Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu ya bajeti kuu ya Serikali. Kwanza nianze kumshukuru Rais kwa kazi nzuri anayoifanya hasa kwa kutengeneza ile filamu ya Royal Tour ambayo tumeshuhudia na tumepata taarifa kwamba tayari wageni wengi wanaanza kumiminika hasa Kanda hii ya Kaskazini kwa sababu ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimnukuu Isaac Newton alisema, “an object will remain at its original state or rest until a relevant force is applied.” Kwamba kitu kitakaa katika hali yake ya kawaida au katika eneo lake la asili mpaka nguvu fulani itumike kukisukuma na ndiyo hicho ambacho Rais amefanya, amesukuma utalii wetu na sasa tunaona matokeo. Ni kweli kulikuwa kuna sababu ya kuutangaza utalii kwa sababu katika sehemu nyingi za dunia wenzetu wamekuwa wakitumia fursa hasa ya kutangaza Mlima Kilimanjaro na maeneo mengine kupita njia za nchi za jirani ili kuingia kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, hiki ni kitu kizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamekuwa wakilalamika kwamba sasa kwa nini utangazwe utalii kwa wakati huu na tuko kwenye mfumuko wa bei na mambo mengi? Nimnukuu tena mwanaharakati mwingine ambaye anaitwa John Mason wa Insight International, yeye alisema hivi, “in trying times we should not stop try.” Katika nyakati ngumu na nyakati za majaribu tusiache kuthubutu wala tusiache kujaribu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru Rais kwa hilo, amethubutu na kwa vile maisha hayaishi leo, ni lazima tuendelee kufanya mambo ambayo yatakayosaidia Taifa liende mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiangalia hapo hapo kwenye utalii, kule Iringa tunayo ile Mbuga ya Ruaha National Pack, ukiangalia kitakwimu ni kwamba ile mbuga ni ya pili hapa Tanzania ikiwa na eneo kubwa la kilomita za mraba 20,226 ambayo ni ya pili kwa Tanzania. Ilikuwa ya kwanza, lakini sasa Mwalimu Nyerere imeizidi, mwaka 2008 tulivyoongeza lile Bonde la Usangu ilikuwa ya kwanza, lakini sasa ni ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia duniani ni mbuga ya sita, lakini pia wanasema kwamba ni ya 10 duniani kwa kuwa na simba wengi. Hata hivyo mbuga hii ya wanyama inatembelewa na jamii ya ndege wapatao 574; kabila za ndege mbalimbali duniani ambao wanatoka Ulaya, Australia, Madagaska na nchi nyingine za Afrika, wanakwenda Mbuga ya Ruaha kwa nyakati tofauti. Kwa hiyo, kuna kuhama kwa hawa ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukiangalia katika nchi hii ndiyo mbuga ambayo haitembelewi kabisa. Sababu ni nini? Sababu ni miundombinu, lakini tunamshukuru Rais, sasa amesaini mkataba ambao utakwenda kujenga barabara ya kwenda Ruaha National Pack na hivyo huu utalii utakwenda kukua hata Nyanda za Juu Kusini. Na kama ambavyo tumekuwa tukizungumza mara zote, ni muhimu sana sasa watalii wakatawanywa katika nchi yote ili sasa kupunguza uharibifu unaoendelea kule Kanda ya Kaskazini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuhusiana na Royal Tour kwamba amefanya sehemu ya kwanza, ni sehemu ndogo, kwa sababu ya mafanikio ambayo tayari tumeanza kuyaona, nashauri kwamba hii Royal Tour iwe kwenye series, yaani kuwe kuna toleo lingine tena. Hili toleo litakalofuata liingize mbuga za Ruaha ambazo kipekee utakuta kuna mnyama pale anaitwa tandala ambaye hayupo sehemu nyingine; utaingiza Mbuga za Kitulo na maeneo mengine kama Kalambo Falls na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya namna hiyo, tutakuwa tumeutangaza utalii vizuri na utalii wetu utaendelea kukua. Pia kwenye utalii ni muhimu sana sasa kama nchi tusiangalie utalii wa wanyama peke yake, tuangalie utalii wa namna tofauti. Unaweza ukawa utalii wa mavazi. Kwa mfano, kule Iringa tuna mambo yale ya migolole, ni utalii. Kwa hiyo, tuangalie utalii kwa mapana yake, tusiangalie tu utalii wa wanyama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wenzetu walioko kwenye utalii naomba waweze kuangalia kwa mapana yake. Kule kwetu kuna mapango ambayo Mkwawa alikuwa anajificha; nayo yanaweza yakaingizwa kwenye utalii. Viko vitu vingi. Kwa hiyo, tuwaanchie wao, naona watafikiria namna ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ule mradi wa Regrow ambao ulikuwa na mpango wa kuifanya nchi Nyanda za Juu Kusini iwe hadhi ya utalii. Tuna kituo kinatakiwa kijengwe pale Iringa, tunaamini Serikali itakwenda kwa haraka kufanya hivyo, tukiunganisha pamoja na uwanja wa ndege ambao inaonekana kwamba sasa hivi wamegundua kuna mwamba pale chini ambapo inaonesha kwamba tutachelewa kumaliza ule uwanja kwa miezi 36 zaidi. Naiomba Serikali ione namna gani ya kuweza kuharakisha hilo ili tufanye utalii wetu kuwafungamanishi tukiwa na ndege, barabara na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikizungumzia ile Bodi ya Stakabadhi Ghalani. Nimezungumzia kwenye biashara, na pia nilizungumzia kwenye kilimo. Sasa