Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali jioni hii. Kwanza kabla ya kuchangia nilikuwa nataka nitoe pongezi zangu kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa statement ya kusamehe madeni ya wafanyabiashara ya miaka ya nyuma. Jambo hili ni kubwa, limejenga confidence kwa wafanyabiashara, limeleta harmonization na sasa wafanyabiashara wetu wanafanya biashara zao kwa amani. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la elimu bila malipo. Tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa kutoa dira na sasa tutakuwa na wanafunzi wanasoma kuanzia Darasa la Kwanza mpaka Kidato cha Sita bure. Kwa sisi ambao tumetoka kwenye jamii za wakulima na wafugaji tunajua thamani ya jambo hili, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni nyongeza ya mishahara kwa Watumishi wa Umma. Mheshimiwa Rais ameongeza mshahara kwa watumishi wa Umma, tunamshukuru pia kwa hili, kwa kuona hii sekta ya muhimu katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na jambo la nne ambalo ningependa kutoa pongezi ni suala la udhibiti na usimamizi wa fedha za umma. Tunashukuru sana kwa Serikali kuchukua mawazo mbalimbali ya Bunge toka bajeti ya mwaka 2021 tulipokuwa tukichangia na Mpango wa Maendeleo ya Taifa, tulisema kwamba, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali zijengewe uwezo; na kwa safari hii wameliona, ofisi zote mbili, kwa maana ya Internal Auditor General na Ofisi ya CAG kwa maana ya National Audit Office wamejengewa uwezo na wametengewa fedha za kutosha kwa ajili ya kuimarisha kazi zao. Tunawashukuru na kuwapongeza Serikali kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo takribani sita ningependa niyachangie jioni hii, ambapo nitayachangia kwa ufupi ili niweze kuyamaliza. Jambo la kwanza nitachangia ni mfumo wa kodi na ukusanyaji wa mapato nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1977 ilipovunjika Jumuiya ya Afrika Mashariki tulianza mchakato wa kuirejesha mwaka 1999 na mwaka 2000 Jumuiya ya Afrika Mashariki ikawa imeanza. Tuliporudi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki nchi zilizokuwa tatu zikiunda Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo, kila moja ilikuja imeboresha mfumo wake wa ukusanyaji kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uganda walikuja na mamlaka yao ya mapato wanaita Uganda Revenue Authority ambayo waliitengeneza mwaka 1991. Kenya walikuja na mamlaka yao ya mapato wanaita Kenya Revenue Authority, (Mamlaka ya ukusanyaji Mapato ya Kenya) ambayo waliitengeneza mwaka 1995, na sisi Tanzania tukaingia na mamlaka yetu ya ukusanyaji wa mapato ambayo tuliitengeneza mwaka 1995 chini ya utawala wa Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifuatilia study mbalimbali na chambuzi mbalimbali, mpaka sasa tunapoongea Mamlaka yetu ya Mapato Tanzania ni moja ya mamlaka za mapato bora sana katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tuna mfumo mzuri wa uendeshaji, lakini tuna mfumo mzuri wa muundo kwa maana ya institution, lakini tuna changamoto ambayo tukiweza kui-address inaweza ikawa na msaada sana katika ukusanyaji wetu wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa mapato, tuna kodi za aina mbili; tuna kodi za moja kwa moja kwa maana ya kusema direct tax. Pia tuna kodi ambazo siyo za moja kwa moja kwa maana ya indirect tax kwa mfano VAT. Changamoto kubwa tuliyonayo ni kwenye kodi za moja kwa moja na hususan hapa tunapokenda kwenye income tax. Nitaongea kidogo, niwaombe Serikali mlichukue mliangalie, hata kama siyo bajeti ya mwaka huu, basi bajeti ya mwakani mnaweza mkaliangalia, kwani litapunguza sana usumbufu kwa wafanyabiashara wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kodi ambazo ni direct, (za moja kwa moja), kwa mfano tuna corporate tax, tuna withholding