Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii ambayo ni Bajeti Kuu ya mwaka 2022 kuelekea 2023. Mheshimiwa Waziri ametuwasilishia bajeti hii ambayo imekuja na vitabu vinne, nimeipitia na kwa kweli lengo kubwa ni kutafuta, na namna gani tukishatafuta, tuweze kutumia. Nami nimepata jambo la kuweza kusema ili kumshauri Mheshimiwa Waziri aweze kuangalia namna gani anaweza akayafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii smeelezea vipaumbele ambavyo ndivyo atakavyoviweka mbele na ambavyo vitamwezesha katika kukusanya na wapi atapata mapato hayo. Kipaumbele cha kwanza amesema mwenyewe kwenye bajeti yake page ya 33, amezungumza kwamba atafanya kipaumbele cha kwanza kuwa ni kilimo na atakifanya sana sana kilimo cha Chikichi kuwa Kigoma ndiyo iwe kitovu kikubwa cha kilimo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, palm economy ndiyo uchumi wenyewe sasa hivi ambao unaweza ukaleta majibu makubwa ya inflation yoyote ambayo inaweza ikapatikana kwenye bei ya cooking oil. Changamoto hii inaweza ikatatuliwa na palm oil peke yake tu. Kabla ya kwenda mbele kabisa nimwoneshe Mheshimiwa Waziri kwamba, sisi wenyewe hata kwenye ripoti yake ya hali ya uchumi amezungumza hili jambo, lakini Waziri mwenye dhamana amezungumza hili jambo kwenye bajeti yake, Bwana Bashe. Nimepitia sana hii bajeti yake page namba 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe anatuonesha kwamba mazao ambayo yanazaa mbegu hizi za mafuta katika namna zilivyozaa kuanzia mwaka 2017 mpaka mwaka 2020, kwenye Jedwali namba 12 ameonesha Waziri mwenye dhamana ya kwamba zao ambalo limeonesha kuzaa kwa negative ndani ya miaka mitano, ni alizeti; na limeshuka kwa asilimia 26.3 kutoka mwaka 2017 mpaka mwaka 2021. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipomfuatilia Waziri, anaonesha kabisa jitihada kubwa bado ameiweka kwenye alizeti. Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti ukija ukatazama Jiografia ambapo alizeti inamea ni semidesert, yaani ni nusu jangwa. Kwa maana hiyo ukienda kuweka matumaini ya Taifa kwamba ulilishe Taifa mafuta ya kula kutoka kwenye alizeti, unaliweka Taifa kwenye hali ya hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Kigoma tuna hali ya Jiografia safi kabisa, mvua hazina changamoto hata kidogo kwetu. Siyo hivyo tu, alizeti ni zao ambalo linaweza likapandwa kwa mwaka na baadaye likishavunwa haliwezi tena kuvunwa mpaka lipandwe tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini chikichi, ukiipanda; sisi tumezaliwa tunakuta michikichi ya miaka 80; mpaka sasa hivi miaka 30 bado ipo. Haja kubwa ipo katika kutazama zao la Chikichi. Jaribu kuangalia, hata juzi tumehudhuria semina hapo, watu wa Benki ya Dunia wameonesha wengi kuwa na statements mbili tofauti, lakini statement moja ambayo hata sisi tunajichanganya, wengi wanasema mfumuko wa bei kwenye mafuta ya kula ni kwa sababu ya vita vya Ukraine; uongo mkubwa kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema, mfumuko wa bei kwenye mafuta ya kula unasababishwa na mipango yetu sisi wenyewe kama nchi, wala siyo vita hata kidogo, kwa sababu hivi ni vitu ambavyo tunaweza tukazalisha wenyewe endapo tutaweza kuweka mipango madhubuti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jaribu kutazama kwenye jambo hili; ikiwa tunaweza tukakusanya fedha zetu wenyewe, hizi za madafu, tukatenga Shilingi bilioni 480 tukaenda kuagiza mafuta haya kutoka nje, kiasi kikubwa kama hicho, na kule tunapoagiza ndiko kwa watu waliokuja kujifunza hiki kilimo cha Chikichi kwetu; tunatoa fedha zetu tunazipeleka kule kwao, tunakuwa