Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia katika Wizara hii ya Fedha. Kwa vile muda wangu ni mfupi nitasema kwa points zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Kamati ya Bajeti kwa jinsi ambavyo wameweza kuchanganua hii bajeti na pia kwa maagizo waliyotoa au ushauri walioutoa ambao ninaamini utasaidia sana katika kusimamia fedha za umma. Lakini pili nichukue nafasi hii kumshukuru Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuweza kuonesha yale maeneo mbalimbali ambayo yana ubadhirifu wa fedha ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mimi nizungumzie kuhusu Deni la Taifa. Fungu hili 22 limekuwa likipata hati isiyoridhisha kwa muda mrefu. Hii inatokana na mfumo ambao sio thabiti wa usimamizi wa kumbukumbu za madeni. Kwa hiyo, ningeishauri Serikali kwamba, iimarishe kitengo chake cha Debt Management Office ili kiweze kuweka kumbukumbu hizi vizuri, vinginevyo tutapata taarifa ambazo si sahihi. Na Kamati ya Bajeti nafikiri nimesikia wakishauri lianzishwe Fungu jipya na mimi naunga mkono, ili waweze kusimamia vizuri Deni la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili nizungumzie kuhusu Consolidated National Accounts yaani Hesabu Jumuifu ya Taifa. Na fungu hili pia limepata hati ya mashaka kwa muda mrefu. Kwa miaka kadhaa hesabu za hili fungu jumuishi zimekuwa zikipata hati yenye mashaka kutokana na kutokamilika kwa taarifa zake. Hivyo Wizara iimarishe ofisi hii ili iweze kufanya kazi yake kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo pia niungane na wenzangu walionitangulia kwamba tax base ya nchi hii iongezwe kutokana na kwamba mpaka sasa hivi walipa kodi ni wachache sana. So far inaonesha ni kama watu milioni 2.7 ambao wanalipa kodi, ukiangalia nchi hii ilivyo kubwa na population ilivyo kubwa naamini wenzangu waliopita walivyoweza kushauri basi kuwe na wasimamizi wa kodi wanaoenda mpaka kwenye kata kule wanaweza kupata walipakodi wazuri. Kwa hiyo, ningeshauri kwamba TRA izidishe kuongeza waajiri wenye utaalamu ambao wanaweza kwenda mpaka sehemu za kata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna malalamiko kwamba EFD machines kwanza ni chache, pili hazifanyi kazi vizuri. Kila ukienda kununua kitu unaambiwa mashine hazifanyi kazi, kwa hiyo, ni vyema Wizara ikaangalia jinsi ya kuimarisha hizi EFD machines. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nije na wazo ambalo nilifikiri kwamba linaweza likatusaidia sana, hapo nyuma tulikuwa na Tume ya Mipango ambayo ilikuwa haiko pamoja na Wizara hii ya Fedha. naamini kwamba, Tume ya Mipango ingeanzishwa au ingekuwa re-established naamini kwamba ingesaidia sana katika kuangalia mipango yetu na kuona priority areas zetu ambazo zinatakiwa ziangaliwe na zitengewe fedha zaidi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, kengele hiyo sijui ni ya kwanza? Au ya pili?

Mheshimiwa Spika, anyway, naamini kwamba Tume hii ya Mipango ni muhimu sana katika nchi yetu. Maana sasa hivi Wizara ya Fedha ndio yenyewe ikae ipange, yenyewe ikae itoe fedha, hii sio sahihi kabisa. Tunatakiwa tuwe na tume ambayo ni independent… (Makofi)

SPIKA: Haya, sekunde 30 malizia sentensi.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, mimi niendelee kusema tu kwamba, niombe Ofisi ya CAG wapewe hela nyingi ili waweze kuibua sehemu mbalimbali ambazo zinatumia vibaya fedha za umma ili waweze kuongeza ile sampling yao. Ahsante sana. (Makofi)