Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia bajeti yetu ya Serikali. Awali ya yote nianze kumpongeza Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa anayoifanya. Pia nampongeza Naibu wake, Katibu Mkuu na management nzima ya Wizara ya Fedha. Hakika wanafanya kazi kubwa, kazi nzuri na tunaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitachangia vitu kama vitatu. Nitachangia kuhusu force account, lakini mambo ya TANePS ambayo yameongelewa kwenye bajeti yetu. Vile vile nitachangia kodi ya ardhi, na muda ukinitosha nitaongeza na block farm, maana hii ni ajenda yangu ya kila siku mpaka kieleweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipate nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa, hakuna mtu asiyejua. Mheshimiwa Rais anapambana usiku na mchana kuhakikisha maendeleo ya Watanzania yanapatikana; lakini tu siyo maendeleo ya vitu au maendeleo ya majengo, anataka maendeleo ya Mtanzania mmoja mmoja aonekane na yeye anaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezoea kusema uchumi umepanda sijui kwa five point six, seven point ngapi, lakini Mtanzania wa kawaida mfukoni kwake hakuna hela. Nadhani Mheshimiwa Rais amejikita kuleta maendeleo kama Taifa na pia kuleta maendeleo kwa Mtanzania mmoja mmoja. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, anafanya kazi kubwa, tumemwona kwenye Royal Tour kule maporini kazi anayoifanya. Yote hiyo ni kuhangaika Watanzania wawe na maisha mazuri. Amekuwa ni Rais lakini ni mama, sisi wote ni watu wake, akituangalia nadhani halali usiku, anaendelea kuhangaika kwenye Mataifa mbalimbali kuhakikisha hatukwami na mambo yanaenda. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, tunamtakia kila la heri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais aendelee kusafiri ili watoto wake tuendelee kuneemeka. Yeye ni baba sasa, lazima atoke akahangaike kuhakikisha nchi yake inaenda vizuri. Tunampongeza sana. Kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais ungeniuliza mimi ningesema basi Mheshimiwa huyu apate nafasi 2025 Watanzania wote tumuunge mkono bila kuleta mgombea yeyote wa chama chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia na force account. Serikali imepeleka pesa nyingi sana za maendeleo kwenye halmashauri zetu, lakini miradi mingi inasimamiwa na force account. Sasa tunazungumzia bajeti kupanua wigo wa kodi. Naangalia miradi hii yote iliyofanywa na force account mafundi wote wa force account hawalipi kodi yoyote ya Serikali. Akishalipwa ile pesa ni ya kwake halipi kodi yoyote ya TRA. Sasa niiulize Serikali, kwa nini miradi hii isijengwe na wakandarasi? Mkandarasi atamwajiri huyo fundi anayejenga kwa force account ataajiriwa na mkandarasi. Mkandarasi ataajiri vijana wetu, mainjinia waliosoma wako mtaani, ataweka kama mainjinia wake; ataajiri vibarua; pia mkandarasi huyu atalipa kodi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapopeleka force account unakuta halmashauri ina miradi 18 au ina miradi 19 inaiendesha lakini ina injinia mmoja au mainjinia wawili. Hawa mainjinia wawili wanawezaje kwa pamoja kusimamia miradi 19? Unakuta value for money haiko sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, sera yetu ni makandarasi, ma-contractor kufanya kazi. Rudisheni kazi hizi kwa ma-contractor. Force account kwanza ilitoka wapi jamani? Yaani mimi hata sijui ilipotokea. Tupelekeni kazi kwa makandarasi, watalipa kodi ya Serikali. Hawa force account, mafundi wote mliowaweka hawajawahi kulipa kodi ya Serikali, wala hawalipi, wala hawajulikani kwenye Serikali wala hawajasajiliwa sehemu yoyote, wala hawana leseni, wala hawana TIN, wala hawana VAT, lakini wanafanya kazi za Serikali na wanalipwa pesa na Serikali. Kwa hiyo, mnapoteza mapato mengi sana kwa miradi yote hii iliyotendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani tumekuwa tunafanya vitu vya ajabu ajabu! Kwa mfano, hela zinakwenda kwenye shule za kujenga madarasa na kadhalika. Anaambiwa Mwalimu Mkuu asimamie majengo yale. Mwalimu Mkuu ana utaalam gani wa kusimamia majengo? Mwalimu Mkuu asimamie zile fedha na atakuja kukaguliwa. Hakusomea Uhasibu Mwalimu Mkuu; lakini shule hiyo ina Walimu saba tu au nane. Mnamtoa Mwalimu Mkuu kwenye kazi yake kwenda kusimamia majengo, na wakati huo huo tunalalamika Walimu wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itafute wataalam wa kufanya hiyo kazi na Walimu waachwe wafanye kazi zao za kiualimu. Naiomba sana Serikali yetu iwe makini sana katika hili jambo. Walimu wamekuwa wanalaumiwa. Kwa mfano, Mwalimu shule yake iko hapa, anayesimamia jengo lake la Walimu ambalo liko labda kilomita moja, nani anampa nauli huyo Mwalimu Mkuu kwenda kusimamia huko hilo jengo? Nani anamlipa posho ya kukaa kule mpaka jioni kusimamia hilo jengo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali, watumishi wengine wanavyokaa maofisini wanavyolipwa posho, basi na Walimu hawa kama mmeshindwa kuweka wataalam basi muwalipe; na muache kuwakamata wanapokuwa wanashindwa kuweka hesabu vizuri kwa sababu siyo masomo yao waliyoyasomea. Wala kujenga majengo wao sio mainjinia. Huwezi kumwambia Mwalimu asimamie ujenzi wa shule, halafu baadaye unakuja kumuuliza…

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Munde, subiri taarifa.

