Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii. Nianze kwanza kwa kuipongeza Serikali kwa bajeti nzuri sana ambayo kwa kweli imeleta matumaini makubwa kwa Watanzania na hasa wanyonge. Pia nimpongeze Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo amekuwa akituletea maendeleo. Vile vile niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Naibu wake kwa kutusomea bajeti nzuri sana yenye matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo mchumi, lakini nizungumze kidogo kuhusu mambo ya inflation. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Mwigulu, Waziri wa Fedha ni kwamba hali ya uchumi sasa hivi kidunia imepungua kwa asilimia 3.1, badala ya matarajio ambayo ilikuwa ni asilimia 6.0. Katika hilo hilo suala la inflation wanasema kwamba mpaka hapa tulipo katika soko la dunia bidhaa nyingi zimepanda kwa asilimia 24, lakini mfumuko wa bei kwenye soko la dunia kwamba umeongezeka kwa asilimia 5.7 kwa nchi zilizoendelea na kwa nchi zinazoendelea ni asilimia 8.7, maana yake ni kwamba bidhaa zitaendelea kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zimetolewa sababu nyingi ambazo kwamba mojawapo ni hii ambayo ni ya vita ya Ukraine na Russia, lakini na suala la UVIKO 19, tunashukuru Mheshimiwa Spika alituletea wale wataalam jana ambao wengine walikuwa wametoka BoT na wengine wa Serikalini kwa ajilli ya kutupitisha sehemu mbalimbali katika kuangalia mambo ya uchumi. Moja ya kitu ambacho kinahitaji elimu ya kutosha, ni pale waliposema kwamba hata kusingekuwa na vita ya Ukraine na Russia, bado bei kwa mfano za bidhaa zilizopo sasa zingeendelea kuwepo hapa zilipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mwananchi wa kawaida inatakiwa kutolewa elimu ya kutosha ili ajue tunafikaje hapo, kwa sababu hawa wataalam wetu pia ndiyo wanapita na mitaani na wananchi pia wanawasikiliza, kwa hiyo siyo kitu cha ajabu kumwona mwananchi wa kawaida akisema uchumi huu kudorora au bei kupanda siyo kwa sababu ya vita ya Russia na Ukraine, ni kwa sababu ya elimu kama hii. Kwa hiyo kuna umuhimu wa kutoa elimu ya kutosha ili watu waelewe maana ya mfumuko wa bei ni nini, lakini pia kuwapa wananchi njia mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuna suala pia la umwagiliaji kwenye kilimo. Kwa kuwa hali ya hewa si nzuri sana kwa nchi yetu na huenda kukawa pia hatutarajii lakini pengine sehemu zingine zikapata upungufu kidogo wa chakula, kuna umuhimu sana wa kuimarisha hizi skimu za umwagiliaji ili tuweze kufanikiwa katika kujihami na suala la chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sekta ya Afya Mheshimiwa Mwigulu alituambia kwamba sasa hivi baada ya miundombinu kuboreshwa, tatizo kidogo limekuwa kwenye upungufu wa wahudumu wa afya. Tunaomba hiyo miundombinu ambayo tayari imejengwa kwa muda sasa na iko kwenye mafanikio mazuri, ili iweze kuwa na ufanisi, basi Serikali ifanye jitihada za kutosha kupatikana kwa hawa wahudumu wa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la elimu, Serikali imefanya vizuri, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwarudisha mashuleni wale watoto wa kike ambao walikuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ujauzito. Hata hivyo, pia kumekuwa na changamoto, kwenye elimu pia kuna upungufu mkubwa sana wa Walimu na hasa vijijini. Sehemu nyingi vijijini bado kuna upungufu wa Walimu, Serikali ifanye mkakati wa kutosha na ikiwezekana hata kurekebisha baadhi ya kanuni au Sheria za kuwalazimisha Walimu wakae vijijini. Vinginevyo hili tatizo litakuwa ni la kudumu na tutaendelea kuliimba kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu bure mpaka kidato cha sita tunaipongeza sana Serikali kwa kuamua