Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ndiyo ananipa uwezo wa kusimama hapa leo kuongea.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais ambaye ndiye Kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuja na Sera ya kupunguza ada kwa wanafunzi wetu wa form five na form six. Vile vile nampongeza kwa kuangalia maslahi ya watumishi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara ya Fedha, wamekuja na Bajeti ambayo ni nzuri, bajeti inayogusa wananchi, bajeti ambayo imeangalia kila kona na bajeti ambayo inaenda kuleta maendeleo. Pamoja na kuja na bajeti nzuri nitakuwa na ushauri katika bajeti hii. Nianze na ushauri waliokuja nao wa kupunguza mishahara ya watumishi wale wanaokuwa wamepewa vyeo vya madaraka, kwamba madaraka yanapotoka mshahara wake uondolewe. Hili kwa kweli halitaleta tija bali linaenda kuleta mgogoro kati ya watumishi na Serikali yao. Wanakwenda kumletea mgogoro Mheshimiwa mama Ndalichako na Vyama vya Wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Sheria ya Utumishi Na.8 kifungu cha 3 kinaongelea mishahara ya mtumishi na haki zake za kimshahara. Ndiyo maana tukihamisha mtumishi kutoka Taasisi, tunajua Taasisi zina mishahara mikubwa, tukimleta Serikalini huwa hatupunguzi mshahara wake, anaendelea na mshahara wake binafsi, lakini kwa hawa wateule tunasema tuwapunguze mishahara. Hapa naomba nishauri kitu cha kufanya, kaumri kangu haka ni Serikali ya Awamu ya Kwanza ndio sijafanya nao kazi, lakini Serikali zilizobaki zote nimefanya nazo kazi. Zamani uteuzi wa District Executive Directors, District Administrative Secretaries na Regional Administrative Secretaries, uteuzi wote walikuwa wanaenda kwa watumishi ambao wameshakomaa ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mtumishi alikuwa akifika cheo cha Muundo cha mwisho Principal Serikalini, mnaanza kumtania kwamba wewe subiri mwenye mamlaka akuone, kwa sababu hawezi kwenda popote na huyu ameiva kabisa, lakini tuangalie sasa hivi tunawatumia? Hatuwatumii. Kwa hiyo unakuta mtu anaweza akateuliwa kuwa DED au DAS amemaliza Chuo Kikuu tu, hajapata uzoefu ndani ya Serikali, huyu akienda lazima mambo hayatakwenda vizuri na huyu akirudi sasa ndiyo hawa Wakurugenzi Mheshimiwa Waziri ametaja kwamba tunao 300, wamekuja kwa muundo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zamani hawa wateule, walikuwa wanachujwa na Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ndiyo kazi yake kuchuja hawa wateule na walikuwa wakienda wanafanya kazi kwelikweli, lakini hawa tunaopeleka sasa hivi watu wamekuwa wateule wa Mheshimiwa Rais. Unakuta DC anamwambia DED mimi ni mteule wa Rais, DED naye anamwambia mimi ni mteule wa Rais, kazi zinaanza kushindwa kwenda hapa. Sasa ili waweke vizuri lazima mmoja atapigwa chini, sasa huyu anayepigwa anaongeza idadi hiyo ambayo Mheshimiwa Waziri amekuja nayo.

Mheshimiwa Spika, sasa leo tunasema tuanze kuwashusha mishahara, kushusha mshahara mtumishi inatakiwa uunde Tume, umfungulie mashtaka, Tume ije na majibu kusema anatakiwa kati ya adhabu tatu apate mojawapo. Moja huwa ni kushushwa cheo ambayo mmeshampa sasa, mmepiga chini; pili ni kupunguziwa mshahara na tatu ni kufukuzwa kazi. Sasa hizi adhabu tunazoenda kuwapa za kuwapunguzia mishahara Tume gani tumeunda ikakwambia huyu anafaa kupunguziwa mshahara. Hapa naomba Serikali iliangalie kwa mapana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara imesema viongozi wakopeshwe magari, nakubaliana nalo kabisa, lakini tunaweza tukaenda kupoteza viongozi. Awamu ya Tatu ilijaribu wakakopeshwa magari lakini tulipata ajali nyingi sana za viongozi. Anatoka Ofisini amechoka anajiendesha kurudi nyumbani anagonga, saa zingine anawaza Mkuu wake wa Kazi kashampa mikakati ya ajabu, ataifanyaje mwisho wanagonga magari. Tuliwahi kumpoteza Kamishna mmoja alikuwa Kamishna wa Madini, kwa ajali ya kutoka usiku kazini, tuliangalie nalo kwa mapana.

