Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa kibali cha kuweza kujadili bajeti yetu ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika siku hii ya leo, lakini kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini nimpongeze sana kwa kuipa kipaumbele sekta hii ya maliasili na utalii ambapo hivi karibuni ameweza kuzindua filamu ya Royal Tour na kwa kiasi kikubwa na kiwango kikubwa ameweza kuhamasisha utalii wa ndani na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyoongea sasa ndani ya miei minne ya Januari mpaka Aprili tumekuwa na ongezeko la watalii wengi sana na kuanzia mwezi Mei mpaka Disemba hoteli nyingi hifadhini zimejaa kwa maana ya booking. Hivyo ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuipa kipaumbele sekta hii ya muhimu ambayo kiukweli sisi tukishindwa kutekeleza majukumu haya basi tulaumiwe sisi. (Makofi)
Kwa hiyo, tumhakikishie tu Mheshimiwa Rais kwamba tutaendelea kutangaza utalii, tutaendelea kuhabarisha habari njema za vivutio vyetu tulivyonavyo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo nichukue nafasi hii kwanza kuwashukuru Wabunge wote kwa michango yao mizuri sana na mingi imekuwa ni ya kutuelekeza, lakini pia kutuonesha namna ambavyo tunataka kwenda, tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara yetu hii ya Maliasili na Utalii ina changamoto nyingi sana na sisi tunatambua hilo na tumeyapokea mengi ambayo mmetuonesha njia na sisi tunawaahidi kwamba tutaenda kuyatekeleza na yale magumu ambayo tutaona yanatushinda sana basi tutashirikiana na ninyi kuhakikisha kwamba sekta ya utalii inapaa na zaidi tunamsaidia Mheshimiwa Rais kuendeleza sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema machache ili niunge hoja; kwanza kabisa nipende tu kusema kwamba jukumu la Wizara ya Maliasili na Utalii ni kulinda, kutunza, kuhifadhi, lakini pia na kuendeleza utalii. Sisi kama Wizara tumepewa jukumu hili la kuangalia maeneo yote yaliyohifadhiwa, tunayatunza, tunayalinda, tunayahifadhi, lakini yanapoleta kivutio kizuri basi tunahamasisha utalii ili watu waone maeneo haya kwamba tumeyatunza kwa namna gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo ndani ya maeneo haya tunatunza vyanzo vya maji, lakini tunatunza misitu, lakini tunadhibiti mabadiliko ya tabianchi, sambamba na hilo tunatunza mazingira. Sekta nyingi zinaitegemea sana sekta hii ya maliasili; nikianza na sekta ya nishati, bila kuwa na vyanzo vizuri vya maji hatuna umeme, kwa hiyo, uchumi wan chi unategemea sana katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ninapoenda kwenye misitu pia, misitu yetu tukiimaliza tukashindwa kuitunza vizuri hatutaweza kuishi. Tunasema misitu ni uhai, lakini sambamba na hilo tunapata maji kutoka kwenye maeneo yale kwa hiyo, ningependa kuliweka wazi hili tutambue kwamba tunapoyahifadhi haya maeneo tuna lengo zuri kabisa la kuhakikisha kwamba sisi tunaishi na Mungu aliyaweka haya maeneo ili yaweze kutufanya tuishi vizuri. Tunapata hewa nzuri kutoka kwenye maeneo haya. Wizara ya Muungano na Mazingira wanatutegemea sisi, tukisema leo maliasili tutelekeze haya maeneo hizi sekta nyingine zote haziwezi kuendelea. (Makofi)
Kwa hiyo, niendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge pamoja na kuwa na changamoto nyingi katika sekta hii, lakini bado tuone na upande wa pili wa umuhimu wa sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta hii unategemewa sana na sekta mbalimbali. Nikienda kwenye sekta ya mifugo, tunapoleta mtalii hapa ndani lazima mtalii atakula, nikisema uvuvi atakula samaki, nikienda kwenye usafirishaji pia tutasafirisha abiria, nikienda kwenye kilimo pia tutauza mazao yetu kwa huyu mtalii anayekuja, lakini tutauza maji, lakini kwa wakati huohuo sekta hii inatuletea watalii wengi ambao wanatuongezea uchumi wetu katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitaenda moja kwa moja kwenye eneo la migogoro ya mipaka; sekta hii ni kweli tumekuwa na changamoto nyingi sana za mipaka, migongano kati ya hifadhi na wananchi na inaleta hatari kubwa na pengine wananchi wanapoteza maisha.