hivyo. Hata hivyo, Serikali iangalie uwezekano wa kutoa chakula, kama haiwezekani kwa shule zote, basi angalau shule ambazo ziko kwenye remote areas ambako wanafunzi kupata chakula inakuwa siyo rahisi. Miaka ya nyuma iliwezekana, mimi binafsi shule ya msingi nilisoma chakula kilikuwepo shuleni, wale ambao mmesoma miaka ambayo na mimi nimesoma, ile ya 1970, tulikuwa tunakula chakula shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunakula chakula ambacho kama mnakumbuka, tulikuwa tunakula mpaka ngano, tulikuwa tunaita bulga. Kulikuwa na siku maalum ya kula bulga lakini pia tulikuwa tunaletewa chakula na watu wale wa chakula barafu walikuwa wanatuletea samaki wale ambao wamegandishwa. Kwa hiyo tulikuwa tunapata elimu ya namna hiyo, lakini hata madaftari likiisha ulikuwa unampelekea Mwalimu, anaangalia kama limejaa anakupa daftari lingine. Kwa hiyo tunaomba pia Serikali iangalie kutoa nafuu za namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie suala hili la utalii, utalii ndugu zangu ni muhimu na nchi yetu imepiga hatua kubwa sana sasa hivi kuhusu utalii. Mheshimiwa Rais ametuongoza vizuri katika eneo hili. Utalii wetu umekua kwa kiwango kikubwa, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan na hasa hili suala la Royal Tour. Kama ilivyo kawaida penye mafanikio hapakosi changamoto, wenzetu wameanza kutuchafua ili tusifanye vizuri. Katika hili niko tofauti kidogo na wenzangu kwenye kuchangia eneo hili. Naona hapa nia siyo watu kuhamishwa au watu kuhama, hapa wanalenga utalii wetu ili wale wenzetu ambao wanakuja kwenye kufanya huo utalii waone kule Tanzania kuna sehemu haina amani. Hawa wenzetu Wzungu na watalii wengine, mara nyingi hawaendi sehemu ambayo wanajua kuna machafuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wenzetu hawa wanaotumia lugha hizi mbalimbali za kwamba kuna kitu fulani kinafanyika watu wanahamishwa, tena watu wenyewe wanahamishwa kwa hiyari yao wala siyo vurugu, lakini bado wanaingilia kutupakazia. Nchi hii siyo mara ya kwanza kuhamisha watu, kulikuwepo na suala la operation vijiji miaka ya 70, watu walihamishwa mpaka kupelekwa Gezaulole na Mwanadilatu, hatukuona watu wakiingilia na kusema hawa wamehamishwa kinyume cha sheria. Vile vile bomoa bomoa nyingi zimepita, ardhi ya nchi hii ni mali ya umma chini ya udhamini wa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanahamishwa kwa kutumia taratibu na wanakuwa compensated. Sasa leo anapotokea mtu anaingilia kitu ambacho ni cha nchini mwetu; na ninaomba kidogo ninukuu, hii ni sovereign. Hii term inatumika kimataifa na maana yake naomba noisome. Maana yake ni the supreme absolute uncontrollable power by which an independent state is governed and from which or specific political powers are delivered. Inaendelea kusema, the international independence of a state, combined with rights and powers of regulating its internal affairs without foreign interference. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tuna regulate mambo yetu wenyewe na tuna taratibu ambazo hatujakiuka any international law yoyote. Kwa hiyo, ndiyo maana nimesema wanalenga utalii wetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na hasa Wizara yetu ya Utalii, hapa tunachafuliwa, kulenga namba ya wale watalii ambao wanaongezeka hapa nchini. Hata hili alilolianzisha Mheshimiwa Rais, la Royal Tour, haya ndiyo yanayolengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwe waangalifu, wanataka paonekane kwetu hapana utulivu ili waweze kutupunguzia idadi yetu ya Utaliiā€¦ (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwakasaka. Muda mrefu kengele ilishagongwa.

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)