Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa Timu yetu ya Serengeti Girls kwa ushindi waliopata kwa kuwakilisha kwenye Kombe la Dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza sana Wizara hii ya utamaduni kwa kazi kubwa wanazofanya katika kuhakikisha sanaa, utamaduni, michezo vinaleta tija katika Taifa hili, lakini pia vinaleta tija kwa wanamichezo na wasanii wenyewe. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhati kabisa kwa kupenda na kukuza michezo na vipaji vya wanamichezo mbalimbali, kuvithamini na kutaka vipaji hivyo viendelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza na mchango wangu katika eneo la lugha ya Kiswahili. Napongeza kwanza taasisi zote zinazojihusisha na uendelezaji na ukuzaji wa Kiswahili, zikiwemo BAKITA, BAKIZA, kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuendeleza Kiswahili ambapo kwa mchango wao huo umefanikisha leo Kiswahili kuwa lugha inayotumika kwa kazi kwa Afrika, lakini pia ni lugha ambayo inatumika kikanda na kimataifa. Nawapongeza sana. Kiswahili ni bidhaa, Kiswahili ni ajira, lakini Kiswahili ni utambulisho wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lugha ya Kiswahili imesheheni maneno mengi ambayo tumetohoa na mengine tumeazima kutoka lugha mbalimbali. Kiswahili chetu hiki kimeunganishwa na kutohoa maneno mbalimbali ikiwemo Kiingereza, Kijerumani, Kiarabu, Kiajemi, Kichina, Kijapani, Kigiriki, Kihindu ambapo Kihindu kuna Kihindu, kuna Punjab, kuna Hindu kuna Ghujrat yote haya yapo katika Kiswahili, tumetohoa na kuazima haya maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutohoa na kuazima huko Kiswahili hiki kimetohoa kwenye vyakula, wanyama na kwenye mambo mbalimbali. Kwa mfano, nataka kutoa mifano michache tu, kwenye lugha ya Kihindi tumetoghoa chapati, fenesi, bagia, kachori, achari, karakana, madhubuti, tamasha, kitabu, pesa, meza, bangili, gari na mengineyo. Kiarabu tumetohoa ghali, amiri, dhambi, ridhaa, kasi, dhaifu, nafsi, kalamu, hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea kwenye Kijerumani tumetohoa neno soli. Kwenye Kigiriki tumetohoa neno lami, kwenye Kireno tumetohoa neno gereza, dama, lakini kwenye Kiajemi tumetohoa bahati, bahati nasibu, jambazi, balungi, hili balungi ni tunda. Kijapani tumetohoa judo, kichinchiri, kichinchiri maana yake ni kitoto kidogodogo kinachokuakua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maneno tumetohoa ambayo yanaingiliana na lugha nyingine. Mfano, soko Kiswahili lakini Kihindi ni sok na Kiarabu ni suuq. Kiswahili dua, kiarabu dua, kihindi dua. shukurani Kiswahili, shukria Kihindi, lakini shukra Kiarabu na mengi mengineyo kama madarasa, madras na madrasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka kujenga hoja, kwenye Kingereza tumetohoa penseli, pencil, baskeli, bicycle, ringi, ring na mengi mengineyo, hayo ni machache tu. Ninachotaka kusema tunataka kutumia Kiswahili kwa kuunganisha na kuongeza utalii nchini. Utalii nchini kwa kutumia Kiswahili, wanaotaka kujifunza Kiswahili wanakuja nchini na wengine wanataka Walimu wapelekwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hoja yangu ni hapa, kilio huanza mfiwa ndipo na wa mbali akalia, lakini pia, kibaya chako si chema cha mwenzako, tutukuze Kiswahili chetu. Kiswahili ni hazina, Kiswahili ni rasilimali ya nchi, tukikitumia vizuri, tukikiendeleza vizuri tutapata tija kubwa kupitia lugha yetu ya Kiswahili duniani na kuitangaza nchi yetu ya Tanzania tukiunganisha na kutangaza utalii wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninachotaka kusema katika kukiendeleza Kiswahili, tujitahidi basi tutumie lugha nyepesi, lugha ambayo inaweza kusomeka, kuandikika na kujifunza. Nimetoa mifano kwamba, hapa tumetohoa, mfano neno television linatumika karibu ulimwenguni kote television; Sudan television, Comoro television, Kifaransa télévision. Sasa maneno kama haya, tujaribu ndio tunataka tutumie maneno yetu ya kibantu, maneno yetu ya asili, lakini tutumie maneno mepesi kwa sababu kuna maneno tunayatumia sasa hivi hata mimi Mswahili nafikiri vile kitu gani vile? Nafikiri, nikishindwa natumia