Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii nami nichangie hotuba hii ya Serikali, Bajeti Kuu. Nami nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo amezifanya hapa kati, ametuonesha kwamba fedha kiasi akiutumia mtiririko ambao ameutumia hapa juzi, una matokeo chanya zaidi kuliko mfumo ambao tunautumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipopata zile Shilingi trilioni 1.3 alizigawa na akatoa maelekezo ya moja kwa moja zikajenge vituo shikizi na hospitali kwa maana ya vituo vya afya na maeneo mengine. Tumeona jinsi ambavyo kwa kutumia Force Account, tumejenga vitu vizuri sana na vya thamani na thamani ya fedha imeonekana. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuleta fedha hizi kule kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Waziri na Naibu Wake, Katibu Mkuu ambaye ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Watumishi wa Wizara ya Fedha na Kamati ya Bajeti kwa kutusaidia. Wameonesha namna ambayo kwa miaka mingi ya nyuma, usikivu wa Waziri wa Fedha umekuwa mkubwa sana kwa kipindi hiki. Amesikia ushauri mkubwa wa Wabunge tuliochangia katika Bajeti za Wizara na Serikali imekuja na majibu mengi ya hoja za Wabunge ambazo tulikuwanazo kipindi cha miaka miwili mitatu hapo nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo ambalo lilikuwa ni mwiba sana, kuunganisha mikoa kwa barabara. Mkoa ambao mimi natoka, Singida, kelele ya miaka mingi kwa Marais zaidi ya wanne nyuma, ilikuwa ni kuunganisha na Mkoa wa Mbeya kwa barabara ya lami. Nashukuru sana sasa Serikali imeitaja moja kwa moja kwenye bajeti. Sasa hivi ninavyozungumza, Mkandarasi ameshapewa na kiwanja cha kujenga kwa ajili ya kupeleka vifaa vya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napongeza sana kwa hatua hii ambayo, wananchi wa Mkoa wa Singida hasa Jimbo ambalo mimi natoka la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi, wanaenda kufurahia matunda ya Serikali yao. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii ambayo wananchi wa Itigi wanaanza kufarijika na kuona nao ni wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida bado pia haujaunganishwa na Mkoa wa Simiyu, kitu ambacho kina karaha. Naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Waziri wa Ujenzi, kupitia daraja la Sibiti, waone namna ya kuunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya. Wameitaja barabara ile ambayo inakwenda kule Hydom na kwenda kwa Mheshimiwa Flatei huyu mpiga sarakasi ambaye hapa huwa ananisababishia shida. Sasa kipande ambacho kinatakiwa kiwepo katika mpango kutoka Iguguno mpaka Ibaga, tutakuwa tumeiunga mikoa kwa barabara za lami. Pia ni barabara ambazo kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika hotuba yake, kwamba ni barabara za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaunga barabara hii nayo tayari tutakuwa tumetenda haki kwa watu wa Mkoa wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo tumeona baada ya kuletea mapesa yale mengi na Mheshimiwa Rais, yamefanya kazi, kuna uchache wa watumishi na hasa Walimu na Watumishi wa Afya. Katika kada hizi mbili kumekuwa na changamoto kubwa. Tumejenga shule ambazo tulikuwa tunaziita shikizi. Vituo shikizi sasa ni shule kamili na zimesajiliwa. Kwenye Jimbo langu tumeshasajili tayari shule 20 mpya zenye madarasa mapya kabisa manane, saba, sita; lakini walimu hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ione hasa katika jimbo langu la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi, kuona namna ambavyo itaweza kuongeza walimu ili wanafunzi hao wanaoenda kuanza shule hizi, waweze kupata elimu ambayo ni bora. Tumejenga vituo vya afya, na sasa tunajenga Hospitali ya Wilaya pale Itigi, pia tunahitaji watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo halijazungumzwa na Wabunge wengi. Tunaposimamia fedha hizi; Mheshimiwa Kakunda hapa amesema, sisi tunapiga maneno hapa tunaiambia Serikali, Serikali sikivu inapeleka fedha kwenye Halmashauri zetu. Wanaosimamia kule ni Madiwani, lakini Madiwani hawa hatujawaona katika hii bajeti. Madiwani wetu, posho zao baada ya kupelekwa Serikali Kuu na hasa wale ambao Halmashauri zao zinakusanya chini ya Shilingi bilioni tano, vipato vyao ni duni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha iangalie jambo hili na ikiwezekana waje na majibu na wenyewe tuwaone. Mheshimiwa Rais ameongeza watumishi kwa asilimia 23, hawa Madiwani hupewa tu posho, basi hata zile posho hatuwezi kuziongeza? Hebu naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapokuja, aangalie basi hawa watu ambao tunapoenda kwenye chaguzi wao ndio wanaomba kura na pia baadaye wanasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunafika maeneo mengi, Mheshimiwa Rais maeneo mengine hafiki, lakini tunazungumza kule kwamba tunaomba kura mafika matatu, lakini haya mafika mawili tunayafanyia vizuri, hili figa moja mbona tunalisahau? Hebu tuangalie watu hawa ambao kwa hakika wanafanya kazi ya kujitolea kwa kiwango kikubwa sana, na fedha zile kule kwetu hazijaliwa hata senti mbili. Zote zimetumika katika mtiririko mzuri kwa maana ya usimamizi wao mzuri. Sasa tunawapongezaje watu hawa? Kama watumishi wameongezwa mishahara, nao kwa nini tusiwaone? Naomba niishauri Serikali iangalie katika jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine, tunapoenda kumaliza kujenga Stiegler’s Gorge, tunapoendelea kujenga reli, basi huko baadaye tuangalie ni namna gani tunakabiliana na hali hii ya upandaji wa mafuta? Sisi tunayo fursa hapa kwamba nchi yetu ina gesi. Ni namna ya kuichakata tu ile gesi na kuifanya iweze kutumika kwenye magari madogo. Gesi iliyopo inaweza kutumika kwenye magari makubwa, lakini bado haioneshi dalili. Tumeona hapa magari ya Dangote, wameweza kuichakata ile gesi na kuitumia kwenye magari yao, sasa sisi tunashindwa nini? Kwa nini Serikali nayo isianze kutumia gesi katika magari yake ya Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, wakati tunasubiri kuchakata LNG, hii CNG iliyopo ianze kutumika. Tumeshindwa kuisambaza; hapo hapo Dar es Salaam ni viwanda vichache sana vinavyotumia gesi hii. Hebu tuone sasa fursa tuliyonayo ili kupunguza uagizaji wa mafuta tuweze kufanya gesi hii iliyopo nchini mwetu. Kama kuna tatizo la umiliki, mikataba ilikuwa ya ovyo; tumeweza kufumua mikataba katika migodi mikubwa ya dhahabu, tunashindwaje hapa kwenye gesi ili kuinufaisha nchi hii, tupunguze uagizaji wa petroli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunaagizi LPG, gesi ya kupikia wakati ambapo tuna LNG hapa, tuna CNG ambayo tunaweza kutumia direct kwa kupikia. Tunafanyaje kwa namna hii? Kwa nini tusitafute namna ya kuwekeza basi? Najua uwekezaji ni mkubwa, tulishatumia zaidi ya Dola bilioni tatu, tukatengeneza bomba kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam, leo hatuwezi kutafuta hata bomba dogo likasogea Dodoma au likaenda Mwanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kufikiri tuone tu namna gani wataalam wetu wanaweza kutusaidia ili tuondokane na hali hii tunayokwenda nayo katika kuagiza mafuta ya petroli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.