Mheshimiwa Spika, pia imesema CAG wanamwongezea nguvu. Twende tuangalie hayo matumizi, tuwabane kwenye matumizi, tuwabane kwenye manunuzi, ndiko kunakoharibu fedha nyingi ya Serikali, lakini siyo kusema kwamba tuwape magari, tuliwapa halafu baadaye tukaendela kuwapa magari ya Serikali, hapo sioni kama tutaweza kwenda napo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishauri kwenye ukusanyaji wa mapato. Tumeangalia tu ukusanyaji wa mapato, lakini tumejisahau kwenye maduhuli ya Serikali na haya ndiyo makubwa zaidi na hapo ndipo tunapopoteza mapato. Maafisa Masuuli wetu wamepewa mamlaka ya kusimamia matumizi, lakini kwenye mapato wanapasahau. Sasa sijui utasimamiaje matumizi kama hutafuti hayo mapato ili uje kuyatumia. Niishauri Serikali tu Mlipaji Mkuu wa Serikali aingie mikataba na Maafisa Masuuli ya kukusanya maduhuli, asipofikia kiwango cha kukusanya, basi matumizi wasimpe, kwa sababu hakusanyi anachotaka kuja kutumia na mianya inayoleta maduhuli haya yasikusanywe ipo mingi.

Mheshimiwa Spika, twende kwenye pass za kusafiria, passport ambayo ni haki ya kila Mtanzania kuipata nchini humu, angalia utaratibu wake wa kuitafuta, unajaza mafomu, ukijaza ukifika Uhamiaji kwenye counter pale, unakutana na Maafisa wanakwambia hii font uliyotumia, mjazo uliojaza siyo wa kiuhamiaji, rudi ukaanze upya, lakini wanakuelekeza nenda hapo nje. Ukienda Kurasini pale nje, stationery zipo kama uyoga, Ofisi za Wanasheria zipo kibao, unaenda kuanza upya. Sasa kuanza upya kama huyu raia hana safari anarudi nyumbani anaachana navyo kwa sababu alishapanga Sh.20,000 ya Mwanasheria mara ya kwanza amelipa imeharibika, kulipa tena hawezi na muda wake unapotea.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa napiga hesabu kidogo tu ya kujumlisha na kutoa, Watanzania 2,000,000 wakirudi nyumbani bila kuendelea na pass hizo 50 mara 2,000,000 tunapoteza bilioni 100 hapo za maduhuli zinaondoka, lakini sasa aliyepenyeza akapata hiyo passport ikiisha, akirudi anaanza utaratibu uleule wa usumbufu, lakini hii si ni elektroniki, ukiweka kitambulisho changu cha NIDA si unaona rekodi zangu zote. TRA wanawezaje, mbona ukienda leseni imeisha, wakiweka ile leseni, wanatoa wanakuona rekodi zako, unalipa 70,000 wanakupa leseni yako mpya unaondoka. Huku kwenye passport tunashindwaje, kuweka ile NIDA tukaona rekodi za huyo raia, tukampa pass yake ya kusafiria. Kwa hiyo sasa pass imebaki siyo Sheria ya Kikatiba kwamba tuna haki ya kumiliki pass za kusafiria, imebakia unaitafuta wakati unataka kusafiri. Hapa ukitupa safari ndiyo tutahangaika kutafuta pass kwa sababu unaona unahangaika bure, hapo tunapoteza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuje NIDA, NIDA napo kuna mapato yanapotea kwa kuzungusha raia kupata vitambulisho vya NIDA na penyewe ukichukua tu watu 2,000,000 waone huu usumbufu waache waende pembeni, kwa 20,000 tunapoteza bilioni 40, hapo ni kwenye NIDA napo pia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, niongeze dakika mbili tu nimalizie.

SPIKA: Mbili utakuwa unampunguzia mwenzako mwenye muda wake, sekunde 30 malizia sentensi.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Twende kwenye NIKONEKT ya TANESCO waliyoanzisha, si rafiki kwa raia. Napeleka kadi ya NIDA wanaweka namba, lakini ile fomu ina maswali, inakuuliza mpaka babu wa bibi yako. Babu wa bibi yako nani? Jina lako nani? Shule ya msingi umesoma wapi? Wakiweka namba za NIDA si wanaona hivyo vitu. Naomba wafanye hii mitandao yote isomane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono, ahsante sana. (Makofi)