Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Elly Marko Macha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi uliyonipa ya kuchangia Mpango ulioko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza kwa suala zima la upunguzaji wa umaskini. Katika jamii watu ambao ni maskini kuliko wote ni watu wenye ulemavu kwa sababu ulemavu unasababisha umaskini na umaskini unasababisha ulemavu. Pia niseme kwamba hapa Tanzania statistics tunazotumia katika kuelezea idadi ya watu wenye ulemavu katika nchi hii zina upungufu mkubwa. Tanzania Bureau of Standard wanasema asilimia nne, tano au milioni mbili ndiyo watu wanaoishi na ulemavu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa sensa hakuna ushirikishi katika kuhakikisha kwamba masuala ya watu wenye ulemavu yanajumuishwa katika sensa. Kuna ulemavu wa aina nyingi mwingine unaonekana kama mimi nilivyo sioni, naonekana kama sioni, lakini kuna ulemavu ambao hauonekani (hidden disability) kama viziwi au watu wa pyschosocial, watu wa down syndrome, dyslexia, huwezi kuona. Kwa hiyo, wanapofanya zile sensa wanasahau kujumlisha aina nyingi sana za ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mipango yetu katika Wizara zote tufuate ile statistic iliyotolewa na WHO pamoja na World Bank kwenye Disability World Report ya 2011 inayosema kwamba katika kila nchi asilimia 15 ni watu wenye ulemavu. Sasa basi sisi Tanzania ambao tuko milioni 46 mpaka 50 tukitumia hiyo statistic ya World Report ina maana kwamba watu wenye ulemavu nchi hii ni kati ya milioni 6.2 mpaka milioni 7.0, hii si idadi ndogo. Naomba Mipango inapopangwa itumie hiyo ripoti mpaka hapo itakapofanyika sensa nyingine ya kuonyesha jinsi data ya watu wenye ulemavu itakavyokuwa captured katika sensa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ulemavu unasababisha umaskini na umaskini unasababisha ulemavu, unakuta watu wenye ulemavu wako katika hali mbaya. Nataka kusema kwamba hii bajeti inayokuja izingatie kuweka bajeti kwa ajili ya maendeleo ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, mtu asiyeona akitaka kwenda hospitali inabidi aende na msindikizaji au kiziwi inabidi aende na mkalimani na unapokwenda na msindikizaji ina maana kwamba unalipa nauli yako na ya msindikizaji wako na kiziwi inabidi alipe nauli yake na ya mkalimani wake. Ina maana kwamba spending ya mtu mwenye ulemavu ni mara mbili kuliko ya mtu asiyekuwa na ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo basi naomba familia zile zenye watu wenye ulemavu ambao ni severely disability, kuna familia ambazo zina watoto wenye ulemavu ambao hawawezi kutembea, hawawezi kuongea, hawawezi chochote na anahitaji uangalizi masaa 24 siku saba. Hizi familia ni nyingi, nimeshaanza kufanya data collection, wafikiriwe kupewa cash ya kuwawezesha kuishi. Kwa mfano, hawa akinamama ambao wanatunza watoto ambao ni severely disabled hawana nafasi kabisa ya kufanya kitu chochote kile cha kuwasaidia kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inaposema itafikiria pension kwa wazee, ifikirie pia pension kwa wale members of family ambao hawana nafasi hata kidogo ya kutafuta kibarua ili aweze kuishi. Mtu anakuwa na mtoto mwenye ulemavu kuanzia asubuhi mpaka jioni na siku zote hana nafasi ya kutafuta chakula. Kwa hiyo, nao wapewe hiyo pension angalau hata Sh.30,000 kwa mwezi kwa maana ya Sh.1000 kwa siku ili waweze kununua chakula cha kuishi kwa sababu hawana nafasi kabisa ya kushughulika na shughuli za kujiongezea kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo cash transfer wenzetu wengine wameshaanza ku-effect, nchi kama Malawi na Kenya. Nafikiri sisi siyo maskini kuliko Malawi lakini wanafikiria pamoja na wazee na wale severely disabled people wapewe hiyo cash transfer ili waweze kuishi. Utakuta wengi ambao wanaachwa na hawa watoto ambao ni severely disabled ni akinamama kwa sababu baada ya mama kupata mtoto mlemavu au mtoto aliyelemaa, waume zao huwakimbia na kuwaacha akinamama wakihangaika na hao watoto. Naomba Serikali ifikirie kuwapa jinsi kuishi hizi familia ambazo zina walemavu ambao ni severely. