Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyopo mezani kwetu ambayo ni hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2022/2023. Nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na kukutana asubuhi ya leo. Pili, nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuiletea nchi yetu maendeleo. Tumeona kwa vitendo mambo mbalimbali ambayo yanajitokeza baada ya kuwa yeye ametoa kauli na kuonyesha utashi wake wa kweli katika kuiletea Tanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata leo hii bajeti ambayo imesomwa na kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha imeonyesha wazi maono yake, imeonyesha wazi dhamira yake na imeonyesha wazi namna ambavyo anaitekeleza vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa nimetoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais, sasa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri mtoa hoja, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa kazi nzuri aliyoifanya kutuletea hoja hii ambayo imeonyesha wazi bajeti hii itakwenda kuondoa maumivu yaliyokuwepo kwa wananchi. Bajeti hii imegusa nyanja mbalimbali za kimaendeleo, bajeti hii imegusa sekta zote kwa umakini mkubwa, lakini zaidi imeonyesha waziwazi kwamba imeenda kumgusa mnyonge chini kabisa pale. Kwa hiyo, naamini kabisa kama bajeti hii itaenda kufanyiwa kazi itaenda kuleta mabadiliko na kufanya mapinduzi makubwa ya uchumi wa nchi yetu. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake ndugu yangu Mheshimiwa Chande na Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kushukuru sana, nimeona kwenye bajeti hii pamoja na bajeti za kisekta ambazo tumekuwa tumepitisha, tumeona katika Jimbo langu, Wilaya yangu ya Ikungi tumeona namna ambavyo tumepata mgao wa fedha, tumepata mgao kwenye maeneo ya afya, maji, elimu huduma mbalimbali za kijamii zinaenda kuguswa, lakini kama haitoshi tumeona namna ambavyo miundombinu ya barabara itaenda kuletewa fedha kwa ajili ya kutengeneza lami katika maeneo ya Mji wa Ikungi ambapo tunapata kilometa mbili, zitaenda kujengwa pamoja na taa zitawaka katika mji wetu. Hii italeta mabadiliko makubwa sana, hivyo, tunaishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru kwa namna ambavyo imeamua sasa kujenga barabara ile ya Singida - Kwa Mtoro – Ugashi - Tanga ambayo imekuwa tukisemea kwa muda mrefu. Kilometa 462 zikienda kujengwa itaenda kuchachua uchumi wa wananchi wetu na tutaona maendeleo ya haraka yatapatikana. Tumekuwa tukisema Bungeni na leo nashukuru Mheshimiwa Waziri ameitaja barabara hii, tunaamini wananchi wanaisubiri na tunaomba sana mchakato ufanywe mapema, tupate mkandarasi ili barabara iende kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza hayo, naomba niende kwenye eneo ambalo nimesoma katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, eneo la ukuzaji wa uchumi. Eneo hili tumeelezwa vizuri mpango wa Serikali namna ambavyo tutakuza uchumi, lakini tumeelezwa kwamba ukuaji wa uchumi wanategemea mpaka mwakani 2023 tutafikia wastani wa ukuaji wa pato la Taifa kwa asilimia 5.3, wakati huo wastani wa Ilani wa CCM inasema asilimia 6.9. Kama Serikali ikiangalia vizuri tumekuwa tunapanda kwa taratibu sana kwa sababu kuna baadhi ya vyanzo vya mapato hatujaviangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitazungumzia sana sekta ya uchumi wa makaa ya mawe pamoja na chuma kilichopo kule Ludewa. Tumekuwa na changamoto kubwa ya kuwa tunatamka lakini hatuchukui hatua. Eneo hili tumekuwa tukilizungumza kwa miaka mingi, lakini leo tutaangalia kwamba kwenye Ilani ya CCM imeeleza wazi kwamba mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu, Ibara ile ya 17, imeelekeza waziwazi kwamba kutumia rasilimali za Taifa kwa ajili ya maendeleo na manufaa ya Watanzania. Leo hii tunavyoongea makaa yale yalioko pale Ludewa hatujayachimba, leo tunavyozungumza tunazo leseni tulizowapa NDC ambao wamepewa leseni zipatazo nane, lakini wamezishikilia tu, hawajawahi kufanya utafiti, hawajawahi kuchimba, mali iko pale ardhini haijawahi kuguswa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ukienda utasikitika, Kamati yetu ilifika kule, imeona namna ambavyo yale makaa ya mawe huhitaji kuchimba wala kutumia nguvu kubwa. Unachukua chepe tu, unachimba, unachukua yale makaa ya mawe unaenda kuuza. Hayahitaji kutumia fedha nyingi. Leo hatujaweza kuyachimba, hivi ninavyoongea, NDC wamepewa leseni nane kama nilivyosema, PL 6986 ya mwaka 2012, PL 6710 ya mwaka 2010, PL 10263 ya mwaka 2014 pamoja na ya 2015, zote hizi hazijawahi kuchimbwa mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, leo hii kwa sababu ni kampuni ya Serikali, ni vizuri waruhusu sekta binafsi waingie kwenye uchimbaji wa madini haya ambayo kimsingi wataenda kwa kasi kwa sababu wao wanaangalia faida. Inawezekana hawa NDC kwa kuwa wao ni Serikali hawaoni manufaa sana na hawaoni haja hiyo kwa sababu haiko kwenye mipango yake, lakini