Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Utamaduni. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya, hasa kutuzindua na kutuonesha umuhimu wa sisi Watanzania kuhamasisha ama kujali utamaduni wetu. Ziara aliyoifanya kule Mwanza, Magu katika tamasha la machifu na ngoma za utamaduni ni kiashiria ambacho kinaonesha commitment yake kwa utamaduni wa Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipee pia nakupongeza wewe Spika wetu Tulia Ackson kwa jinsi ambavyo unaendesha tamasha la utamaduni kule Mbeya. Tamasha hili tunalifuatilia kwa ukaribu, lakini pia ni model ambayo inapaswa kuigwa Tanzania nzima. Kwa kweli kama tunaweza kumnukuu Mwalimu Nyerere, alisema kwamba utamaduni ni kiini ama roho ya Taifa lolote lile. Taifa ambalo halina utamaduni, ni mkusanyiko wa watu ambao hawana roho. Kwa hiyo, jitihada hizi ambazo mnazifanya, zinaonesha jinsi gani viongozi wetu mnatuonesha njia ya kupambania utamaduni wetu ambao ndiyo roho ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hilo, wakati nachangia Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje, nilizungumzia umuhimu wa economic diplomacy, nikaeleza kwamba wakati umefika sasa wa ku-adapt kitu kinachoitwa innovative diplomacy. Alichokifanya Rais wetu, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia Royal Tour, ni hicho ambacho tunakiita innovative diplomacy. Kupitia Royal Tour tumeweza kuuza utamaduni wetu, tumeweza kuwafikia wananchi ndani ya nchi na tumeweza kuifikia dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dunia sasa hivi, hasa huko tunakoelekea, Taifa kama Tanzania hatuwezi kwenda ku-influence wenzetu ama kutafuta ama kupigania nafasi yetu kwenye dunia hii kwa kutumia mizinga ama bunduki, lakini kuna kitu kinaitwa soft power approach ambayo pia ni sehemu ya innovative diplomacy ambapo tunaweza tukafikia dunia kupitia sanaa utamaduni na michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hili hatujalifanyia kazi vya kutosha, lakini nilikuwa naomba kusema kwamba tunaona jitihada ambazo Serikali inazifanya. Kwa mfano, kama jana tumeona timu yetu ya Taifa imeweza kufuzu Kombe la Dunia. Hizi ni jitihada ambazo zinaashiria kwamba tuna commitment ya kutangaza jina la Tanzania nje ya mipaka ya Tanzania na inshallah tunatumaini kwamba timu yetu itaenda kufanya vizuri na kuliuza jina letu huko.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kuna mengi ambayo yamefanywa katika tasnia ya utamaduni, utamaduni wa utalii bado hatujautendea haki. Huko tunakoenda hatutaendelea tena kuuza milima, misitu na bahari. Utamaduni unaenda kuwa bidhaa ambayo bado hatujaitumia kikamilifu kama chanzo cha mapato.

Mheshimiwa Spika, nina matumaini makubwa kwa Rais wetu na pia nina matumaini makubwa kwa timu ambayo ipo Wizara ya Utamaduni ikiongozwa na ndugu yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Naibu wake, dada yangu Mheshimiwa Pauline Gekul, Hassan Abbas na ndugu yetu Hassan Yakubu, wanafanya kazi kubwa ya kuiamsha Wizara na kutuonesha kwamba Wizara ya Utamaduni imepata wadau ambao wanaweza kuipambania na sisi tukaitumia kama tool ya kufikia dunia kupitia sanaa na utamaduni.

Mheshimiwa Spika, wanasema kwamba kinga ni bora kuliko tiba. Michezo ni kitu muhimu sana katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza. Kwa mujibu wa tafiti za Muhimbili Costech na hata NIMR, wanazungumza kwamba asilimia 41 ya vifo, vinatokana na maradhi yasiyoambukizwa. Vifo hivi ni mara mbili ya vifo ambavyo vilikuwa vinatokea miaka 25 iliyopita. Taifa kama letu ambalo linapambana ku-transform uchumi wetu, tunatumia zaidi ya dola milioni 700 kwa ajili ya kutibu, hatujajikita kwenye kuzuia. Ila kuzuia magonjwa kama ya moyo shinikizo la damu na kisukari, ni michezo.

Mheshimiwa Spika, michezo inaweza ikasaidia ku-save kiasi kikubwa cha fedha, lakini kwenye hili, kwa nini Watanzania wengi hawajihusishi na michezo? Wengine wanashindwa kujihusisha kwa sababu tu ya gharama kubwa ya vifaa. Kama wanapata access ya vifaa wanaweza wakaweza kushiriki michezo.

Mheshimiwa Spika, katika hili naomba Wizara yetu ya Fedha inapoenda kutoa hotuba yake, ituambie ni kwa jinsi gani imejipanga kupunguza kodi ama kutoa nafuu ya kodi kwenye vifaa vya michezo ili ku- encourage Watanzania wengi zaidi kushiriki michezo kwa ajili ya ku-prevent afya zao ili ikoe fedha nyingi za nchi kwenye kutibu maradhi badala ya kukinga maradhi. Katika hili, matumizi ya kodi ambazo zinapitishwa na Bunge hili, naomba sana ndugu zetu wa TRA, Hazina wasizitumie vibaya kuumiza shughuli ama jitihada za michezo.

