Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini niipongeze sana Wizara, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kwa jinsi alivyoitengeneza hii bajeti, inaonekana hakika ni bajeti ya Watanzania. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jambo jema alilolifanya la kuongeza elimu bure mpaka kidato cha sita. Hii inaonesha ni jinsi gani Ilani ya CCM inavyotekelezwa na ziada maana huu hakika ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lakini ni jinsi gani Mheshimiwa wetu Rais anaonesha anawajali Watanzania na hasa akinamama, maana akinamama ndio wenye mzigo mkubwa ndani ya familia. Hili jambo ni zuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kutokana na suala hili zuri liongezeke pia suala la ajira kwa Walimu ili wawe wengi kwa ajili ya kuleta tija kutokana na hii elimu bure. Isije tu ikawa elimu bure lakini madarasani Walimu hawatoshi. Ni wananchi wengi sana ambao hawana ajira wako mtaani, kutokana na suala hili mimi ninaamini kabisa Serikali imelenga huko huko, japokuwa tu tunashauri na sisi kama Wabunge, lakini naamini kabisa lengo la Serikali pia hapa ni kuongeza ajira kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee pia suala kama aliloongea Mheshimiwa Mbunge mwenzangu kuhusiana na hili suala la asilimia 10. Serikali iangalie sehemu ya kutoa hii fedha asilimia hii kwa ajili ya shughuli inayotakiwa kufanyika. Ni jambo zuri na ni jambo jema, lakini naamini kabisa wajasiriamali wengi mtaani ni vijana, akinamama lakini pia wamepunguza idadi ya mambo ambayo yangefanyika hasa kwa hawa vijana ambao wanajiajiri wenyewe ambao labda wangefanya uhalifu, uharibifu, lakini wamejiajiri kutokana na hii mikopo midogo midogo.
Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ikiwaondolea tena hii asilimia itabaki nini kwa maana moja au nyingine ile asilimia waliyokuwa wanapata vijana asilimia nne akinamama asilimia nne na walemavu asilimia mbili na hapo sasa hatuoni kitu cha kubaki. Sidhani kama mimi ni mmojawapo wa ku-support suala hili. Kwa kweli tuiombe Serikali iondokane na wazo hili la kuondoa hii fedha ibaki pale pale na ikiwezekana bajeti ijayo wawaongezee, hii fedha ni kidogo sana haitoshi, huko mtaani watu hawana ajira na wamejiajiri wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende pia kwenye suala la kumpongeza sana mama yangu Mheshimiwa Rais kwa hili suala la kuanzisha Chuo Kikuu cha TEHAMA hapa Dodoma. Ameupiga mwingi sana, kwa kweli amefanya jambo zuri sana kwa sababu pia itaongeza ajira kwa vijana. Hata hivyo, niishauri Serikali na ombi langu kwa Serikali, Mkoa wa Mara ni Mkoa ambao unatakiwa uangaliwe kipekee kwa sababu ni mkoa uliomtoa muasisi wa Taifa hili Hayati Nyerere. Katika mazingira hayo kutokana na nchi za wenzetu tunavyoziona mikoa kama hii ya watu muhimu kama hawa huwa ni mikoa ya kihistoria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutukubalia suala la kuweka eneo la historia au eneo la utalii pale Butiama, lakini haitoshi na sisi pia Mkoa wa Mara tunapaswa kuwa na vyuo vya ziada ambavyo vitakuwa ni mfano, lakini vitakuwa ni vyuo ambavyo vinaonesha kabisa muasisi wa Taifa hili ametokea Mkoa wa Mara; na sisi pia Mkoa wa Mara tungeomba basi baadaye tuletewe Chuo cha TEHAMA ili kusudi kuutambulisha Mkoa wa Mara kwamba ndio mkoa aliotoka muasisi wa Taifa hili na vyuo vingine pia vya mahesabu, lakini pia na vyuo vikuu mbalimbali. Kwa hili nimpongeze sana mama yangu lakini ombi hili kwa Serikali naomba sana lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna hili suala la matatizo yaliyotokea kwa wenzetu. Niwaombe ndugu zetu au majirani zetu wa nchi Jirani, sisi Watanzania tuna amani yetu ya kutosha, lakini wanapaswa kujua kabisa kwamba Tanzania ni nchi huru nchi inayojitegemea. Masuala ya kuingilia uhuru wetu haiwahusu wao washughulikie matatizo yao, sisi kama ni furaha yetu tutashughulikia wenyewe, kama ni matatizo yetu tutashughulikia wenyewe kama nchi, wao hawapaswi kuingilia masuala ya Tanzania na kuleta chokochoko zao Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli hiki ni kitendo ambacho tunakilaani sana na sisi Watanzania au wawakilishi wa Watanzania tunawaambia wasirudie tena na hasa wale wenzetu ambao pia wanafikia hatua hata ya kumtusi Mheshimiwa Rais wetu, wajue kwamba yule ndio kiongozi wa nchi yetu. Wanapomtusi Mheshimiwa Rais wanatutusi sisi wenyewe Watanzania. Watanzania tushikamane kwa pamoja tuiangalie nchi yetu tukijua kabisa hii ni vita ya kiuchumi, mbona haya hayajatokea kabla mama hajaanza kutangaza Royal Tour? Wameona sasa Tanzania tunakwenda juu sana katika utalii wameona sasa waanze kuleta chokochoko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi tuseme tuko pamoja Watanzania tuungane kwa pamoja matatizo yetu tutayamaliza wenyewe na mambo ya Tanzania tutayashughulikia wenyewe, hatumhitaji mtu yeyote wa nchi ya jirani kuja kushughulikia matatizo ya Tanzania au kuendelea kuleta matatizo ndani ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tunawaambia wakae wakijua Tanzania ina Majeshi ya kutosha, lakini Tanzania ni nchi ambayo iko imara, wakituletea chokochoko, Mheshimiwa Rais akija akisimama akisema, wajue kabisa watakiona na wasirudie tena kumtusi Mheshimiwa Rais. (Makofi) [Maneno haya siyo sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)