Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza kwa jioni ya leo. Nianze tu kwa kusema naunga mkono hoja ya Bajeti ya Serikali, lakini pia nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wasaidizi wake wote Makamu wa Rais, Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wa Wizara hii kwa bajeti nzuri ambayo kimsingi imekidhi mahitaji na matakwa ya wananchi, lakini pia wame-consider kwa kiasi kikubwa sana maoni ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu nimwombe tu Mheshimiwa Waziri atakapopata nafasi aweze kuielezea ile factor ya kusema kwamba mtumishi hasa watumishi wa kuteuliwa atakapokuwa amepoteza nafasi yake basi anarudi nyuma kukidhi kwa maana ya kuchukua mshahara ule ambao alikuwa analipwa mwanzo. Yaani maana yake ni kwamba kama mtu alikuwa ni Afisa Mtendaji wa Kata mamlaka zikamwona kutokana na utendaji wake mzuri, akateuliwa akawa Mkuu wa Wilaya, baada ya mwaka mmoja au miaka miwili akapanda akawa Mkuu wa Mkoa, kwa sababu utendaji wa kazi ndiyo unamfanya apande hizo nafasi na namna mamlaka zinavyomwona, lakini pale utumishi wake unaposita anarudi kuchukua mshahara ule wa Mtendaji wa Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kuna miaka mitatu hapa amepoteza, nataka nijue anarudi kwenye mshahara upi? Kwenye mshahara ule wa awali kipindi anateuliwa kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya au atarudi kwenye mshahara upi? Kwa sababu hapo miaka mitatu naamini wenzake pia kuna mishahara imeongezeka. Sasa nataka nijue tu na Mheshimiwa Waziri atakapopata nafasi aielezee kwa sababu hii ndiyo watumishi wengi hasa hawa ambao wanakumbwa na nafasi za uteuzi wametengeneza taharuki hiyo. Mtu alikuwa ni Mwalimu analipwa Sh.400,000, ameonwa na mamlaka amekuwa Mkuu wa Wilaya ana-stop Ukuu wake wa Wilaya anarudi kwenye mshahara wa Sh.400,000 ule ule au wata-consider na ile miaka yote ambayo amepoteza kwenye nafasi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite kwenye mchango wangu na nitachangia katika maeneo matatu. Eneo la kwanza, kama nilivyoanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, nimesoma vizuri sana bajeti hii na nimekesha vizuri, nimeisoma kwa kiwango kikubwa, lakini niseme na kwa kumkumbusha sekta ya ardhi kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha hajaiweka. Sekta ya Ardhi haijapewa kipaumbele kama zilivyopewa sekta nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisema na tumekuwa tukishauri hapa, ukisoma yale maeneo yote ambayo fedha za Serikali zinakwenda kwenye mahitaji muhimu kwenye sekta mbalimbali, ardhi haijaguswa na nimekuwa nikisema na tumekuwa tukisema hapa Mheshimiwa Waziri atakumbuka ardhi ni rasilimali asilia, ardhi ni mtaji, lakini ardhi pia ni chanzo cha mapato. Bahati nzuri kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri amesema kwamba dhima ya bajeti ni kwenda kujenga uchumi shindani wa viwanda na maendeleo ya watu. Huwezi kujenga uchumi shindani wa maendeleo ya watu kwenye viwanda kama ardhi haijazungumzwia kwa kiwango hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapopata nafasi mwishoni wakati wa majumuisho yake, aje aizungumzie ardhi kama sekta ambayo ni sekta mtambuka, ni sekta ambayo haya mengine yote tunayoyafanya ya uchumi wa maendeleo ya viwanda hayawezi kufanyika bila kuwekeza kwenye ardhi. Ningetamani Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anazungumza ajikite kwenye maeneo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kutambua umuhimu wa sekta ya ardhi, mwaka jana alitoa zaidi ya bilioni 50 kwa ajili ya kwenda kwenye mamlaka za upangaji na upimaji