Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hii. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa maandalizi ya hotuba nzuri ya bajeti. Nawapongeza vilevile kwa sababu wametuletea bajeti nzuri ambayo inaleta matumaini kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bajeti hii inalenga kukuza uchumi. Nataka kuanza na Mkoa wa Kagera. Mkoa wa Kagera, uchumi umeanguka, uchumi umekwenda chini sana. Ukiingia leo hii kwenye mitandao wale wakazi wa Kagera na wazaliwa wa Kagera wameunda makundi mengi, wote wanajadili hali mbaya, hali ya kuanguka kwa uchumi Mkoani Kagera. Hata wewe mwenyewe ukiwa unapita kule vijijini, ukaangalia wale watu, unaona kabisa kwamba uchumi umeenda chini na unaona kabisa kwamba umasikini umeongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu inayotoa orodha ya mikoa against GBP per capita ambalo ni pato la Taifa kwa kila mtu, inaonesha kwamba Mkoa wa Kagera sasa ni wa 23 katika Mikoa ya Tanzania Bara. Sisi tunashangaa mkoa ambao una misimu miwili ya mvua, mkoa ambao mvua wastani wake kwa mwaka ni milimita 500 mpaka 1,000. Kwa hiyo, ina maana kwamba mazao mengi yanaweza kuota, lakini unakuwa karibu kwenye mkia kiuchumi katika Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, nina uhakika Serikali inaliona hili, nina uhakika na nyie mnapita kwenye mtandao mnaona yale majadiliano yanayoendelea kuhusu Mkoa wa Kagera. Tunaomba sasa na nategemea kwamba Serikali inakwenda kuja na mkakati wa maksudi wa kuunusuru Mkoa wa Kagera. Ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Kagera ninayo mapendekezo kadhaa.

Mheshimiwa Spika, kwanza, Serikali iwezeshe biashara ya mipakani. Kagera Region is strategical located, imezungukwa na Nchi nyingine kama vile Burundi, Rwanda, Uganda, vilevile ina mpaka kwa kupitia maji Kenya. Hata hivyo, pia ukiangalia wakazi wa East Africa ambao kuna South Sudan, Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda population yake ni watu karibu milioni 195. Hilo ni soko kubwa sana ambalo tukilitumia vizuri tunaweza kuinua uchumi wa Tanzania na tunaweza tukainua uchumi wa Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tufungulie masoko ya mpakani pale Kabanga, Ngara kwenye mpaka wa Burundi, Rusumo kwenye mpaka wa Rwanda, Mutukula kwenye mpaka wa Missenyi, Nyakanazi, Murongo kwenye mpaka wa Kyerwa. Vilevile yako maeneo mengine kama Kashenye, Rubafu, wakiyafungua yale masoko pale, masoko makubwa ya ndizi, masoko makubwa ya mazao mbalimbali, minada mikubwa ya mifugo, utakuta kwamba tutakuwa tumefungua uchumi wa Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sasa ukienda kwenye hiyo mipaka niliyoizungumzia, upande wa nchi jirani unachangamka kibishara, lakini ukiangalia upande wetu wa Tanzania umedorora. Kwa hiyo, hapa kinachohitajika ni kuondoa vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi kwenye sheria za biashara ili ziweze kuwa nzuri, ziwavutie wenzetu wapende kufanya biashara kwenye upande wa kwetu.