tax, tuna income tax, tuna service levy, na kadhalika; ukija katika mfumo wa hizi kodi za moja kwa moja kwa mfano kodi ambazo zinahusisha vibali na leseni, huwa hazina changamoto sana kwa sababu, zenyewe zina tozo ambazo zimepangwa ziko fixed. Kwa hiyo, mtu anajua mimi ninapotaka kuanzisha biashara, leseni yangu ni kiasi fulani. Nataka nisajili kampuni, badaye nitatakiwa kulipa kiasi fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inakuja kwenye hizi biashara ambazo tunahitaji kufanya bargaining, kwa wafanyabiashara wa hizi biashara zetu za kawaida kwenye kodi ya mapato, ndiyo shida kubwa inapoanzia hapo inaleta manung’uniko. Inasababisha mambo makubwa matatu; jambo la kwanza, kunakuwa kuna inconsistency. Unakuta mfanyabiashara mmoja ana kiwango sawa na biashara ya mwingine na mtaji sawa, lakini mapato na kodi wanalipa tofauti. Matokeo yake inaleta malalamiko kwa wafanyabiashara wetu. Kwa hiyo, tunaomba Serikali mlichukue hili mchakate vichwa na wataalamu wenu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, muweze kuja na mpango mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbele ya safari mje na scientific approach ya kukusanya hizi kodi, tuondokane na huu mfumo wa bargaining na ku-compromise, unasababisha pia rushwa kwa wananchi, matokeo yake tunajikuta kwamba Maafisa wetu wa TRA wengi wana-compromise wanaingia katika mitego ya rushwa. Anakwambia ili nikukadirie kodi kiasi fulani, basi hii hela nyingine nipe mimi, weka pembeni au kampatie mtu fulani. Hii ndiyo msingi wa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, kama Wizara, kama taasisi mliopewa dhamana ya kusimamia masuala ya kodi nchini chakateni vichwa, tumieni wataalamu wenu, shirikisheni wasomi mbalimbali mje na schedule, au scientific approach itakayotusaidia kama nchi kutoka hapa tulipo tusiendelee kuwa na mfumo wa kodi wa kufanya bargaining na matokeo yake inasababisha rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia madhara ya huu mfumo Serikalini yanaleta inefficiency, maana yake ufanisi unakuwa haupo, na ndio maana unakuta tunakadiria kodi, tunasema tutakusanya Shilingi trilioni 31, matokeo yake tunaishia kwenye Shilingi trilioni 27. Hii ni kwa sababu tunajikuta tunaweka viwango ambavyo siyo realistic. Kwa hiyo, katika hilo naiomba Serikali ilichukue na ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili la msingi ninalopenda kuchangia ni ushirikiano kati ya Serikali na wafanyabiashara katika dhana ya kujenga uchumi jumuishi. Tunasema tunajenga uchumi jumuishi na uchumi wa watu. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba hili tuliangalie, kuna wafanyabiashara wa juu, wa kati na wa chini. Wote katika kipindi hiki ambacho tunafanya transformation, basi tujitahidi kuwagusa kadiri ya changamoto wanazokabiliananazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi naweza nikatolea mfano kwangu pale Igunga, kuna wafanyabiashara takribani 209 walinyang’anywa vibanda na Serikali kwa maana ya kupitia Halmashauri. Mheshimiwa Jafo alianza kulifanyia kazi hili, akaja Mheshimiwa Ummy na nimemuona Mheshimiwa Bashungwa. Tunaomba hili Serikali mlichukue mlifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara ambao ndio chanzo cha kutoa kodi, na pia ni wadau wa maendeleo katika maeneo yetu ambao wanatoa ushirikiano kwa Serikali na kwa chama chetu, wanapokuwa wanasumbuliwa na kunyang’anywa vibanda vyao kabla ya mkataba; mkataba umenyang’anywa na Serikali kabla ya miaka miwili, tunaomba Serikali ilimalize hili, wafanyabiashara wetu warudishiwe vibanda vyao. Mkataba wao utakapoisha, watakaa mezani na Serikali, wataweza kujadiliana. Tunafungua nchi. Katika kufungua nchi, ndiyo namna hii ya kuwasaidia wafanyabiashara hata wa ngazi ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu napenda kuchangia jioni hii ni suala la mafao ya wastaafu. Katika nchi mpaka sasa tunafanya vizuri na niwapongeze Serikali mnakwenda vizuri; kumekuwa na changamoto moja katika suala la mafao. Unakuta mstaafu anastaafu kwa Daraja F, lakini mafao analipwa kwa Daraja E. Hii nayo imekuwa ni changamoto kubwa na ninadhani maeneo mengi katika nchi hili limekuwa ni tatizo. Mwingine amestaafu kwa kutumia Daraja G, lakini analipwa Daraja F. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaombe Serikali muweke modality nzuri ya kuhakikisha mtu anapofikia hatua amestaafu, kuna zile tunaita declaration; katika zile fomu asaini tamko la mwisho kwamba hiki ndiyo kiwango cha mafao yangu nitakayoyapata, ili tuepushe usumbufu kwa hawa watu wanapostaafu. Kwani hela wanazopewa za pension wanaanza tena kutumia katika nauli za kuja Dodoma au kwenda Dar es Salaam katika kufuatilia mafao yao. Ni usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapofikia mwisho mtu anastaafu, akiwa anaondoka kwa Afisa Utumishi wake au kwa mwajiri wake anajua mimi nitapokea Shilingi milioni 50, hii mwisho na anaweka saini kwenye tamko, maana yake hatakuwa na usumbufu mwingine wowote. Hawa ma-accounting officers kwa maana ya waajiri, kama mtu bado ana tatizo kuhusu mafao yake asiruhusiwe kusaini ile declaration kwa sababu inakuja kuwa ni usumbufu baadaye. Kwa hiyo, naomba Serikali mlichukue na lenyewe muweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ningependa kuchangia jioni hii ni suala la ruzuku ya pembejeo za kilimo. Naishukuru na kuipongeza Serikali, mmeongeza fedha kwenye kilimo, mmeweka fedha za pembejeo. Hapa Serikali naomba mtusaidie maeneo mawili, jambo la kwanza Serikali tunaomba ruzuku iliyotolewa iwahusishe walengwa, iwafikie walengwa ambao ni wakulima wetu wote ambao wapo katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. Kumekuwa na tabia au ukiangalia historia, maeneo mengi ambayo fedha za Serikali huwa zinapigwa, ni ama zimetoka kwenye ruzuku kwa maana ya subsidy au zile stimulus package. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba katika hili Serikali, naamini Wizara ya Kilimo kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe na kaka yangu Mheshimiwa Mavunde mtalisimamia vizuri, ruzuku hii iweze kuwanufaisha wakulima wetu. Jambo la pili mtakalotusaidia hapa, ruzuku hiyo ifike katika kipindi kinachoendana na misimu ya kilimo. Tunaomba kama ni pembejeo tutakapozipata zikitoka ambazo zimeambatanishwa kwa ruzuku hii, basi zifike katika kipindi kinachohusisha misimu ya kilimo tusije tukapishana na msimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano ni suala la nishati. Napenda kuchangia kwenye suala la umeme na mradi wa bomba la mafuta la kutoka Uganda kwenda Tanga. Sisi Igunga hili bomba linapota pale. Kuna baadhi ya wananchi walipitiwa, wanatakiwa kulipwa fidia. Walishafanyiwa assessment, wamefungua account, lakini mpaka leo hawajalipwa fidia zao. Naomba wananchi wa Igunga walipwe hii fidia. Wamelipa fidia eneo la Bulyang’ombe tu pale ambapo wanajenga site camp, lakini maeneo ambayo bomba linapita bado hawajalipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna vitongoji ambapo bomba linapita walisema wakati wanatambulisha mradi kwamba watapeleka umeme.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba pia umeme katika hivi vitongoji uweze kupelekwa ili hata watakapoanza shughuli zao za bomba basi umeme uwepo wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kuchangia jioni hii ni suala la…

MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ilishalia.

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Naam!

MWENYEKITI: Kengele yako ilishalia, nimekuachia umalizie hiyo sentensi.

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru. Naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)