kama tunataka kuangalia chanzo cha uhakika, lazima tuangalie namna ya kuchimba ile chuma, namna ambavyo tutachimba yale makaa ya mawe ambayo kimsingi yataenda kuleta kwa sababu yana soko nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, tutaunganisha na namna ambavyo tutakuza bandari hii ya Mtwara. Bandari ya Mtwara itapata mzigo wa kutosha kupeleka nje. Tumeanza kuona saivi kuna meli zinaondoka zinakwenda India kutokea Bandari ya Mtwara. Kwa hiyo, uwekezaji wa Bandari ya Mtwara kama tutaweza kupeleka mzigo wa kutosha, utakuwa na maana na utarudisha fedha ambazo Serikali imewekeza. Kwa hiyo, niombe sana, eneo hili waliangalie kwa makini ili waweze kuona namna ambayo tutaongeza pato la Taifa ambalo kimsingi kwetu ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili niwaombe, kuna barabara ya kutoka pale Njombe kwenda mpaka Manda Ludewa. Barabara ina kilomita 210, Serikali imeanza kujenga kilomita 50 kwa kutumia concreate, leo hii wameshajenga kilomita kama 30 na kitu hivi. Kwa hiyo, niombe sana, kilomita zilizobaki ziweze kujengwa kwa sababu kutakuwa na movement kubwa ya magari ambayo yatakuwa yanatoka kule kwa ajili ya kupeleka kwenye Bandari zetu za Tanga na eneo lingine. Kwa hiyo, eneo hili tukilifanyia kazi vizuri, tutafikia lengo ambalo liko mbele yetu la kukuza uchumi na kuongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili niongelee sekta ya utalii. Utalii ndiyo unatuingizia fedha nyingi kuliko sekta yoyote katika nchi yetu. Utalii huu ambao tumepewa kama tunu na Mwenyezi Mungu, lazima tulinde rasilimali tulizonazo na vivutio ambavyo tunavyo. Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri ya kutangaza vivutio vyetu kupitia royal tour. Tunaona matokeo yake, watu wanakuja kuona. Hivi leo hii tukitangaza vivutio ambavyo kesho havipo, inakuwa haina maana hata juhudi zote za kutangaza vivutio hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tunasema wote kwa pamoja, utalii unatuingizia fedha. Tunawavutia watalii waje waone, hivi wakialikwa, wakaja kukuta vivutio vimekwisha itakuwa na maana gani? Niombe sana Serikali ijikite katika kulinda rasilimali zetu. Isiache watu wachache ambao hawana nia njema wakaharibu vivutio vyetu, kwa sababu tu ya lengo, wengine wanakuja na sababu ndogo tu, kwamba Serikali inajali wanyama kuliko wananchi, si kweli. Wote wanaishi nchi hii, lazima tuwe na vipaumbele, tulinde vivutio na huku tunalinda na binadamu, ndiyo maana wanapewa huduma. Hatuwezi kuruhusu hali hii kwa sababu eti kuna watu fulani wataona wanaonewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Pori la Loliondo lilianzishwa mwaka 1951. Mpaka leo kama ingekuwa hatujatunza vizuri, maana yake leo hii tungekuwa hatuna vivutio hivyo. Hatuwezi kuacha watu wachache wakatuharibia, tena bahati mbaya wanatumika na nchi zingine kuharibu kwa sababu ya ushindani wa utalii. Niombe sana Serikali iwe makini kuhakikisha inalinda ili tuendelee kuwa na hali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusipoangalia hili jambo, tutaanza kuingia kwenye huruma ambazo nyingine hazina sababu, wengine wana ajenda zao na kwa hakika leo hii pori lile lilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 4,000. Serikali imepunguza 2,500 imewaachia kule wananchi waweze kufanya shughuli. 1,500 ambayo ni chanzo cha ikolojia ya kulinda kule Serengeti ambayo tunasifiwa leo, ni mbuga ambayo inasifika duniani. Watu wengi wanataka kuja kuona pale Serengeti, leo hii tukiua ile, ikolojia ile ya kutunza wale wanyama, nyumbu wanapita kila mwaka kwenda pale wanazaliana. Nyumbu zaidi ya 600,000 wa ndama wanapatikana pale, kupitia ikolojia hii ya njia hiyo. Leo hii tukiacha pale, vyanzo vya maji ambavyo vinapatikana kwenda kutunza kule Serengeti vinapitia pale Loliondo. Leo hii tukianza kuja na sababu ndogo ndogo tu, nyingine hazina mashiko, hatutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi ni kubwa, kama kunaonekana watu eneo lile hawana sehemu nzuri ni ukame na nini, wapatiwe eneo lingine la kwenda kuishi, Tanzania bado ni kubwa. Ardhi hii iko chini ya Mheshimiwa Rais. Aruhusu waende popote, waweze kuacha eneo lile liweze kulindwa na liweze kuhifadhiwa na tuweze kuendelea kupata utalii kama ambavyo tumeendelea kulinda katika miaka yote, toka mwaka 1951.

Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii bado sisi tunaendelea kuona kama ndiyo mboni ya jicho letu. Serikali isisite, ichukue hatua, isimamie na wale waliopewa kazi hii ya kuhifadhi, wafanye kazi yao kwa mujibu wa sheria. Eneo hili naomba sana kama kuna watu ambao wanafanya tofauti na haki za binadamu, wachukuliwe kama wao siyo ionekane kama Serikali nzima haijatenda haki kwa wananchi wale. Kwa hiyo, nilitaka nieleze eneo hili ili tukuze uchumi wetu. Zaidi naomba nirudie tena kushukuru sana na kuipongeza Serikali kwa kuleta bajeti ambayo leo inaenda kutuheshimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)