alama ya mipaka iweke ili kuepusha migongano kati ya wahifadhi na wavuvi na sita, kwenye forodha ya Ilanga Muze inayopakana na Hifadhi ya Lwafi, ziwekwe upya alama zilizoonesha maeneo ya kuvua kulingana na makubaliano ya awali kati ya wavuvi na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Mlele Mpimbwe kabla ya TAWA kuja kwani utaratibu wa mwanzo ulikua mzuri.

Mheshimiwa Spika, kutokana na malalamiko haya kujirudia mara nyingi na wavuvi kuathiriwa sana tunaomba zoezi la kuwakamata wavuvi wakiwa ziwani kusubiri mpaka hapo alama za utambuzi zitakapowekwa. Kwani wavuvi wanashindwa kujua mipaka ya eneo la hifadhi na eneo lisilo hifadhi. Wavuvi waliahidiwa kwa muda mrefu kuwekewa alama mpaka sasa hamna kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, wavuvi wanaokamatwa hasa kwenye forodha ya Ilanga iliyopo Halmashauri ya Sumbawanga, wasipelekwe Halmashaurui ya Mlele Mkoa wa Katavi kwani ni mbali sana. Hii inapelekea wao kukosa haki zao kwa sababu wanakuwa hawana hata mtu wa kuwadhamini na inapokuwa kesi imeenda mahakamani inakuwa shida kupata dhamana.

Mheshimiwa Spika, tunaomba kuwepo na vikao au mkutano ya pamoja kati ya askari wako wanapoingia ili kuweka mahusiano mazuri kati ya wavuvi na askari wanyama pori. Pia tunaomba jambo lolote linalowahusu wavuvi au taarifa yoyote ile ya wavuvi itolewe kupitia vyama vyao, Wenyeviti wa Makambini siyo mtu binafsi ili kuondoa makanganyiko na habari za uzushi kusambaa.

Kuhusu taarifa ya Mawaziri Wanane wanaotatua migogoro itoke mapema ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao. Kwani kwenye Jimbo langu la Kwela tuna vijiji 16 wenye mgogoro na hifadhi ya Uwanda na mwaka huu ndio hali ni mbaya kabisa, wananchi wameshindwa hata kufanya shughuli za kilimo kutokana na mgogoro huo, kwani walizuiliwa na wahifadhi kulima hata maeneo ambayo wamekuwa wanalima miaka ya yote ya nyuma. Sababu ya wahifadhi kwa wananchi ni kwamba wasubiri ripoti ya Mawaziri Wanane ambayo waliahidiwa ingetoka mwaka jana mwezi wa nane, lakini mpaka leo kimya.

Mheshimiwa Spika, kama itakupendeza Mheshimiwa Waziri upange ziara uje kujionea mwenyewe hali halisi juu ya mgogoro huu ulioathiri wakulima, wavuvi na wafugaji kwa kipindi kirefu sana. Kwa mfano ndani ya Jimbo langu la Kwela zaidi ya kata nane zipo kwenye mgogoro huu, hii ni hatari. Alikuja mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM Taifa na Naibu Waziri wako waliona hali ya malalamiko kwa wananchi yalivyokuwa makubwa.

Mheshimiwa Spika, wahifadhi waache kutumia nguvu kubwa kupita kiasi wanapokabiliana na wananchi hasa wavuvi, kwani vifo vilivyotokea na watu kupata ulemavu vimezidisha chuki kati wananchi na Serikali. Hatua kali zichukuliwe hasa kwa askari wanaofanya vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu, mfano yule anayetuhumiwa kufanya mauaji ya mvuvi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.