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nilioutoa, kuna wafanyakazi ambao wana ulemavu matumizi yao yako juu, Serikali inaonaje kuanza kuwapunguzia ile tax ya Pay As You Earn (PAYE) kwa sababu hizo nilizozieleza. Mtu mwenye ulemavu anatumia zaidi kuliko mtu asiye mlemavu. Kwa hiyo, Serikali imsaidie yule anayefanya kazi kwa kumpunguzia kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, wenzetu wa Kenya Serikali yao ilishaona hili miaka mitano iliyopita, sasa hivi mwenye ulemavu yeyote pale Kenya anayelipwa mshahara wa kuanzia Sh.1-150,0000 ya Kenya ina maana Sh.3,000,000 ya Tanzania, inapozidi Sh.151,000 ile Sh.1 ndiyo wanaanza kuitoza kodi lakini ile Sh.150,000 wanamuachia kwa sababu wanajua matumizi ya mtu mwenye ulemavu ni makubwa. Naomba Serikali hii ifikirie katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika suala la elimu, kweli elimu imetolewa bure mpaka kidato cha Nne. Nategemea watoto wenye ulemavu pamoja na kwamba watasoma bure lakini vifaa vyao ambavyo vingi havipatikani hapa Tanzania vinaagizwa, vitabu vyao vinachapishwa katika maandishi ambayo wanaweza kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu ina mtambo wa kuchapisha vitabu vya wasioona lakini huu mtambo kwa miaka mingi umefanya kazi chini ya kiwango chake. Hauna vifaa, hauna fedha za kununua makaratasi, matokeo yake ni kwamba watoto wasioona ambao wanahitaji braille na wale wa uoni hafifu ambao wanahitaji large print hawana vitabu vya kiada katika shule mbalimbali hapa nchini. Serikali kupitia Wizara ya Elimu ifikirie kukiboresha kile kiwanda cha kuchapisha vitabu vya wasioona na wale wenye uoni hafifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala lingine la uchukuzi. Kama Waheshimiwa Wabunge wengi mnavyojua usafiri wa bodaboda unasababisha vifo na ajali nyingi na vina-create ulemavu kwa watu wengi sana hapa nchini. Baada ya miaka mingi mtakuta Watanzania wamelemaa kwa ajili ya hizi bodaboda. Nashauri Serikali iweke measures za kusimamia hawa waendesha bodaboda, aidha wawapatie training au watafute njia nyingine ili kupunguza watu wanaolemaa migongo, wamekatika miguu kutokana na hizi ajali nyingi zinazosababishwa na bodaboda.
kwamba kuna mkakati wa kufufua viwanda. Naomba Serikali ikumbuke kwamba watu wenye ulemavu pia wanahitaji ajira, hivyo viwanda viwe accessible ili waweze kuajiriwa kama wanavyoajiriwa Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuhi nilisikitika kwa vile nilinyoosha mkono niulize swali la nyongeza sikupata nafasi. Waziri alipokuwa anazungumzia Morogoro akasema kuna asilimia tano ya fedha za TASAF kwa ajili ya wanawake, asilimia tano kwa ajili ya vijana, kwa nini hakuna asilimia tano kwa ajili ya watu wenye ulemavu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kusema kwamba Tanzania iliridhia ule Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa 2006 na pia ikaja na Sheria Na.9 ya 2010 kuhusu Watu Wenye Ulemavu. Naomba sasa implementation ya hizi sheria ifanyike kwa sababu hakuna maana ya kusaini na ku-ratify and then hakuna implementation.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kuomba Serikali isaini ule Mkataba wa Kimataifa kuhusu copyright kwamba watu wenye matatizo ya kusoma maandishi ya kawaida wakiwepo wasioona, wenye uoni hafifu, wenye dyslexia, wenye down syndrome, wale publishers wa-publish kazi zao kwa maandishi ambayo ni accessible ili watu wenye ulemavu waweze kusoma vitabu. Naomba Serikali isaini na kuridhia ule Mkataba ili na sisi watu wenye ulemavu wa kutoweza kusoma maandishi ya kawaida tufaidike na treaty hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)