Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hoja hii muhimu. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwanza kwa kuaminiwa kuongoza Wizara hii nyeti, lakini pia kwa kazi nzuri ambayo wameifanya na hasa kwa kuleta bajeti ya matumaini makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, bajeti hii kwa maoni yangu ni kweli kabisa imezingatia lile azimio la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba tuwe na bajeti ambazo zinachochea kukua kwa uchumi wa nchi na kuwapunguzia wananchi ugumu wa maisha. Naiona sura hiyo katika bajeti yetu kwa kiasi kikubwa. Hii ni bajeti shirikishi ambayo imeanzia chini kabisa kwenye halmashauri zetu, ikapanda ikatufikia huku juu, kwa hiyo ni rahisi hata utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona jinsi ambavyo bajeti hii imesisitiza juu ya kuongeza pato la Taifa kwa kuweka msisitizo mkubwa katika sekta ya kilimo, madini na hata sekta ya utalii na pia kuongeza mzunguko wa fedha kwa kutenga fedha za kulipa madeni hasa ya wakandarasi na wazabuni wengine na pia fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya kimkakati iliyokuwa inaendelea. Hii itainufaisha sana nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia yako marekebisho ya sheria na baadhi ya tozo ambazo zimeondolewa na nini zote zikielekezwa katika kuchochea sekta binafsi ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia suala zima la kusisitiza juu ya value for money yaani thamani ya kazi kwa fedha zinazotolewa. Nimeona kwa namna pekee kabisa, Ofisi ya CAG inaongezewa wataalam wa fani zingine ili kuipa nguvu zaidi katika kuhakikisha kwamba miradi inakaguliwa kwa uhakika zaidi na kwamba tuendelee kupata thamani halisi ya fedha ambazo tunatoa. Nimewahi kulisema hili katika Bunge hili kwamba hata matumizi yetu ya force account kwenye halmashauri zetu na maeneo mengine yanahitaji sana kupelekewa wataalam wa fani zote ili kwamba tunapofanya kazi hasa za ujenzi tuweze kupata kitu ambacho ni cha uhakika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, iko hofu ambayo inaendelea duniani kote juu ya hili suala la inflation na mdororo wa uchumi. Ukiangalia sana kinacholeta hofu hii ni vita ya Ukraine na Urusi, lakini nasema vita ya Ukraine na Urusi, risasi hazifiki huku, kinachofika huku ni madhara yanayotokana na bei za mafuta na suala zima la chakula. Kwa upande wa bei za mafuta naweza nikasema ni changamoto, lakini upande wa chakula kwetu inaweza ikawa fursa vilevile.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu tukijikita kwenye kilimo kwa nguvu zote ikawa kama vita, kuhakikisha kwamba kila ardhi inayofaa kulimwa, inalimwa na inalimwa mazao ambayo kitaalam yamekubalika kwamba yatatuletea tija, tutafika mahali pazuri. Hata ardhi ya mtu ambaye hajaitumia, kama hailimi sasa either ikodishwe alipwe rent ilimwe au apewe hisa kwa mwekezaji ambaye ataingia pale ili ardhi yote inayofaa kulimwa, ilimike.

Mheshimiwa Spika, mwaka 45 yuko mpiga kura wangu mmoja wa enzi hizo kabla sijawa Mbunge alikuwa anaitwa Reverent Silas Msangi alitunga ule wimbo unaosema Tanzania, Tanzania nakupenda kwa moyo wote. Akaelezea jinsi ambavyo watu watakuja kukimbilia Tanzania ili waweze kupigana kwa ajili ya kupata uhuru kwao. Unabii huo unaweza ukatimia tena na hilo lilitimia kwa sababu ule wimbo ule ulitungwa mwaka 45 ikaja kutimia mpaka kesho asubuhi. Hata sasa hivi tukijikita vizuri kwenye sekta ya kilimo watu watakuja kufatuta chakula kwetu na nchi hii itaendelea kukimbiliwa na watu kama sehemu pekee ambayo itakuwa inapatikana chakula kwa sababu kama ni ardhi tunayo kubwa kuliko ya Ukraine, kama ni hali ya hewa, ni nzuri na hatuna uhaba wa wataalam, watu wamesoma vizuri na uwezo wa kufanya kazi wanao.

Mheshimiwa Spika, nashauri, tujikite kwenye sekta ya kilimo kwa nguvu kama ambavyo tuliingia kwenye sekta ya miundombinu tukaanzisha miradi ambayo ilikuwa ni ya kufikirika na ikatimia. Kwa hiyo, tukiingia kwenye sekta ya kilimo kwa nguvu kwa kiasi hicho tunaweza tukafika mahali pazuri sana. Tusiende tu kwenye hali ile ya kusema, tumetenga fedha nyingi lakini tunaziingiza kwenye miradi kama, sisemi vibaya lakini kilimo kwanza labda na nini ambayo tunaishia kuongeza matrekta ambayo yanaharibika siku mbili. Twende kwenye hali halisi, mazao gani yanafaa hapa, ardhi kiasi gani ipo, yalimwe, yasimamiwe ili tuweze kutoka sisi na kuitoa East Africa yote katika matatizo haya ya chakula.

