Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya upendeleo. Awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa na kwa dedication na dhamira ya dhati aliyonayo kwenye masuala mazima ya TEHAMA. Tumeona mipango yake mizuri kwenye masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu, kwa kweli nimpongeze Mheshimiwa Rais na nimwambie tu kwamba anawatendea haki Watanzania. Takwimu zinatuonesha kwamba ikifika mwaka 2065 katika nchi zote za Afrika, Nchi za Afrika Mashariki ndizo zitakazoongoza kwa idadi kubwa ya watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, takwimu zinatuambia katika nchi nne za Afrika Mashariki ikifika mwaka 2065 idadi kubwa ya watu watakuwa ni vijana yaani tutakuwa tuna the most youthful population Afrika nzima. Takwimu zinatuambia ikifika mwaka 2065 tutakuwa tumekwenda mara tatu ya idadi ya watu ambayo tunayo sasa hivi. Yaani kwa mfano Kenya watatoka milioni 56 watafika milioni 115, Uganda watatoka milioni 48 watakwenda milioni 141, Rwanda watatoka milioni 11 watakwenda milioni 25 na sisi Watanzania tutatoka milioni 60 mpaka milioni 186. Sasa takwimu hizo zinatuambia katika idadi hii ya watu asilimia 62 watakuwa ni vijana kuanzia miaka 18 mpaka miaka 35. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna nyingine takwimu zinatuambia hawa ndio watakuwa walipakodi wetu wakubwa. Idadi hii ya watu katika umri huu ndio ambao watakuwa tegemezi la Taifa letu kwa miaka kadhaa ijayo. Sasa nasema haya kwa sababu kwanza ningependa niwapongeze vijana wenzangu katika Taifa hili, pamoja na changamoto za ajira, vijana wanamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kujiajiri kwa shughuli ndogo ndogo. Kwa kweli niwapongeze sana, pamoja na changamoto mbalimbali za miundombinu, lakini vijana wa Taifa hili hawajaacha kupambana kwenye kujiajiri ili kusaidia shughuli za maendeleo ya Taifa lao. Niwatie shime vijana wenzangu na niwaambie waendelee katika kutafuta mbadala wa ajira bila kuchoka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vijana hawa wanajitahidi sana, ningependa nimwombe Mheshimiwa Waziri awafute jasho vijana. Awafute jasho vijana kwenye kuwasaidia kutengeneza faida kwenye shughuli za kimaendeleo wanazozifanya, kwa kuondoa vikwazo vidogo vidogo vya kibiashara ambavyo vinawarudisha nyuma. Wote tunafahamu katika vitu ambavyo vitasaidia kuondoa changamoto ya ajira katika Taifa hili ni teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna applications ndogo ndogo zinatumika ambavyo zimeajiri mamia ya vijana, wote tunaifahamu taxify pamoja na changamoto zake imewaondoa vijana mtaani imeajiri Malaki ya vijana, wanapata ajira ndogo ndogo. Kwa hiyo, tunafahamu kumbe application moja ikiajiri vijana karibu laki moja, tukiweka mazingira wenzeshi ina maana vijana wengi sana wataajirika kwenye hiyo, lakini sasa changamoto ni moja. Kama applications hizi zinaleta ajira tunajiuliza kwa nini vijana wengi sasa hawaleti ubunifu ili application hizi ziajiri wengine? Bunifu wanazo, tatizo ni uwezeshaji wa kimiundombinu, hawana fedha za kusimamisha biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mikopo tunayotoa leo tunataka vijana wetu waende wakajenge matofali, wakafanye ujenzi, wasage unga, haiwezekani ajira hizi haziwezi kuajiri vijana wengi kwa wakati mmoja. Kuna tatizo gani la hatimiliki za application za vijana kutumika kama dhamana ya mikopo yao? Kwa sababu ni vitu ambavyo ndio vinawaletea fedha. Duniani kote intellectual property inatumika kama dhamana kwenye mikopo, lakini hii mikopo yetu ya halmashauri nani ametuwekea uzio tusiwape vijana wabunifu mikopo ili iweze kuwasaidia? Kwa hiyo, nadhani tuanze kufikiria tofauti, sio lazima tu tufanye kazi hizi physical katika kuwapa vijana mikopo, tufikirie na hawa vijana ambao bunifu zao zitaajiri vijana wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka pia nishauri jambo moja, nimeliongea hapa Bungeni mara nyingi sana na nitaongea kwa masikitiko makubwa sana. Nilisema vijana wa Kitanzania wanapambana sana, lakini kuna mifumo ambayo ipo kwenye mikono ya Mheshimiwa Waziri, kanuni Mheshimiwa Waziri ndiye mwenye mamlaka nazo, suala la PayPal itatuingizia kodi, PayPal itaongeza fedha kwenye Serikali yetu, sasa kigugumizi kiko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilivyofuatilia kuhusu PayPal nikaambiwa kwamba, PayPal wenyewe wanasema hawana soko Tanzania. Jamani, Tanzania ndio inaongoza kwa idadi kubwa ya watu Afrika Mashariki, soko lipo Tanzania, tatizo jirani yetu ni janjajanja sana, ndio maana anataka fedha zetu zipitie kwake. Sasa wataalam wetu wasipoenda hatua mbele zaidi kugundua vikwazo kama hivi vya majirani zetu ambao wanatufinya ili vijana wetu wasiweze kupata fursa kama hizi, inakuwa ni shida. Ndio maana leo hapa tunawalaani kwa kuingilia kwenye masuala yetu kama ya Loliondo.
Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri suala la PayPal, Tanzania is the biggest market, kwa hiyo, tusipoenda hatua mbele kujua kwamba, jirani yetu anatuwekea janjajanja ili fedha zetu tuzipitishe kwake, vijana wetu wataendelea kutaabika kwa kiasi kikubwa mno kwa sababu, kama kweli hamna biashara kwa nini wanaruhusu tuwalipe kupitia application yao? Kwa nini wao hawaruhusu sisi tusilipe kupitia application yao? Yaani tunalipa, lakini hatuwezi kulipwa, hatuwatendei haki vijana wa Kitanzania. Naongea kwa masikitiko makubwa kwa sababu, suala hili lina miaka 10 nyuma, hatuwezi kukaa hapa kila Bunge tukazungumza masuala ya PayPal. Mheshimiwa Spika alilitolea maelekezo mwaka jana, nilitegemea mpaka kufikia kipindi hiki tutakuwa tumepiga hatua kwenye masuala ya mustakabali wa vijana wa Taifa hili, wanaohangaika kutafuta ajira na kujiajiri. Hatuwezi kukubali wakwamishwe na vikwazo vidogo vidogo ambavyo vikitatuliwa vitaleta nafuu kwa wao pamoja na Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye suala la PayPal naomba alitafutie muarobaini kwa sababu, kama kuongea tumeshaongea sana. Labda sasa watuambie tufanye nini? Sisi kama vijana hatuwezi ku-match kwenda kwenye Makao Makuu ya PayPal kwa sababu, uwezo hatuna. Tunaamini Serikali yetu kama inataka kodi itatuwekea mazingira wezeshi ya kutusaidia ili tuweze kufanya biashara na tuweze kupata malipo ya kulipa kodi. Kama suala ni wao kuja kuweka physical presence in Tanzania wanaweza wakashirikiana na makampuni mengine kwa ajili ya kuwa wawakilishi wao hapa nchini kwetu Tanzania. Pia kama suala ni kodi, Serikali inaweza ikapata kodi kupitia mwakilishi ambaye ni kampuni. Kwa hiyo, kwa kweli kwenye suala la PayPal naomba Mheshimiwa Waziri alivalie njuga. Sisi tunalipa hatulipwi, hatuwezi kwenda kupitisha fedha kwa jirani. Naongea hili suala la PayPal l kwa uchungu kwa sababu tulishaliongea sana, Mheshimiwa Waziri naomba atusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye suala lingine la masuala ya ubunifu. Vijana wa Kitanzania hawajaanza kubuni magari leo, wameanza kubuni magari siku nyingi sana, lakini tujiulize kwa nini haviendelei? Hata hivyo, juzi alitokea mbunifu mmoja akabuni watu wote wakaenda kwake. Ni vizuri, lakini tumesahau vijana wa Taifa hili wameanza bunifu siku nyingi mno, lakini kuna vikwazo vya kibiashara na vikwazo vinaanzia TRA. Tunataka tu-recognize vitu tu ambavyo vinatoka nje ya nchi, yaani mpaka uthibitishwe kwamba, bidhaa yako uliyobuni inafaa kwa matumizi ya Watanzania, unasota ile mbaya. Sasa hawa vijana ambao wanabuni tunawarudisha hatua 10 nyuma, yaani mifumo nyetu yenyewe inatambua vitu vya wenzetu kuliko vitu vyetu sisi wenyewe. Naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri. Kama kweli tunataka mabadiliko kwenye masuala ya sayansi na teknolojia, lazima tuanze kwenye kubadili mifumo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimalize na jambo la mwisho kuhusiana na uwezeshwaji wa vijana. Wote tunafahamu maendeleo makubwa kwenye nchi mbalimbali yameletwa na viongozi ambao ni vijana, ikiwemo sisi hapa Tanzania; Uhuru wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliupambania akiwa na umri wa kijana. Kwa hiyo, nasema hivyo kwa maana moja, naunga mkono kwamba, yatupasa tuwe na vijana ambao wametayarishwa kwa ajili ya kushika nafasi za kimaamuzi, lakini haimaanishi vijana wa Taifa hili hawawezi kushika nyadhifa za uongozi katika Taifa hili, vijana wanaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningependa nishauri kwenye hili suala zima la nafasi za teuzi, pale ambapo wanashushwa nafasi. Huyu mtu kama alikuwepo Serikalini, ana nafasi yake ya mwisho, kuna nafasi ya mwisho ya juu kabisa kwenye rank husika. Kwa mfano, kama ulikuwa lawyer, nafasi ya mwisho kabisa pale juu kwenye lawyer basi arudishwe pale juu, lakini sio nafasi zote za teuzi ni kwa ajili ya watu ambao wako Serikalini peke yake, kuna watu wa sekta binafsi. Kwa hiyo, leo hii tukisema vijana wasipewe nafasi kisa tu hawakufanya kazi Serikalini, hatutendi haki na vilevile ikifika 2065 population kubwa ni vijana whether tunataka ama hatutaki, lazima tuwa-groom waweze kuja kuwa viongozi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie vijana wanafaa kuwa viongozi wa Taifa hili, let’s groom them, tuwatayarishe kuja kushika nafasi za kimaamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)