tumepeleka vitu vingi sana, hatujapeleka fedha tu. Tumepeleka fedha za kigeni, tumepeleka ajira za watu wetu, tumewahamishia wale watu waliopata akili mapema wakaweza wakaweka mipango Madhubuti, ndiyo tunakwenda kununua kule. Tunakuwa tumenunua na vingi, tumebadilishana na vingi kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikufahamishe tu jambo usilolijua au mwingine anaweza asilifahamu, mafuta yote tunayokula hapa Tanzania, asilimia 98 yanatokana na Mawese. Ukichukua Korie, ni zao la Mawese. Ni nini kinachofanyika ambacho kinatufanya tuweze kutumia kitu ambacho tunaweza tukazalisha wenyewe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo teknolojia mbili tu duniani ambazo Malaysia na Indonesia wanazitumia. Hata sisi wenyewe wafanyabiashara wetu wanakwenda kuchukua kule kutoka kwa hao watu wanakuja huku wanafanya packaging tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mawese wanachokifanya, wanatumia teknolojia ambayo inaitwa deodorization, wanaondoa harufu ya yale mafuta ya mawese. Wakimaliza pale, wanafanya teknolojia ya pili inaitwa colorization, wanaondoa ile rangi ya mawese unayoiona. Ikishatoka pale, ni Korie halisi, tayari kwa packing, inakwenda kutumika kwenye soko letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri jambo hili analiweza sana, na kuliweza ni yeye tu, amezungumza kwenye hali ya kubana matumizi, hata hapa mpaka sasa anaweza aka-cutoff kwenye hii bajeti nusu tu, itazaa viwanda vikubwa sana Mkoani Kigoma ili tuweze kuzalisha kwa asilimia kubwa na hatutaagiza mafuta nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu jambo moja ya kwamba kwa kuweza kujibana hata mwaka mmoja katika bajeti zetu, tunaweza tukapunguza lita hizo tunazoagiza nje kwa kiwango kikubwa sana. Ni sisi tu kuamua leo. Mheshimiwa Waziri na Wizara yako, chukueni uamuzi leo mweze kulifanyia kazi hili, tutakuwa tumekwenda kurekebisha katika mfumuko huu na hali ya mafuta ya kula ambayo inasumbua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa gharama hiyo hiyo, hata technical team imefanya research yake, ipo Ofisi ya Waziri Mkuu na ninadhani na Mheshimiwa Waziri utakuwa umeipata. Hii technical team inaongozwa na Mzee mmoja yupo pale Kigoma, wameweza kuangalia namna gani ambavyo kama Kigoma na maeneo mengine ambayo yamezungumzwa kwenye bajeti ikiwemo Mkoa wa Kagera na Mikoa mingine ya jirani katika bonde lile la Mto Tanganyika likitumiwa kwa bajeti hii hii, tunakwenda kuweka mabadiliko makubwa kwenye hali hii ya mafuta ya kula tunayoagiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende hoja ya pili, ni suala la reli. Mheshimiwa Waziri, kwanza tunakushukuru sana na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa jambo kubwa hili alilolifanya. Sisi tulikuwa na hofu sana. Kwa mchumi yeyote kwa mpango ule wa kwanza uliokuwepo, tulikuwa tuna hofu nchi yetu inakwenda kutengeneza uneconomic hub kwenye nchi jirani. Ila kwa kitendo Mheshimiwa Rais alichokifanya, akaleta ile reli ikaenda kupita pale Uvinza ipande Msongati, iende Gitega, iende Bujumbura na baada ya hapo itokee pale pale Uvinza ifike mpaka Kindu nchini Kongo, ni jambo la kupongezwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasema Mheshimiwa Rais ameweza kupaona hapo. Wale walikuwa wametutega, kwa sababu tunakwenda kutengeneza hub katika nchi yetu wenyewe. Watu wa Kigoma tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hilo aliloliona, nasi tunasema tutakuwa pamoja naye na tutamuunga mkono. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Assa.
ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)