Mheshimiwa Spika, tunakushukuru sana jana ulituletea wataalam kutoka Benki Kuu pamoja na Taasisi za Fedha, wakatoa mawasilisho yao. Ukiangalia yale mawasilisho yao yameendana kabisa na review ya PricewaterhouseCoopers wanaofanya juu ya bajeti hii. Jambo kubwa sana la msingi lililojitokeza ni juu ya ukweli kwamba inflation kwa sisi Tanzania tuko vizuri kuliko Nchi zote za Afrika Mashariki pamoja na SADC. Wataalam hawa wasingeweza kudanganya. Jambo hili si jambo la kuchuliwa kwa mchezo mchezo, ni jambo ambalo ni la muhimu sana, tukianzia hapa tunaweza kufika mbali.

Mheshimiwa Spika, sasa ukiacha hapa tulipofikia, pamoja na changamoto za corona na za vita vya Ukraine, bado taarifa zinakuja kwamba hoteli zetu na booking zetu za utalii zimejaa na hii itakuwa endelevu kwa sababu ya royal tour. Tukiipokea hii vizuri, Tanzania itapaa na ikipaa tusitegemee mazuri tu, tutegemee na maadui pia wa kiuchumi. Tumeona hapa kiongozi mkubwa wa nchi moja jirani wa cheo cha Senator anatoa kauli za kashfa kashfa za kuingilia suala la ndani ya nchi yetu. Inasemekana basi kama taarifa za kwenye mtandao ni za kutegemea sana, kwamba nchi yetu imepelekwa ICJ. Siamini kwa sababu sioni kwamba lililotokea linaweza kupelekwa ICJ kwa sababu ICJ ina mamlaka za aina mbili. Kwanza, ni juu ya contentious matters ambazo ni ugomvi wa mipaka, ambayo ni magomvi kati ya nchi nan chi, ambalo sasa sio hilo. Lingine labda ni kwenda kutafuta ushauri tu.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba jambo hilo linachochewa na nchi nyingine, inaonesha kabisa kwamba hii ni vita ya kiuchumi ambayo inatokana na hali hii tunayoisema, Tanzania hii tunayoijua ambayo watu wamekuwa wakiitazama kwa jicho kama vile sisi sio watu wa kupiga hatua sana, lakini leo hii tukiambiwa kwamba inflation yetu ipo chini kuliko Nchi zote za Afrika Mashariki na SADC, lazima wajitokeza maadui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani Vyuo Vikuu vilipoanza hapa Afrika Mashariki, Kitivo cha kwanza kilikuwa ni cha Sheria, kwa hiyo naamini kimejizatiti, hata wakienda ICJ twendeni, nina hakika tutajieleza vizuri na tutashinda na tutaendelea kukuza uchumi wetu kwa njia hizo za utalii, kilimo, madini na hata sekta zingine kama za ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amezungumza vizuri Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha juu ya ubora wa barabara zetu na kadhalika na kadhalika. Ukweli tumekuwa tukisema Serikali iwape kipaumbele wakandarasi wazalendo, lakini pia na wao ni vizuri wakaji-link na juhudi kubwa za innovation ambazo zinafanyika katika sekta ya ujenzi duniani ambazo zinahusisha makundi matatu. Kundi la kwanza, ni watengenezaji wa materials za ujenzi na kundi la pili ni wateja pamoja na wajenzi. Teknolojia imepanda sana, hata kama tutajaribu kuwa-favour watu wetu kwa kuwapa mitaji na kadhalika lakini kama watakuwa hawajaweza kuifahamu teknolojia iliyopo sasa, bado wanapokuja watu wa nje kwenye miradi wataonekana bei zao zipo chini na wataweza kupata miradi na miradi yao itakuwa bora zaidi kwa sababu ya teknolojia.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kusema hayo, kusisitiza kwamba tunahitaji kwenda na teknolojia ya dunia na sasa hivi tunaishukuru Serikali, nimeona kwenye bajeti ya Waziri wa Fedha amezunguma juu ya suala la kuzingatia masuala ya TEHAMA katika kuendesha nchi, atatupunguzia gharama na atatuongezea na ubora wa kazi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni hili la ku-take advantage ya hali ya uchumi ilivyo sasa hivi, tunataka tuvuke kwenda mbele lakini tujipange pia kuwa maadui watakuwepo hasa kwa hili ambalo limejitokeza. Nimeona kabisa kwamba hili limejitokeza kwenye sekta ya utalii, sijiingizi kusema kwamba nani yuko sahihi na wapi, lakini suala zima la kuingiliwa na nchi ya nje katika mipango ya utekelezaji wa sheria zetu za ndani sio sahihi.

Mheshimiwa Spika, nilipata kusoma mahali kwamba masuala kama haya ya Loliondo na Ngorongoro mradi tu yanafanyika kwa mujibu wa sheria zetu, hakuna matatizo yoyote, ni jambo la kawaida ambalo linafanyika kila wakati katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, wala halina sura ya ukabila wala ya uonevu, lakini sasa anayeingilia kutoka nje hapo ndiyo inabidi tujipange kwamba kwa kweli hii sasa ni vita. Mara nyingi mti ambao hauna matunda huwa haupigwi jiwe hata na mtoto mdogo, kwa hiyo ukiona mawe yameanza ujue mti wetu una matunda.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naomba Wabunge wenzangu waunge mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)