Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bajeti yetu hii na Hali nzima ya Uchumi wa Nchi. Kabla sijaanza kuchangia bajeti hii naomba kwanza nichukue fursa hii kwa heshima, taadhima na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika Taifa hili ili kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda moja kwa moja katika kuchangia bajeti hii, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika Taifa hili. Sambamba na hili kabla sijachangia bajeti hii sina budi kuzungumza yale mazuri ambayo Mheshimiwa Rais ameweza kuyafanya mpaka hivi sasa na hasa nataka nizungumze miradi mikubwa mikubwa.

Mheshimiwa Spika, katika miradi mikubwa mikubwa ambayo Mheshimiwa Rais aliweza kuirithi kutoka kwa predecessor wake tunazungumzia Mradi wa Rufiji Hydroelectric Power, mradi ule fedha zipo, mkandarasi yupo site na shughuli zinaendelea. Sambamba na hilo, kuna Mradi ule wa SGR Dar es Salaam – Morogoro pamekamilika, Morogoro – Dodoma pako vizuri, Dodoma – Makutupora kwenda Tabora, Mheshimiwa Rais tayari ameshaini mkataba wa trilioni 4.41 na hivi ninavyozungumza shughuli zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sio hivyo tu, katika barabara kubwa kubwa zile na madaraja Mheshimiwa Rais ameweza ku-sign off certificate ya mwisho na kumlipa mkandarasi na amefungua Daraja la Tanzania pale Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, sio hivyo tu lakini marafiki zangu, wajomba zangu kule Wasukuma pale Busisi -Kigongo daraja lile linaendelea kujengwa na shughuli zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amekwenda mbali zaidi, katika suala zima la usafirishaji wa anga, tayari amesaini mkataba wa kununua ndege tano zikiwemo mbili zile kubwa kubwa na mambo mazuri yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, niliona ni vema kuyazungumza haya kwa sababu Mheshimiwa Rais ameweza ku-prove doubt as wrong, kuna wengi walikuwa na wasiwasi kwamba itakuwa vipi, lakini kwa kufanya hivyo tu, Mheshimiwa Rais amekwenda mbali zaidi, ameanzisha miradi yeye mwenyewe ambayo miradi hiyo historia yake ni ya ajabu sana, niseme tu katika moja kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya ni kusaini mkataba wa LNG trilioni 70, fedha ambazo kwa namna moja au nyingine ni historia ambayo itaendelea kukumbukwa ndani ya Taifa hili. Nani kama Mama Samia?

WABUNGE FULANI: Hakuna.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee mbele. Naomba sasa nijikite katika bajeti hii. Bajeti hii malengo yake makubwa ni matatu. Lengo la kwanza ni kuweza kufufua uchumi; lakini lengo la pili ni kuboresha sekta za uzalishaji na lengo lingine ni kuhakikisha kwamba bajeti inakwenda kusaidia kasi ya maisha.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli ulio wazi kabisa, hakuna ambaye anapinga, dunia imekumbwa na msukosuko mkubwa katika suala zima la mambo ya kiuchumi, tukianza na suala zima la corona na vile vile katika vita vinavyoendelea hivi sasa. Kwa tafsiri hiyo maana yake ni nini? Ni kwamba gharama za maisha zimekuwa kubwa sana duniani sio Tanzania tu. Bajeti hii naomba niseme tu, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, inamfanya awe very popular Finance Minister japokuwa mwenyewe huwa anasema kwamba hii bajeti inamfanya asiwe popular Finance Minister. Kwa tafsiri hiyo maana yake ni nini? Imemfanya kuwa very popular Finance Minister kuliko kumchukua mtendaji fulani akampeleka katika timu fulani ambayo haipo hata katika kumi bora