kwa maana halmashauri na ilikwenda kazi ya kupanga, kupima na kurasimisha. Ukisoma kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri haizungumzwi. Pia tunatambua mwaka huu ametenga zaidi ya bilioni 345 ambayo inakwenda kwa ajili ya kuhakikisha hizo kazi za kuboresha miundombinu ya sekta ya ardhi kupanga na kupima na maeneo mengine ningetamani nayo aielezee kwa maana sekta ya ardhi ni sekta mtambuka na kwa kutoa maelekezo namna fedha hizi zitakavyoenda kunufaisha sekta ya ardhi na maeneo mengine. Siyo hivyo tu, tuna zaidi ya bilioni 130 ambazo zimetoka Korea, hii yote ni michango ya Mheshimiwa Rais. Ukisoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ardhi ni kama vile haijaguswa kwa ukubwa unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho mwishoni aiweke na aizungumze ili angalau mamlaka za upangaji na upimaji na wananchi na wadau wengine wa sekta ya ardhi, lakini wajue ni namna gani ambavyo Serikali imejipanga kwenda kuboresha kwenye sekta ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni miradi ya kimkakati pamoja na vyanzo vya mapato ya halmashauri. Kwa kuwa Wizara ya Mheshimiwa Waziri ndiyo imekuwa ikijikita sana kwenye kupanga matumizi na kupeleka fedha za miradi ya kimkakati, zipo halmashauri ambazo ni za kimkakati lakini mapato yake ni madogo sana. Mathalan, Wilaya yangu ya Rorya, ndiyo maana tuliwahi kushauri hapa, ni vema Wizara ya Fedha ikafanya mchanganuo wa halmashauri ambazo zipo mipakani, mapato yake ni madogo, siyo stable, haya-sustain na wakati mwingine wanakusanya kwa kujinyima kweli kweli, hawa ndiyo wapewe fedha za miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaona kwenye mapendekezo ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba sasa tunakwenda kuiboresha, kuichanganua ile 10% iliyokuwa inatoka, kwamba itoke asilimia tano, asilimia mbili mbili. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi, kuna halmashauri ambazo kwa mwezi wanakusanya milioni 40 peke yake, mfano kwangu Rorya, ukikusanya milioni 40 Rorya, ukitoa asilimia kumi ni milioni nne, ukianza kuigawanya kwa kipindi hiki kwa sasa kwa asilimia 4:4:2, maana yake unaweza ukaona kwamba vijana walikuwa wanapata milioni 1.6 peke yake, Sh.1,600,000 kikundi cha watu 10 wanaitumia vipi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa umeenda tena umeinyambulisha, umeigawa, unasema itakwenda 2%, yaani maana yake wale waliokuwa wanapata Sh.1,600,000, kikundi cha vijana 10 wanapata 800,000 kwenye halmashauri zenye mapato madogo kama Rorya. Kwa hiyo naomba kama kuna uwezekano tuiache ile10% iende vile vile 4:4:2, ile fedha 5% ambayo ilikuwa inakwenda kwa ajili ya Wamachinga, tuendelee na mkakati ambao Mheshimiwa Rais ameshatusaidia, amepeleka zaidi ya bilioni 10 kwenye kila mkoa, ziende zikaboreshe maeneo ya Machinga, tusiguse kule, kwa sababu ukigusa kule kwa sababu ukigusa kule, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi vijana sasa kwa kasi inayokwenda, kwa growth rate ambayo inakwenda mpaka kufika 2025 kutakuwa na vijana wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tulipo kuna msururu wa vijana, makundi ya vijana wameomba mikopo kwenye halmashauri zetu, lakini hawajapewa. Sasa ukipunguza kile kiwango kwenye halmashauri inayopokea milioni 40, wapo watu 10 wanapokea milioni nane, haitafaa hata kidogo. Kwa hiyo naomba nishauri kwenye hilo, tuone namna ya kulifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, ni namna ya kuboresha kwenye maeneo ya mipaka. Niliwahi kuchangia hapa kutumia fursa za kimpaka kati ya halmashauri ambazo ziko ndani ya nchi na