Mheshimiwa Spika, kuna vitu ambavyo vimezungumzwa kuhusiana na madeni ya Simba na Yanga, lakini ndugu zetu wa TFF wanadaiwa zaidi ya Shilingi bilioni 10, sasa hivi wamelipa Shilingi bilioni tano na haya ni malimbikizo ya madeni ya nyuma. Sasa kwa taasisi ama chama cha michezo kama hiki ambacho kinajikokota kwenye kukuza michezo, kinadaiwa kodi ya Shilingi bilioni 10; na sasa hivi kinajiandaa kuleta AFCON nchini, chama ambacho kina madeni lukuki; hivi kama kuna moja ya criteria ambazo zitatumika na CUF kuleta mashindano hapa ni madeni kwa chama, tutafanikiwa kweli!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye majumuhisho, naomba tuone namna bora ya kusaidia vyama vyetu vya michezo na hasa timu zetu. Azam wamejitolea kudhamini ligi, wanatoa shilingi milioni 40 kwa kila timu, lakini katika shilingi milioni 40 hizo, shilingi milioni sita zinarudi TRA. Sasa haya ni maeneo ambayo yanakuza ajira na kupanua fursa kwa vijana wetu. Shilingi milioni 40 ni kitu gani ambacho unakata kama withholding tax? na mbaya zaidi, shilingi milioni sita ni hela nyingi sana kwa timu zetu ambazo zinachechemea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba tuangalie kwa jicho la huruma kama fursa kwa watoto masikini, tuone namna bora ya kupeleka ujumbe kwao kwa kukuza vibaji vyao na pia kwa kuangalia kodi ambazo zinaweza zikawa-encourage na siyo kuwa-discourage.
Mheshimiwa Spika, pia kuna umuhimu wa kusamehe kwenye vifaa vya michezo hasa kwa watoto wadogo. Inaumiza sana unapoona timu ya watoto 22 wanacheza, watano wana viatu, 15 hawana viatu, inaumiza sana na ni kwa sababu tu ni gharama, wazazi hawewezi ku-afford. Kama tunataka ku-train vijana wetu, kujenga haiba na utamaduni wa kuheshimu sheria na taratibu, kuthaminiana, kupendana, lazima tu-invest kwenye michezo na kwa kuanzia tuweze kusamehe vifaa vya michezo, kodi hasa vifaa vya watoto wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawapongeza ndugu zetu au wadau wetu wakubwa wa michezo; kuna Dkt. Singo, ndugu yangu Askalia na dada yetu Neema Msita, wamefanya jitihada kubwa za kuboresha utawala bora kwenye michezo, lakini tunahitaji wapatiwe bajeti ya kutosha ili waendeleze michezo.

Mheshimiwa Spika, kwenye tasnia ya filamu tumeona imekua kwa kasi, kuna zaidi ya filamu 1,500 kwa mwaka ukilinganisha na 200 mwaka 2011. Wastani wa filamu 116 kila mwezi, 29 kila wiki, na nne kwa siku. Sekta hii imeajiri zaidi ya vijana 30,000. Sekta ya filamu ambazo zinatengenezwa ndani ya nchi ni kubwa sana kwa idadi katika Bara la Afrika. Kwa idadi ya filamu 1,500 kwa mwaka, Tanzania ni ya pili kwa wingi wa filamu ambazo ni local produced ikifuata Nigeria. Kwa hiyo, sekta hii ni muhimu sana na inakua kwa asilimia 14, tunahitaji kui-support.

Mheshimiwa Spika, tumezungumzia umuhimu wa Kiswahili kama roho ya Taifa. Kuna vijana ambao wamejitahidi kutengeneza movie documentaries ambazo Kimataifa zimeweza kuuza jina la Tanzania. Filamu kama ya Vuta Nikuvute ambayo imetengenezwa na Mtanzania Amil Shivji, imesadifu riwaya mashuhuri ya mwandishi Shafi Adam Shafi na imetayarishwa na Watanzania. Filamu hii imewezwa kuchezwa kule Toronto, Seto, Ottawa na maeneo mengine mbalimbali kama Burkina Faso na hata Zanzibar inaenda kutumika kwenye tamasha la filamu.

Mheshimiwa Spika, filamu kama “Binti” ambayo imewezwa kutengenezwa na dada yangu Seko Shamte, filamu kama “Jua Kali” imetengezwa na dada yetu Lea Mwendamseke; ni filamu ambazo zinaibeba nchi yetu, zinabeba lugha yetu na utamaduni wetu. Serikali inafanya nini sasa kuzalisha akina Shivji wengine, akina Mwenda Mseke wengine na akina Shamte wengine? (Makofi)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, mwisho naomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja tu, namalizia.

SPIKA: Sekunde thelathini.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nilikuwa na ombi moja, fedha ni changamoto kukuza tasnia ya Sanaa na michezo. Naomba 4% ya Skills Development iende kukuza vipaji na ujuzi mbalimbali hasa michezo na utamaduni na 5% ya mapato yote ambayo yanatokana na michezo ya kubahatisha iende kwenye mifuko ya kuendeleza michezo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, na ninakushukuru. (Makofi)