Barani Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee mbele, bajeti hii imekwenda kugusa maeneo makubwa mawili; katika level ya kwanza kwenye level ya micro economy na level ya pili katika micro economy Kitaifa zaidi. Ninapozungumza katika eneo la micro economy, bajeti hii ni bajeti ya wananchi kweli kweli kwa sababu: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameweza kuongeza mishahara kwa watumishi na sasa hivi tunakwenda kuzungumzia asilimia 23. Hili ni jambo la msingi sana. Tunajua gharama za maisha zimeongezeka, kwa tafsiri hiyo hiyo ni lazima vile vile tuweze ku-mitigate na mambo mazima ya mshahara na hilo limefanyika katika bajeti hii. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, bajeti hii vile vile imekwenda kugusa wananchi wa kawaida sana, nini maana yake? Hivi tunavyozungumza wanafunzi wanakwenda kusoma bure form five and six. Hii inatuambia kwamba, sasa sisi Watanzania kwa raha zetu. Kazi yetu ukipata mtoto, hangaika naye kulea mpaka miaka saba, akitoka hapo darasa la kwanza mpaka la saba bure. Akitoka hapo form one mpaka form four bure. Akitoka hapo form five mpaka form six bure. Akitoka hapo kwenda Chuo Kikuu kuna fedha bilioni mia tano na sabini Mheshimiwa Rais ameziweka zinasubiri vijana kwenda kuchukua mikopo, nini maana yake? Maana yake ni kwamba, wanafunzi kutoka Mbeya, wanafunzi kutoka Songwe, wanafunzi kutoka Handeni, wanafunzi kutoka Kibiti, wanafunzi kutoka Mtama kwa Wamakonde kule, wote wanakwenda Chuo Kikuu bila shida yoyote nani kama Mama Samia. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Hakuna.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee mbele, bajeti hii katika mambo mengine makubwa na mazuri ambayo imeweza kuyafanya imekwenda vilevile kugusa katika ngazi ile ya micro Kitaifa zaidi. Tafsiri hiyo maana yake ni nini, Mheshimiwa Rais amekwenda mbali zaidi, katika Sekta nzima ya Kilimo na inajulikana wazi kabisa Tanzania asilimia 65 tunategemea kilimo. Pale Mheshimiwa Rais amekwenda kutumbukiza fedha takribani shilingi bilioni 954, nani kama Mama Samia. Kwa kufanya hivyo tafsiri yake ni nini, tunakwenda sasa kuboresha sekta nzima ya mambo ya uzalishaji. Kwani tunajua kule kwenye kilimo ndipo tutakapokwenda kupata malighafi ambazo zitakwenda kusaidia kuzalisha products nyingine zikiwepo vilevile za mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Rais ameenda mbali zaidi katika kuhakikisha kwamba tunakwenda ku-protect viwanda vyetu vya ndani, amefanya jambo kubwa sana, kuna baadhi ya bidhaa ambazo zimekwenda kuongezewa tozo. Kwa kufanya hivyo nini tafsiri yake? Tafsiri yake ni kwamba, tunakwenda ku-discourage importation na kwa maana hiyo tunakwenda ku-stimulate uchumi ndani ili wazalishaji wetu waweze kuendelea. Kwa tafsiri pana ya kiuchumi maana yake ni nini, wale waliosoma commerce wanajua, hapa kinachokwenda kufanyika tunakwenda kufanya mitigation kwenye balance of trade ili twende kwenye balance of payment. Nimwambie tu Mheshimiwa Mwigulu, bajeti hii ni bajeti ya kisayansi zaidi.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee mbele. Pamoja na yote haya naomba niweke nukta zifuatazo vizuri zaidi. Mheshimiwa Waziri wakati ana-present bajeti hapa alizungumza suala la vijana wenye miaka 18 waanze kulipa kodi. Niki-quote hapa kwa ruhusa yako, kwenye chombo kimoja cha habari cha Global Publish kinasema, samahani na-quote:

“Waziri Mwigulu - kila Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 kuanza kulipa kodi”.

