Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami nichangie hotuba ya bajeti hii ya mwaka 2022/2023. Niianze kwa kuunga mkono bajeti hii kwa sababu bajeti hii inakwenda kujibu matatizo, na shida za wananchi wetu. Ni bajeti ambayo mama amekwenda kusikiliza kilio cha Wabunge na kilio cha Wabunge ni kilio cha wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ilivyo ada, naweza nikasema mengi kusifia bajeti hii, lakini kwa sababu mengi yameshazungumzwa, niende moja kwa moja kwenye mada ambayo imenisimamisha. Nianze na nukuu ya Mwalimu Nyerere, ili Watanzania tuweze kupata maendeleo, Mwalimu Nyerere anasema, tunahitaji watu, ardhi, siasa safi, na uongozi bora. Sasa mimi nitajikita kwenye uongozi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, namna nzuri ya kwenda kutekeleza hii bajeti ni lazima tuwe na watu wanaokwenda kusimamia kwa uadilifu, wanaokwenda kufuata misingi ya utawala bora. Ili tuweze kuwapata hawa watu, ni lazima Serikali ijikite kuimarisha vyuo vyetu vya utawala bora. Serikali ijikite kuhakikisha wananchi wanapata mafunzo wawapo kazini, lakini kama haitoshi, basi kuwepo na semina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameanza kuwaamini vijana, ni jambo jema sana, lakini vijana hawa walio wengi bado hawajapita kwenye vyuo vya Utumishi wa Umma. Kwa hiyo, ni muhimu sana tuwapeleke kwenye semina, tuwapeleke kwenye semina elekezi ili waweze kujua mipaka ya majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niongeze na mfano kidogo. Leo hii wako wateule wa Mheshimiwa Rais; wako ma-DC na ma-RC. Zipo sheria zinazowalinda na zipo sheria ambazo wanazitumia. Labda kwa kutokuzijua au kwa makusudi, iko sheria moja ya saa 24 kwa ma-DC na saa 48 kwa Wakuu wa Mikoa. Sheria hii ilikuwa ikiwaumiza sana wananchi. Matumizi ya sheria hii yamekuwa yakiwaumiza sana wananchi kwa sababu wako ma-DC na ma-RC wanaitumia sheria hii kinyume na utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sijasahau, Mheshimiwa Mkuchika alipokuwa Waziri wa Utawala Bora alituletea somo hapa, alituambia mtu ambaye anapaswa kukaa ndani saa 24, kwanza ni kwa sababu yeye kuwepo kwake nje kutahatarisha usalama wake; au la, kuwepo kwake nje kutahatarisha usalama wa jamii. Leo hii sheria hii inatumika bila mpangilio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo, huyo mtu akishawekwa ndani, kama ni Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, lazima akaandike kwenye kitabu cha Polisi pale kwamba, amewekwa ndani saa 24 kwa sababu gani? Kesho yake anatakiwa afikishwe Mahakamani; nitoe mfano mmoja. Mimi kwenye Wilaya yangu ya Liwale ninaye DC sasa hivi ana mwaka mmoja, tayari watu 20 wameshawekwa ndani. Kati ya hao 20 hakuna hata mmoja aliyefunguliwa mashitaka. Yuko Diwani wa Kata ya Nangano, Abdallah Lilombe kawekwa ndani. Yupo Mtendaji wa Kata, wa Kata hiyo hiyo Erick Mpinga kawekwa ndani; yupo Mtendaji wa Kijiji, Neema Kibasi kawekwa ndani; Kata ya Ngongowele yupo Mganga Mfawidhi wa Zahanati kawekwa ndani saa 24; kwenye Kata ya Kimambi yuko Afisa Maliasili na Uvuvi kashawekwa ndani; Afisa Mifugo wa Wilaya kashakaa ndani, Afisa Mifugo wa Kata kashawekwa ndani; na Afisa Manunuzi wa Wilaya kashawekwa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine ni kwenye Kata ya Makata yuko Mwenyekiti wa AMCOS kashawekwa ndani; Katibu wa AMCOS kashawekwa ndani; dereva kashawekwa ndani; utingo kashawekwa ndani. Orodha ni ndefu, lakini kati ya hawa hakuna aliyefunguliwa mashitaka hata mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini? Ni kwamba tunakwenda kushusha