Kwanza nitoe pole sana kwa wananchi ambao wanakumbana na kadhia hii, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Rais alianzisha Kamati ya Mawaziri Nane na sambamba na hilo tumeendelea kuhabarisha umma, pale ambapo kuna migogoro mipya wailete tuitatue na changamoto hizi tumeshaanza kuzipokea na Serikali ya Awamu ya Sita imeweza kuachia vijiji 920 ambavyo vilikuwa ndani ya hifadhi, lakini kwa huruma ya Mheshimiwa Rais amevirudisha kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo migogoro mipya bado tunaipitia ili tuhakikishe kwamba mwananchi kwanza, hifadhi tunaiangalia baadae. (Makofi)
Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba ndio maana kuna Kamati hii ambayo inazunguka nchi nzima, lengo ni kutokuwepo na taharuki kwa wananchi. Na haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais na tunayatekelea kwa sababu alisema sitaki kusikia taharuki yoyote. (Makofi)
Niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, tunaenda kutatua matatizo haya kwa mashirikiano baina ya wananchi na wahifadhi, ili kuleta amani nzuri na wahifadhi wawe na amani ya kuyasimamia yale maeneo ambayo yatakuwa yameachiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuendelee kuipongeza Serikali na tuendelee kuwa-support Maliasili na Utalii ili tuweze kufikia mahali ambapo jamii zitambue uhifadhi ni sehemu ya maisha yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitapenda pia niongelee eneo la tozo. Waheshimiwa Wabunge baadhi wameongelea kuhusu tozo; ni kweli sisi tuna tozo, lakini tunaangalia hizi tozo tukijilinganisha na washindani wenzetu. Tuna washindani wa nchi jirani ambao tunapopanga hizi tozo tunaangalia na wenzetu wana tozo za aina gani.
Mheshimiwa Spika, mfano nitapenda kuongelea katika hifadhi zetu nne ambazo mwaka jana tulipandisha kiwango cha kiingilio kutoka dola 60 kwenda dola 70, tuliongeza dola 10. Ukilinganisha na washindani wetu mpaka sasa nikisema hata Masai Mara sisi tunapotoza Serengeti kwa dola 70 wenzetu wako dola 80. Serengeti ni hifadhi bora Barani Afrika, unapoiongelea Serengeti huilinganishi na Masai Mara, lakini bado Serengeti iko chini ya Masai Mara, kwa hiyo, tunapoongelea hizi tozo lazima tujilinganishe na wenzetu wana kiwango gani na sisi tuna kiwango gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo tulipandisha kwenye maeneo ya Tarangire, Arusha pamoja na Ziwa Manyara ambapo tulitoka dola 45 kwenda dola 50, tumeongeza dola tano. Kwa hiyo, tuangalie tozo zetu hizi ziko na ni kipindi cha peak, kipindi cha high season. Tunapoenda kwenye low season tunaenda kwenye tozo ya kawaida ambayo ilikuwa ni ya miaka ya nyuma. (Makofi)
Kwa hiyo, bado ukilinganisha na vivutio vyetu vilivyo bora tuko kwenye standard nzuri na watalii wanaendelea kuongezeka. Niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo hili tumejipanga vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo nataka niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kuhusu miundombinu katika maeneo ya hifadhi. Tumshukuru sana Mheshimiwa Rais amweweza kutupatia fedha shilingi bilioni 90.2 za kujenga miundombinu ya barabara katika maeneo ya hifadhi. Fedha hizi tumezielekeza kununua miundombinu ya mitambo, lakini pia na ujenzi wa barabara. (Makofi)
Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba utekelezaji wa fedha hizi utakapokamilika tutaondokana na kero ya uharibifu wa barabara wa mara kwa mara ndani ya hifadhi kwa sababu tutakuwa na mitambo ambayo hii mitambo itakuwa inatengeneza hizi barabara mara kwa mara na wakati huo huo Royal Tour imeshatufungulia utalii, tunaamini utalii utakuwa juu na barabara zitakuwa zinatengenezwa kila wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna eneo lingine ambalo wameweza kuliongelea…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, muda wako umekwisha. Dakika moja malizia.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nilitaka tu niongelee kidogo kwenye eneo la REGROW kwamba, eneo la REGROW lime-cover hifadhi nne ya Ruaha, Mikumi, Nyerere National Park pamoja na Udzungwa, sio Mikumi tu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mary Masanja, sasa kwa sababu umetaja hapo majina ya hifadhi na kumbukumbu zetu ili zikae sawa sawa hii inayoitwa Selous, hii inayoitwa Nyerere watu wamesema Selous humu ndani wewe umeita Nyerere sasa sema jambo hapo ili Wabunge wajue inaitwa nini sasa hivi.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kabla ya Nyerere National Park kupandishwa hadhi kuwa national park lilikuwa ni pori la akiba ambalo lilikuwa linaitwa Selous. Baada ya Nyerere National Park kupandishwa hadhi lilimegwa pori la Selous likabaki sehemu kuwa pori la akiba na Nyerere National Park ikapandishwa kuwa Hifadhi ya Taifa, kwa hiyo tuna Game Reserve ya Selous na wakati huo huo tuna Nyerere National Park. (Makofi)