Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe miongoni mwa wachangiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wenzangu kwa namna ambavyo tunamshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti iliyosomwa na Dkt. Mwigulu, bajeti nzuri yenye mwelekeo mzuri kwa ajili ya Watanzania na Majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunasema Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri? Moja, mpaka hivi sasa, haki ya Mungu kwa muda wa mwaka mmoja haijawahi kutokea fedha nyingi tunazo katika Halmashauri zetu, nyingi sana. Kwa hiyo, tunakushukuru sana. La pili, tukushukuru Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu wako na Katibu Mkuu wako na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri mnayoifanya juu ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Mama amefungua milango ya nchi yetu. Kwa hiyo, Dkt. Mwigulu unakwenda katika njia hiyo, hongera, fanya kazi, chapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nawapongeza na Mawaziri wote na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri mnayoifanya. Mnaiga mfano, mnafanya kazi nzuri sana. Wako watu hapa ambao wanabeza baadhi ya Mawaziri kwa kazi wanazozifanya. Jamani tuache ubinafsi, tuongee ukweli. Mawaziri mnafanya kazi nzuri, nzuri sana, chapeni kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna suala la maji ambalo katika Miji 28, Serikali zote zilishindwa, haijawahi kutokea, Mama ameweza, tunashukuru sana. Miradi hii ya Miji 28 ikiwepo na Mji wa Makambako, sasa Watanzania na hasa wa Mji wangu wa Makambako, mradi huu ambao tayari umesainiwa, juzi tulikuwa Ikulu, tunashukuru sana. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu hakikisha unasimamia fedha ziende kule Makambako zikafanye kazi ya mradi huu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu kule Kusini wakulima wetu wana tatizo la mbolea hasa ya DAP na UREA, lakini kutokana na Wizara ya Kilimo, kupitia hili Waziri wa Kilimo alilowasilisha juzi hapa kwamba Serikali sasa itakwenda kutoa ruzuku, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tunaomba ruzuku hiyo, tunaisubiri kwa hamu ili kusudi mbolea hii iweze kupungua bei. Ni imani yangu kazi hii Mheshimiwa Dkt. Mwigulu utaifanya ili kusudi wananchi wetu waweze kupata mbolea yenye bei nafuu kwa ajili ya wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sikutaka kuchangia, maana bajeti hii inajieleza, iko vizuri. Iko vizuri! Changamoto kwenye Jimbo la Makambako; tuna fidia ambayo imechukua muda mrefu pale Idofi kwa ajili ya kujenga kituo cha One Stop Center. Serikali imeshatoa fidia zaidi ya Shilingi milioni 870, bado Shilingi bilioni tatu na something. Tunaomba fedha hizo ziende ili kituo cha One Stop Center kiweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna Kituo cha Polisi Makambako; eneo lile lilozungukwa wananchi pale wanataka kulipwa fidia, zililetwa fedha zaidi ya Shilingi milioni 200, fedha zile baadaye wananchi walipokataa kupokea kwamba ni ndogo na baadaye tulipoongea nao wakakubali fedha zile zikahamishwa zikaenda kujenga Kituo cha Polisi Wanging’ombe. Ombi langu Mheshimiwa Waziri, Hazina toeni fedha sasa walipwe wale wananchi wanateseka sana, sana sana. Kwa sababu ni eneo ambalo muda mrefu limechukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia nyingine ya tatu ni suala la Soko la Kimataifa. Serikali ilishatoa Shilingi bilioni 3.1, fedha zilizobaki ni ndogo kwa ajili ya wananchi 18 na wananchi hawa walikuwa wanashughulikiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara. Ombi langu sasa, Hazina itoe fedha ili wananchi hawa nao walingane na wenzao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la fidia ni suala la umeme wa upepo. Pia tunaomba Hazina wamalize mazungumzo na TANESCO ili wananchi hawa waweze kulipwa fidia za maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kuna miji 45 ambayo inakwenda kujengwa masoko na stendi ikiwepo na Makambako. Tunaomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu miji hii iweze kuanza hasa ukizingatia pale Makambako ndiyo center ya kwenda Songea, Mbeya, Malawi, na kadhalika. Kwa hiyo, tunaomba jambo hili lianze mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ambalo limezungumziwa kuhusu kulipa magari; malori, mabasi na kadhalika Shilingi 3,500,000/=. Jambo hili Mheshimiwa Dkt. Mwigulu wananchi wamelipokea, wamenipigia sana simu, wanaomba bei ipungue iwe kati ya Shilingi 2,000,000/= na Shilingi 2,500,000/=. Mmelifanya jambo zuri kwamba sasa litakuwa halina longolongo, watu wakishalipa basi, tunakutana mwaka mwingine. Jambo hili wamelipokea vizuri, lakini wanaomba bei ipungue. Shilingi 3,500,000/= ni fedha nyingi. Tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yako, mkae tena upya, mpange, bei ipungue ili wananchi waweze kumudu kulipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile watu wa vituo vya mafuta nao wanaomba iwe kama hii mliyopanga ya magari. Vituo vya mafuta kwa lita moja wanapata faida ya Shilingi 100/=, na katika faida ya Shilingi 100/= ninyi mnachukua Shilingi 20/= wanabaki na Shilingi 80/=. Halafu mnakuja kukokotoa tena kodi. Kwa nini na wenyewe mnapochukua Shilingi 20/= iwe basi, shughuli imeisha? Litakuwa ni jambo jema sana na mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la muda mrefu la hawa waliyosambaza pembejeo, wamekuwa wakidai fedha zao kwa muda mrefu. Ombi langu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kama watu hawa wapo ambao walikuwa waaminifu, walifanya kazi vizuri, walipwe fedha zao kwa sababu jambo hili limechukua muda mrefu, na Serikali hampo kwa ajili ya kuwadhulumu watu, mpo kwa ajili ya kuwalipa. Tunaomba wale ambao mmehakiki fedha zao, wanatakiwa kulipwa, basi walipwe Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu jambo lingine ni mikopo ya benki. Mikopo hii, naiomba Serikali, benki zetu, ukienda benki nyingine riba ni asilimia 21, wengine 18, wengine 19, wengine 17. Kwa nini isiwe moja? Tunaomba kwenye benki, sisi ni wakopaji, tukope asilimia isizidi 15 ili tuweze kumudu kulipa madeni haya ambayo tumekopa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Deo Sanga. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliweke vizuri.
MWENYEKITI: Ahsante, kengele ilishalia.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekunde moja.
MWENYEKITI: Nilikuongezea, kengele ililia nikaona unaongelea mambo ya muhimu ya benki.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu chapa kazi, fanya kazi na Mama fanya kazi vizuri na Mawaziri wote fanyeni kazi vizuri, mko vizuri na Manaibu Waziri. Ahsanteni sana. (Makofi)