Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu. Bajeti yoyote inapopangwa na hasa ya Serikali ni makisio au matarajio ya nini kitakusanywa ili yale tuliyojipangia kwa maana ya matumizi na maendeleo yaweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba mfumo wa bajeti yetu hapa nchini ni cash budget, kwamba tukusanye, tupate ndiyo tuitumie kwa jinsi ambavyo tumeipitisha. Ila mfumo huo wa cash budget inahitaji Serikali kuwa makini na kuweka mikakati ya ukusanyaji kwenye maeneo yote ambayo kodi inapaswa kukusanywa na kuhakikisha hakuna upotevu wowote wa kodi, lakini kuweka mazingira rafiki ambayo kila mlipa kodi atakuwa anatamani kulipa kodi na siyo kwa kulazimisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tumekuwa tukiweka makisio ya bajeti kubwa na hatufikii malengo ya ukusanyaji. Miaka mitano ya fedha iliyopita makisio yetu ya bajeti hayajawahi kufikiwa. Tumetekeleza bajeti hiyo kwa kukusanya na kupata haya matarajio ya kodi kwa kiasi cha asilimia 78 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo tunaimalizia, lengo lilikuwa ni kukusanya Shilingi trilioni 37.99 kutoka vyanzo vyote, lakini hadi Aprili Serikali imeweza kukusanya Shilingi trilioni 29. Unaona hapo kuna utofauti kati ya Shilingi trilioni nane, lakini hapo hujachukua mwezi wa Tano na wa Sita kwa sababu ripoti inasema ni mwezi wa Nne ndiyo wamekusanya kwa kiwango hicho. Kwa hiyo, hata ukichukua mwezi wa Tano na wa Nne, ukakisia tu labda mtakusanya Shilingi trilioni nne, bado unaona, kuna upungufu wa takribani Shilingi trilioni nne kulingana na makisio ya bajeti ambayo tulijiwekea kwa mwaka uliopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tunajadili tena bajeti ya mwaka 2022/2023, tunaweka tena malengo makubwa ya Shilingi trilioni 41, wakati kule nyuma tuna upungufu, lakini leo tunaongeza 8% tena ya makisio ya bajeti. Sasa naishauri Serikali kwamba haya makisio mnayoyaweka nadhani mfikirie huko mbele, kutokuweka makisio ambayo hatuwezi kuyafikia. Ni bora hata tuweke pungufu, hata ikija zaidi inakuwa ni bora zaidi kuliko kuweka kwenye makaratasi matarajio makubwa halafu hatuyafikii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hayo, kuna mambo mengi ambayo yanapaswa kutazamwa ili tuweze kufikia hiki ambacho tunakitarajia. Sasa nini kifanyike? Kuna mianya mingi sana ya upotevu wa kodi. Ukisoma uchambuzi wa Shirika la Action Aid, kuna upotevu mkubwa sana kwenye maeneo mengi kama yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamefanya uchambuzi kati ya mwaka 2013 na mwaka 2021; kwenye sekta isiyo rasmi tunapoteza Shilingi trilioni 6.5. Sasa tukiweka mikakati; mikakati rafiki lakini, siyo ile ya kutumia task force, siyo ile ya kubambikiza kodi, hapana. Tuweke mifumo rafiki ya kuzitambua sekta hizi zisizo rasmi, tuwajengee mazingira, tukusanye kodi ambazo zinapotea, tutaweza kufikia haya malengo ambayo tumejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni misamaha ya kodi isiyokuwa ya lazima. Kuna misamaha ya kodi isiyokuwa ya lazima ya Shilingi trilioni 1.1. Hii ni misamaha mingi sana. Kwa hiyo, ni lazima mfikirie aina ya misamaha inayotolewa kwa hawa wanaopata hii misamaha, na kama hiyo misamaha kweli ina tija, ili tuhakikishe tunapunguza misamaha hii ili hizi fedha ambazo zinachukuliwa kama misamaha basi ziingie kwenda kutekeleza na kufanikisha hilo lengo mlilojiwekea la Shilingi trilioni 41.48. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye utakatishaji wa fedha au fedha haramu. Uchambuzi wa Action Aid unaonesha kwamba kuna Shilingi trilioni 1.4 ambayo inapotea katika eneo hili. Haya mambo yapo, kuna wachambuzi wanafanya kupitia taarifa zenu wenyewe Serikali, zipo, mzisimamie, mzifanyie kazi ili tuhakikishe haya malengo mliyojiwekea yaweze kufikiwa na Watanzania waweze kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni lazima kuhakikisha tunaimarisha ukusanyaji wa ndani kwa kuweka mazingira rafiki, lakini kuweka masharti rafiki na rahisi kuanzisha na kufanya biashara. Tunaposema masharti rafiki, ni kuangalia mazingira ya watu wanaotaka kufanya biashara, yawe ni rafiki. Leo wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha wakitaka kuomba leseni maana yake, anatakiwa awe na mtaji wa Shilingi bilioni moja. Hii sijui imewahi kutokea wapi? Yaani ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa nini tusiweke kiwango kidogo ambacho