utendaji kwenye Halmashauri. Leo Halmashauri ime-paralyze, hakuna anayefanya kazi kwa kujiamini, watu wanasubiri maelekezo. Unamweka ndani Afisa Mfawidhi, Mganga Mfawidhi unamweka ndani kwa kosa la kwamba jengo limejengwa vibaya. Yeye sio engineer wala sio Afisa Manunuzi. Halafu ukishamweka ndani humpeleki Mahakamani, inasaidia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa Mheshimiwa Waziri tuimarishe kitengo cha utawala bora. Tupeleke hawa wateule wote kwenye vyuo vya utawala bora wakajifunze; na vilevile wapewe instrument yao wasome, waambiwe mipaka yao ni ipi? Unamweka ndani saa 24 mtu, kwa lipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nimelizungumza kwa msisitizo mkubwa kwa sababu, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ime-paralyze sasa hivi hakuna anayefanya kazi, wote wanasubiri kuwekwa ndani. Kila mtu anajua kwamba hapa akipita Mkuu wa Wilaya mimi ni kuwekwa ndani bila hata sababu ya msingi. Kwa hiyo, jambo hili linakwenda kuondoa maana ya utawala bora na Halmashauri zetu zinaenda ku-paralyze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Diwani ameshawekwa ndani, hata Mbunge naye atawekwa ndani. Kwa hiyo, nashauri sana, naomba kuimarisha utawala bora. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba nilizungumze kuhusiana na barabara. Nilipopitia bajeti ya kisekta tulipoingia kwenye bajeti ya miundombinu, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Liwale niliridhika kidogo baada ya kuona barabara ya Masasi – Nachingwea; Nachingwea – Liwale imekwenda kuwekwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Tena Mheshimiwa Waziri alisema kwamba, barabara hii anakwenda kuijenga kwa PPP, ule mpango wa EPS plus F, lakini kwa masikitiko makubwa jana Mheshimiwa Waziri wakati anaizungumza, ametaja barabara kadhaa, lakini barabara ya Masasi – Nachingwea; Nachingwea – Liwale sikuiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu Mheshimiwa Waziri utakaposimama ku-wind up hapo mwisho wa hotuba yako, naomba uniambie barabara ya Masasi – Nachingwea; Nachingwea – Liwale, nini hatima yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, siyo kwa umuhimu, naomba niende kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii. Wakati nachangia kwenye sekta ya maliasili nilizungumzia suala la Wizara hii kutupatia Maafisa wa Wanyamapori kwenye Kata zetu, kutupatia vituo kwenye Kata zetu, lakini kwenye bajeti hii kubwa sijaliona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, wakati nachangia pale nilisema kabisa kwamba kwenye bajeti hii mtarajie kutuletea chakula Liwale, kwa sababu sisi kule mazao yanavunwa mwezi wa Sita na wa Saba, lakini wakulima tayari tangu mwezi wa Nne wamesharudi baada ya mazao yao kuliwa na tembo. Nikapendekeza hapa kwamba tuletewe maaskari kwenye kata zetu kama ilivyo mapolisi kata kwenye kata zile zote ambazo ziko pembezoni mwa hifadhi, tunaomba hawa mapolisi waje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nikapendekeza tuwe na vituo. Wilaya ya Liwale asilimia 60 iko Selous. Tunacho kituo kimoja. Kituo hiki kiko pale Liwale Mjini. Nikapendekeza awali kituo kile kilitakiwa kijengwe kwenye Kata ya Barikiwa, nikapendekeza kirudishwe kule kwa sababu umbali wa kutoka Barikiwa mpaka Liwale Mjini ni zaidi ya Kilometa 70. Kwa hiyo, hayo ndiyo mapendekezo niliyatoa kwenye bajeti ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye ku-wind up hotuba yake naomba kupata majibu ya hayo mapendekezo yangu kama yalipuuzwa au yamechukuliwa hatua gani? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)