TAARIFA

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka nimpe taarifa dada yangu Mheshimiwa Munde kwamba force account zilikuwa zinasaidia sana. Mpaka sasa zinasaidia kwanza kuokoa fedha za Serikali ambazo zimekuwa zikipotea sana na pia zinawasaidia wale mafundi wetu wa ndani ambao hawawezi kukaa kwenye kampuni kuweza kufanya kazi nyingi ambazo tunaziona zimesaidia sana hii miradi ya Serikali ambayo imetekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Munde unaipokea hiyo taarifa?

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei kabisa, kwa sababu hawa makandarasi pia ni Watanzania, wako hapa hapa na wameajiriwa. Hawa makandarasi sio mafundi, wana kampuni zao, wanaajiri mafundi hao hao na wanawalipa pesa, lakini wanalipa kodi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunaongelea kuongeza kodi ya Serikali. Tunaongelea kuongeza mapato. Bajeti yetu tuliyonayo sasa hivi asilimia 28 tunategemea wafadhili, lakini tunatamani siku moja tuwe na bajeti yetu asilimia 100 ambayo tutajitosheleza sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kusema kwamba tunaomba makandarasi wafanye kazi ya ukandarasi kama sera zetu zilivyo, siyo ma-local fundi. Hao ma-local wataajiriwa na makandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee sasa kuhusu TANePS. Sasa mimi sitaki taarifa, muwe mnachangia wenyewe jamani, mnatutuoa kwenye reli.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Munde taarifa ni kwa mujibu wa kanuni.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimekusikia. Niongelee suala zima la TANePS. Nimesikia kwenye bajeti ya Waziri amesema sasa hivi ataweka bei fixed kwenye TANePS. Kwa hiyo, kwenye zile bei kutakuwa hakuna ushindani kama vile kutangaza tenda na watu kushindana. Kutakuwa na bei fixed kwenye TANePS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, kwa mfano ream ya karatasi Serikali itaweka bei ya Masumini ambaye ndio tajiri au mwenye kiwanda. Mimi nauliza, yule mwenye duka kule Irambo kwa kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, duka la mtaani, ambaye halmashauri ilikuwa inafanya naye kazi ya kununua ream ya Masumini Shilingi 8,000/=, yeye anauza Shilingi 11,000/= au Shilingi 9,000/=. Je, Serikali itaenda kununua kwa Shilingi 11,000/= iache Shilingi 8,000/= kwa Masumini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa local content iko wapi? Yakija makampuni ya kigeni unaambiwa lazima mwaajiri Watanzania. Nanyi lazima mfanye kazi na Watanzania wote, siyo matajiri tu. Hamwezi kufanya kazi na viwanda; najua hizo bei zitakuwa za viwanda, zitakuwa za ma-agent wakubwa. Sasa huyu mfanyabiashara mdogo ambaye alikuwa na cement yake kwenye halmashauri atauzaje kwenye Serikali tena? Serikali itanunua kiwandani moja kwa moja ndiyo itakuwa bei fixed ambayo iko kwenye TANePS. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa na miradi ya UVIKO walianza hivyo hivyo, tununue moja kwa moja kwenye viwanda. Ndiyo maana nimesema, Mheshimiwa Rais anataka pesa ziingie kwenye Serikali lakini na mtu mmoja mmoja. Akasema pesa hizi zipelekwe halmashauri na vitu vinunuliwe kwenye halmashauri husika, na pesa zilionekana, kwenye Serikali mambo yalionekana, na kwa mtu mmoja mmoja Watanzania walipata pesa. Ila Mheshimiwa Waziri mambo ya kutuwekea bei za fixed kwenye TANePS mjue kabisa masikini wote hawatauza, watauza matajiri na wenye viwanda tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mkurugenzi wa Halmashauri hawezi kununua pia kwenye halmashauri yake ream ya Shilingi 12,000/= wakati Masumini Dar es Salaam ni Shilingi 8,000/=. Sasa napata shida, naangalia bajeti ya Kamati ya Fedha Shilingi 700,000/= pamoja na posho za Madiwani. Anaanzaje kuagiza ream za Shilingi 200,000/= kwa Masumini? Maana akinunua hapa itakuwa bei siyo ya kwenye TANePS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie hili suala vizuri, iache ushindani wa bei. Wameongeza, Mheshimiwa Waziri amesema hapa anaongeza exchequer auditor, amewapa pesa ili waongeze kuajiri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Kazi ya Serikali ni hiyo, kuangalia mapato yake yasivuje, lakini siyo kuwabana Watanzania waache kufanya biashara. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Munde, kengele ya pili imelia, nilikuachia umalizie sentesi yako.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.