kila mtu ataweza, halafu kama mnahisi kwamba haya maduka ya kubadilishia fedha labda yana tabia ya kuficha fedha au fedha haramu, wekeni mazingira ya kuratibu na ku-control, lakini tuweke kodi ambazo mtu akitaka kuanzisha biashara anaweza kwa sababu kuna kiwango kidogo ambacho anakimudu na ataanzisha biashara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuondoe urasimu wa ufanyaji wa biashara au upatikanaji wa leseni. Leo mfanyabiashara labda kwenye Kijiji X akitaka kuanzisha biashara yake, ataenda Halmashauri kukata leseni, atalipia, lakini hatapewa kile kitambulisho cha leseni mpaka arudi TRA apate Tax Clearance. Atafika TRA ata-print Tax Clearance halafu atarudi tena Manispaa au Halmashauri na kupewa ile risiti ya leseni ya biashara. Sasa unaona mnavyomsumbua huyu mfanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini mifumo isiongee kwa pamoja? Akienda Halmashauri mtu wa Halmashauri, wajue huyu mtu hadaiwi kodi yoyote, ana Tax Clearance ambayo iko kwenye mfumo inaonesha. Au akienda kama anadaiwa basi mfumo uoneshe moja kwa moja. Kwa hiyo, tuweke mazingira ambayo yanaoana (mazingira ya Kiserikali) ambayo mtu akienda eneo hili anapata huduma zote kwa mara moja na siyo kuhangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, mmeondoa ada kwa Kidato cha Tano na cha Sita, ni vizuri, ni jambo jema, lakini ada ni kitu kidogo katika michango mingine mingi sana iliyopo. Leo mtoto wa Kidato cha Tano na cha Sita anapoenda kuanza, anapelekewa Joining Instruction ambayo ina michango mingi kuliko hata ile ada iliyoondolewa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema, mmefanya vyema kwa sababu mnataka kuondoa hiyo ada na kusema elimu bila ada, lakini tukumbuke pia Kidato cha Tano na cha Sita, siyo elimu ya lazima. Kuanzia Darasa la Kwanza mpaka Form Four ndiyo elimu ya lazima na kila mwanafunzi aende. Sasa hawa wanaoenda ni option tu, lakini kuna hao wengine ambao ni wa Kidato cha Nne kurudi chini, hawa nao hawalipi ada, lakini huku nako kuna michango. Kwa hiyo, ni vyema sana tuboreshe hii ya lazima ambayo inawachukua kila mtu; Darasa la Kwanza mpaka Kidato cha Nne, tupunguze na tuhakikishe pia hata hii ambayo imeondolewa kwenye Kidato cha Tano na cha Sita; na Mheshimiwa Kakunda alisema vizuri pia kwamba tuangalie kwenye vyuo vya kati kuwaondolea ada wabaki labda na michango midogo tu ya kuwezesha utekelezaji wa hizo shughuli za kielimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba hili jambo ni jema, tumewapunguzia akina mama mzigo ambao kwa namna moja ama nyingine walikuwa wanahangaika kupata ada huko vijijini, lakini tuone pia namna ya kuwapunguzia mzigo kwenye suala la michango, imekuwa mingi mno ambayo inawekwa na shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, tumeweka kipaumbele kwenye kilimo na Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yako umesema kwamba kipaumbele this time itakuwa kilimo, ni vizuri mmefanya vizuri kwa sababu kilimo ni ajira, kilimo kinachangia kwenye uchumi wa nchi, kilimo ni kila kitu. Tunamshukuru Mungu kwa sababu tuna ardhi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ardhi ya Tanzania ikitumika vizuri kulingana na kanda zetu, na hali ya hewa kwenye maeneo yetu, kwa kweli sisi ni matajiri sana sana. Tunahitaji kutumia ardhi kupitia kilimo kuhakikisha uchumi wa nchi unakua, uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa jamii unakua. Ila tunahitaji bajeti itosheleze, bajeti za utafiti ziwepo kwenye suala la kilimo, bajeti husika ya Wizara ambayo imeomba ipatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tuna kilio kikubwa sana, tunapitisha bajeti ya Wizara hapa mfano Kilimo, haiendi kama ambavyo imepitishwa. Kwa hiyo, tunategemea safari hii kama kweli mmesema kilimo ni kipaumbele, tuone basi kwa matendo kwa kuhakikisha kwamba, hiyo bajeti ya WIzara ya Kilimo ambayo tumepitisha hapa Bungeni inatolewa kwa wakati na inakwenda kufanya yale ambayo yamekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala la kilimo tunahitaji utashi wa kisiasa. Kama kuna utashi wa kisiasa wa kufanya kilimo ndiyo kipaumbele, tunahitaji kufanya kilimo ndiyo kisaidie uchumi wa mtu mmoja mmoja, kwa jamii na nchi kwa ujumla, basi tuone kwa matendo suala la kilimo mnalipa kipaumbele. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Tayari! Mh!

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)