lile la Kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa lugha isiwe ngumu. Zamani lugha yetu inasema lugha nyepesi, mwananchi au wageni wanaifahamu kwa urahisi zaidi. Kwa hivyo, tuendeleze, tutohoe pia maneno yetu ya kibantu, lakini mengine ambayo ni magumu sana tumeyasahau, sitaki kuyataja hayo maneno yanajulikana, magumu. Unakifikiri kitu mara tatu, vile nini, vile nini? Hata ukilipata. Sasa hapa tuboreshe Kiswahili kiwe chepesi lugha inayoweza kuzungumzika ili kujenga ule uimara na watu kuja kujifunza kwa wingi Kiswahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Kiswahili tunataka kiwe kama ajira, nashauri vijana wetu wajifunze lugha zaidi ya mbili kwa maana ya Kiswahili, achanganye Kiingereza na Kifaransa au Kiswahili, Kingereza na Kihispania, ili lile soko la ajira la ukalimani, soko la ajira la kusomesha, liwe linapatikana kwa urahisi kwa vijana wetu kujua lugha zaidi ya mbili au tatu. Hiyo itasaidia zaidi kukitangaza Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea na mchango wangu napongeza sana wasanii hapa nchini kwa kazi kubwa mbalimbali wanazofanya kuhakikisha sanaa inakua. Nashauri Serikali iendelee kuinua na kuibua vipaji vipya na kuviendeleza, lakini katika kuinua vipaji vipya hivyo tuangalie na sheria hasa kule kwenye halmashauri kuna sheria nyingi zinakandamiza wasanii wasije juu kwa sababu ya kodi na ushuru mkubwa au malipo makubwa ya vibali kwenye halmashauri. Msanii ndio kwanza anataka kuanza anaambiwa lipa 70,000, ndio kwanza, atajitangaza vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuweke muda maalum, kikundi kimeshakua, baadaye tuwatoze hizo kodi au tuwatoze hizo tozo, ili tuibue vikundi, kuwe na motisha fulani ya kuibua vile vipaji tuviendeleze. Vinaibuliwa vingi, lakini vinaishia hukohuko chini, wakati mwingine ni sheria tu kandamizi ambazo hazitaki kuinua vipaji vya wasanii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea hapo sekta ya utamaduni. Utamaduni ni mpana sana, ni mpana kwa maana binadamu anapozaliwa anazaliwa kwenye utamaduni, analelewa kwenye utamaduni, anakuwa kwenye utamaduni, harusi ni utamaduni, mpaka anazikwa binadamu anazikwa kwenye utamaduni kutokana na eneo husika na nchi husika. Kwa hivyo, suala la utamaduni ni utambulisho mkubwa wa nchi, tunataka kuliendeleza ili liendelee kuitangaza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea kuwapongeza wasanii, kuna suala moja linajitokeza, haki miliki. Wasanii wetu haki miliki zao bado zinadhulumiwa, kwa maana kuna nchi au mataifa wanatumia nyimbo zao wanazibadilisha lugha, lakini mdundo, muziki ni uleule, wimbo ni uleule na wanapata fedha nyingi kupitia hizo nyimbo zetu za Watanzania wetu wakiwemo akina Diamond na wenzake, tulinde haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kuna wasanii wa zamani wa nyuma wameimba nyimbo nyingi, lakini zinaimbwa na sasa hivi, anaonekana mmiliki ni yule wa sasa hivi, lakini kumbe ile nyimbo ni ya zamani na imetungwa zamani. Tuweke kumbukumbu wimbo huu umetungwa lini? Muimbaji alikuwa nani? Aliyetia sauti ni nani? Aliyetunga shairi ni nani ili kizazi na kizazi kiweze kujua wimbo huu ulikuwa ni wa nani? Hata kama utaimbwa tena mara ya tatu, mara ya nne, basi mmiliki awe na haki zake kwa uhalisi wake anapata zile kutokana na jasho lake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sanaa tunaipenda. Tunasikia wasanii mara wanafungiwa, hivi, nataka niongee kidogo tu; mimi niliwahi kutumikia chombo cha sanaa, niliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi Idara ya Sanaa Zanzibar, tulikuwa na chombo kinaitwa Sensor Board, muziki, shairi lolote kabla halijatoka linakwenda kwenye Sensor Board kwanza. Hii inaifanya taasisi ya muziki ule wasipate hasara baadaye ya kuja kufungiwa muziki wao, lakini inataka mashirikiano ya pamoja kati ya wasanii na hivi vyombo. Wawe wakweli na wa wazi kupeleka mashairi yao, maudhui yao, ili wasije wakafungiwa na kupata hasara isiyokuwa ya lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo yanaepukika. Tujitahidi kuwaonesha sanaa zenye kupendeza, lakini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)