Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ENG. DKT. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika hoja hii ya Bajeti Kuu ya Taifa. Kwanza napenda kuunga mkono hoja ya bajeti hii ambayo ni bajeti ya wananchi iliyowasilishwa na Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda kutoa pongezi kwa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti ya wananchi ambayo kwa kweli imekidhi mambo mengi. Kwanza imeongezeka kwa asilimia 8.1 ambayo inaashiria kwamba vitu vingi vimeongezeka, huduma nyingi zimeongezeka. Pili, amefuta ada na mambo mengine mazuri. Pia ni bajeti ambayo ina mambo mengi mazuri ambayo hata muda wa kuyaelezea unakuwa ni kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nitoe pongezi kwa Mawaziri wote, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu kwa kazi nzuri wanayofanya ya kumsaidia Mama kutuletea maendeleo katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia bajeti yetu ilivyopangwa na kuletwa, utekelezaji wake utahitaji mambo mawili makubwa, ambayo kwanza ni kuongeza mapato; na pili, ni kubana matumizi. Tunanipongeza bajeti hii kwani hayo yote mawili yamejitokeza mabaya na katika uwasilishaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 ni kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya Taifa. Sasa mimi nitaelekeza mchango wangu katika viwanda vya vifaa vya ujenzi, wajenzi wenyewe yaani Wakandarasi na tatu, ni uhai wa matokeo yao ya ujenzi huo kwamba ni nini ambacho kinaendelea?

Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa vya ujenzi kutoka nje au vyenye kutumia bidhaa nyingi kutoka nje vimepanda sana. Kwa mfano, tukichukua mabati ya kuezekea, bei yake imepanda kidogo. Kwa hiyo, hapa katika bajeti hii, ushauri ambao tunaoutoa ni kwamba tutumie vifaa vingi vyenye asili ya hapa nyumbani ili tuweze kupunguza utegemezi mkubwa kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ambao nitautoa hapa ni huo huo wa mabati kwamba kwa miaka ya nyuma tumekuwa tukiona majengo mengi ya Serikali yalikuwa yakiezekwa kwa vigae na kwa kweli yamekuwa yakidumu kwa muda mrefu; na huko nyuma tulikuwa vilevile na viwanda vya vigae. Ukiangalia vigae hivi vinahitaji vitu viwili tu, udongo ambao ni mwingi sana tunao hapa nchini, na vilevile kama ni malighafi ya kuchomea, tukiokoa misitu yetu tunaweza tukatumia hata gesi ili tuweze kuchoma vigae tuvipate kwa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tukipunguza utegemezi wa vifaa ambavyo vinatengenezwa nje na tukaongeza vifaa ambavyo vinatengenezwa ndani ya nchi tutakuwa tumemsaidia sana Mama katika bajeti yake hii ya wananchi kwani tutakuwa tumepunguza utegemezi kutoka nje na vilevile tutakuwa tumepunguza utegemezi wa dhana ya imported inflation kwani bidhaa nyingi kutoka nje zinakuwa na mfumuko wa bei ambao hauko ndani ya uwezo wetu katika udhibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili nitajielekeza kwa Wakandarasi. Tumekuwa na miradi mingi ambayo tunaitekeleza hapa nchini, lakini miradi hiyo mingi inatekelezwa na Wakandarasi kutoka nje. Hii inatokana na vigezo ambavyo vinawekwa katika tathmini kwamba uwezo, uzoefu na kadhalika; na katika hilo nashauri tuendelee kujenga uwezo wa makandarasi wetu wa ndani ili waweze kujenga hii miradi mikubwa. Tufanye juhudi za makusudi za kuwawezesha watendaji wa ndani hawa Wakandarasi ili waweze kutekeleza hii miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ambao tunaipongeza Serikali kwa kuwa imefanya hilo, imeweza kuwakusanya Wakandarasi katika miradi minne ya majaribio ambayo imewajengea uwezo. Kuna daraja la Mbutu ambalo limejengwa na Wakandarasi wa ndani, wameungana Wakandarasi 10 ambao imewasaidia kujenga uwezo wa kutekeleza mradi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna barabara ya Dumila - Kilosa ambayo hadi sasa hivi inajengwa na ina mkusanyiko wa Makandarasi 10 ambao nao vilevile tunawajengea uwezo wa kujenga barabara hizo. Barabara ya Urambo - Kaliuwa nayo imejengwa na Wakandarasi wa ndani lakini kwa mkusanyiko huo huo wa kuwajengea uwezo; na vilevile kuna barabara ya Makutano - Sanzate.