Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu, kwanza nimpongeze sana Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya katika Wizara hii, lakini sambama na naye nimpongeze Naibu Waziri Mheshimiwa Pauline Gekul kwa kazi nzuri sana unaifanya mama endelea tupo nyuma yako tunaunga mkono, lakini kipekee niwapongeze watendaji wa Wizara hii ndugu yangu Dkt. Abbas lakini pia Naibu Katibu Mkuu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mchango wangu utajikita sana katika mambo ya soka, lakini nikiangalia zaidi eneo la mapato. Nilikuwa ninamuuliza Mheshimiwa Mwijage hapa kwamba kuna wakati wa Yesu, kuna yule Zakayo ambaye alikuwa ni mtoza ushuru, sasa kwa bahati leo tupo na Mkurugenzi wa Singida Big Stars ambaye pia ndio mtoza ushuru wetu hapa Tanzania na kwa babati nzuri na yeye ana timu inacheza ligi kuu katika msimu huo unaokuja, sasa nikakumbuka ile methali ya mwenda tezi na omo marejeo ngamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilabu vya Simba na Yanga vimeanishwa muda mrefu sana, lakini vilabu havijiendeshi kibiashara, bado ni vilabu ambavyo vinategemea ruzuku za wanachama, lakini michango mbalimbali na kwa bahati mbaya sana huko nyuma walikuwa na mfumo ambao sio mzuri sana wa usajili kiasi kwamba walikuwa wanasajili wachezaji, hasa wachezaji wa nje…
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa.
T A A R I F A
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba vilabu ambavyo havijiendeshwi kibiashara sio vyote, Young Africans sasa hivi ipo kwenye kumalizia kujiendesha kibiashara na muda mfupi tu watakamilisha mpango huo na itakuwa inajiendesha kibiashara sawa sawa. Kwa hiyo nampa taarifa na aipokee, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shangazi sidhani kama ni taarifa, lakini ni …
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, sio taarifa, kwanza angetega sikio asikie nazungumza nini ndio ataelewa kwamba kuna biashara inafanyika au hakuna biashara. Simba na Yanga peke yake hadi sasa hivi zinadaiwa na Mamlaka ya Kodi Tanzania bilioni kumi na hizi ni fedha ambazo zinatokana na…
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Fedha.
T A A R I F A
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mbili mzungumzaji; moja sikuwa najua…
NAIBU SPIKA: Taarifa moja tu.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji sikuwa najuwa anavyoongea Zakayo anamaanisha mimi, lakini nilitaka nimpe taarifa kwamba mimi similiki timu ni mdau tu wa michezo ya hapa Tanzania, kwa hiyo… (Makofi)
NAIBU SPIKA: ahsante lakini sidhani kama ulitajwa. (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, niliona anaongelea Zakayo. (Kicheko)
NAIBU SPIKA: Naona unajishuku, haukutajwa popote hapa yametajwa mambo ya Yanga na madeni ya TRA nilifikiri unasimama kuhusu unasamehe madeni ya TRA ya vilabu vikubwa. Haya Mheshimiwa Shangazi endelea.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naona mambo yanakuwa mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Simba na Yanga kwa umoja wao wanadaiwa takribani shilingi bilioni kumi na Mamlaka ya Kodi Tanzania na fedha hizi zinatokana na pays as you earn, lakini skills development levy ambazo hawakukusanya tangu wakati ule ambapo walikuwa wanaendesha katika mfumo ambao sio rasmi sana kama ambavyo sasa hivi angalau wanaelekea kwenye mfumo ambao unaeleweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunawomba sana Wizara ya Fedha hivi vilabu kwasababu havijiendeshi kibiashara, havina mahali popote vinaweza kuja ku-retire hivi amount, basi wasamehe hizi kodi ili sasa virudi katika mfumo wa kuweza kuwa na compliance wakati huu ambapo sasa vimeanza kujiendesha katika mfumo ambao ni