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu Mkoa wa Kagera uko mbali sana na Dar es Salaam. Vifaa vingi kwa mfano vya ujenzi vinatoka Dar es Salaam, kwa sababu ya umbali ule unakuta by the time ile product inafika Mkoa wa Kagera gharama imeshakuwa kubwa sana. Kwa mfano, mfuko wa cement unakwenda mpaka unafikia hata Sh.23,000 au Sh.25,000. Kwa hiyo, napendekeza Mkoa wa Kagera upewe upendeleo maalum, differential treatment kwenye sheria, kwenye sera, kwenye kanuni za kibiashara ili sasa kuweza kuvutia wawekezaji na kuwekeza nchi za jirani ili wapende kufanya na sisi biashara.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera ni mkoa wa wakulima, wafugaji na wavuvi na Mwenyezi Mungu alitujalia akatupa Ziwa Victoria. Naomba Wizara zinazohusika wawawezeshe watu waweze kufuga samaki kwenye ziwa kwa kutumia vizimba (cage fishing), lakini vilevile hata kwenye mabwawa, watuwezeshe waweke viwanda vya kuzalisha mbegu, kwa sababu hata wale wanaofuga samaki kwenye mabwawa inafika mpaka miezi tisa bado kasamaki ni kadogo kwa sababu hawana mbegu bora.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa kilimo, Mkoa wa Kagera ni namba moja kwenye kilimo cha ndizi, lakini zile ndizi hazina soko maalum ambalo linaeleweka. Kwa hiyo, unakuta wakati wa kiangazi ambapo ndizi ni nyingi, mkungu bei inaporomoka mpaka Sh.2,000. Kwa hiyo, huyu mkulima anaenda kupata hasara. Tunaomba wapewe Maafisa Ugani wafundishwe matumizi sahihi ya mbolea, mboji, samadi na mbolea za viwandani, lakini watafutiwe soko.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani mpaka leo Kagera tukaendelea kulima mazao yaleyale, kahawa, ndizi, ndizi, kahawa. Lazima tubadilike, hatuwezi kuendelea na traditional crops peke yake. Naomba Serikali waende wahamasishe, tuweze kuanzisha haya mazao mbadala, kwa mfano vanilla, michikichi, parachichi, alizeti, vyote vinaweza kuota Mkoa wa Kagera, hili linaweza likachechemua ukuaji wa uchumi ndani ya Mkoa wa Kagera. Tusiwaache watu wakalima tu. Kwanza tutafute masoko kusudi watakaokuja kulima mazao hayo walime kwa standards zinazohitajika kwenye soko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya ni kwamba labda na uchumi uliendelea kuporomoka Mkoa wa Kagera kwa sababu hakuna zao hata moja la biashara ambalo lina bei nzuri. On that note, napenda nimpongeze sana na nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimshukuru Waziri wa Kilimo kwa juhudi zao za dhati ambazo wamezionesha. Waziri Mkuu ameenda zaidi ya mara tatu, mara nne kuangalia kama anaweza kuchechemua na kuongeza bei ya zao la kahawa. Kwanza alienda kukemea ile ya kuuza butura, kudhibiti butura, wakaondoa tozo kibao kwenye bei ya kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wametuletea mfumo mzuri wa manunuzi kupitia minada na kwa mara ya kwanza katika historia ya Mkoa wa Kagera namna iliyofanyika last time, kilo moja ya kahawa ya arabika imeweza kuuzwa kwa Sh.3,740 ambako tumezoea Sh.1,000 au Sh.1,200. Sasa hivi tulikuwa tunasubiri kuona sasa itakuwaje kwenye hii robusta ambayo ni kahawa ambayo inalimwa na wengi kama na bei na yenyewe inaweza ikapanda vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyowapenda Watanzania. Kwa sasa hivi ametuletea bajeti nzuri, bajeti ya wananchi, kwa sasabu pamoja na matatizo yote yanayoendelea duniani, ambayo yanatokana na athari za UVIKO na vita vinavyoendelea Ukraine huko, lakini yeye ameweza ku-inject ruzuku ya bilioni 100 kupunguza bei ya mafuta.

Mheshimiwa Spika, vilevile tumeona bajeti ya kilimo, sekta ambayo inagusa watu wengi, bajeti yake inapanda kutoka kwenye bilioni 264 kwenda kwenye bilioni 954. Mifugo bajeti yake inapanda kwa bilioni 100. Serikali imenunua boti zaidi ya 250 za kisasa zile za faida, zinaenda kupelekwa kwa wavuvi. Vilevile, wale watumishi wa Serikali ambao wamefikia hadhi ya kupewa magari wanaenda kukopeshwa na hii itaipunguzia Serikali gharama kwa bilioni 500.

Mheshimiwa Spika, vilevile amepandisha mshahara, kitu kilichowafurahisha Watanzania kima cha chini kikapanda kwa asilimia 23.5. Pia wastaafu ile hela yao ya mwisho wanayopewa ya mkupuo imepanda kutoka kwenye asilimia 23 mpaka 33.

Mheshimiwa Spika, elimu ni bure, watoto wetu wanasoma tangu awali mpaka kidato cha sita bila ada. Naishukuru sana Serikali kwa sababu bajeti hii inaenda kuondoa umaskini, bajeti hii inaenda kuongeza uchumi, bajeti hii inaenda kuongeza ajira, bajeti hii inaenda kupunguza makali ya maisha, kweli ni bajeti ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)