hapa nataka kushauri nini? Wakati tunaanzisha hii Bodi ya Stakabadhi Ghalani mwaka 2005, kulikuwa kuna kipengele katika sheria ambacho kilikuwa kinaipa hii mamlaka kujasili maghala yote yaliyoko nchini. Isipokuwa tulipofanya marekebisho mwaka 2016, hiki kipengele kikaondolewa. Maana yake sasa tumemwondolea mamlaka huyu Mkurugenzi wa Bodi za Maghala, hana meno tena ya kuweza kusajili maghala yote yaliyoko nchini pamoja na yale ya binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ni muhimu kusajiliwa? Ni lazima kwa sababu tukisajili haya maghala yatatusaidia kujua mazao ambayo tunakuwa nayo tangu kutoka kule chini vijijini. Kwa hiyo, naiomba Serikali na Waziri husika kwa wakati unaofaa wailete hii sheria tuifanyie marekebisho ili tumpe meno huyu Mkurugenzi wa Bodi za Stakabadhi Ghalani aanze kusajili maghala yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia jambo lingine, tunazungumzia suala la bajeti, lakini pia kuna changamoto kubwa ambayo imeanza kujitokeza sasa hivi, watu kutotoa hizi risiti za EFD. Mtu mmoja mwenye hekima alisema, “men were created to be controlled and guided.” Kwa maana gani? Kwamba wanadamu waliumbwa ili wasimamiwe na waongozwe. Tukiwaacha hawa wanadamu, wanafanya mambo wanayotaka. Kwa hiyo, sasa hivi hawatoi risiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna bidhaa nyingi ambazo zinaingia kutoka nje kupitia hii mipaka, ni kama panya road fulani hivi, maeneo ya Bagamoyo, Tunduru na maeneo ya mipaka mbalimbali ya nchi. Kwa hiyo, bidhaa nyingi zinaingia kwa njia ya panya road. Sasa kama tukiacha hii iendelee, tutafifisha nguvu ya Serikali kuweza kukusanya mapato na kuhudumia wananchi wake na kufanya miradi mingi ambayo Serikali inatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, tumeongeza ajira nyingi, tumeongeza mishahara, lakini sasa kama hatuwezi kukusanya kodi, itakuwa ni kazi kubwa sana Serikali kuweza kutima malengo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nigusie hili suala linaloendelea kuhusu Ngorongoro. Najua rafiki yangu Mheshimiwa Shangai tumekuwa tukizungumza mambo mengi, lakini nizungumzie suala hili, kwamba ni kweli mchango mkubwa wa utalii kwenye nchi hii unatokana pia na Kanda ya Kaskazini hasa eneo la Ngorongoro. Katika sheria za nchi hii ni kwamba hakuna Mtanzania, mimi au yeyote mwenye haki ya kusema kwamba hii ni ardhi yangu nitakaa milele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anayemiliki ardhi katika nchi hii ni Rais na Serikali inaweza wakati wowote inavyoona inafaa ikaichukua ile ardhi kwa matumizi ambayo yana faida pana kwenye Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama walivyosema wenzangu, mwaka 1974 nchi hii iliamua kuhamisha watu kutoka katika maeneo waliyokuwa wamekaa, wametawanyika, kuwaleta kwenye vijiji. Sababu zilikuwa nyingi, pamoja na kuwapa huduma kwa karibu na mambo mengine. Ila ili nasi tuweze kuendelea kuutunza utalii wetu, iko sababu ya kuendelea kuilinda Ngorongoro na nchi hii kama unavyosema kwamba hakuna kabila ambalo linaweza lika-claim kwamba hapa ni pakwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda hata kule Iringa utakuwa Wamasai wengi sana wanaishi kule na wamegombea mpaka Ubunge. Ukiangalia pale Isimani wapo, huwa wanagombea gombea mpaka Ubunge. Kwa hiyo, tusilete chokochoko kuonekana kwamba kuna kabila fulani moja au Wahehe au Wapare wenye uhalali sana kwamba hii ardhi ni ya kwao; Sukuma land or Hehe land au Masai land. Nafikiri tusilete huu mchanganyiko, tunafanya hili jambo liwe gumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweka uzalendo mbele, tujue kwamba nchi hii ni ya kwetu, na kama kuna chokochoko yoyote ambayo inagusa maslahi ya nchi, ni lazima wote tuungane kwa ajili ya kusudi jema la kuhakikisha kwamba nchi yetu inaimarika kiuchumi na tunakuwa wamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala lingine kuhusu Bandari ya Bagamoyo. Bandari hii ni muhimu sana katika uchumi wa nchi. Ni kweli kumekuwa kuna malalamiko mengi kwamba namna mikataba hii ambavyo ilikuwa imesainiwa ambayo hata sisi hatuijui, ilikuwa ya ovyo. Hata hivyo, bado kuna sababu ya kuendeleza hii Bandari ya Bagamoyo kwa sababu ziko meli kubwa sana duniani ambazo haziwezi kutua katika nchi yetu ya Tanzania, sasa lile eneo la Bagamoyo lina upana mkubwa ambapo tunaweza tukalipanua na tukaleta meli kubwa na uchumi wetu ukaweza kwenda kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali ione ni namna gani inaweza kuendeleza ile Bagamoyo, na mfumo wa uendeshaji wa hizi bandari nashauri uwe kwa mfumo wa kushirikiana kati ya private sector na Serikali ili kuweza kuharakisha maendeleo. Kwa sababu private sector inavyoingia kwenye kuendesha jambo, maamuzi yake yanakuwa ya haraka. Ila mara nyingi kwenye Serikali zote duniani maamuzi huwa yanakuwa ni ya polepole sana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)