Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia na mimi bajeti hii kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Bajeti hii ukiingalia kwenye karatasi ni nzuri, lakini kazi ipo kwenye utekelezaji. Utekelezaji ndiyo changamoto kwa bajeti nyingi, hatujawahi kufikia asilimia 80 ya utekelezaji wa bajeti. Kwa hiyo, hata kama Mama alishasema kwamba yeye hawezi kuzungumza kwa kufoka, lakini tujitafsiri sisi kama Serikali na kama Watanzania kuhakikisha kwamba bajeti hii inatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa kuangalia; hii ni bajeti ya pili kwa mpango wa miaka mitano ambayo ni 2021/2022 – 2025/2026. Dhima yake ilikuwa ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Hiyo ndiyo dhima kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuweka vipaumbele vyake ambapo ameweka kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, uwekezaji na biashara. Hivi alivyoviweka kama kipaumbele, kama kweli vitafanyiwa kazi, tuna miaka siyo miwili au mitatu, tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono suala la mkakati wa kubana matumizi ya Serikali. Naunga mkono kwa sababu Watanzania kwa kweli wana hali ngumu na tumeona. Kwa mfano, masual ya magari, utaona jinsi magari anavyotumika ndivyo sivyo. Tukiangalia wenzetu tu nchi ya Jirani; Uganda, wanatumia magari yao binafsi na wanakwenda wanafanya kazi vizuri. Cha muhimu, lazima kuwe na utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba wale ambao umewaweka katika categorization zenu za uongozi basi wawekewe mkakati Madhubuti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la kupunguza ukubwa wa uwakilishi, nalo naliunga mkono katika vikao kusafiri umbali mrefu, kutumia TEHAMA, ni vitu ambavyo ni muhimu, hata alipokuja Mheshimiwa Rais hapa Bungeni tarehe 22/4/2022 alihimiza mambo kama hayo, TEHAMA itumike, na ndiyo vitu ambavyo tunaomba Mheshimiwa Waziri akafanyie kazi vizuri. Pia kufanyia kazi huko kuendane na kuboresha wafanyakazi ambao watakuwepo katika sekta mbalimbali za maeneo ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tujiulize, mfumo wa kuendesha uchumi wa nchi yetu ni upi? Hamjawahi kututanabaisha kwamba mfumo wetu ni upi? Ni ujamaa na kujitegemea? Ni mfumo gani? Hatuna mfumo ambao tunaufahamu. Kwa sababu kama huufahamu vizuri, utapanga na utatekeleza vitu ambavyo hujui unakwenda wapi? Tujipambanue na tutafsiri mfumo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kujibu hoja, atuambie tuko wapi sasa hivi ili tuweze kujua tunafanya nini? Kwa sababu kila aina ya uchumi inajipambanua. Hata kama ni Bima ya Afya ya Ujamaa ni tofauti na Bima ya Afya ya Ubepari au Bima ya Afya ya kitu kingine. Kwa hiyo, tukijipambanua tutajua tunawekaje mambo yetu yaende sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alizungumza kwamba, naomba ninukuu: “Maendeleo lazima yawe na uhusiano na watu.” Pia Hayati Rais Benjamin Mkapa, alisema katika kitabu chake, naomba ninukuu, anatamani mfumo wa uchumi ambao ni shirikishi. Hii ina maana gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya asilimia 67 ya watu nchini ni vijana. Kati ya hiyo asilimia 67, asilimia 13 ya hao hawazalishi hata Shilingi 100/=. Tupo kwenye majimbo yetu, tupo katika nchi yetu, nayo ni nguvu kazi. Sasa ni heri kuibua kichwa kimoja chenye ubunifu kuliko madini tuliyonayo. Kwa sababu tunaweza tukayaibua hayo madini lakini watu wa kuja kuyatumia wasiwepo. Tunataka uzalishaji wenye tija. Kama hatujawekeza vizuri kwa vijana hawa, uzalishaji utakuwa ni ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji mfumo wa kuinua sekta binafsi ili tuibue mabilionea wengie. Hebu tujiulize Tanzania, tuna mabilionea wangapi Mheshimiwa Waziri wa Fedha? Tunao wangapi? Nchi kama Finland, Ghana, Norway, Ujerumani, zimeweza kuwatumia wazawa wao, zimewawezesha na mpaka wameweza kufanya uchumi wao unakuwa stable. Sasa sisi tunajipambanuaje kwa hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa soko huria la kijamii (social market economy) ni mfumo unaochukua mazuri ya Ujamaa na mazuri ya Ubepari kwa pamoja, kisha wanapata mfumo mmoja wa kuhakikisha uchumi wa mtu mmoja mmoja unakua. Sasa hiki ndiyo kitu ambacho kama Serikali itaweza kutumia mfumo huu, tunaweza tukafika mbali. Ila mfumo huu ni endelevu, misingi yake mikubwa, lazima kuwe na sera na sheria zinazotabirika kwa wawekezaji. Hatuna sera zinazotabirika kwa wawekezaji. Rais amejitahidi sasa hivi, lakini tunaomba matokeo ya utekelezaji wa sera hizo. Vile vile kuwe na ushindani, uwajibikaji, soko, umoja, motisha na ushindani mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Tanzania anayeanza biashara leo, mtu kama anataka kuanza biashara leo, anaanza kulipa lini? Tujiulize wote, anaanza kulipa lini? Lazima tuwatengenezee mazingira ambayo huyu mtu anayeanza biashara leo tumpe muda wa kuuza kulipa. Hiyo ndiyo changamoto tunayopata. Pia, kodi kiasi gani? Hiyo kodi atakayolipa itakuwa ni kiasi gani? Lazima tuwashike mkono hao wote ambao watakuja kutaka kuwekeza. Tusipofanya hivyo itakuwa ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni wazo langu la mwanzo. Naenda katika kipengele cha Bodi ya Mikopo. Katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri, sijaona mahali ambapo amezungumzuzia kabisa kuongeza posho ya wanafunzi wa vyuo vikuu. Ni jambo jema kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita kusoma bure, sawa; lakini kule chuo kikuu, toka miaka hiyo wanapewa Shilingi 8,500/= wakati Dola bado ni Shilingi 1,600/=, mpaka leo Dola imepanda kuwa Shilingi 2,300/= mpaka Shilingi 2,400/=, bado wanapata kiasi kile kile, Hapana. Tuwaboreshee na hao. Pia mishahara imepanda. Kwa hiyo, tuangalie na hawa vijana tuweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine tuwaongezee pia ile capitation grants, tulipanga Dola moja, Shilingi 10,000/= tukawa tunawapa, tuwaongezee nao angalau ifike Shilingi 25,000/= kwa Primary School na Secondary, tuwaongezee hata ifike Shilingi 50,000/=. Hii itawasaidia watoto wetu kuweza kupata huduma bora za kielimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nizungumzie sasa kuhusu usimamizi na udhibiti wa upotevu wa mapato. Kama tunatenga hizi pesa lakini hazina udhibiti mzuri, tunatwanga maji kwenye kinu. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, ameweza kumwongezea fedha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, na vile vile ameweza kuwapa vote wale internal auditors. Nashukuru kwa sababu kumekuwa na changamoto kubwa katika uwasilishaji wa taarifa za masuala haya. Tukifanya hivyo, ndipo uwajibikaji tutauona, uwazi tutauona, tutaona tija ya fedha zetu ambazo tunazipeleka katika sekta mbalimbali huko katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)