nchi. Kwangu Rorya, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami nimekuwa nikisema hapa tuna Bandari ya Sota, pale ndani ya wilaya yangu, lakini hatujawahi kuona namna gani inanufaisha uchumi wa nchi yetu. Tuna mipaka yetu pale Kirongwe, nichukue nafasi kwanza kuwashukuru watu wa TRA, baada ya kuona nimezungumza kwa muda mrefu, sasa wameweza angalau kuboresha sehemu ile, lakini tukumbuke ndani ya kilometa 35 hakuna udhibiti wowote. Niliwahi kusema hapa kuna ng’ombe wanavuka, wanapita ndani ya mpaka ule kwa siku siyo chini ya ng’ombe 200 au 300, Serikali inapoteza fedha pale, ningetamani kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri aone namna ya kusaidia haya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia kwenye maeneo ya mnada wa upili kwenye maeneo ya mipaka kupitia Wizara ya Mifugo, nimekuwa nikisema vile vile zaidi ya kilometa 35 mpaka 40 ili uweze kutembea pako wazi, pale chochote kinafanyika, inawezekana ninavyozungumza kuna watu wanavusha mifugo, Serikali inapoteza mapato mengi sana pale, niombe sana nalo hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kwenye suala la kulipa kodi, nimpongeze na nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo ameona kwamba sasa vijana wote ambao wanafikisha miaka 18 waweze kuwa na TIN Namba. Nimekuwa nikisema hapa na ningetamani mwishoni nalo pia alitolee maelezo, tunazo Taasisi za umma ambazo zinadaiwa zaidi bilioni 78 na Wizara ya Ardhi kama kodi ya ardhi, hawana tofauti hawa watu na mwananchi mnyonge ambaye tunamwambia nenda kalipe kodi yako leo na wakati tunayo mataasisi ya umma, mashirika ya umma yanadaiwa zaidi ya milioni 78. Yaani kama ndiyo hivyo kama tunashughulika na mwananchi kumwambia nenda kalipe kodi, haya mashirika yetu ambayo tunayo zaidi ya 114, lini wanalipa hizo hela?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema nimpongeze Waziri namna alivyosema kwamba Wakurugenzi wa hizi Taasisi wawe wanaingia kwa kufanya interview, lakini naomba asiishie hapo tu, aende awaambie Mkurugenzi asiyeweza kulipa kodi ya Serikali kama ambavyo tunashughulika, wao ndiyo wanatakiwa wawe mfano, hawalipi zile fedha, matokeo yake ni kwamba, Wizara ya Ardhi kila mwaka ikipanga bajeti zaidi ya 35% ya bajeti ya Wizara ya Ardhi kwenye kodi ya ardhi inategemewa kupatikana kutoka kwenye mashirika ya umma. Halafu ndani ya 35% hayo mashirika hayalipi hiyo fedha, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri aikazie hii, haya mashirika ya umma yanayodaiwa fedha za Serikali, walipe tusiwe tunakwenda tunamng’ang’ania tu mwananchi kulipa halafu tunayo mashirika ndani yetu na hayalipi kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwa umuhimu wake, niombe sana Mheshimiwa Waziri wanapopanga hii bajeti na wanapokwenda kutengeneza mipango waangalie mazao ya kimkakati ya kila mkoa. Nilikuwa naona hapa kwenye kilimo Mkoa wangu wa Mara kila nikiusoma sioni, nilikuwa natamani sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alione hili, hatuna zao la kibiashara la kimkoa ambalo tunatakiwa litunyanyue sisi kama mkoa, tunaona mikoa mingine inavyokwenda, lakini Mkoa wa Mara hatujafika mahali tukaona namna gani Serikali imepanga mikakati ya kutengeneza zao la kibiashara na likasimamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo maeneo mengi ya kiuchumi kama viwanda vimekufa, Bandari ya Musoma imekufa, tulitamani angalau na sisi kupitia kilimo tuone ni zao gani ambalo Wizara imefanya utafiti na twende kutoa elimu kwa wananchi ili angalau liwe ni zao la kutubeba watu wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)