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa utaona kwamba tukiziendelea juhudi hizi ambazo tunawapa uwezo Wakandarasi wa ndani kuweza kujenga miradi mikubwa, tutapunguza sana gharama za matumizi au utegemezi wa makapuni ya nje ambayo yana bei kubwa, na hiyo itatusaidia kabisa katika kutekeleza bajeti hii ya wananchi ambayo Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametuletea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kumshauri Waziri wa Fedha na Mipango kwamba Sheria ya Ununuzi iko Wizarani kwake. Kwa hiyo, anaweza kabisa kufanya juhudi za makusudi za kuweza kulirekebisha hili au kujenga uwezo wa Makandarasi wetu kwa kuwatengea miradi ya mifano au miradi ya kuweza kuwajengea uwezo ili waweze kuendelea na kuhakikisha kwamba katika miradi mikubwa inayofuata au inayokuja tuwe na ushiriki mkubwa zaidi wa Wakandarasi wetu wa ndani ili bei iweze kupungua na vilevile na fedha nyingi zaidi iweze kubaki hapa kwetu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa tatu, napenda kuelekeza katika matokeo ya ujenzi huu ambao unafanywa. Mama yetu ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa miradi mingi; zahanati, hospitali, barabara, na kadhalika. Sasa tunajiuliza; je, katika fedha hizo ambazo zimetengwa, miradi hiyo uhai wake utakuwaje? Kwa hiyo, hapo tunatoa tena ushauri kwamba ili tuweze kuwa na matumizi mazuri zaidi ya fedha zetu na kuhakikisha kwamba fedha hii ambayo inatolewa na Mama inatupa value for money, basi tutumie vifaa bora ambavyo vitaakisi matokeo ya kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa ndiyo kuna changamoto kwa sababu vifaa bora vinakuwa na bei kubwa kidogo kuliko vifaa duni, lakini ukiangalia uhai wa vile vifaa unakuta kwamba ni tofauti sana. Sasa katika bajeti yako tumeona kwamba Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ameongezewa bajeti na hii inampa uwezo wa kukagua zaidi, basi huyu CAG naye ajengewe uwezo wa kuhakikisha kwamba anapata uwezo wa kutathmini life cycle cost ya mradi mzima. Tusipotoshwe na bei ndogo ya mwanzo ambayo unakuta kwamba mradi huo ukikamilika unaweza kuwa una maisha mafupi zaidi kuliko kutumia vifaa bora zaidi ambavyo vitakuwa na maisha marefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukikamilisha jengo lako ambalo litakaa miaka miwili halafu linakuwa limekwisha kwa gharama nafuu, lakini ukitumia vifaa bora ambavyo utaweza kupata jengo hilohilo kwa gharama kubwa kidogo lakini likakaa miaka mingi zaidi, utakuta kwamba ukifanya tathmini kwa life cycle cost utakuta ni kwamba ni bora utumie vifaa bora lakini upate kitu kizuri kitakachodumu miaka mingi kuliko kuwa unafanya marekebisho na matengenezo kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili linahitaji tujengeane uwezo kidogo kwani inatia hamasa sana kuchukua vifaa vya bei nafuu ambavyo vina uhai mfupi, badala ya vifaa vya kudumu muda mrefu. Wote ni mashahidi kwamba katika majumba yetu huko unaweza ukanunua bomba la bei nafuu la Shilingi Elfu Tano, lakini kila baada ya miezi miwili au mitatu unalibadilisha, ukinunua bomba la 15,000 ungekuta bomba linakaa miaka mitatu, ukijumlilsha utaona kwamba ni heri ununue kile ambacho kinadumu kuliko kununua kile kitu ambacho ni rahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa Wizara hii kuleta bajeti ambayo imeakisi hayo matakwa na ninaunga mkono hoja. (Makofi)