Mheshimiwa Spika, hii imeweza kuleta tafaruku kubwa katika mitandao, lakini Serikali na Mheshimiwa Waziri kwa nini namwambia bajeti hii imemfanya awe very popular Finance Minister, hapa kinachoenda kufanyika siyo kwamba mwanafunzi akifika umri wa miaka 18 alipe kodi. Determine factor hapa tunayoizungumza ni suala zima la kipato. Kwa hiyo kwa tafsiri hiyo, nilipa bahati ya kuishi kwa Wamakonde pale Uingereza, wao wanachokifanya, unapofika umri wa miaka 18 unapewa kitu kinachoitwa National Insurance Number Card, nini tafsiri yake? Tafsiri yake ni kwamba unapokuwa tayari ume-graduate umemaliza masomo, unapokwenda kufanya kazi tayari mfumo unakufahamu na hiki ndicho kilichoweza kufanyika katika bajeti hii. Kwa hiyo naomba niliweke hili liwe wazi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na haya yote, naomba vilevile niweze kuweka nukta nyingine sawa na nukta hii ninayoiweka sawa ni nukta inayohusiana na suala zima la Royal Tour. Mheshimiwa Rais amefanya kitu kikubwa sana katika kuifungua Tanzania, kwenye Royal Tour tunajua kwamba tunakwenda kupata mapato makubwa sana kule katika suala zima la utalii. Naiomba tu Serikali, Wizara husika zote lazima ziweze kuchukua nafasi yake, royal tour kama royal tour siyo kazi peke yake ya Wizara ya Utalii; Wizara ya Ardhi lazima sasa muweze kuhakikisha mnakwenda kupima ardhi katika maeneo husika ili wawekezaji wanapokuja siyo wanakwenda kwa Mwenyekiti wa Kijiji kwenda kuomba ardhi kwa ajili ya kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, kama hivyo haitoshi, Wizara vilevile inayohusiana na mambo ya Miundombinu lazima wahakikishe kwamba wanakwenda kufungua miundombinu katika sehemu tofauti, siyo mwekezaji anataka kwenda kuwekeza katika maeneo kama Kibiti maana yake Mukuranga sasa hizi kumeshajaa viwanda, watu wanaanza kuhangaika na mambo ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hayo tu katika Sekta nzima ya mambo ya Mawasiliano, pale ni lazima tuhakikishe tunakwenda kuweka mikonga ambayo itatusaidia. Wawekezaji watakapokuja siyo waanze kusumbuka, mtu kwenda kupiga simu anaenda kupanda katika mti halafu anaanza kupiga simu. Kwa kusema hivi niseme tu, Wizara husika lazima wayaangalie haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, vilevile Wizara ya Nishati lazima wawe makini kuhusu kupeleka umeme kwenye sehemu husika. Wawekezaji wanapokuja siyo tena tuanze kuhangaika kuchukua majenereta na kuanza kuwasha umeme.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, naomba niweke jambo vizuri sana na hili ndiyo la msingi kwelikweli. Pamekuwa na chokochoko kidogo zinaendelea katika mitandao ya kijamii na suala hili linahusiana na suala zima la mambo ya Ngorongoro. Kwanza naomba niipongeze sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kutenga eneo kwa wenzetu ambao wameamua kuhama kwa hiari kwenda kuishi katika maeneo ya Handeni.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, naomba niongee kwa dhati kabisa, sisi Watanzania wote kwa ujumla wake tunajua wafugaji waliopo katika eneo la Ngorongoro ni Watanzania wenzetu na hatukubali waweze kupata shida, lakini pia tunajua Serikali kama Serikali ina nia nzuri kabisa ya kulitatua tatizo hili amicably. Kwa hiyo naomba nisisitize, wale wenzetu majirani katika kipindi cha mwaka 1974 mpaka 1978, wakati huo akili yangu ilikuwa inafanya kazi, zilianza chokochoko kama mzaha hivihivi, kuna watu fulani fulani walikuwa wanataka kuchukua mipaka yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima kwa Kanuni zetu sitoweza kutaja jina la nchi yoyote ile, lakini niseme tu wale majirani zetu ambao wanajaribu kutuingilia katika mambo yetu ya ndani, wakome mara moja, hii hakubaliki. Hii ni Tanzania, sisi tuna uwezo wa kuamua mambo yetu ya ndani, hatuhitaji msaada wa kutoka sehemu nyingine yoyote ile. Inashangaza sana leo hii ukiangalia kwenye mitandao huko utakuta kabisa kwamba kuna maandamano yameandaliwa katika maeneo fulani ya majirani zetu. Sitaki kutaja jina, lakini niseme tu vita hii ni vita ya kiuchumi, Watanzania tuamke, Watanzania lazima walielewe hili, tuweze kushikamana na wenzetu waliopo Ngorongoro, tuweze kuisaidia Serikali ili tuweze kutatua matatizo yaliyopo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)