rasmi. Lakini bila kusamehe hili deni ipo siku Mamlaka ya Mapato ikiamua kuvifungia hivi vilabu hatutakuwa na kitu kinachoitwa Simba wala Yanga kwa sababu wana deni kubwa ambalo haliwezi kulipika. Kwa hiyo, nikuombe sana Waziri wa Fedha lakini nikuomba Waziri wa Michezo ufuatilie hili jambo ili vilabu vyetu viweze kupata hiyo nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine ambalo nilitaka kulichangia pia ni kwenye eneo ambalo sasa linawahusu hata wale wamiliki wa Singida Big Stars, lakini wengine ni wa Namungo, Simba, Azam na kadhalika. Hili ni eneo ambalo lina kodi ya zuio (withholding tax); TFF wameingia mkataba na Kampuni ya Azam ya kuonesha matangazo ya mpira, lakini kulikuwa kuna kipengele cha withholding tax ambacho vilabu vilikuwa havikuambiwa, kwa hiyo wakati sasa vilabu vinapewa fedha na Azam inabidi sasa wa-retire ile amount ya withholding tax kitu ambacho kimepunguza kile kiwango ambacho tumetangaziwa pale awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inavifanya vilabu sasa vikose fedha za kutosha za kuweza kujikimu kama ambavyo mdhamini alikusudia kwa hiyo tunaiomba Wizara ya Fedha, lakini pia Wizara ya Michezo ikae ikae katikati iangalie, kwa sababu vilabu vyote tunavyozungumza hapa havina mahali ambapo mwisho wa mwaka wanaweza wakaonesha hesabu ili waweze kurudishiwa hizi fedha, kwa sababu vilabu vyetu bado vipo katika mfumo wa ridhaa, kwa hiyo namna pekee ya kuwasaidia ni kuwasamehe hii kodi ya zuio katika hii biashara ya matangazo kupitia Azam TV.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulichangia ni suala la kwenye michezo ya kubahatisha (betting). Ningeomba sana kwanza nawapongeza sana SportPesa kwa kazi nzuri ambayo wanafanya, wameweza kudhamini Simba na Yanga takribani miaka mitano na wametoa zaidi ya shilingi bilioni 6.6. Lakini pia walikuwa wanadhamini vilabu vingine kama Singida United, wamedhamini Namungo tumeona wakiwa na msaada mkubwa. Lakini nitoe rai sasa kwa Wizara ya Michezo iweze kuongea na kampuni nyingine za michezo ya kubahatisha kwa maana ya betting sasa hivi tunazo kampuni zaidi ya 20 twende kuwaeleza kwamba ili aweze kupata leseni ni lazima angalau adhamini pia japo timu moja, kama ambavyo tumeona kuna 10Bet wanadhamini timu ya Dodoma Jiji hapa, basi na hizi kampuni nyingine za betting zichukue japo timu moja ya ligi kuu au kama sio ya ligi kuu basi hata ya ligi daraja la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia sana kwa sababu maudhui wanayokwenda kushindania yanatokana na mpira, kwa hiyo ni lazima wawekeze pia katika kuendeleza tasnia nzima ya mchezo ili waweze pia kupata malighafi ya kuzalisha kwa ajli ya hizo kampuni zao za ku-bet. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa nilisemee ni eneo la kwa ujumla kuwapongeza wale ambao wanafanya vizuri katika udhamini kwa maana ya Azam kupitia Azam Sports wanafanya kazi nzuri sana. Lakini wadhamini wengine kama SportPesa wadhamini wengine kama Mohamed Dewji kupitia kampuni yake ya MO29 wanafanya vizuri kiasi kwamba sasa tumeona namna ambavyo Simba inaendelea kufanya vizuri katika Taifa hili, takribani kipindi cha miaka mitano tumeingia katika hatua ya robo fainali na tumeliwakilisha vyema Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia hata katika hii Royal Tour, Simba ndio tumeanza kwa sababu katika kuweka jezi ya Simba ile ya Visit Tanzania hao watalii ambao tunawaona kuna mchango mkubwa sana wa Simba Sports Club. Kwa hiyo ninakubaliana na wewe sasa kwamba na michezo nayo iingie hapa i-chip in kwenye hii Royal Tour kwenye sports ili tuweze kufanya michezo yetu iweze kuwa na msaada mzuri kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)